Mwanza
Na Mwandishi Wetu
Simanzi imetawala katika Kanisa Katoliki nchini, kutokana na msiba mzito wa vifo vya Watawa wanne, wa Shirika la Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu pamoja na dereva wao, waliofariki dunia katika ajali ya gari mkoani Mwanza.
Waliofariki dunia ni Mama Mkuu wa Shirika la Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu duniani, Katibu Mkuu wa Shirika hilo, Masista wawili pamoja na dereva wao, katika ajali baada ya gari walilokuwa wakisafiria, kugongana na gari jingine.
Watawa hao ni Sista Lilian Kapongo (raia wa Tanzania), Mama Mkuu wa Shirika hilo duniani, Sista Nerina De Simone (raia wa Italia), Katibu Mkuu wa Shirika hilo duniani, Sista Damaris Matheka (raia wa Kenya), Sista Stellamaris Muthini (raia wa Kenya), na dereva wao Boniphace Peter Msonola, mkazi wa Bukumbi Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.