Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha
Makala

Makala (21)

Dar es Salaam

Na Edvesta Tarimo

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia (World Bank -2023), inakadiriwa kuwa uzalishaji wa taka utaongezeka kwa 70% kutoka tani bilioni 2.01 hadi bilioni 3.40 ifikapo mwaka 2050.
Kulingana na ripoti ya taarifa ya kiuchumi ya Urejelezaji wa Marekani
(U.S Recycling Economic Information - REI), San Francisco, Marekani, ni jiji la kijani kibichi hasa, na linatajwa kama kinara kwa urejeshaji wa taka (recycling), kwa zaidi ya asilimia 80 ya taka zake.
Urejelezaji wa taka na mifumo mizuri ya kushughulika na majitaka, utasaidia kuongeza ajira, kuongeza viwanda vidogo vidogo, kuongeza teknolojia mpya, pamoja na kipato ambacho kimekuwa kikipotea, ikiwa ni pamoja na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.
Majiji mengine yanayofanya vizuri kwenye urejeshaji wa takataka ni pamoja na Curitiba - Brazil, iliyofanikiwa kwa asilimia 70, pamoja na Vancouver-Canada, waliofanikiwa kwa asilimia 60 wakiwa na lengo la kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2040.
Wanafanyaje? Kwa kushikamana na mipango madhubuti ya kuchakata taka na sera ya kulipa fedha kadri wakazi wake wanavyotupa taka zisizoweza kutumika tena, huwafanya wananchi wawe na ufahamu zaidi wa mazingira, hasa kuhusu bidhaa wanazonunua katika kuepuka kulipishwa fedha zaidi za taka.
Nini kifanyike kukabiliana na hili?
Jiji la Dar es salaam ambalo linatajwa kuwa kitovu cha biashara, lenyewe linakadiriwa kuzalisha zaidi ya tani 4,252 za taka kwa siku moja. Kati ya taka hizo, ni asilimia 50 tu ndizo zinazopokelewa kwenye maeneo maalumu, nyingine zikisalia na kutupwa kwenye mitaro, maeneo ya wazi, na hata barabarani.
Hapa Tanzania, baadhi ya wadau wa mazingira wamekuja na mpango mkakati wa kuweka mazingira katika hali safi kwa kukusanya takataka, na kwa kupita baadhi ya masoko katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kama vile Ilala, Buguruni. n.k.
Alpha Ntibachunya  ameamua kushiriki katika utunzaji wa mazingira kwa kuanzisha kampuni ya LIMA ya kurejeleza taka ngumu katika matumizi mengine, badala ya kutupwa na kuchafua mazingira.
Ntibachunya anasema kuwa yeye na mwenzake walifanya utafiti wa kujua takataka zinazotupwa zinapelekwa wapi baada ya kukusanywa, na baada ya utafiti, waligundua kuwa kuna fursa nyingi zinazopatikana kwenye takataka.
“Kilichotupelekea tukaanzisha huu mradi, tulikaa tukafanya utafiti na kugundua kwamba kuna changamoto, baada ya hapo tukapata wazo linguine, tukaja na wazo hili la kuzalisha chakula cha kulishia mifugo, na mbolea ambayo tulitazama zaidi wakulima wadogo, hasa wa vijijini,” anasema Ntibachunya.
Anaongeza kusema kuwa njia mbili tofauti wanazotumia katika kukusanya taka, kwa kwenda sokoni, mfano soko la matunda Buguruni, hotelini na kutumia njia ya boksi hai ambalo hupeleka majumbani mwa watu kwa ajili ya kukusanyia mabaki ya vyakula majumbani mwa watu, kisha wanakwenda kuzichukua na kwenda kuzichakata.
Anasema kuwa wametumia changamoto ya mlundikano wa takataka katika maeneo tofauti tofauti katika jiji kugeuza kuwa sehemu ya kujipatia ajira, na kuajiri vijana wengine katika kukusanya na kuzichakata na kuwa chakula cha kulishia mifugo, na mbolea ambayo ni halisia isiyokuwa na makemiko ya aina yoyote.
Ntibachunya anasema kwamba uchakataji wa taka katika matumizi mengine umekuwa mchango mkubwa wa nafasi ya ajira kwa vijana wengi, kwani uzalishaji wake hauhitaji kiwango cha elimu, bali utayari wa kijana wa kuelekezwa kufanya kazi hiyo.
Kuchakata taka kunanufaisha mazingira, na kunatoa ajira kwa vijana, kunakuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Kwa kutenganisha taka zinazoweza kutumika tena kama karatasi, nguo chakavu, glasi, plastiki, aluminium na mabaki ya vyakula na taka za elektroniki, watumiaji wanaweza kusaidia kuunda kijani kibichi kwenye majiji makubwa duniani.
Anitha Erasmi ni mama wa watoto wanne, anasema kuwa uchakataji wa taka umekuwa sehemu yake ya kujipatia kipato cha kuendesha maisha ya familia yake, licha ya ndugu kumwona kama amechanganyikiwa.
“Mwandishi, ndugu zangu na jamii, iliniona kama chizi, lakini mimi sikujali kwa sababu mjini kama huna kazi, ukichagua kazi utashindwa kuishi. Nakusanya mamboga mboga nazipeleka kuziuza, napewa pesa,” anasema Anitha.
Philbert Alphonce mkazi wa Goba jijini Dar es Salaam, anasema kwamba amekuwa anakikusanya taka ngumu kutoka soko na kuzipeleka sehemu wanakozichakata na kuzirejelesha katika matumizi ya kulisha baadhi ya mifugo, na pia mbolea asilia ambayo hutumiwa na wakulima wadogo wadogo kuweka kwenye mashamba ya mboga na maua.
Alphonce anasema amekuwa akiendesha familia yake ya mke na watoto wawili kupitia kazi yake ya ukusanyaji wa mabaki ya mbogamboga na kwenda kuziuza, ambapo kwa wiki anakwenda sokoni mara mbili, huku siku nyingine akizitumia kwa shughuli zake nyingine.
NEMC,Wadau watoa neno
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (National Environment Management Council – NEMC), Dk. immaculate Sware Semesi anasema NEMC, na taasisi ya mazingira, kituo cha Sayansi cha Mazingira (Centre for Science and Environment - CSE), kutoka India, wamekutana nchini Tanzania kujenga uelewa wa nini kifanyike katika taka ngumu, kuchukua takwimu ni taka kiasi gani zinazalishwa na zinatunzwaje, ili ziwe fursa badala ya kuwa uchafuzi wa mazingira.
Dk.Semesi anasema sambamba na hilo, kutambua ni teknolojia gani itumike ili kufanya taka zisiwe kero katika manispaa na jiji, bali ziwe fursa ya kuzalisha ajira au nishati kutokana na taka.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila katika moja ya hotuba yake alisema kwamba anaiona fursa kubwa kwenye wingi wa taka hizo, na tayari alisafiri mara moja kwenda kwenye jiji la Bursan nchini Korea Kusini kujifunza namna wenzetu walivyofanikiwa kwenye urejelezaji wa taka, na kuzifungamanisha na fursa kwa vijana wa rika mbalimbali.
Chalamila anasema kwamba jiji la Dar es salaam linaweza kuwa mfano kwa majiji mengine nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa fursa ya ajira kwa njia ya urejeleshaji wa taka, endapo juhudi za makusudi zitachukuliwa na kufanyiwa kazi kwa vitendo.
Anaongeza kuwa urejelezaji wa taka (recycling) ni mchakato wa kutibu taka kwa lengo la kuokoa malighafi zilizopo ndani ya taka na kuzirejesha kwenye matumizi ya kiuchumi.
Vifaa vya kielektroniki kama simu na kompyuta hurejelezwa na kutumika tena katika kutengeneza matofali, saruji na vyombo vipya vya glasi.
Taka za kaboni kama maganda ya matunda na mbogamboga, zinatumika kutengeneza mbolea na karatasi zikirejelezwa na kutumika kama makasha ya mayai na vifungashio vya bidhaa mbalimbali.
Ripoti ya Benki ya Dunia kuhusu maendeleo ya miji, inaonesha kuwa Afrika huzalisha tani milioni 70 za taka kwa mwaka.
Wakati huu ambapo ongezeko la watu wanaohamia mijini linaongezeka kwa kiasi kikubwa, Benki ya Dunia inasema kuwa kufikia mwaka 2025, uzalishaji wa taka huenda ukafikia tani milioni 160 kwa mwaka.
Tafiti zinasema kwamba ni rahisi kutengeneza bidhaa kutoka nyenzo zilizorejelezwa, kwani bidhaa kama ya aluminium iliyorejelezwa inaweza kuandaliwa tena na kuuzwa kwa bei nusu, kutokana na kuhitajika nishati kidogo ya kuchakata aluminium iliyorejelezwa, kuliko kutumia aluminium mbichi ya kiwandani inayotumika kwa mara ya kwanza.
Urejelezaji pia huepusha gharama ya utupaji wa taka kwenye dampo na vichomaji (incinerators), kwani baada ya kuanza kwa urejelezaji, dampo chache zitahitajika, na ardhi zaidi zilizokuwa zimetengwa kuhifadhi taka huweza kutumika kiuchumi.
Aidha, mapato ni sehemu nyingine aliyoiona Chalamila, kwani urejelezaji huimarisha tasnia ya uchakataji, na hivyo kutengeneza nafasi mpya za kazi kwenye viwanda vidogo vitakavyoundwa, kama viwanda vya chuma, karatasi, glasi, pamoja na ajira kwenye vituo vya ukusanyaji taka, na hata warejeshaji husika.
Utafiti wa U. S Recycling unaonesha kuwa nguvukazi ya kuchakata na kutumia tena malighafi zinazotokana na taka, imekuwa kubwa zaidi kwenye mataifa mengi, zaidi ya nguvukazi inayotumika kwenye uchimbaji wa madini na usimamizi wa taka zisizorejelezwa.Mashirika yanayorejeleza taka, huzalisha takribani dola bilioni 240 kwenye mapato ya kila mwaka.
Huko Carolina kusini pekee, zaidi ya wafanyakazi 15,000 na dola za Marekani milioni 69 za ushuru, hutokana na uchakataji wa taka, huku Carlifonia urejelezaji wa taka ukiajiri watu 85,000.
Kila mwaka, dunia inageuka kuwa makao ya takribani tani bilioni 2.01 za taka ngumu, na idadi hiyo inatarajiwa kufikia bilioni 3.40 miaka 30 ijayo, sawa na ongezeko la 70%.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, (World Bank – WB), mataifa yenye kipato cha juu inaonesha kwa siku kuna ongezeko la 19%, huku mataifa yenye uchumi wa kati na chini, ukiongezeka kwa 40% au zaidi.

Katika safu hii wiki kadhaa ziliyopita, tulisoma Historia ya Kanisa la Misri na Uinjilishaji wa Misri na Kanisa la Kaskazini mwa Afrika pamoja na kuangazia Uislam ulivyoingia Afrika. Leo tusome jinsi Uislam ulivyoiteka Afrika Kaskazini. Sasa Endelea…

Baada ya dola ya Kirumi Magharibi kuanguka, Wavandali waliokuwa wameiteka Afrika ya Kaskazini, walishindwa na Kaizari wa Mashariki katika dola ya Kostantinopoli. Kaizari alimweka gavana kutawala kwa niaba yake.
Mwaka 647 Gavana Gregori wa Kartago aliwaasi wakubwa zake wa Konstantinopoli. Waislamu walipokuja toka Misri chini ya Ukba Ibn Nafi, alidhania wanakuja kumsaidia dhidi ya Konstantinopoli, hivyo akawaunga mkono wakaingia kwa urahisi.
Baadaye walimgeuka na kuteka Afrika ya Kaskazini. Wakristo Wazungu yaani wenye asili ya Ulaya walikimbilia Ulaya na wakabaki Waberba wenye asili ya Afrika, kutetea Ukristo na nchi yao.
Mwaka 711, Mussa alimtuma Tarik (riq ibn Ziyd) jemadari wa Kiberba aliyeongokea Uislamu na jeshi lao la watu 7,000 kushambulia Uhispania. Walipoanza kupata mafanikio naye alikwenda na jeshi lake, wakateka pamoja Uhispania.
Katika kugawanya nyara hizo, Waarabu na Waberba wakawa marafiki. Guba la Gilbraltar ni ukumbusho wake ‘Gebel al Tarik’. Waberba wengi waliongoka na kuwa Waislamu kwa sababu bila kuwa Mwislamu, wasingepata sehemu ya hizo nyara na marupuuupu mbalimbali.
Mwishoni mwa karne ya 8, Afrika ya Kaskazini yote ilishakuwa ya Kiislamu. Wakati wa Mtakatifu Augustino, Afrika ya Kaskazini palikuwepo na maaskofu 700, lakini walipovamia Waislamu walibakia 35, na katika karne ya 12 walikosa maaskofu watatu wa kumweka wakfu mwenzao; na karne ya 14 hapakuwepo hata askofu mmoja.
Tofauti na Misri, ambapo ingawa lilidhoofishwa, bado Wakristo wapo licha ya unyanyasaji. Kanisa huko Afrika ya Kaskazini, maarufu kwa watakatifu na wanateologia kama Sipriani, Tertuliani na Augustino, lilitoweka kabisa.
Kosa kubwa la kwanza la Kanisa hilo ni kwamba lilijipenda na kujiendeleza kwa ndani, lakini likasahau kuinjilisha. Dini ilibaki tu katika mwambao wa dola ya Kirumi, tofauti na Misri waliotoka nje na kwenda Nubia hadi Uhabeshi.
Vilevile, dini ilibakia katika utamaduni wa kikoloni wa Kilatini hata wakawa Walatini kuzidi Roma. Hata mtakatifu Augustino ambaye mama yake alikuwa Mberba, hakuandika chochote katika lugha yao au kuingiza utamaduni wake katika Ukristo.
Wazawa walijua Ukristo kama waliingia utamaduni wa wakoloni wao. Hivyo wakoloni walipoondoka na lugha ya Kilatini, Dini ikatoweka pamoja nao. Misri waliendeleza lugha yao na kutengeneza ibada ya Kikopti, tofauti na Kigiriki.
Kanisa lisiloinjilisha na kutamadunisha, hufa. Hivyo, ile tabaka ya juu ya Walatini ambao ndio walikuwa Wakristo walipovamiwa na Waislamu, wao walikimbilia Ulaya pamoja na Maaskofu na Mapadre. Hili ni somo kubwa kwetu, Kanisa ili lidumu lazima liingie katika utamaduni na masiha ya kila siku ya watu, la sivyo litabaki kama vazi la Jumapili.
Waislamu katika Nubia (Sudan ya Sasa):
Baada ya kuiteka Misri, mwaka 641, Abdallah Ibn Saad aliishambulia Nubia. Ili kuhimili mashambulio hayo, falme mbili za Kaskazini Nobatia na Makuria ziliungana na kuwa ufalme wa makuria.
Kwa pamoja, zilishinda dhidi ya mashambulizi. Baadaye ufalme wa Makuria ulifanya umoja na ule wa Kusini wa Alodia na kupata nguvu kiasi kwamba mwaka 737 walituma kikosi hadi Aleksandria, Misri kumtoa mahabusu Patriarka aliyekuwa ametekwa na Waislamu.
Miaka kati ya 700 hadi 1250, kilikuwa kipindi cha maendeleo mazuri kwa Nubia. Walijenga makanisa mazuri, na hata mengine yamevumbuliwa na wachimbaji wa mambo ya kale. Alodia peke yake ilikuwa na makanisa zaidi ya 400 na monasteri nyingi. Pamevumbulika na maandishi mengi waliyoyaacha yakielezea ibada zao, na hasa sala.
Mwaka 1172 Misri ilitawaliwa na Waturuki wa Mamluki ambao walikuwa na nguvu na vilevile wakatili sana. Hawa walizonga Nubia, na ili kujihami, Misri iliweka Waislamu Kaskazini mwa Makuria kama ugo dhidi ya mashambulizi.
Bahati mbaya Nubia ilikuwa imekatwa kutoka ulimwengu mwingine wa Wakristo, na baadaye pakawepo mfarakano katika urithi wa wafalme. Hata hivyo waliweza kuwahimili Waislamu hadi mwaka 1504 ufalme ulipotekwa na Waislamu kutoka Misri.
Kwa miaka 1,000 walikuwa na Ukristo imara. Wamisionari waliporudi mwaka 1845 hawakukuta alama zo zote za Ukristo. Ilibidi waanze upya kati ya Waafrika weusi wa Sudan ya Kusini.
Uhabeshi (Ethipia ya sasa) na Uislamu
Uhabeshi ilikuwa na bahati ya kunusurika kutekwa na Waislamu. Sababu za kunusurika kwake kwanza ni kwamba Muhammad alipofukuzwa kutoka Mekka, Waislamu wengine walikimbilia Axum, Mji Mkuu wa Uhabeshi na kupokelewa vizuri.
Kwa sababu hiyo, Muhammad aliagiza katika Korani kwamba Uhabeshi  isishambuliwe, labda kama ni kujikinga.  Mwanzoni agizo hilo liliheshimiwa sana. Pili, nchi ya Uhabeshi iko milimani na si rahisi kuifikia na kuishambulia.
Wote waliozunguka Uhabeshi walitekwa na Waislamu, na yenyewe ikabaki kama kisiwa. Hata hivyo, Waislamu wengine waliingia mipakani na kuishi pembezoni na Waislamu wafanya biashara walioingia ndani walipeleka pamoja nao mawazo ya dini yao.
Mara nyingine ilikuwa vigumu kumpata askofu (Abuna) kutoka Misri, na hivyo kukaa miaka bila askofu au uongozi imara. Ili kujikinga na Waislamu, Wakristo walikimbilia zaidi ndani na milimani.
Kwa kwenda ndani ilisaidia kuinjilisha wazawa wa ndani ya nchi, na kuingiza zaidi utamaduni wao katika maisha ya dini. Ndani ya nchi yalikuwemo makabila ya Wahabeshi (Abyssinia), na mchanganyiko ukazaa utamaduni mpya wa Kihabeshi wenye lugha ya Amharic, ambayo sasa ndiyo lugha rasmi ya taifa, lakini lugha ya ibada iliendelea kuwa ‘Gaez’, lugha ya zamani ya Axum.
Mwaka 1270 Mfalme Yekuno Amlak (1270 - 85) na baadaye Mfalme Amda Seyon (1312 - 1342), walifufua kwa nguvu ukoo wa ufalme wa Suleman ambao ulikuwa umepoteza madaraka kwa Wazagwe tangu mwaka 1137.
Mfalme Zara Yokob (1411-1468), alifikisha katika kilele ustawi wa ufalme wa Uhabeshi. Akitaka kuimarisha nguvu zake dhidi ya Waislamu Wasomalia waliosaidiwa na Waturuki, alituma ujumbe Roma kwa Papa kuomba msaada.
Kama Konstantino kwa Warumi, naye alilazimisha ustaarabu wa Kikristo kwa Wahabeshi wote hata kwa wapagani, yakiwemo maadili ya Kikristo kama ndoa ya mke mmoja. Mkuu wa Kanisa la Uhabeshi alikuwa ni ‘Abuna’ aliyetumwa kutoka Misri kama kiungo cha umoja na Kanisa mama.
Chini yake alikuwepo ‘Echege’ aliyemsaidia Abuna katika mambo ya utamaduni na desturi mahalia. Hata hivyo, kiongozi halisi wa Kanisa hilo alikuwa ni ‘Negus Negasti,’ ikimaanisha ‘Mfalme wa Wafalme’. Hii iliendelea  mpaka wakati wa Negus Haile Sellasie katika karne ya 20.
Malkia Helena akishikilia kama mlezi kwa ajili ya mtoto wake mdogo Negus Lebna Dengel, upinzani wa dola za Kiislamu za Kisomali uliongezeka kwa vita vikali, naye aliomba msaada kwa Wareno.  Mjumbe Mreno alipofika kukagua alikuta mfalme Lebna Dengel (1508-40) amekimbilia milimani, na nchi yake imeharibiwa na Wasomali wa Haral chini ya Ahmedi Ihn Ibrahim, wakisaidiwa na bunduki za Waturuki.
Mwaka 1543 Wareno walituma askari 400 wenye bunduki wakawashinda Wasomali, Ahmedi akauawa vitani. Hii ilinusuru ufalme wa Ethiopia na kufungua uhusiano na nchi za nje. Hapo kinaishia kipindi cha kwanza ambapo Ethiopia ilikuwa imefungwa bila uhusiano na nchi za nje za Kikristu.

MWANZA

Na Paul Mabuga

Biashara ya huduma ya usafiri wa pikipiki maarufu hapa Afrika Mashariki na hata katika miji na vijiji vyetu kama bodaboda, ni ajira ya uhai na kifo!
Ni kazi ya raha kwa kuwa inaiingiza  kipato, lakini pia ni ya karaha kutokana na wakati mwingine jamii inavyowatazama wanaoiendesha.
Pia, kazi hii imejaa mzuka wa kilele cha tijira kwa vijana wa fasheni, wanaopenda muziki ‘mnene’ na bomba la moshi linalobalaruka kwa sauti kubwa.
Kwao, hawa hii ni ruya ya kupaa hadi anga la saba na kujisikia katika ndoto ya kilele cha furaha, na hili ni zilizala katika ajira hii, ikisimuliwa kwa Tumaini Letu na waendesha bodaboda watatu kutoka katika Jiji la Mwanza.
Wa kwanza ni Emmanuel Kalima mwenye umri wa miaka 32 hivi sasa na mkazi wa Ilemela katika jiiji la Mwanza. Leo  analazimika kuendesha bajaji katika  kituo cha Sabasaba jijini humo baada ya kupata ulenavu uliotokana na kukatwa mguu wa kulia  kufuatia ajali aliyoipata miaka tisa iliyopita  wakati akiwa na kazi ya kuendesha bodaboda.
Kalima yupo katika kituo chake cha kazi akisubiri abiria, akiwa na Rozari yake shingoni, bila shaka ana matumaini kibao kwamba  maombi yake yatasikika, pengine leo kama jana atapata fedha ya kutosha kununua chakula kwa  familia yake ya  watoto wawili na mke, pia kumudu mahitaji ya shule kwa wanae wawili  wakubwa wanaosoma darasa la kwanza na la pili mtawalia. Lakini pia ana jukumu la kupeleka hesabu kwa mmiliki wa chombo hicho cha usafiri.
“Nipo naishi na mke wangu na watoto, na maisha ni ya furaha, hakuna unyanyapaa ndani ya familia yangu, na kuna mapenzi makubwa. Tunafurahia maisha kwa wakati huu,” anasema Kalima ambaye mara baada ya kumaliza elimu yake ya Kidato cha Nne  mwaka 2007, aliingia katika mapambano ya kutafuta naisha.
Wa pili ni Nhumba Mihaye ambaye pia aliacha kazi ya udereva wa bodada aliyokuwa akiifanya katika jiji la Mwanza na  kuamua kuedesha bajaji katika kituo cha Buswelu jijini humo.
Kwa sasa ana umri kama wa miaka 55 hivi na alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuanza biashara hiyo ya huduma katika jiji hilo. Kama ilivyo kwa Kalima, Mihaye naye anatakiwa kukamilisha hesabu ya ‘bosi’ na nyingine ya kujikimu kwa familia yake.
“Boda hapa ziliingia mwaka 2008, na mie wakati huo niliingia kufanya kazi hiyo. Ili kumudu maisha na mipango yangu, nilikuwa nakesha na  kipindi hicho kupata hesabu ya shilingi 70,000/- hadi 80,000/- kwa siku, ilikuwa ni kawaida.
 Ingawa abiria walikuwa wachache, lakini na sisi watoa huduma tulikuwa wachache, na  kazi ilikuwa nzuri kwa kweli kulinganisha na sasa  hivi ambapo ushindani ni mkubwa, na watu wamepigika, hawana fedha hadi wengine wanatembea kwa miguu” anasema Mihaye.
Anashukur u kwa kazi hiyo kwa kuwa ameweza kujenga nyumba, na ana watoto ambao angalau wamesoma hadi chuo kikuu. Lakini changamoto alizokutana nazo wakati huo ndizo zilizomfanya aachane na udereva wa  bodaboda, hasa baada ya kuona kuwa anaweza kupoteza maisha.
Wa tatu ni Bahati Yohane, mkazi wa Kiseke Jijini humo, na  yeye anashukuru kwa kazi ya bodaboda kwa kuwa  ilimfanya akapata mke ambaye anaye hadi sasa. Anasema wakati huo anaendesha boda boda, mambo yalikuwa mazuri na hata alimudu kila mahitaji katika familia yake.
“Kutokana na kuwa na fedha nyingi, nilijikuta naongoza matumizi ambapo kila baada ya kazi kabla ya kurudi nyumbani, nilikuwa napita baa na kupata  [nakunywa bia] kidogo.  Ilifikia mahali, mke wangu alikuwa anagomba sana kuendesha piki piki nikiwa nimelewa, lakini sikukoma, hadi nilipokomeshwa, na ndiyo maana unaniona hivi, nachechemea,” anasema Yohane ambaye ana umri wa miaka 46, ambaye kwa sasa amehamia kwenye bajaji.
Yohane anasema kuwa nyakati hizo wandesha bodaboda walikuwa wakituhumiwa  kuwapa ujauzito mabinti wanafunzi, na anadai kwamba kwa siku hizi hilo limepungua  kwa kuwa wasichana wengi wamejitambua na hawadanganyiki na vitu vidogo vidogo kama ilivyokuwa zamani. Na pia wazazi wametambua majukumu yao ya kuwatimizia mahitaji mabinti zao.
Anasema pia ni kweli wapo waendesha boda boda  ambao hata wanafikia hatua ya  kufukuzwa kwenye vituo kutokana na tuhuma za unyanyasaji wa kingono kwa abiria wao, wakiwemo watoto na wanawake. Anaongeza kuwa licha ya tabia hizi mbaya  kupungua, lakini zimekuwa zikijenga taswira mbaya ya kazi hiyo machoni pa jamii.
“Ila kisa cha kuacha kazi ya bodaboda, ilikuwa ni siku moja pale Kiseke, nilikuwa nimekunywa pombe na naendesha, nikajikuta naingia  barabara kubwa bila tahadhari. Ilitoka huko, bodaboda kwenye barabara kuu ikiwa kasi na kunichota kama  mwewe anavyonyakua ikifaranga. Kutoka hapo sikujitambua hadi nilipojikuta  hospitalini natibiwa na hicho ndicho kisa cha huu ulemavu nilionao,” anasimulia Yohane.
Kwa upande wake Mihaye anasema kuwa kuna mtindo wa vijana, kupanua mabomba ya moshi ya pikipiki zao ili zitoe mlio mkubwa wakiendesha, wengine wanaweka muziki sauti ya juu kujifirahisha na hata kuzing’oa sight mirror  [vioo vye pembeni; na kuweka urembo mwingine kama fasheni.
“Ila wengi wanaong’oa vioo vya pembeni, huwa ni wahalifu, nia yao huwa ni kwamba wakimkwapua abiria wa pikipiki ya mbele yao au mtembea kwa miguu, wakimbie bila kikwazo cha kuona kuna mtu anawafuata, wanaamini kwamba, wakiwa wanaona wanafuatwa wataghafirika na kupunguza mwendo,” anasema Mihaye na kuongeza,
“Kuna siku nilikuwa na abiria mwanamke napita barabara ya hospitali ya mkoa  wa Mwanza, Sekou Toure. Vijana wanamna walikuwa nyuma yangu na pikipiki yao, wakakwapua mkoba wa abiria huyo. Niliamua kumshusha na kuanza kuwafukuza.
Walikuwa  wakikata mitaa ninao, huku ninapiga kelele  za mwizi, na walipoona ninawakaribia wakautupa chini mkoba, nikauchukua na kumrejeshea abiria kule  nilikomuacha baada ya kuachana na wezi hao.”
Na kuhusu kisa cha kuachana na udereva bodaboda, anasema kuwa, siku moja saa nane za usiku, alimpakia abiria mwanamke na hakujua kuwa yule alikuwa ni sehemu  ya majambazi, “ilikuwa ni ile njia ya kutoka Ilemela Mahakamani kuja njia  ya lami, tulipokaribia sehemu yenye miti isiyo na watu wengi, yule abiria alianza kujichezesha nyuma ili  nipunguze mwendo ama kuanguka, na kwa mbele nikaona kundi la vijana wakiwa na nondo na mapanga.
“Nilipoona hivyo, nikaendesha pikipiki kuwafuata waliko ili niwagonge, wakatawanyika na kujiweka mbali  walipoona hivyo, nikashuka na kumg’amg’amia yule mwanamke kwenye pikipiki,huku nikimpiga na kumgeuza kinga endapo wangenishambulia;
“Waligundua manbo ni magumu, wakakimbia na nikabaki na yule abiria feki, nikamwambia alete hela yangu, akabisha, nikamsachi na kumkuta ana shilingi 15,000/= nikamnyang’anya, nikamwambia ondoka naye akatimka kama hana akili sawa sawa.  Na huo ndio mwisho wangu na bodaboda,” anasimulia Mihaye.
Kalima yeye anasema kwamba kwa siku hizi mambo mengi yamebadilika, uhasama wa wenye magari au madereva wa daladala na waendesha bodaboda kitu ambacho kilikuwa chanzo cha ajali nyingi, umepungua baada ya kila upande kuuheshimu mwingine.  Pia uelewa wa sheria miongoni mwa madereva wa bodboda kumeondoa pia ile tabia ya wao kufukuzana na askari wa usalama barabarani.
“Nimeshuhudia vifo vya madereva boda boda sita ama saba hivi kutokana na ajali zilizo katika mazingira haya tangu nianze kuendesha bodaboda mwaka 2010,” anasimulia Kalima ambaye kabla ya kujinunulia pikipiki yake alifanya kazi ya ajira Halmashauri ya Jiji la Mwanza kama mhudumu, na baadaye hotelini, na hivyo kujipatia fedha kwa ajili hiyo.
“Hata hivyo siku moja mwaka 2015,  nikiwa naendesha pikipiki kuelekea mjini kutoka Airport na abiria wangu akiwa dereva bodaboda mwenzagu, na wakati trafiki wameyazuia magari ya  upande mmoja wa barabara, [wakati huo barabara ya Aiport haijawa na njia mbili] ili kuruhusu basi la timu ya Mbao iliyokuwa ikifanya mazoeazi katika viwanja vya DIT hapa Mwanza, kuingia barabara kuu ili waelekee upande wa kulia kwetu,  lilikuja gari moja likiwa na mwendo mkali.
Gari hilo ni kama lilikataa amri ya trafiki na kuingia upande wetu ulioruhusiwa,  na hivyo kukutana uso kwa uso na sisi  na kutugonga. Ilikuwa ajali mbaya sana. Tulipakiwa katika magari mawili tofauti, mwenzangu akapelekwa Sekou Toure na mimi nikapelekwa Bugando [hospuali] na huko, baada ya kulazwa kama mwezi mzima wakanikata mguu,” anasimulia Kalima, na kuongeza kuwa, “ Baada ya kukatwa mguu, nilikaa siku tatu bila fahamu, baadaye nilijitambua na kujiona mwenye afya na nikawa nakula chakula kama kawaida.
Nilishtuka  baada ya kuona kama kuna wepesi usio wa kawaida kwenye mguu wa kulia, na ndipo nilpotambua kuwa umekatwa. Nilisikitika sana, wakanipa moyo kuwa, utaota na kurejea hali ya kawaida, na nikayaamini haya maneno.”
Anasema aliielewa hali hiyo baadaye na kuendelea kuisha nayo.  Ila kwa sasa anawaomba wasamaria wema kama wanaweza kusaidia  fedha za kupata mguu bandia ili maisha yake yaendee kawaaida. Anapatikana kwa namba  0786858676, mwenye kuwiwa kumsaidia anaweza kuwasiliana nae. Kwa naelezo ya awali anadai mguu bandia  unaweza kugharimu kati ya shilingi milioni mbili hadi tatu.

Na Joseph Mihangwa

LIPOISHIAI
...Ni utawala wa Chama dola na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Ingawa tumeingia mfumo wa Vyama vingi, Katiba inanuka harufu ya Chama kimoja kiasi cha watu wengine kukiita Chama kilichoshinda “Chama dola”, wakati ukweli dola si ya Chama, bali ni ya wananchi!.

ENDELEA...
Mhimili wa Chama na Ujamaa kati ya mitatu umekwishavunjika; Sera za Ujamaa na kujitegemea zimevunjwa na Azimio la Zanzibar mwaka 1992; nao mfumo wa Chama kimoja umeuawa na mfumo wa Vyama vingi vya siasa tangu mwaka 1992. Mfumo huu na ule wa uchumi huria, havikuwa katika mawazo ya watunga Katiba ya 1977. Ndiyo maana, Katiba ya sasa inakinzana kwa sehemu kubwa na mengi yanayotokea nchini.
Tunachosema hapa ni kwamba madaraka makubwa ya Rais asiyeambilika, yalidumu na kuweza kufanya kazi tu kwa msaada wa mafiga mawili yaliyovunjika – [Ujamaa na Chama kimoja], na kwamba, maadam sasa msaada huo haupo tena, madaraka makubwa ya Rais yataendelea kuelea na kupwaya kwa vigezo vyovyote vya utawala wa Sheria, demokrasia na utawala bora. Na pale Rais atajaribu kutenda kwa ubunifu wake binafsi kinyume na haya, hataepuka kuitwa “dikteta”.
Tunaambiwa, nchi yetu inafuata mfumo wa Utawala wa “Westminster”, unaozingatia Mgawanyo wa Madaraka.  Chini ya mfumo huo, muhimili mmoja wa Serikali unakatazwa kuingilia kazi za muhimili mwingine ili kila muhimili uchunge mwenendo wa muhimili mwingine.  Dhana hii sasa ipo kwa jina tu kama tutakavyoona hivi punde.
Marekebisho ya hapa na pale yaliyofanyika baadaye kwenye Katiba hayakugusa madaraka ya Rais, lakini badala yake, kadri sekta ya umma ilivyozidi kupanuka na ukuu wa mfumo wa Chama kimoja kujiimarisha, ndivyo jinsi madaraka ya Rais yalivyozidi kuwa makubwa. 
Aliweza kutumia nyundo ya Chama wakati huo huo kama Rais wa Nchi, na aliweza kutumia pia ngao ya Rais kulinda Chama wakati huo huo kama Mwenyekiti wa Chama. Rais wa Nchi na Mwenyekiti wa Chama Taifa kilikuwa na hadi leo ni kitu kimoja. Na ndiyo sababu ya Chama madarakani kuitwa “chama dola”! Kwa sababu hii, madaraka ya Rais yalipanuka kinyemela kuanzia na Katiba ya Nchi, hadi kwenye Katiba ya Chama cha Siasa tawala. Kwa sababu hii, Rais asiyeambilika [The Imperial Presidency], anachukuliwa kama moja ya nguzo au misingi mikuu mitatu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, inayoendelea kutumika hadi leo.
Uhalali wa madaraka makubwa ya Rais kwa mtazamo wa Watawala wa enzi hizo, ulikuwa ni kuharakisha maendeleo kwa njia ya “udikteta” wa Mkuu wa Nchi, ili asiulizwe ulizwe.  Mtazamo huu unadumu hadi leo.
Na katika kutekeleza hilo, Katiba ilitungwa kwa lengo la kuweka madarakani mtawala mwenye nguvu za imla, kwanza kuonesha kwamba Watanganyika sasa walikuwa huru kuweza kuendesha mambo yao wenyewe.
Pili, ilikuwa ni kuwezesha Serikali kuingilia kikamilifu [na bila ya kuhojiwa] katika maisha ya kijamii na kiuchumi ya wananchi, ili kuharakisha maendeleo kwa nguvu na imla ya kiutawala kwa “kushikisha adabu” waliohoji mwenendo wa nchi na wa watawala katika “kusukuma gurudumu la maendeleo.”
Maandalizi ya uchaguzi wa kwanza wa Rais asiyeambilika yalianza Juni 18 mwaka 1962 kwa kuandikisha wapiga kura 1,800,000 katika majimbo 50 ya uchaguzi. Wagombea walikuwa wawili – Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Chama cha TANU, na Bwana Zuberi Mtemvu, Rais wa Chama cha African National Congress – ANC. Uchaguzi ulifanyika Novemba 1, 1962 ambapo Mtemvu alishindwa vibaya kwa kupata kura 21,276, na Mwalimu Nyerere alipata kura 1,127,978.
Kuanzia hapo, Katiba ya nchi imekuwa ikiandikwa au kurekebishwa kukiwa na uwepo wa Rais, Mwalimu Nyerere vichwani mwa Waandishi wa Katiba. Hali haijabadilika.  Katiba yetu [ibara ya 63] inamfanya Rais kuwa sehemu ya Bunge la nchi kama njia ya kudhibiti demokrasia, kinyume na dhana ya Mgawanyo wa madaraka. Na ingawa mamlaka yote ya kutunga Sheria yamo mikononi mwa Bunge [ibara 64], lakini muswada wa Sheria hauwezi kuwa Sheria mpaka utiwe sahihi na Rais. Hakuna muda maalum aliopewa Rais kwa ajili hiyo; anaweza kukalia muswada kwa muda wowote atakavyo, kana kwamba yuko juu ya Wananchi kupitia Bunge.
Endapo atakataa kutia sahihi muswada asioutaka, na Bunge likashikilia msimamo wake juu ya muswada huo, Rais ana uwezo wa kulivunja Bunge na kuitisha uchaguzi mpya. Haya ni madaraka makubwa mno kwa Rais dhidi ya wawakilishi wa wananchi. Maana yake ni kwamba ingawa Bunge laweza kupitisha Muswada wa Sheria, ukweli Rais ndiye anayetunga Sheria kwa sababu ana hiari ya kukataa au kukubali Muswada wa Bunge na asiulizwe.
Rais anapogeuka kuwa Mtunga Sheria, Bunge lifanye kazi gani? Ili kulinda hadhi na ukuu wa Bunge linalowasilisha wananchi, busara inaelekeza Bunge lidhibiti bajeti yake, Tume yake ya Utumishi ina uwezo wa kupitisha miswada kuwa Sheria inapotiwa sahihi na Spika.
Kama ilivyokuwa kwenye Katiba ya Jamhuri [1962] kwa Rais kuongoza nchi atakavyo, na kuwa halazimiki kupokea ushauri wa mtu yeyote, Katiba ya sasa [ibara 37] bado inampa ridhaa hiyo, na hawezi kuhojiwa au kushtakiwa kwa vitendo vyovyote alivyofanya akiwa Rais na baada ya hapo [Ibara 46]. Pengine ni kwa sababu hii zama zetu, kumekuwa na vitendo visivyoendana na maadili ya taifa kwenye Ikulu bila ya woga, vilivyomfanya Baba wa Taifa apige kelele kwa kusema “Ikulu ni mahali patakatifu, panatakiwa paheshimiwe”, na akaonya pasigeuzwe pango la wafanyabiashara na walanguzi.
Kama lengo la kuwepo mihimili mitatu [Utawala, Mahakama na Bunge], ni pamoja na kuimarisha demokrasia, demokrasia itatoka wapi mhimili wa utawala unapodhibiti mihimili mingine?. Inapokuwa hivyo, kwa nini tuendelee kudai tunafuata mfumo wa demokrasia wa kibunge [Parliamentary Democracy], wakati vitendo vinaonesha kinyume chake?
Rais ndiye anayeteua Jaji Mkuu na Majaji [wanaosimamia mhimili wa Mahakama], Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Viongozi wengine. Kitendo cha kuteua chenyewe pekee kinamaanisha kwamba wateule hao wanawajibika kwake. Na kwa sababu hiyo mhimili wa kulinda haki [Mahakama], unawajibika kwa Rais pia. Hii inakwenda kinyume na dhana nzima ya mgawanyo wa madaraka na ya utawala wa Sheria kwa ujumla, kwa Rais kudhibiti Bunge na Mahakama, pamoja na Watendaji wake.
Kwa kusema haya, hatumaanishi kwamba kwa watawala kuvuka mipaka ya Kikatiba mara kwa mara hakuzai matunda siku zote, bali kwamba panatakiwa tamko thabiti lenye kueleweka juu ya aina ya demokrasia tunayopaswa kufuata kuweza kujipima na kuweza kupimwa pia kimataifa. Uhuru na demokrasia si lelemama, bali “UHURU”, kama alivyosema Baba wa Taifa, “ni KAZI”.
Tafsiri ya neno “demokrasia” ni pana kwa kuzingatia mahali na mazingira ya nchi. Lakini, kama Katiba ya Nchi ni hati yenye “utakaso”, na pia dira na ramani ya madaraka ya kuzingatiwa na kila mtu, basi, mfumo unaosimikwa na Katiba hiyo unapaswa kufahamika, kuzingatiwa na kuheshimiwa na wote; kinyume chake Katiba na demokrasia inageuka kuwa kejeli kwa wananchi wanaoitunga wakitarajia kwa matarajio kuona inafanya kazi. Ilivyo sasa, nchi yetu inafuata mfumo gani wa demokrasia: demokrasia ya [ukuu wa] kibunge, demokrasia ya kinasaba au ukuu wa kivikundi kwa misingi ya vyama vya siasa?
Tuseme nini zama hizi za siasa na uchumi huria na kwa Serikali kuachia nguvu za “soko” kusimamia sera na uchumi wa nchi na hivyo maisha ya watu, inapotokea mhimili wa Bunge na Utawala kuungana kuwa kitu kimoja?. Uhuru wa Mahakama utatoka wapi, kwa mfano, kwa kulazimisha chungu cha mstakabali wa nchi na demokrasia kukaa juu ya mafiga mawili badala ya matatu?
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
0713-526972

MWANZA

Na Paul Mabuga

Zawadi ya  tuliyopewa na Mungu ya huduma,  uhai na maisha ya mpendwa wetu Edward Lowassa, tuliyemhifadhi katika nyumba yake ya milele hivi majuzi huko Monduli, Mkoani Arusha ina mengi ya kutufundisha, lakini zaidi ni kwamba kila binadamu anazaliwa na haki ya kusifiwa, isipokuwa huwa inaporwa na ndiyo maana inahitaji kulindwa na kutetewa.
Kwamba, binadamu hatapata sifa kwenye familia yake au watu wa karibu nae basi ataitafuta nje yao. Wakati mwingine matokeo yanaweza kujenga uhitaji wa kuilinda haki hiyo huku wengine wakiibomoa katika ushindani ambao unajaa vitimbwi. Lakini wakati mwingine, sifa hutolewa bila kufurahisha wengine.
Kuna picha jongefu fupi mtandaoni ambapo mwongeaji hamasa, anayejitambulisha kwa jina la Michael Maundi, anajizungumzia yeye kama mfano ambapo anasema, tangu wakati anasomasoma shule ya msingi nafasi yake kwenye mitihani  ilikuwa ya 160 na 180, na hata alipofaulu kwenda kidato cha kwanza shule ye sekondari Kibasila mama yake alimuuliza, “huko darasani kwenu hakuna Michael Maundi Mwingine?” Akimaanisha mama yake alikuwa haamini kama amefaulu.
“Watu wote na hasa watoto wadogo walio nyumbani tunapenda sana sifa, tusipoipata nyumbani ama shuleni tunaitafuta mitaani! Mtaa unasifia, mtaa ukipakata kete [dawa za kulevya], mtaa unakuambua mwanangu umetisha… hata .. uki[anaonyesha ishara ya kuvuta bangi] mtaaa unakuambia mwanangu mwanangu, yaani wewe bonge la Mwambaaa!” anasema akionyesha umuhimu wa kuwasifia  watoto kabla ya kupata zile zisizo na maana.
“Mtoto anafanya kitu kikubwa nyumbani  wewe hata hushangilii, hustuki,[ inatakiwa] hata kama unakijua unashangaa, heee umejuaji mwanangu! Mtoto anapata moyo wa kutafuta vitu vingine kujua ili kuhadithia, … siyo anakuja kukuelezea kuhusu mto Kirumi uko hivi na hivi, halafu wewe unamvwambia, kwa hiyo wewe ndiyo umejua leo!” anaeleza Maundi katika kadamnasi inayomtazama katika picha hiyo fupi jongefu.
Kinyume chake anasema mwalimu wake wa darasa la saba wakatti anapata hesabu alama saba kwa hamsini kwenye mtihani wa kwanza,alimwambia Maundi una akili sana ili huitumii vuzuri. Wa pili alipopata 11 ya hamsini, akamyanyua juu na kumwambia, wewe ni nomaa, wewe ni mkemia mkuu, na mtihani uliofuata alipata alama zote.
“Mtoto mdogo atakuja kukupa kile [anachokiona] unachokiamini! Ukimuaminisha anaweza [ukimsifia unampa deni kubwa sana, … lakini kimuambua mjinga  mpumbavu mende paka .. atakuwa akijisemea hata mama anajua kuwa mimi ni paka!” anasema Maundi na kuongeza kuwa watu wengi duniani wamefanya makubwa kutokana na kulelewa katika miingi hiyp ya motisha ya kusifiwa.
Pia kuna majadiliano katika mtandao wa facebook  kupitia uzi mmoja ulioanzishwa na chombo kimoja cha habari nchini Kenya, ambapo inaonekana hoja ni Tanzania angalau kucheza Afcon 2023 iliyomalizika hivi karibuni, ambapo mmoja wa wachangiaji raia wa nchi hiyo ya awali anaandika katika hali ambayo inaonyesha pengine kutofurahia sifa za nchi yake ya jirani.
“Jirani hana dollar, jirani hana umeme, jirani hajui kizungu, jirani hakushinda hata mechi moja Afcon, jirani ana shida kweli kweli,” analeza Ogeto Nyamwange katika mtandani huo. Wapo pia engi waolichangia katika mtazamo huo. Mtanzania Caroline P Mwaipungu  anajibu, “Majirani mnajikutaga wazungu etu? Kama wa ulaya vile wakati hatutofautiani shida… eti kuzungu nini?? Mko na umbea mwingi loo!
Ingawa ni utani wa kawaida ambao hata umekuwepo kwa muda sasa kati ya raia wa nchi hizi lakini umekuwa hauna madhara. Zaidi utani huu ni kielelezo cha namna ambavyo binadamu anahitaji sifa, na anapohisi inachukuliwa anaona kuna haja ya kuilinda.
Usishangae binti akiingia gharama ya usafiri kurudi nyumbani kubadili mavazi baada ya kuambiwa aliyoyavaa hayajampendeza. Tunaponunua nguo tunalipia kupendeza siyo mavazi. Hii ni hoja ya kale kina binadamu alivyo.
Tukirejea katika enzi za uhai wake Lowassa  licha kusifiwa ambako kwa hakika kulijengwa na kupendwa kutokana na wasifu wake, na hata kuwa kipenzi cha watu, lakinini pia ni ukweli kuwa katika kipindi chake cha kazi na maisha aliukutana na bête noire [tanka bete nwaa], ikiwa na maana ya hali ya  kuchukiwa na sehemu fulani ya jamii..
Katika pande zote alizokuwa katika kazi zake, alikuwa kipenzi  na kupewa  sifa kem kem kwa upande mmoja huku kwa upande mwingine akipata bête noire.  Upande mmoja wa binadamu hao hao wakimpa sifa na kumtetea kwa nguvu zote wakati wa pili ukizipopoa sifa hizo ili kumpa bête noire kwa kila gharama yoyote.
Kitu kimoja cha msingi ni kwamba wakati kunyang’anywa kwa haki ya asili ya kusifiwa kunaweza kusababisha athari za kiafya katika maisha ya binadamu, lakini mara nyingi tumekuwa hatujali na  hatutoki mbele na kuwanusuru.  Watu walioporwa sifa wanazostahili kwa haki tumekuwa  tunasubiri wakati wakiaga dunia ili kuwasifia.
Na adui mkubwa wa sifa kwa mwanadamu ni ubinafsi ambao kila mmoja wetu anao. Yaani tunajijali zaidi kwanza sisi, na tunapoona ubinafsi wetu unatishia sifa zetu, tunapambana hata kama katika kufanya hivyo tunawanyang’anya wengine stahiki zao. Siyo lazima kila sifa imfurahishe mwingine, lakini inapaswa kuwa haki ya mmiliki.

Na Dk. Deoscorous B. Ndoloi

Mpendwa msomaji, karibu tena katika makala yetu juu ya mikabala ya ushawishi, wakati wa kuzungumza katika hadhara. Tayari tumekwishaona aina saba za mikabala, kama ifuatavyo: kutishia (kutia hofu), kukaripia, kususa, kutoa mchapo au hadithi fupi (anecdote), kuuliza maswali balagha (rhetorical questions), kutangaza ole, na kutoa mlinganisho. Kabla hatujaendelea, ni vema kutambua kwamba kuorodhesha hii mikabala (kama vile inajitegemea) kunatusaidia kuielewa zaidi kuliko kuizungumzia kwa pamoja. Lakini ukweli ni kwamba katika wasilisho moja unaweza kutumia mikabala zaidi ya mmoja kulingana na lengo la wasilisho, mazingira, aina ya wasikilizaji, na mabadiliko unayotarajia kwa hadhira husika. Katika makala hii, tumalizie mada hii juu ya mikabala ya ushawishi.
Mkabaka wa aina ya nane wa ushawishi ni kufanya rejeo katika ushahidi unatokana na tafiti za kisayansi. Binadamu tumeumbwa na ‘katatizo’ kadogo ka kutilia mashaka hasa vitu ambavyo aidha hatujavizoea ama hatujawahi kuviona. Hili linasaidia wakati mwingine kwa vile huweza kuibua hali ya udadisi na kutaka kupata taarifa sahihi. Kwa mfano, inaweza kuwa vigumu katika wasilisho kuhusu afya, kuwashawishi wavuta sigara waache kwa vile kuna madhara makubwa kiafya. Kwa vile kuvuta sigara ni uraibu na siyo rahisi kuacha, wapo wasikilizaji wengine watasema, “Mbona yuko mzee mmoja anavuta sana sigara na ana umri wa miaka 80, madhara yako wapi”? Ikiwa mwasilishaji anajua yapo mawazo kama haya miongoni mwa wasikilizaji, anaweza kutoa ushawishi kwa kutumia takwimu za vifo vinavyotokana na uvutaji wa sigara. Kwa mfano anaweza kusema, “Kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani, vifo vinavyotokana na uvutaji wa sigara kwa mwaka ni watu milioni nane (WHO, Januari 2022). Hawa ni kama watu wote wa Mkoa wa Dar es Salaam, wanafariki kila mwaka”. Takwimu hizi zinatisha, wapo wanaoweza kushawishika kuacha kabisa sigara. Siyo maneno ya mwasilishaji, bali ya utafiti wa kisayansi. Dhamira ya msikilizaji inaweza kumsuta ikamwambia, “Kama na hilo huliamini, endelea kuvuta”.
Mkabala wa aina ya tisa wa ushawishi ni kupeana kazi ya nyumbani (homework) baada ya wasilisho. Ushawishi huu ni tofauti kidogo kwa sababu wasikilizaji wako watashawishika baada ya kuondoka katika mhadhara. Kwa mfano unatoa wasilisho juu ya afya ya akili (mental health), na kwamba kukosa amani katika familia mara nyingi kunapandisha mhemko, mfadhaiko, msongo, shinikizo, na kupelekea kushindwa kujenga familia zenye ustawi wa mwili, akili, mali, elimu, mahusiano, afya, nk. Unaweza kuwaambia wasikilizaji wako, “Ukitoka hapa, angalia watoto mtaani wanapiganapigana kila wakati; je nyumbani kwao unakujua? Wazazi wao wakoje? Ukitoka hapa kachunguze mtu yeyote unayefikiri ana makelele sana, wakati mwingine, yasiyo na sababu. Watu wa familia yake unawajua? Wakoje? Baada ya semina hii, nataka ukachunguze watu ambao unafikiri wanahamakihamaki sana, na hawana utulivu wa kufikiri na kupambanua mambo. Angalia uhusiano wake na ndugu au marafiki zake. Utakachogundua, njoo utueleze. Kaangalie watoto ambao hawataki kabisa kucheza na wenzao, kitu ambacho kwa mtoto siyo kawaida. Chunguza wazazi wake. Ndiyo utakuja kukubalian na mimi kwamba afya ya akili, kwa kiasi kikubwa, inahusiana na kiwango cha amani anachokuwa nacho mtu”. Hapa unawapa ushawishi rejea (protracted persuasion), na watashawishika baadaye, na kila mtu kwa muda wake.

Mkabala wa aina ya kumi wa ushawishi ni kuonesha thamani ya wanaokusikiliza. Watu wote wanapenda sifa (tabia ya binadamu). Hapo awali, katika makala ya tano ya mwezi Septemba 2023, tuliona kwamba binadamu hapendi sana kuoneshwa kwamba yeye ana mapungufu, hasa pale anapoambiwa kwa namna ya kudharauliwa. Niliwahi kusema kwamba binadamu anataka kuambiwa kwamba, “Kama yai, yeye anaweza kuwa na ufa kidogo, lakini ubora wake kama yai uko palepale, likikaangwa linaliwa bila shida”. Ninachotaka kusema ni kwamba ushawishi unaweza kutokana na wewe mwasilishaji kuwahakikishia wasikilizaji kwamba wana thamani katika hilo unalolisema. Wahakikishie kwamba wewe ni mchokoza mada tu, na ni tegemeo lako kwamba una mengi ya kujifunza toka kwao. Wakitoa mchango wa mawazo, sema, “Asante, kwa mawazo mazuri, na mimi nimepata faida hapo”. Kuionesha hadhira kwamba na wewe unajifunza, siyo tu dalili ya unyenyekevu, unawashawishi hata kukubali unayosema.
Mkabala wa aina ya kumi na moja wa ushawishi ni kutumia vema mawasiliano silonge (non-verbal communication), au kuongea kwa matendo. Ili uweze kushawishi watu – zungumza kwa mdomo, lakini ongea na mwili mzima. Huwezi kushawishi watu ukiwa umeweka mikono mfukoni. Huwezi kushawishi watu ukiwa umekaa. Huwezi kushawishi watu ukiwa umesimama sehemu moja muda wote. Huwezi kushawishi watu ukiwa umenuna. Huwezi kushawishi watu ukiwa huwatazami. Kila sehemu ya mwili wako ichangie katika kutoa taarifa na maarifa. Wale wachekeshaji (comedians) maarufu wanavunja watu mbavu kwa yale wanayosema, lakini kwa kiasi kikubwa wanavyoyasema na kwa matendo yao.

Wiki ijayo tutaona kanuni za kuandaa na kutumia zana (presentation aids) wakati wa kuzungumza katika hadhara, na pengine tutakuwa tumefikia mwisho wa hii mada ya kuzungumza katika hadhara, ili tuanze mada mpya.  Tumsifu Yesu Kristu!
Itaendelea wiki ijayo.

Na Pd. Raymond Sangu, OCD

SWALI LIMEULIZWA: Je, Ni sahihi kwa Wakristo kuadhimisha/kusherehekea VALENTINE’S DAY, yaani Siku ya Wapendanao? – Evelyne, wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – TANZANIA, anauliza.
MAJIBU, mpendwa Evelyne, kulingana na swali lako, nitakupa maelezo kuhusu mambo manne kama ifuatavyo: Jina VALENTINE, kwa nini ni tarehe 14 FEBRUARI, rangi NYEKUNDU na mwisho MAANA YA SIKU HII KWA MKRISTO.
HISTORIA YA JINA VALENTINE Valentine alikuwa Padre Mkatoliki wakati mtawala wa Kirumi aliyeitwa Klaudio alipokuwa akilitesa Kanisa. Padre huyo alizaliwa mwaka 226 BK huko Terni nchini Italia, na kufariki Februari 14 mwaka 269 BK huko Roma, Italia. Valentine ndiye mtakatifu msimamizi wa wapendanao.
KWA NINI FEBRUARI 14 INAITWA SIKU YA VALENTINE? Mtawala wa Kirumi Klaudio alikuwa ametoa amri/agizo lililokataza vijana wasifunge ndoa. Hii ilitokana na dhana kwamba askari ambao hawajaoa, walipigana vizuri zaidi kuliko askari waliooa.
Hii ni kwa sababu askari waliooa wangeweza kuogopa nini kingetokea kwa wake zao na familia zao ikiwa askari hao wangekufa. Valentine aliwafungisha ndoa vijana kwa siri, kinyume na amri/agizo/katazo la Mfalme Klaudio. Hatimaye alikamatwa, akateswa na kufungwa kwa kukiuka amri ya Mfalme.
Mnamo Februari 14 mwaka 269 BK, Valentine alihukumiwa kifo kwa hatua tatu, kwanza kipigo, pili kupigwa mawe, na hatimaye kukatwa kichwa. Yote haya yalisababishwa na msimamo wake kuhusu ndoa ya Kikristo.
KWA NINI RANGI NYEKUNDU? Kadri ya vyanzo mbalimbali, rangi nyekundu inaashiria sadaka, hisia na upendo wa kina, kwa wale wanaopendana, au walio katika uhusiano, au wale wanaotarajia hilo. Ni rangi inayohusishwa na kuamsha hisia au upendo. Ndiyo maana rangi hii hutumika katika ya Siku ya Wapendanao.
VALENTINE YA KWELI: Februari 14 ni siku ya kusherehekea upendo. Lakini sio tu ule wenye uelekeo wa uhusiano wa kimapenzi. Ikiwa huna valentine katika maana inayoshabikiwa na watu wengi, wala usifadhaike. Kuna mazuri mengi yanayoweza kutokana na kuwa ‘single’.
Kuwa ‘single’ hukupa fursa ya kuwa huru, kujitambua wewe ni nani, unapenda nini, nini hupendi, na ni kitu gani kinachofaa zaidi kwako. Usiruhusu tarehe 14 Februari kuwa ukumbusho wa jinsi ulivyoshindwa kupata upendo. Ikiwa uko kwenye uhusiano, Februari 14 siyo siku ya kuthibitisha upendo, badala yake ni siku ya kuendelea kuondoa matabaka na makandokando yanayozuia upendo kushamiri katika uhusiano wako.
HITIMISHO: Februari 14 ni siku ya kusherehekea upendo. Kujipenda mwenyewe, kupenda maisha yako, kupenda mapambano ya maisha, kumpenda kila mtu maishani, aliyeko katika maisha yako, na vile vile kumpenda hata yule ambaye yuko nje ya maisha yako. Ikiwa hujaoa au kuolewa, tarehe 14 Februari ni siku nzuri ya kusherehekea uhuru wako na kukumbatia ujasiri wa kuwa radhi ya kuwapokea watu wote, kupenda zaidi na kujifunza zaidi kuhusu upendo.
Baada ya maelezo marefu, nihitimishe kwa kusema kwamba hata Wakristo pia wanapaswa kuadhimisha na kusherehekea SIKUKUU YA WAPENDANAO, al maarufu kama VALENTINE’S DAY, ambayo mwaka huu imeangukia katika siku nzuri sana ya TOBA, yaani JUMATANO YA MAJIVU! Happy Valentine’s Day in Advance, Kheri ya Siku ya Wapendanao, lakini zaidi sana KHERI YA SIKU YA JUMATANO YA MAJIVU – Februari 14 mwaka 2024! -----------------------
“Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. Upendo haufurahii matendo mabaya, bali hufurahi pamoja na kweli. Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.” – 1 Wakorintho, 13:4-7 ----------------------
Rev. Fr. Raymond Sangu, OCD, Shirika la Wakarmeli Tanzania ambaye yuko Roma, Italia: Maoni WhatsApp +255 755 223 657

Na Askofu Method Kilaini

Katika safu hii wiki iliyopita, tuliendelea kuwaletea jinsi himaya za kipagani zilivyokuwa kigingi kwa wakristo na pingamizi toka kwa watawala wa enzi hizo. Leo tunaanza sehemu nyingine ya Historia ya Kanisa Afrika. Sasa Endelea…

UTANGULIZI
Afrika iliinjilishwa katika vipindi vitatu katika historia yake. Kipindi cha kwanza ni kuanzia siku ya Pentekoste hadi karne ya nane. Katika kipindi hiki nchi ya kwanza kuinjilishwa  ilikuwa ni Misri kufuatana na uhusiano wake wa karibu na Palestina. Kutoka Misri dini ilienea hadi Nubia ambayo sasa ni Sudan na Ethiopia au Abyssinia. Sehemu ya  pili kuinjilishwa ilikuwa Afrika ya Kaskazini ambayo ilikuwa inatawaliwa na Warumi.
Isipokuwa Ethiopia katika sehemu nyingine Ukristo ulitoweka au kudhoofika shauri ya Uislamu. Kipindi hiki kwa sehemu kubwa kilisimuliwa katika historia ya jumla ya kanisa.
Hapa tutaongelea kwa ufipi ili kuiunganisha na historia nyingine ya Afrika. Katika historia ya jumla tuliongelea sana juu ya dhuluma na mateso dhidi ya Wakristo kati ya mwaka 64 BK hadi mwaka 313 BK. Katika dhuluma hiyo Wakristo Waafrika wengi walikufa kwa ajili ya imani yao.
Vile vile katika historia jumla tuliongelea juu ya uzushi na mitaguso mbali mbali iliyojaribu kusuluhisha na kuleta umoja na amani ndani ya kanisa.
Kipindi cha pili kilikuwa katika karne ya 15 hadi 17. Wareno katika uvumbuzi wao na ukoloni waliambatana na wamisionari kuanzia Afrika ya Magharibi, ya kati, ya kusini na ya mashariki. Uinjilishaji wa kipindi hiki haukudumu isipokuwa katika sehemu chache sana kwa sababu ulitegemea sana nguvu za Wareno wakoloni. Ukoloni uliposhindwa na dini ilitoweka.
Kipindi cha tatu ni kuanzia karene ya 18 hadi sasa. Wamisionari Wakatoliki na Waprotestanti walijitosa bila kungojea wakoloni na kuwainjilisha Waafrika moja kwa moja hasa chini ya Sahara kwa mafanikio makubwa. Hadi leo Ukristo Afrika unakua kwa kasi kuliko bara lingine lo lote lile. Kipindi hiki ndicho cha uinjilishaji halisi wa Afrika.
KANISA LA MISRI
Misri ilikuwa na usataarabu miaka mingi sana kabla ya Kristo. Watu wemgi waliishi kwenye mwambao wa bahari ya Mediteranea na ukingo wa mto Nile. Nje ya hapo lilikuwa ni jangwa bila watu. Miaka 300 kabla ya Kristo Misri ilitekwa na Aleksanda Mkuu, mfalme huyu  Mgriki alijenga mji wa Aleksandria na kuingiza utamaduni wa Kigriki. Miaka 30 KK Misri ilitekwa na Warumi kisiasa lakini kiutamaduni ilibakia ya Kigriki kama sehemu nyingine za mashariki ya kati. Aleksandria ulikuwa mji wa pili kwa ukubwa na umaarufu katika dola ya Kirumi baada ya Roma. Hata hivyo huko Misri utamaduni wa Kigriki ulikuwa kwa ajili ya wasomi wachache, wengi hasa mashambani na nje ya miji walikuwa Wakopti, wengi wao wakiwa maskini.
Kwa zaidi ya miaka 2000 KK, Misri ilikuwa na uhusiano wa karibu na Palestina na Syria. Tunasoma katika biblia hata Ibrahimu na Yakobo walikwenda Misri. Wakati wa Kristo ikiwa chini ya Waruni ilikuwa na zaidi ya Wayahudi milioni moja na mji wa Aleksandira ulikuwa na Wayahudi zaidi ya 200,000 au 2/5 ya wakazi wa mji huo.
UINJILISHAJI WA MISRI
Katika Agano Jipya, Misri inatajwa mara kadhaa, kwa mfano Maria na Yoseph walimkimbiza mtoto Yesu Misri asiuawe na Herode, (Mt. 2:13); Simoni wa Kirene alitoka Misri (sehemu hiyo siku hizi iko Libya), (Lk. 23:26); na Apolo alikuwa mzaliwa wa Aleksandria (Mat. 18:24). Katika mapokeo ya mitume inaaminika kwamba Mtakatifu Tomaso akielekea India alipitia Misri na kuinjilisha na baadaye alikuwa mwinjilisti Marko aliyeinjilisha Misri na kufia huko kama shahidi.
Wamisri wa kwanza kuongoka walikuwa wale walioongea Kigriki hasa watu wa mataifa waliokuwa wamekubali desturi za Kiyahudi. Hawa tayari waliijua biblia ya Kigriki ‘Septuagint’. Kwa ajili yao biblia ilikuwa imetafriwa kutoka katika Kiebrania. Hawa Wamisri-Wagriki walianza kuelezea Ukristo katika lugha na falsafa ya Kigriki.
Aleksandria palifunguliwa shule maarufu ya dini chini ya Panteanus na baadaye ikawa na waalimu mashuhuri kama Clementi wa Alexandria na Origen. Katika kanisa la mwanzo kanisa la Aleksandria lilikuwa la pili kwa umaarufu baada ya Roma. Mwishowe askofu wa Aleksandria alitambuliwa kama patriarka akiwa na mamlaka karibu yote katika kanisa la Misri.
Mwishoni mwa karne ya pili Ukristo ulienea mashambani kati ya Wakopti. Mwaka 202 wakati wa mateso ya mfalme Kaizari Septimus Severus wanatajwa Wakristo Wakopti wengi waliouawa mashahidi kwa ajili ya imani yao. Katika dhuluma hiyo dhidi ya Ukristo, viongozi wa dini walipopelekwa uhamishoni mashambani kama adhabu, lilikuwa kosa lenye heri kwa sababu liliwapa fursa nzuri ya kuanzisha makanisa imara huko mashambani. Hata biblia ilitafsiriwa katika lugha ya Kikopti katika kilugha (dialect) cha Bohairic ambayo baadaye ilikuwa lugha rasmi ya kanisa la Kikopti na kanisa zima la Misri. Wakati Misri ilikuwa imetawaliwa na Warumi toka Roma au Konstantinopole, dini ndiyo iliwaunganisha katika utaifa wao.
 Wakati Wakristo wa Misri wa lugha ya Kigriki walichangia sana katika kuunda teologia ya kanisa zima la ulimwengu, Wakristo Wamisri - Wakopti walichangia katika kuanzisha umonaki wa wakaa pweke kama Paulo wa Thabes na Antoni wa Jangwani na umonaki wa monasteri kubwa ulioanzishwa na Pakomius. Mwishowe pole pole Wakristo wa Misri  walitengeneza utamaduni mmoja wa Kikopti na kuacha lugha ya Kigriki.
Ingawa kanisa la Misri lilijulikana kwa mafundisho yao sahihi likiongozwa na mapatriarka shupavu kama Aleksanda na Atanasio waliotetea Utatu Mtakatifu, bahati mbaya mwishowe alikuja patriarka Dioscorus aliyekosea na kufundisha kwamba Kristo ni Mungu tu ambaye  utu wake uliliwa na umungu wake. Huu ulikuwa ni uzushi wa monofisiti  uliopingwa na Mtaguso Mkuu wa Kalcedoni mwaka 451 BK.
Bahati mbaya kanisa la Misri wakati zamani lilifurahia ushindi katika mitaguso mbali mbali huko nyuma halikutaka kushindwa na kukubali uamuzi wa mtaguso nkuu huo bali lilijitenga. Kujitenga kwao kuliwagonganisha na kanisa la Konstantinopoli na wafalme wao na kuleta uhathama kati yake na kanisa la ulimwengu. Ingawa utengano ulisaidia kujenga kanisa imara la kitaifa, kanisa la Misri lilijifungia peke yake na kuwa kisiwa likiacha kuchangia katika mawazo ya ulimwengu yaliyolikuza hadi hapo.
Vile vile wamonaki ambao walikuwa ngome kubwa ya kanisa la Misiri bahati mbaya kufikia karne ya tano na kuendelea watu wengi mno wenye uwezo walikimbilia milimani na jangwani kuwa wamonaki wakaa pweke na miji ikabaki na watoto na wazee ambao hawakuweza kuendeleza nchi au kuilinda dhidi ya maadui.  Vile ile wamonaki hao mara nyingi walipokuja mjini wakati wa migongano na mafarakano, walitetea upande mmoja kisiasa na kufanya fujo na hili lilidhoofisha kanisa la Misri.
 Uislamu ulipokuja katika karne ya sita ulikuta kanisa limedhoofika na kutengana na kanisa la ulimwengu la Roma na Konstantinopoli. Siyo tu Kanisa la Kikopti la Misri halikuwa na nguvu ya kugigana na majeshi wa Waislaamu lakini mara nyingine liliungana nao kupigana na Wakristu wengine wa Konstantinopoli.
KANISA LA AFRIKA YA KASKAZINI
Afrika ya kaskazini ilikuwa sehemu ya mwambao yenye upana wa kilometa 320 kuanzia Libya ya leo hadi Morroco.  Mji mkuu wa sehemu hiyo ulikuwa Kartago, ulioanzishwa na wapuniki kutoka Lebanoni karibu miaka 1,000 Kabla ya Kristo, (KK).
Dola ya kipuniki ilienea hadi Sierra Leone. Baada ya vita vya karibu miaka 100, gemadali Mpuniki Hannibal alishindwa na Warumi mwaka 146KK. Warumi walipoteza sehemu kubwa ya dola na kubakia tu na sehemu ya upana wa kilomita 320 kwa sababu wao walijali tu kutunza mipaka kwa usalama wa dola yao.
Wakati wa dola ya Kirumi kuanzia mwaka 146 ustaarabu wa Kirumi uliletwa hasa na maaskari pamoja na wahamiaji wachache na kuenea sehemu zilizotekwa. Wapuniki kwa kiasi fulani waliingia katika utamaduni wa Kirumi lakini wazawa, Waberba, ambao leo tunawaita wabeduini wengi wao walibaki katika utamaduni wao. Hivyo utamaduni wa Kirumi au Kilatini ulibakia wa waja.
Itaendelea wiki ijayo.
UINJILISHAJI WA AFRIKA YA KASKAZINI
Mapokeo yanasimulia kwamba mtume Filipo aliinjilisha Kartago katika safari zake za kimisionari. Maandishi ya kwanza ya kuthibitisha Ukristo ni ya mwaka 180 BK ambapo watu 12 (wanaume saba na wanawake watano) walihukumiwa kuuawa wakati wa mateso ya Marko Aurelio kwa kukataa kumkana Yesu. Tangia hapo Afrika ilikuwa na mashahidi wengi waliofia dini. Mwanateologia maarufu, Tertullian aliandika kwamba ‘damu ya mashahidi ndiyo mbegu ya Ukristo’.
Kartago ulikuwa ndiyo mji wa fasihi ya Kilatini katika dola ya kirumi, wasomi wake walijivunia namna ya kuongea Kilatini kuliko hata katika mji wa Roma wenyewe. Vile vile walifundisha wanasheria wengi na stadi mpaka mji huo ukaitwa kiota cha wanasheria. Kanisa la Afrika Kaskazini lilifuata nyayo likawa kanisa la Kilatini na sheria.
Kanisa la Afrika ndilo lilitafsiri kwa mara ya kwanza Biblia Takatifu katika Kilatini. Kanisa lilitoa wanateologia wakubwa kama Tertullian, Cyprian na Augustino walioweka misingi ya teologia ya kanisa lote la magharibi au kanisa la Roma. Tertulian anaitwa baba wa teologia ya Kilatini. Wanateologia hawa wenye misingi ya kisheria walielezea mafundisho katika maneno ya msamiati wa kisheria yasiyo na ncha mbili au maana zenye utata. Ni kwa sababu hiyo kanisa la magharibi halikuwa na uzishi ya kinadharia bali uzushi wa utendaji na hukumu kati ya dhambi na haki pamoja na adhabu zake.
UZUSHI KATIKA KANISA LA AFRIKA YA KASKAZINI MAGHARIBI
Kwa sababu kanisa la Afrika ya kaskazini magharibi lilitwama juu ya sheria, hivyo hata teologia yake ilikuwa ya mambo ya kimatendo na si kinadharia. Hasa walitaka Mkristu aishi maisha ya utauwa kiasi kwamba ionekane tofauti kati ya maisha yake na yale ya wapagani. Bahati mbaya hii ilielekea kwenye dini kuwa na msimamo mkali na hivyo uzushi wa msimamo mkali ulipata ardhi nzuri ya kusitawi.
Uzushi wa Montanus ilifundisha juu ya maono binafsi kama chanzo cha imani ya kanisa. Ulisisitiza juu ya ulazima wa kuwa mashahidi hivyo ilikuwa dhambi kujificha au kukimbia. Mbaya zaidi walisistiza kwamba dhambi kubwa tatu yaani kuua, kuzini na kuabudu miungu zisingeliweza kuondolewa au kusamehewa. Mtu akifanya hizo dhanbi hawezi kusamehewa na kanisa au kushiriki tena na wanakanisa wenzake. Hii siasa kali iliwateka wengi Afrika akiwamo hata mwanateologia mkuu Tertullian. Uzushi huu ulisumbua kanisa la Afrika hadi Karne ya sita.
Uzushi mbaya zaidi ulikuwa ule wa Donatus. Kwake yule aliyetenda dhambi kama kumkana Kristu kwa woga wa kuuawa alipoteza ukristo wake na inabidi abatizwe upya. Vile vile sakramenti inayotolewa na yule aliye na dhambi si halari lazima irudiwe. Kwa namna hiyo wote waliopewa upadre na uaskofu na maaskofu waliokuwa wametoa vitabu vitakatifu vichomwe hawakuwatambua. Hili lilileta mgawanyiko mkubwa sana. Hawa wafuasi wa Donatus walianza kanisa lao na walikuwa na nguvu hasa mashambani. Ilichukua nguvu za Mtakatifu Augustino kwa maandishi yake (393-411) na majeshi ya Mfalme Kaizari Honorius (398) kuwashinda. Ila vita hivyo vilidhoofisha sana kanisa la Afrika hasa mashambani na kulibakiza kanisa la Warumi tu.
Uzushi mwingine ulikuwa ule wa Pelagius ambaye ili kuwapinga wale waliofanya dhambi bila kujali, kwa kisingizio kwamba binadamu ni dhaifu sababu ya dhambi ya asili ya Adamu na Hawa, alifundisha kwamba binadamu anaweza kwa nguvu zake tu kufanya mema akitaka. Waafrika wengi walimfuata. Mtakatifu Augustino aliandika sana juu ya neema ya Mungu kumpinga mpaka akaitwa ‘Daktari wa neema ya Mungu’.  Alitetea kwamba binadamu hawezi kufanya lolote jema bila msaada wa neema ya Mungu, ila Mungu anatupa neema yake kila mara na tuna uhuru wa kuipokea.
Uzushi wa Afrika ya kaskazini magharibi kama unavyoonyeshwa unatafuta ukweli juu ya matendo ya binadamu, lipi ni sahihi na lipi ni dhambi, mtu afanye nini ili aokoke na ni nani mwenye uwezo wa kutoa huduma za kanisa. Siyo maswali ya kifalsafa kama kanisa la Kigriki la Mashariki ikiwemo Misri bali ya kisheria au kiutendaji.
UVAMIZI WA WAVANDALI
Katika karne ya tano dola ya kirumi ilidhoofika na washenzi mipakani mwake wakaanza kuivamia. Dola ya Kirumi ya magharibi, ambayo ndiyo hasa dola ya Kirumi mji wake mkuu ukiwa Roma, ilisambaratika kabisa mwaka 476. Tangia hapo hapakuwapo tena utawala wa kuunganisha dola nzima hapo Roma. Kaizari wa mashariki, Konstantinopole aliendelea kudai kutawala dola yote lakini hakuwa na maaskari au miundombinu ya kutosha kuithibiti, kila mara ilitegemea nguvu alizokuwa nazo.
Wakati sehemu nyingine za Ulaya zilivamiwa na washenzi wapagani kama Wafranki, Wavisigoti,  Wahuni, Wasaksoni, Waburgundi na wengine; Afrika ilikuwa na bahati mbaya kuvamiwa na wavandali. Hawa walikuwa wabaya kuliko wote kwa sababu waliharibu kila kitu walichoona. Kwa lugha za wazungu kusema vandali maanake mharibifu (vandalism). Baada ya kupitia Spain walitua Afrika na kuharibu ustaarabu wote chini ya kiongozi wao Genseriki. Wakiwa wazushi Waariani waliwanyanganya wakatoliki makanisa yao yote na wakawapeleka maaskofu uhamishoni. Walikataza ibada na mafundisho yote ya Kikatoliki na waliokataa kutii amri hiyo waliuawa mashahidi. Walichangia sana kudhoofisha kanisa la Afrika. Majeshi ya Kaizari Justiniani wa mashariki, Konstantinopole, yaliwashinda Wavandari mwaka 535 na kuwafukuza lakini kanisa la Afrika ya Kaskazini halikupata nguvu tena mpaka walipovamiwa na Waislamu katika karne ya nane.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Jumamosi ya Februari 10 mwaka huu majira ya mchana, zilitoka taarifa za kwamba aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Imani Madega, amefariki dunia.
Hakika zilikuwa ni taarifa za ghafla zilizotokana na kifo cha ghafla, kwani inaelezwa kwamba asubuhi ya siku hiyo akiwa nyumbani kwake Chalinze mkoani Pwani, alimuomba mtoto wake ampeleke hospitali kwa madai kwamba anajisikia vibaya, ingawa alikuwa na nguvu zake akitembea mwenyewe, lakini wakati akifanyiwa vipimo na matibabu hospitalini, hali ilibadilika na alifariki kwa tatizo la shinikizo la damu.
Katika kolamu hii, nitakusimulia baadhi ya matukio ambayo Madega aliwahi kuyafanya akiwa na Yanga ambayo aliiongoza kuanzia Mei mwaka 2007 hadi 2010.
APINGA YANGA KAMPUNI
Hiyo ilikuwa ni mwaka 2007 ikiwa ni siku chache baada ya kushinda nafasi ya uenyekiti wa Yanga, ambapo yeye na Viongozi wenzake, waliitwa ofisini kwa Yusuph Manji ambaye wakati huo alikuwa mfadhili.
Katika wito huo, Manji alimtaka atie saini mkataba wa makubaliano ya kuifanya Yanga iwe Kampuni na baada ya hapo Francis Kifukwe angepewa urais ndani ya mfumo huo, kitu ambacho Madega alikataa.
Sababu ya kukataa ni Katiba kutoruhusu kwa wakati huo, huku pia akiwa na wasiwasi kwamba huenda likawa changa la macho la kutaka klabu hiyo kubinafsishwa kihuni.
Madega aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kusema kwamba hawezi kufanya kitu kama hicho na kwamba Manji hana nia nzuri na klabu, hivyo ni vyema awaachie timu yao na wao wapo tayari kupambana nayo ili kuiendesha. Hapo ndipo uhasama kati yake na Manji ulipoanza.
KAULI YA KIBABE BAADA YA YANGA KUTEKWA
Ilikuwa Oktoba mwaka 2007, ambapo wakati huo uhasama kati yake na Manji ulizidi kupamba moto na kuibua makundi mbalimbali ambayo mengine yaikuwa yanampinga yakitaka aondoke madarakani.
Siku moja Yanga ikiwa chini ya kocha Mmalawi, Jack Chamangwana (sasa marehemu), ilitekwa na kundi la makomandoo ambao inasemekana walikuwa upande wa Madega na kwenda kufichwa Morogoro.
Katika mahojiano yake na kipindi cha Spoti Leo cha Redio One, Madega alikaririwa akisema, “Sitakuwa tayari kuiona Yanga ikiuzwa na kutawaliwa na mtu mmoja kwa nguvu ya pesa, masikini na mwanawe, tajiri na mali zake, Manji baki na mali zako au heshimu Katiba. Vinginevyo baki na mali zako au fadhili timu nyingine.” Baada ya sekeseke hilo, baadaye hali ya hewa ilikaa sawa.
AMSHUTUMU MANJI KUHUJUMU TIMU
Mwezi huo huo mwaka 2007, Yanga ilicheza dhidi ya Simba kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro, na Yanga kufungwa bao 1-0. Baada ya mchezo Madega aliibuka na kumshutumu Manji kwamba alitoa pesa kwa wachezaji ili wajifungishe kwa lengo la kumfanya aonekane hafai kuiongoza klabu hiyo na aondolewe kirahisi.
Ikumbukwe kuwa kabla ya mchezo, Manji alitoa Shilingi milioni 40 za maandalizi, huku akitoa na milioni 10 kwa wazee ili wafanye mambo ya kishirikina kwa ajili ya mchezo.
AOMBA RADHI WAZEE/MANJI
Ilikuwa mwishoni mwa mwaka huo huo wa 2007, ambapo siku moja waandishi tuliitwa kwenda kuchukua habari kwenye ukumbi wa hoteli ya Travertine, Magomeni jijini Dar es Salaam ambapo Madega aliingia ukumbini, na wanahabari wote tulitakiwa kusubiri nje kwanza. Baada ya dakika kadhaa tukaitwa na kutaarifiwa kwamba mzozo kati ya Madega, Manji, na wazee umekwisha baada ya Mwenyekiti huyo kuomba radhi.
AONGOZA MKUTANO KWA DAKIKA TATU
Ilikuwa mwaka 2008 ambapo Madega aliitisha mkutano wa wanachama kwenye ukumbi wa Police Officers Mess, na waandishi wa habari tulikwenda kushuhudia kile kilichofanyika. Miongoni mwa yaliyokwenda kufanyika, ni kupitisha baadhi ya marekebisho ya vipengele kwenye katiba.
Kabla ya mkutano kuanza, wanachama walipewa rasimu ya katiba ili kuweza kupitia na kufanya maamuzi. Ilipofika majira kama ya saa 3 na nusu asubuhi, Madega aliingia mkutanoni kuhakiki akidi na moja kwa moja kuhoji wanachama wote kama wanakubali rasimu ipite ama la.
Wanachama wengi walinyoosha mikono juu kuonyesha wameridhia, na hapo hapo Madega alitangaza kuwa rasimu imepita na kufunga mkutano huo, huku akisindikizwa na wimbo wa Pepe Kalle (hayati) wa Young Africans. Mkutano huo ulitumia dakika 3 tu na kuwashangaza wengi.
ATUKANWA NA NICOLAUS MUSONYE
Hilo lilijiri baada ya Yanga kukataa kuingiza timu uwanjani julai mwaka 2008, ambapo ilitakiwa kucheza na Simba kuwania mshindi wa tatu katika michuano ya Kagame. Siku hiyo uwanja ulifurika kuzisubiri timu ziingie uwanjani, lakini walionekana wachezaji wa Simba pekee.
Madega alipoulizwa, alisema kuwa walikubaliana pande zote (Simba na Yanga), kuwa wasipeleke timu uwanja mpya wa Taifa (sasa Benjamin Mkapa) kama matakwa yao yasingetekelezwa na CECAFA (ya mgawo wa mapato ya milangoni), lakini cha kushangaza wenzao wamewasaliti kwa kupeleka timu uwanjani.
Siku moja baada ya tukio hilo, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CECAFA Nicolaus Musonye, alituita wanahabari kwenye ukumbi wa jengo la Millenium Tower, Mwenge, na ‘kuwaponda’ viongozi wa Yanga akidai kwamba wote wakiongozwa na Madega, ni dhaifu, na hawajitambui pamoja na kauli zingine nyingi zisizoandikika, huku wakiifungia Yanga kutoshiriki kwa miaka mitatu.
AIWEKEA NGUMU TBL
Ilikuwa mwaka 2008 ambapo Madega alikataa agizo la wadhamini wao TBL la kutaka waajiri watendaji kama mkataba wao ulivyokuwa unaelekeza.
Madega alisema kuwa hayo hayakuwa makubaliano, bali walikubaliana kuajiri Mweka Hazina kwa sababu hawakuwa na uwezo wa kuwalipa watendaji, kama vile Katibu.
Mvutano huo ulitokea kabla ya Shirikisho la Soka Duniani FIFA kutaka wanachama wake wote kuwa na watendaji wa kuajiriwa, ambapo mwaka 2010 Simba na Yanga zilianza kuajiri Maafisa Habari na Makatibu.
AMSHUSHUA NGASSA
Ilikuwa mwaka 2009 ambapo ilidaiwa kwamba mchezaji Mrisho Ngassa aliuomba uongozi umuongezee mshahara kwa sababu kipindi hicho alikuwa na uwezo mkubwa uwanjani kushinda hata baadhi ya wachezaji wa Kimataifa waliokuwa wanasajiliwa klabuni hapo.
Siku moja Madega alifanya mkutano na waandishi wa habari na kuchomekewa swali hilo, na katika majibu yake, alisema kwamba haiwezekani mchezaji anakwenda Yanga akiwa mnyenyekevu halafu baadaye anatanua mabega akitaka kuongezewa mshahara.
Aliongeza kwa kusema kwamba Ngassa kuna kipindi alikuwa akipewa Shilingi elfu tano tu anatetemeka, hivyo asijifanye ana thamani sana, na badala yake akumbuke alipotoka.
AWEKA MSIMAMO USAJILI WA NGASSA ULAYA
Kuna mwaka ziliibuka taarifa kwamba klabu ya Lov-ham ya Norway ilikuwa inamtaka Ngassa, lakini uongozi ulimzuia.
Madega alitoa ufafanuzi kwa kusema kwamba haiwezekani wakala akawa anazungumza na vyombo vya habari tu bila wao kujua, hivyo suala hilo ni uzushi kwa sababu taarifa rasmi hazijawafikia mezani.
AACHA MILIONI 200 KWENYE AKAUNTI
Mwaka 2010 baada ya muda wake kuisha ndani ya Yanga, Madega hakutaka kutetea tena kiti chake na kuwaachia wengine wagombee. Katika taarifa yake kwenye Mkutano Mkuu wa Uchaguzi, Madega alitangaza rasmi kwamba anaondoka, huku kwenye akaunti ya klabu akiwa ameacha zaidi ya shilingi milioni 200.
Hali hiyo ilimfanya awe Mwenyekiti pekee wa timu za Tanzania kuondoka madarakani na kuacha akaunti zikiwa zimenona.
Huyo ndiyo marehemu Imani Madega na harakati zake ndani ya Yanga. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.

Mwanza

Na Paul Mabuga

Wimbi la watu kuwa na maarifa kutokana na usomi lakini matendo yao yakawa tofauti, wengi wao ni malezi ya wazazi yanayozaa raia magarasa.
Utakuwaje na maarifa na hata fedha lakini maneno yako hayaendani na matendo? Jamii yetu ipo katika madhila ya tatizo hili, na makala haya yanatafuta  majibu ni kwa nini tunakuwa na hali hii.
Anakufuata jamaa mwenye ukwasi, elimu na maarifa ya kutosha anakufuata akilalamika kwamba wenyeji katika eneo ulilotembelea, siyo nje ya mji mmoja kanda ya Ziwa, ni wema kwa kuwa wamemloga mke wake. Ndiyo maana analewa kupita kiasi na binti yake anayesoma Kidato cha Nne, hadi amekataa kwenda shule.
Anakuambia kisa ni kwamba yeye ana fedha na wanamuona kuwa ni tajiri, na hivyo ulozi anaousema unatokana na kuonewa wivu. Ni kweli anamiliki nyumba mbili ambazo hazijaisha wala kukamilika, ila watu wanaziishi kibishibishi, na baiskeli moja ambayo ina kitako ambacho hakifunikwi.
Kimsingi binti yake ni kweli ana kawaida ya siku kadhaa haendi shule, ama anakwenda kwa kuchelewa, na ni wazi kuwa hakuna anayefuatilia kwa vile mama yake muda mrefu anakuwa amelewa, ama kazima data, kama wanavyosema watu wa karne hii.
Inafikirisha sana kupata kauli kama hizi kwa mtu ambaye amekwenda shule na kusoma kwenye vyuo vya uhakika na hata kuwa na uwezo wa kifedha, anakuwa katika hali hiyo. Tena kukuongezea mshangao, ila anakuelezea mambo mengi ya kielimu akikumbuka mambo wakati wa enzi zake akiwa shuleni.
Wakati unashangaa hili, unapanda bajaji kwenda kituo cha basi ili kupata usafiri wa kurudi unakoishi, na abiria wenzako ni familia ya mke na mume ambayo inatoka shamba kulima.
Unawauliza maswali, lakini muhimu wanakuambia, wote ni wahitimu wa Kidato cha Nne na kwamba chanzo chao ni mbegu za mahindi kuziokota zile zilizodondoka mashineni! Unachoka.
Unajiuliza hivi ni kwa nini watu wanashindwa kutumia kiwango bora cha maarifa waliyopata kutokana na elimu waliyopata? Je ni malezi ya helikopta ya kutafutiwa kila kitu katika malezi na elimu yao?
Je, ni kukosa muda wa kufanya kwa uhalisia juu ya kila wanachokisoma na kile ambacho watakutana nacho katika maisha, au tu tumeamua kuwa kizazi cha hovyo?
Je, tunaugua ugonjwa wa akili hadi kufikia hatua hii? Unashangaa nini kama tulitegemea kikombe cha babu wa Loliondo kutibu kila ugonjwa, lakini bado tukajiona tuna maarifa? 
Jiulize tu kama kikombe hicho kingekuwepo hadi leo, ni misiba mingapi ingekuwepo! Hivi ukiambiwa ukila ndizi iliyooshwa kwa maji maalum utapata mchumba, shahada yako ama cheti cha Kidato cha Sita huwa unakuwa umekificha wapi, kama siyo maliwatoni!
Mjini kisomo! Mtaani katika jiji la Mwanza napo unakutana na kijana mwenyeji wa moja ya jamii zinazopatikana katika mkoa wa Arusha, anakupa kikaratasi chenye orodha ya magonjwa 63 ambayo anadai kuyatibu, lakini mikebe ya dawa haizidi mitano, na anakuhakikishia kuwa anapata wateja wa kutosha - majirani.
Cha kushangaza, ukiuliza unataka mchumba, presha ya kupanda, ya kushuka, kisukari na kutafuta kazi, anakupa chupa moja kwa magonjwa yote hayo. Anaongeza kuwa dawa hiyo pia inatibu Uric Acidi iliyozidi mwilini na magonjwa sugu ya njia ya mkojo! Unapata jibu ni kwa nini ana orodha ya magonjwa mengi, lakini mzigo wa dawa kiduchu.
Dk. Nkwabi Sabasaba anasema kwamba kuwa na maarifa na kutenda wakati mwingine vinaweza kuwa tofauti, kwani uwezo wa kufanya mambo huongozwa na ubongo wa mbele ambao pamoja na mambo mengine, una jukumu la kutafsiri kile ulicho nacho katika maarifa, na kukiweka kwenye matendo. Anasema kwamba ubongo unaposhindwa kufanya kazi hiyo kikamilifu, hali tunayoizungumzia hujitokeza.
“Hali hii ya ubongo kushindwa kutafsiri maarifa na ujuzi na kuviweka katika vitendo, inaweza kuwa imesababishwa na mazingira ya malezi ya mteremko, kudekezwa na kushindwa kutenda, na hivyo ubongo unashindwa kupata hamasa ya kujishughulisha, anasema Dk. Nkwabi Sabasaba.
Na anaongeza, “Ukiwafuatilia watu wa namna hii, wengi ni waongeaji sana! Hii inaletwa na mzazi kuona kuwa mtoto hawezi kuhangaika, hawezi kufua, yaani anamlea ki helikopta kwa kujali kuwa mtoto hawezi kuhangaika, na hivyo ubongo wa mbele unakuwa ‘inactive’ [unadumaa].”
Pia, uwezo wa akili kwa maana ya ‘Intelligent quotient [IQ],’ ni tofauti na ule mhemko wa kutenda, ‘emotion quotient [EQ],’ kwamba mtu anaweza kuwa na uwezo mkubwa wa maarifa, lakini hawezi kutenda kutoka na uwezo mdogo wa mhemko.
Dk. Nkwabi anafafanua kuwa katika mwili wa binadamu kuna sehemu ya ubongo ambayo inachochea hamasa ya mhemko wa kutenda, yaani binadamu mathalani anapoona mkufu na akautamani, basi sehemu hii inamhamasisha ili kufanya juhudi aupate, na anapata nguvu zote kuusaka, hii ni EQ.
“Kimsingi EQ ni bora kuliko IQ! Mnaweza mkaingia kazini kwenye ajira wote mkiwa na IQ nzuri  ambazo zimeoneshwa kwenye vyeti vyenu, lakini baada ya muda mwingine akawa na EQ nzuri na akasifiwa kwa utendaji,” anasema Dk. Nkwabi.
Lakini pia anazungumzia kitu kingine katika hali hii kwamba mtu anaweza akawa na IQ kubwa, lakni ule uwezo wake wa kumudu watu wengine [Social Quotient] unakuwa wa chini, na hivyo wakati mwingine kulazimika kutumia fedha kuwamudu.
“Unakuta mtu anaajiri watu wengine kwa kuwalipa fedha ili kumudu familia yake, anaagiza ‘naomba unisaidie kumdhibiti huyu mtoto ama mke ili waondokane na tabia hii ama ile.’ Hii ni dosari ambayo kama mtu anayo, basi hafai kuwa kiongozi,” anaonya Dk. Nkwabi na kusema kuwa mtu anaweza kuwa na uwezo mkubwa wa fedha ‘Financial Quetient’, lakini akakosa EQ na uwezo wa kuwamudu watu wengine.

Page 1 of 2