DAR ES SALAAM
Na Nicolaus Kilowoko
Mchezaji wa zamani wa klabu ya soka ya Simba ambaye alikuwa anakipiga eneo la kiungo, Abdulhalim Humud ameendelea kusisitiza kuwa, bado ana uwezo wa kucheza ligi ya Tanzania na kufanya makubwa.
Humud alisema kuwa wapo ambao wanambeza kuhusu kiwango chake, kuwa hawezi kucheza kwa sasa katika Ligi ya NBC, ambayo imekuwa na ushindani mkubwa.
Alisema kuwa uwezo alionao kwa sasa bado anaweza kumudu vema kabisa kucheza katika Ligi kuu, kutokana na kuwa umri wake unamruhusu kucheza soka kwa kiwango kizuri.
Nyota huyo alisema kwamba wapo mashabiki wa soka ambao wamekuwa wakimbeza, wakidai umri wake umeenda hivyo hawezi kuwa bora tena, kama ambavyo alikiwasha huko nyuma.
“Mimi kwa sasa nina uwezo wa kucheza kwa kiwango bora sana katika Ligi Kuu, japo wengine wanasema umri umeenda, sasa nashangaa kama naweza kucheza vyema katika Ligi ya Zambia, nashindwaje Tanzania”, alisema Humud.
Alisema kuwa Ligi ya Zambia kama utimamu wako wa mwili hauko vizuri, huwezi kucheza kwa kuwa ni moja ya ligi yenye kasha kasha kubwa, kutokana na ubora wa klabu zao.
Humud alisema kuwa matamanio yake ni kurejea tena kucheza katika ligi ya Tanzania, lakini wapo watu wengine ambao wakati mwingine wanakatisha tamaa, na wanatamani usiwe sehemu yao.