Dar es Salaam
Na Israel Mapunda
Paroko wa Parokia ya Familia Takatifu, Mburahati, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Vitalis Kassembo, amesema kwamba kila muamini anatakiwa kuwa shuhuda wa Imani.
Padri Kassembo alisema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na gazeti Tumaini Letu katika mahojiano maalumu yaliyofanyika baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Pasaka, iliyofanyika parokiani hapo.
Alisema kuwa waamini wanapaswa kuendelea kusherehekea Pasaka kwa amani na upendo kwa kumtafuta Bwana Yesu Kristo.
“Tunapaswa tuendelee kuumbwa upya, kwa njia ya Sala, kutenda matendo mema, na kupokea masakramenti,”alisema Padri Kassembo na kuongeza,
“Neema hizi za Pasaka zisikae kwetu tu bali tuwashirikishe na wenzetu kile ambacho Mungu ametujalia, furahini na wengine,”alisema Padri Kassembo.
Naye Katibu Msaidizi wa Parokia ya Mburahati, Edward Alex, alisema kuwa mwaka huu Parokia hiyo inatarajia kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Parokia, hivyo wapo katika harakati za maandalizi kuelekea kwenye jubilei hiyo.
Alisema pia kuwa kila muamini anatakiwa kushirikiana na wenzake katika kutenda matendo mema kwa kusaidia wahitaji kile ambacho wamejaal;iwa na Mwenyezi Mungu.
Naye Katibu Msaidizi wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) wa Parokia hiyo, Magreth Charles, alisema kuwa wanawake wanatakiwa kutulia na kuendelea kulea familia zao.
Alisema kuwa waamini pia nao wanatakiwa kuendelea kushikamana katika kuiishi Imani yao Katoliki, hasa katika kipindi hiki cha Oktava ya Pasaka.