DAR ES SALAAM
Na Laura Chrispin
Paroko Msaidizi wa Parokia Mtakatifu Maximiliam Kolbe, Mwenge, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Daniel Mapunda amewataka Waamini kuachana na wivu, kwani huo ni ushamba wa kutojitambua.
Alisema hayo katika homilia yake wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu iliyoadhimishwa parokiani hapo.
“Wivu ni ile hali ya mtu kutokupenda mafanikio ya mwenzako, lakini inawapasa kutambua kuwa wivu kwa maana nyingine ni ushamba wa mtu kumtolea mwenzako kijicho kwa yale mafanikio aliyopewa na Mungu,”alisema Padri Mapunda.
Padri Mapunda aliwaasa Waamini wazidi kumwomba Mungu ili wajitambue kuwa wao ni nani, na kufahamu uwezo wao waliopewa na Mungu.
Aidha, aliwataka Waamini wafahamu, vizuri jinsi ya kuzitumia karama zao walizojaliwa na Mungu na kuzifahamu kwani hata kama ndugu wamezaliwa tumbo moja hawawezi kufanana karama zao.
Kwa mujibu wa Padri Mapunda, Waamini wanapaswa kufahamu kuwa utajiri wa Mungu hauna mipaka, na kuwataka watambue kuwa Mungu aliwapa Manabii utajiri wa kuhubiri Injili kwa watu wake.
Aliwataka Waamini hao kila mmoja kwa nafasi yake kuonesha utu kila mahali, na kuziheshimu kazi zao.
Padri Mapunda alisema hata katika somo la Injili inaonyesha namna Mungu alivyotoa, talanta na kuwataka Waamini wasizitumie vibaya.
Hata hivyo, aliwaomba Waamini hao kuachana na tabia za kuwakwaza wenzao kwa kuwafabyia matendo ambayo kwa upande wao hawayapendi.