Na Laura Chrispin
Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro – Oyesterbay, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Alister Makubi amewaasa wauguzi kuwa na roho ya huruma na wasiwe wa kwanza kuwakatia tamaa wengine, bali wawe mahujaji wa matumaini, huku wakitambua kuwa Yesu ndiye muuguzi wa kwanza aliyewaponya wagonjwa.
Padri Makubi aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Wauguzi na Wagonjwa, iliyofanyika katika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima – Msimbazi, jimboni humo.
“Muuguzi hutakiwi kumkatia mtu tamaa, bali unatakiwa kuwa ni mtu wa matumaini kama Yesu alivyompa matumaini, yule mgonjwa aliyelala kwa miaka 38 kwa kumwambia ainuke na aende, na kuachana na maji yale yaliyokuwa kwenye birika,” alisema Padri Makubi, na kuongeza.
“Wauguzi kuweni na huruma kwa kuwatakia mema wagonjwa wenu, na kuwaambia wasimame na kuchukua magodoro yao ili waende, kwani wakati mwingine ugonjwa ni kama mradi, kwa sababu mtu anapoumwa, mwingine hufaidika.”
Padri huyo aliendelea kusema kuwa kila mtu anaumwa kimwili na kiroho, na kwamba wamepona kwa kufanya maungamo kwa kusafisha roho zao na kuwa watoto wapya wa Mungu.