Print this page

Jimbo Kuu Dodoma lapata Msaidizi

By February 19, 2024 420 0

DAR ES SALAAM

NA MWANDISHI WETU

Baba Mtakatifu Fransisko amemteua Padri Wilbroad Henry Kibozi kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.
Askofu Mteule Kibozi wa Jimbo Kuu hilo aliteuliwa Februari 12 mwaka huu, ambapo hadi uteuzi huo, yeye alikuwa Makamu Gombera na Profesa wa Seminari Kuu ya Familia Takatifu, Kahama.
Askofu Mteule Wilbroad Henry Kibozi (pichani), alizaliwa Aprili 30 mwaka 1973 mjini Dodoma. Majiundo yake baada ya sekondari, alisoma Falsafa katika Seminari Kuu ya Ntungamo, Jimbo Katoliki la Bukoba, na Taalimungu katika Seminari Kuu ya Kipalapala, Jimbo Kuu Katoliki la Tabora.
Baada ya kufanya shughuli za kichungaji kwa muda wa mwaka mmoja katika Parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji huko Chalinze (Dodoma), aliendelea na masomo na kupata leseni na Shahada ya Udaktari wa Taalimungu katika Kitivo cha Taalimungu cha Italia ya Kati, huko Firenze.
Alipewa Daraja Takatifu la Upadri Julai 9 mwaka 2010, kwa ajili ya Jimbo lake Kuu, Dodoma, Tanzania.
Askofu Mteule Kibozi alishika nyadhifa mbalimbali  kama vile Paroko Msaizidi wa Parokia ya Lumuma, kati ya 2010-2012, Mkurugenzi wa Miito Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma kati ya 2012-2014, Muungamishi katika Nyumba ya Malezi huko Livorno, Italia, kati ya mwaka 2017-2019, Mkufunzi wa Waseminari katika Chuo Kikuu cha Jordan, Jimbo Katoliki la Morogoro, kati ya mwaka 2019-2020. Tangu 2020, amekuwa Makamu Gombera na Profesa katika Seminari Kuu ya Familia Takatifu ya Kahama, Tanzania.

Rate this item
(0 votes)
Japhet