Print this page

Papa afafanua maana ya Ekaristi Takatifu

Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu yaliyoongozwa na Baba Mtakatifu Leo XIV. Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu yaliyoongozwa na Baba Mtakatifu Leo XIV.

VATICANCITY, Vatican

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Ulimwenguni, Baba Mtakatifu Leo XIV, amesema kuwa Ekaristi ni Sakramenti ya upendo, zawadi na sadaka ya Kristo Yesu msalabani.
Papa alisema hayo katika Maadhimisho ya Dominika ya Ekaristi Takatifu, aliyoiongoza katika Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Lateran, Makao Makuu ya Jimbo Kuu la Roma.
Aliongeza kuwa hiyo ni Sakramenti ya Altare, ambapo ndipo mahali pa kukutana na Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai, Mwili na Damu yake Azizi, na kwamba ni fumbo na muhtasari wa imani ya Kanisa, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.
Baba Mtakatifu alibainisha kuwa huo ni mwaliko kwa Waamini kila siku wanaposhiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu, kuwa alama angavu ya dhamana ya Waamini kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli vyombo na mashuhuda wa ushirika, amani, ukarimu na upendo kwa Mungu na kwa jirani zao.
“Ikawadia saa ya majaribu, jua likaanza kuzama pale nyikani na jangwa tupu, hawakuwa na chakula cha kuutosha umati ule wote! Jua lilipokuwa linakuchwa, njaa na hofu vikaongezeka, Mitume wakamtaka Kristo Yesu auage umati ule, lakini akajibu kwa huruma na upendo wake mkuu, akitoa kipaumbele cha kwanza kwa kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu…
“Mitume walikuwa na imani haba, kwa kuogopa kwamba mikate mitano na samaki wawili, wasingeweza kufua dafu kwa umati mkubwa kiasi kile! Kristo Yesu akaizima njaa ya watu wa Mungu kwa huruma na upendo wake; akatazama juu mbinguni, akavibariki, akavimega na kuwapa wawaandikie mkutano,” alisema Papa.
Aliongeza kuwa ishara hiyo ni utambuzi wa uwepo wa Mungu kwa njia ya sala, kielelezo cha ushirika na udugu unaosimikwa na kuenziwa na Roho Mtakatifu.
Baba Mtakatifu Leo XIV alisema, “Leo hii katika Ulimwengu mamboleo kuna watu wanaoteseka na kusiginwa na baa la njaa, kielelezo cha ukosefu wa haki msingi, kunakosababishwa na kiburi na jeuri ya binadamu, kinachowafanya binadamu kushindwa kugawana kikamilifu mazao ya nchi na kazi ya mikono ya wanadamu.”
Katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Baba Mtakatifu Leo XIV alisema kuwa mfano wa Kristo Yesu kuwalisha wenye njaa, ni kigezo cha utendaji kazi na huduma, ili kugawana chakula, na hatimaye kuzidisha matumaini tayari kutangaza na kushuhudia uwepo wa Ufalme wa Mungu.
Aliwasihi Waamini kufahamu kwamba, Kristo Yesu anawaalika waja wake kula na kunywa Mwili na Damu yake Azizi, ili waweze kupata maisha na uzima wa milele, kwani yeye ni chakula na kinywaji hai, na kwamba kwa kula chakula hicho, wataishi milele.
Sambamba na hayo, Baba Mtakatifu Leo XIV alikaza kusema kuwa Maandamano ni sehemu ya hija hiyo ya maisha ya kiroho, ambapo watu wote wa Mungu wanalishwa na kushibishwa na Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, huku wakimwabudu Kristo Yesu wa Ekaristi na kumpitisha kwenye barabara zao kama ushuhuda wa imani.
Aliwaalika Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumbeba Kristo Yesu nyoyoni mwao, kwani huyo anawashirikisha waja wake katika mpango mzima wa Ukombozi, huku akiwasisitiza kushiriki katika Karamu ya uzima wa milele.

Rate this item
(0 votes)
Japhet