DAR ES SALAAM
Na Pd. Audiphace Mujuni
Maana ya Msalaba
Msalaba wa Kristo ni Altare ya Agano Jipya linalotoa Sakramenti za Fumbo la Pasaka, Katekisimu ya Kanisa Katoliki (KKK) Na. 1182. Ni mahali Kristo alipojitoa sadaka kwa ukombozi wetu, hivyo Msalaba ni Altare ya Kwanza ambapo Kristo alijitoa sadaka.
Msalaba ni ishara ya utawala wa Kristo na kushindwa kwa shetani. Msalaba ni Ukombozi wa mwanadamu, Matayo 20:28, “kama vile mwana wa Adam asivyokuja kutumikiwa bali kutumika na kuitoa nafsi yake iwe fidia kwa wengi.” Hii ni Alama Kuu katika Ukristo
Aina Mbalimbali za Misalaba.
Kuna aina nyingi za misalaba kadri ya sehemu na tamaduni husika, lakini yote inamaanisha jambo moja kuu katika Ukristo, kusulibiwa kwa Kristo.
Msalaba wa Kilatini (Crucifix), ndio maarufu zaidi. Msalaba wa Ki-Keltiki (wa Scotland), una duara kuzunguka maunganio ya msalaba. Msalaba wa Kigiriki, una umbo la herufi X. Msalaba wa Yerusalem una umbo kubwa kama wa Kilatini, lakini una misalaba mingine midogo midogo, katika vile vipembe vinne.
Historia ya Msalaba
Msalaba kama alama ya mistari miwili inayokutana katikati, ilikuwapo na ilitumika kama ishara takatifu kwa baadhi ya dini au Imani mbalimbali, hata kabla ya kuzaliwa Kristo. Kadri ya mwana historia Tyack G. S., alama ya msalaba ilitumiwa kama ishara takatifu ya muungu Bacchus wa Kigiriki na muungu Bel wa Wakaldayo miaka mingi kabla ya kuzaliwa Kristo, na waliiweka katika sarafu za pesa zao.
Pia, mwana historia Cutner H. anasema kuwa alama ya msalaba wenye duara juu yake, ilitumika na Wamisri miaka mingi kabla ya kuzaliwa Kristo kama ishara ya muungu wao wa uzazi. Waliiweka kwenye paa za majengo yao na kwenye makaburi yao kama alama takatifu.
Lakini pia, historia inaonesha kuwa kuanzia karne ya 6 Kabla ya Kristo (KK) hadi karne ya 4 Baada ya Kristo (BK), alama ya msalaba ilitumika kama chombo cha utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa watu waliohukumiwa kufa kifo kibaya na cha uchungu au maumivu makubwa.
Aliyehukumiwa alipigiliwa misumari kwenye mbao mbili zilizounganishwa kwa maumbo tofauti tofauti (kama + au X, n.k.), na kumuacha hapo juu afe taratibu. Hii ilifanyika sana nyakati za utawala wa Wagiriki na Warumi katika sehemu walizozitawala na Uyahudi ikiwemo. Hivyo kwa watu hawa, msalaba ilikuwa ishara ya kifo cha aibu, na ni kwa mtazamo huu Yesu pamoja na wafuasi wake wa mwanzo (hasa Mitume), waliuawa msalabani kama ishara ya kuwadhalilisha.
Utamaduni wa kutundika vitu kwenye miti maalum na kutumika kwa ibada, hasa za uponyaji, ulikuwepo pia kati ya Wayahudi tangu mapema. Tunasoma katika kitabu cha Hesabu, 21:4-9 kuwa baada ya manung’uniko na kutenda dhambi, Waisrael waliadhibiwa sana kwa kuletewa nyoka wenye sumu kali na kwasababishia vifo vingi huko jangwani, baadae Mungu akamuamuru Musa atengeneze Nyoka wa shaba na kumtundika juu ya mti ili kila atayemuangalia baada ya kugongwa na nyoka, atapona. Hili lilifanyika, na kweli watu wakapona.
UKUU WA MSALABA
Baada ya kuwa tumeona matumizi mbalimbali ya alama ya msalaba, sasa tuone, Utukufu wa Msalaba unatokea wapi?
“Maana kama vile Musa alivyomuinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo mwana wa Adam hana budi kuinuliwa, ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye,..maana Mungu hakumtuma mwanae ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.” Yohana, 3: 16-17.
Kristo anapoamua kuutumia msalaba kama njia ya ukombozi wa ulimwengu, anaubadilishia maana kutoka kuwa alama ya aibu, uovu, udhaifu na kifo, na kuwa alama ya Ushindi kwa wale wanaomuamini Mungu na Kristo wake. HUU NDIO UKUU WA MSALABA. Msalaba unakuwa ndiyo njia ya kumwendea Mungu. Msalaba unakuwa in ALAMA YA UZIMA WA MILELE.
MAMBO YANAYOAMBATANA NA UKUU WA MSALABA
Msalaba ni hitaji la lazima la kumfuata Yesu.
Luka, 9:23-25, “akawaambia wote, mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.” Bila Imani katika msalaba na kuwajibika kwa mahitaji ya msalaba, hatuwezi kumfuata Kristo, hatuwezi kumfikia Kristo, na hivyo hatuwezi kuokolewa na Kristo.
Msalaba ni Njia ya kueneza na kusimika Ufalme wa Mungu popote.
KKK, (Na. 550,853), “Ni kwa njia ya toba na kujifanya upya, na kwa kufuata njia nyembamba ya msalaba, ndipo taifa la Mungu linapoweza kueneza ufalme wa Mungu.”
Msalaba ni njia ya Utakatifu.
KKK (Na. 2015), “Njia ya ukamilifu hupitia kwa njia ya msalaba. Hakuna utakatifu bila majikatalio na bila vita ya kiroho.”
Msalaba ni mfano wa mshikamano na upendo wa Mungu kwa watu wake, na kati ya watu wenyewe, KKK (Na. 1939).
MSALABA NI ISHARA YA TOBA KAMILI.
Wagalatia, 2:19-21, “…, mimi nimekuwa pamoja na Kristo msalabani, na sasa naishi, lakini si mimi tena, bali Kristo anaishi ndani yangu. Maisha haya ninayoishi sasa, naishi kwa Imani, Imani katika mwana wa Mungu aliyenipenda hata akayatoa maisha yake kwa ajili yangu. Sipendi kuikataa neema ya Mungu,…”
Tukijifungamanisha na msalaba tunastahilishwa kuwa wenye haki, yaani watakatifu (Webrania, 5:9).
Tukifungamanisha na msalaba, tunakuwa huru dhidi ya dhambi, (Wagalatia, 5:1). Tunatakiwa kusimama imara ili tusinaswe tena chini ya konga la dhambi.
Kama tukiukubali Msalaba, unatupa nguvu ya kutubu dhambi, Luka, 23:39-43. Mwizi alikubali msalaba wake na kusamehewa dhambi zake.
“Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuuzi, lakini kwetu sisi tunaokolewa, na ni nguvu ya Mungu,.. kwa Wayahudi jambo hili ni kikwazo na kwa watu wa mataifa ni upumbavu, lakini kwa wale walioitwa Wayahudi kwa Wayunani (watu wa mataifa), Kristo ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu. Maana kinachoonekana kuwa ni upumbavu wa Mungu, kina busara kuliko hekima ya binadamu; na kinachooneka kuwa ni udhaifu wa Mungu, kina nguvu kuliko nguvu za binadamu...” 1Kor. 1:18-32
Tupate nguvu ya kumshinda shetani kwa msalaba wa Kristo. Tupate hekima ya Kimungu kwa msalaba wa Kristo. Weka msalaba uliobarikiwa na Shemasi, Padri au Askofu nyumbani mwako, vaa msalaba huo shingoni, nk, kama ishara ya kuishi na nguvu ya Kristo na kuishi katika Nguvu ya Kristo, na kama ishara ya kuurithi uzima wa milele.
Silaha yetu iwe ni msalaba katika maisha yetu, tukaubebe kijasiri na kusonga mbele kuuelekea uzima wa milele. Msalaba ni alama ya kuzikataa anasa za kidunia. Msalaba ni alama ya kujitoa bila kujibakiza, na Msalaba ni ishara ya sala ya Mnyenyekevu.
Matayo, 12:20, Isaya, 42:1-4, “Tazama mtumishi wangu niliyemteua, mpendwa wangu anipendezaye moyoni. Nitaiweka roho yangu juu yake, naye atatangaza hukumu yangu kwa mataifa yote. Hatakuwa na ubishi wala kupiga kelele, wala sauti yake haitasikika barabarani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi ufukao moshi hatauzima, mpaka atakapoifanya hukumu ya haki itawale. Kwake yeye mataifa yatakuwa na matumaini.”
HITIMISHO
“Kwa sababu neno la Msalaba kwao wanaopotea ni upuuzi, lakini kwetu sisi tunaookolewa, ni nguvu ya Mungu,.. kwa Wayahudi jambo hili ni kikwazo na kwa watu wa mataifa ni upumbavu, lakini kwa wale walioitwa, Wayahudi kwa Wayunani (watu wa mataifa), Kristo ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu, maana kinachoonekana kuwa ni upumbavu wa Mungu, kina busara kuliko hekima ya binadamu; na kinachoonekana kuwa ni udhaifu wa Mungu, kina nguvu kuliko nguvu za binadamu...” 1Kor. 1:18-32
Tupate nguvu ya kumshinda shetani kwa msalaba wa Kristo. Tupate hekima ya Kimungu kwa msalaba wa Kristo. Weka msalaba uliobarikiwa na Shemasi, Padri au Askofu nyumbani mwako, vaa msalaba huo shingoni, n.k., kama ishara ya kuishi na nguvu ya Kristo na kuishi katika Nguvu ya Kristo, na kama ishara ya kuurithi uzima wa milele.
Silaha yetu iwe ni msalaba katika maisha yetu, tukaubebe kijasiri na kusonga mbele kuuelekea uzima wa milele.
Pd. Audiphace Mujuni
Jimbo Katoliki la Bunda.