DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba- OSA, amewataka Waamini kuachana na tabia na mazoea ya kushiriki na kupokea Sakramenti ya Ekaristi Takatifu bila kujiandaa.
Wito huo aliutoa hivi karibuni wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Uzinduzi wa Kigango kipya cha Kuzaliwa Bikira Maria – Kisukuru, Parokia ya Roho Mtakatifu - Segerea, jimboni humo.
“Mkristo lazima ujitakase ukiwa msafi wa roho ili ushiriki chakula cha Bwana. Huyu ni Mungu, lazima ujinyenyekeze kwake ukiwa mkamilifu. Wakristo muwe watu wa kujitakasa muda wote kwa sababu, isipojiandaa mkiwa wenye usafi wa Roho na wenye Imani Moja Takatifu ya Kristo, lazima mjichunguze kwanza mnaishije hapa Duniani kwa imani hii ya Ukristo wenu. Ndugu zangu Waamini, huu Ukristo tuutumie vizuri, maana ndiyo njia yenye ukweli wa kutuongoza katika maisha yetu,” alisema Askofu Musomba.
Aidha, Askofu huyo aliwasihi Waamini wenye tabia ya kutoa mimba au kuzuia ili wasipate mimba, watambue kwamba wametenda dhambi mbele za Mungu.
“Waamini wenye kutoa mimba au kuzuia wasipate mimba wajue kwamba wametenda dhambi kubwa, wameua. Kwa hiyo msifanye hivyo. Wale wenye tabia hiyo, Mungu amewaleta ninyi hapa duniani ili mumtumikie na umtambue, kwa nini ninyi leo mnamzuia mwenzenu wasizaliwe? Acheni kabisa kufanya hivyo,” alisema Askofu Musomba.
Vile vile, aliwaasa Waamini kujiandaa vyema kwa ajili ya kumpokea Masiha, wakitambua kwamba Masiha anazaliwa kwa ajili yao, hivyo wawe tayari kwa ajili ya mapokezi yake, huku wakiwa wasafi wa mioyo, pamoja na kuachana na tabia ya kuwa watu wa chuki.
“Mama Bikira Maria alipopewa taarifa kuwa ni mjamzito, utazaa mtoto mwanaume ingawa alishangaa pia alishtuka, lakini alipokea kwa imani moja kubwa, je, wewe mama leo ungeambiwa hivi ungesema nini? Tuwe watu wa imani kupokea kitu kwa unyenyekevu na furaha, huku tukiwa watu wa imani na unyenyekevu mkubwa,” alisema Askofu huyo.
Askofu Musomba aliwaasa Wanakigango hicho kuwa watu wa kupendana na kuheshimiana, kwani wakifanya hivyo, watafika mbali kimaendeleo katika Kigango chao.
“Mkifanya hivyo, mtafika mbali katika Kigango hiki, ili mje mfikie kuwa Parokia kamili. Mtambue kwamba hakuna Kigango kinachozinduliwa na Askofu, Kigango huwa kinazinduliwa na Paroko tu, lakini ninyi leo mmepata bahati kubwa sana kuzinduliwa na mimi Askofu, msiniangushe, mjitahidi kukua haraka, mjenge kanisa kubwa pia mjenge nyumba ya Mapadri haraka sana...
“Nimefurahishwa sana na makubaliano yenu ninyi Maparoko wawili katika Parokia hizi mbili, Parokia ya Makoka na Parokia ya Segerea, mmetoa Jumuiya zenu na kuunda Kigango, mmefanya vizuri sana, huu ndio Ukristo unaotakiwa, siyo kuwa na malumbano,” alisema Askofu.
Askofu Msaidizi, Mhashamu Stephano Musomba alitangaza kuwa Kigango hicho kitahudumiwa na Mapadri wa Parokia ya Roho Mtakatifu, Segerea.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo ya Segerea, Padri Denis Kunambi aliwaomba Waamini wa Kigango kipya wampe ushirikiano ili waweze kufikia maendeleo zaidi katika Kigango hicho.
Padri Kunambi alisema kuwa Kigango hicho kimezaliwa kwa baraka kubwa, kwa sababu eneo hilo lilinunuliwa na Parokia ya Segerea kwa lengo la kujenga shule kama mradi wa Parokia, lakini sasa wazo hilo limegeuka kuwa Kigango.
Naye Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Gaudence – Makoka, Padri Amaladoss Chinnappan aliwaasa Waamini waliotoka katika Parokia ya Makoka na kujumuika katika Parokia ya Segerea, kupitia Kigango hicho, wasichukie wala kusikitika, bali wafurahi kwa sababu wote ni Waamini Wakatoliki.
Padri Chinnappan alimshukuru Askofu kwa kuwaweka pamoja, kuwapatanisha na kuwapatia Kigango ambacho amekizindua, akiwasihi Waamini kufahamu kwamba huo ndio Ukristo wanaotakiwa kuuishi katika maisha yao ya kila siku.