Dar es Salaam
Na Remigius Mmavele
Alain Yoka Mpela almaarufu Afande, alikuwa akiishi na wazazi wake Manispaa ya Matete Jijini Kinshasa, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Akiwa likizo siku moja Baba yake alimtuma kwenda Manispaa ya Bandalungwa kupeleka barua kwa rafiki yake, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni kubwa.
Baada ya kupeleka barua, kwa kuwa mama yake mdogo alikuwa akiishi pia Bandalungwa, ambayo wanaifupisha na kuiita Bandal, aliamua kumtembelea badala ya kurudi nyumbani kwao moja kwa moja. Alipofika nyumbani kwake hakumkuta, hivyo akaanza kucheza mchezo wa “dames” wakati akimsubiri.
Alipokuwa akicheza, alikuwa akiimba wimbo Abissina wa King Kester Emeneya. Kwa bahati nzuri, Werrason alipita karibu na eneo ambalo Alain Mpela alikuwa anacheza, akasikia sauti ya Alain Mpela akiimba.
Akashangaa na akauliza ni nani huyu kijana, mwenye sauti nzuri tena ya kipekee. Werrason akaenda hadi nyumbani kwa mama mdogo wa Alain Mpela kumsikiliza.