Print this page

‘Watawa msikengeuke’

By February 09, 2024 855 0

DAR ES SALAAM

NA MATHAYO KIJAZI

Watawa nchini Tanzania wametakiwa kutokengeuka, wakidhani mahali walipo wamepotea njia, bali watambue kuwa wanapaswa kuyaishi yale waliyoyapokea kwa furaha, kwa sababu wao ni zawadi kutoka kwa Mungu kwa ajili ya Kanisa.
Hayo yalisemwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, wakati akitoa homilia katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sikukuu ya Watawa iliyoadhimishwa katika Parokia ya Kristo Mfalme – Tabata, jimboni humo.
“Nasema hivyo nikijua kwamba hapa na pale, wapo Watawa wanaokengeuka, wako wanaodhani wamepotea njia, na katika mahangaiko, wanabadili mwelekeo….
“Naomba yale ambayo mmeyapokea kwa unyofu, mmeyapokea kwa furaha, na mmetamka kwa hiari yenu kwamba mtayaishi, basi muyaishi,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Aidha, Askofu Ruwa’ichi aliwashukuru wote kadri ya karama zao mbalimbali, akiwaomba kuziendeleza karama hizo katika maisha yao.
Wakati huo huo, Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwataka Watawa hao kuwa watii kwa Mungu na mpango wake, kwa ajili yao na Kanisa, pia Ulimwengu.
“Tumejitosa kwa nadhiri zetu kumfuata Kristo, Nuru ya Ulimwengu, ambaye ni Mtii, ambaye ni Fukara, ambaye ni mwenye Usafi Kamili wa Moyo.
“Na kama ndivyo, basi tunao wito wa kuwa watii, watii kwa Mungu na mpango wake kwa ajili yetu, kwa ajili ya Kanisa, na kwa ajili ya Ulimwengu,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Alisema kuwa watawa hao wanatakiwa kuwa wasafi wa moyo, wakiishi kitakatifu, wakiishi kwa upendo, na kushuhudia na kuutangazia Ulimwengu upendo wa Mungu.
Kwa mujibu wa Askofu Mkuu Ruwa’ichi katika Ulimwengu wa sasa, wapo wanaowashangaa Watawa kwa kukubali kuishi maisha ya ufukara, usafi wa moyo na utii, wakidhani kwamba wamepotea njia, bali watambue kuwa mbele ya Mungu, maisha ya Wakfu, ni Matakatifu.
Aliwataka Watawa kuuishi utakatifu wa maisha yao pamoja na ushuhuda unaowapasa, ili kwa njia yao, Kristo atambulike, aungamwe, na aaminiwe na wengi.
Askofu Mkuu aliwasisitiza Watawa hao kuwa na shauku ya kumuona, kumpokea, kumuungama, pamoja na kumtukuza Kristo kwa maisha matakatifu na ya kumpendeza Mungu.

Rate this item
(0 votes)
Japhet