NA PAUL MABUGA
Ilikuwa ni usiku wa vilio, hasira, lakini pia fahari kubwa. Jumapili iliyopita nchini Morocco, dunia ilishuhudia vijana wa Taifa Stars wakiondolewa kwenye michuano ya AFCON 2025, kichwa cha juu dhidi ya wenyeji Morocco.
Kufungwa goli 1-0 na timu namba moja barani Afrika, huku mwamuzi Boubou Traoré, akionekana kuwa “mchezaji wa 12” wa wapinzani, ni jambo ambalo halitafutika haraka kwenye akili za Watanzania.
Dakika ya mwisho ya mchezo itabaki kuwa jeraha, mchezaji wa Stars anaangushwa ndani ya kumi na nane, dunia nzima inaona ni penati ya wazi, lakini filimbi ya mwamuzi inabaki kimya, na VAR inajiziba macho.
Tulitolewa kama “ndama” anayepelekwa machinjioni, lakini kabla kisu hakijagusa shingo, ndama huyu alionesha kuwa ana pembe za chuma.
Hata hivyo, kuna mambo matano ya Stars kujivunia katika AFCON hii: Moja ikiwa ni kuvunjwa kwa mwiko wa miaka 45, kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980, Tanzania imeweza kuvuka hatua ya makundi, na kuingia hatua ya mtoano (Round of 16).