Print this page

Papa Pio XI Mwalimu na Mwana diplomasia (1)

Papa Pio XI (1922-1939: wa 259). Papa Pio XI (1922-1939: wa 259).

Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki iliyopita tuliwaletea Kuibuka kwa Kanisa la Misioni Katika Karne ya 20 Sehemu ya Pili. Leo tunawaletea historia jinsi Papa Pio XI kama mwalimu na Mwanadiplomasia, alivyopambana na madikteta na Ukomunisti dhidi ya Kanisa. Sasa endelea…

Kipindi kati ya vita Kuu ya Kwanza na Vita Kuu ya Pili (1918-1939), kilijaa hali ya kutoelewana na serikali, kwa sababu hazikuwa na msimamo thabiti. Kwa upande mmoja, kulikuwa na wale waliopenda demokrasia isiyo na kipimo, ambayo ilipinga hata maadili ya dini kama kandamizi.
Kwa upande mwingine, kulikuwa na udikteta ambao mtu au kundi la watu walitaka kuunda serikali yenye madaraka yote, bila kuingiza mawazo au ushiriki wa wananchi.
Kazi ya kwanza aliyoifanya Papa Pio XI ni kuleta amani na uelewano kati ya serikali ya Italia, na kanisa. Mwaka 1929 aliweza, baada ya majadiliano marefu, kufikia muafaka na serikali ya Italia juu ya nafasi ya Papa kama mtawala huru wa nchi huru ya Vatikano.
Hii ilikuwa hatua kubwa sana.  Alijitahidi kufikia makubaliano na nchi nyingine ambayo yalilinda haki na uhuru wa Kanisa.
Upinzani dhidi ya Udikteta:
Ingawa Papa Pio XI alifikia mapatano na nchi mbalimbali, hili halikumzuia kupinga majaribio ya kuwafanya watawala kuwa miungu, au kufanya serikali kuwa juu ya maadili ya Mungu.
Papa Pio XI anajulikana sana kwa kuweka nguvu zake nyingi katika kuunda “Actio Catolica,” yaani kwetu iliitwa “Aksio Katolika“. Kwa kuunda Aksio Katolika, alikuwa anasisitiza kwamba ni jukumu la walei kushiriki katika kazi ya hierakia ya uinjilishaji.
Hivyo, vyama vya Aksio Katolika, tofauti na vyama vingine vya sala na kujitakatifuza, vilipaswa kutoka nje na kuinjilisha, kuimarisha maadili ya jamii na kuleta uongozi bora wenye sura ya Kikristu katika kila nyanja.
Wana Aksio Katolika kama chama, hawakuingilia siasa ya vyama, ilibidi wawe juu ya vyama, lakini binafsi walihamasishwa kushiriki katika siasa na kuifanya iwe nzuri na takatifu.
Aksio Katolika ilitengeneza waamini walei wenye imani kubwa na nguvu za kutetea imani na Kanisa lao ulimwenguni kote. Kwa sababu hiyo, viongozi wa serikali waliovunja maadili, hawakuwapenda.
Vugu vugu hili lilienea hata mpaka Nchi za Misioni. Tanzania waliitwa “Aksio Katolika” au Waaksio nao walikuwa watu wenye uwezo, na hata mara nyingine walivaa kama Wamisionari na kuongoza Makanisa yaliyokuwa mbali na Wamisionari.
Wengine walitumwa katika sehemu ambazo Wamisionari walikuwa bado kufika, watayarishe watu kupokea imani. Katika siku zetu, vyama kama Wanataaluma Wakatoliki (Catholic Professionals of Tanzania: CPT) wanaoaswa kufanya kazi, ambayo ilikuwa inafanywa na wana Aksio Katolika.
Wakati huo, nchi nyingi zilianza kuingia udikiteta. Watawala madikteta kundi la kwanza ambalo walilipiga vita likikuwa lile la Aksio Katolika kwa sababu walikuwa na nguvu, na hawakuyumba katika imani yao. Walishtakiwa kupokea maagizo kutoka kwa Papa dhidi ya serikali.
Papa Pio XI aliandika barua 31 za kichungaji juu ya mambo mbalimbali. Kati ya hizo, barua tatu zilikuwa na uzito mkubwa kwa sababu aliongelea juu ya hali ya kisiasa, na hasa juu ya unyanyasaji wa wana Aksio Katolika na vyama vingine, hasa vile vya watoto na vijjana au‚ Vijana Wakatoliki.
Italia chini ya uongozi wa Musolini:
Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza, Musolini akiwa na chama kidogo cha mafashisti, alisaidia Italia kuingia katika vita dhidi ya Ujerumani. Baada ya ushindi alilalamika kwamba katika makubalinao ya Versailles, Italia haikupewa ardhi ilizotaka.
Kwa namna hiyo, alitumia utaifa wa Waitaliani na ari waliyoipata wakati wakiwa katika harakati ya kuunganisha Italia, kusema kwamba kuna Waitaliani ambao bado ni mateka katika nchi nyingine, hivyo sehemu zote wanakoishi Waitaliani zinapashwa kuunganishwa na Italia.
Pole pole alitumia malalamiko ya watu juu ya hali mbaya ya uchumi, na hivyo kuunda kikosi cha wanamgambo wafashisti. Mwaka 1922 kikundi hiki kiliingia na kuvamia Roma na kuipindua serikali, na Musolini akawa Waziri Mkuu.
Akiwa madarakani, alitumia kigezo cha utaifa kuvamia nchi kama Ethiopia, ili nao wawe na koloni. Vile vile, alivamia Albania akisema ni sehemu ya Italia. Alipenda kuvamia na kuchukua sehemu nyingine zilizokuwa kando ya Italia.
Ufashisti ni nini?
Ufashisti ni aina ya serikali iliyojumuisha mfumo wa kimabavu na serikali ya uzalendo  kitaifa pamoja na kushirikisha jamii kwa kuwarubuni kiakili kwa mikutano mikubwa na kampeni.
Ni serikali ambayo dikteta au mfalme anaidhibiti serikali, watu wanaotawaliwa inabidi kufuata maagizo ya dikteta wao, la sivyo, wataadhibiwa. Pole pole alichukua madaraka yote.
Mwanzoni alitaka kuwa na amani na Kanisa Katoliki, akijua kwamba lina nguvu. Hii ndiyo sababu aliweza kufikia Makubaliano ya Laterano yaliyounda Nchi ya Vatikano. Lakin siku zilivyoendelea, alianza kupiga vita mafundisho ya Dini yaliyoendana tofauti na mawazo yake.
Alipiga marufuku vyama vya Walei Wakristo. Mfalme Emmanuel III wa Italia alibaki kuwepo bila madaraka. Musolini alijiita “Il Duce” maanake “Kiongozi Mkuu.”
Kwa kupinga hayo yote, Papa Pio XI tarehe 21 Juni 1931, aliandika barua kwa lugha ya Kiitaliano, tofauti na barua nyingine ambazo zilikuwa katika Kilatini, ikiitwa, “Non Abbiami Bisogno“ ikimaanisha “Hatuwahitaji.”
Barua hii ilikuwa inampinga Musolini ambaye alikuwa amefanya serikali itukuzwe sana. Musolini alikuwa ameunda serikali ya kifashisti ambayo ilikuwa serikali ya kidikteta, ambayo ilitaka kutawala kila sehemu.
Musolini alikuwa amepiga marufuku chama cha “Aksio Katolika“ na vikundi na vyama vyote vya watoto na vijana. Musolini alitaka awe na ukiritimba wa elimu ya watoto na vijana na pasiwepo na chama chenye kuhamasisha watu.
Papa Pio XI alikiona chama cha Musolini kama “ibada ya kipagani ya Serikali” (kuabudu Serikali) na “mapinduzi ambayo huwanyakua vijana kutoka kwa Kanisa na kutoka kwa Yesu Kristo, na ambayo hukazia kuingiza ndani ya vijana hao moyo wa chuki, jeuri na ukosefu wa heshima.”
Papa Pio XI alimwita Musolini mpinga Dini, na kwamba sera yake  haiendani na mafundisho ya Kanisa.  Mwanzoni itikadi ya Musolini haikuwa mbaya sana, lakini tangu Mei 1938 Hitler alipotembelea Roma na pamoja wakaunda umoja wa ushrikiano (Axis), mambo yalibadilika. Musolini akaanza kuiga sera za Hitler za Ujerumani, mfano mmojawapo ni ule wa kuwakandamiza, hata kuwaua Wayahudi.

Rate this item
(0 votes)
Japhet

Latest from Japhet