DAR ES SALAAM
Na Arone Mpanduka
Klabu ya Singida Black Stars, imesema kuwa haina ukaribu wala urafiki wowote na klabu ya Yanga, hasa kwenye kupeana wachezaji na kupeana matokeo, kama watu wanavyodai.
Singida imeyasema hayo, wakati wimbi la kuuziana na kupeana wachezaji wa mkopo likishamiri, katika kila dirisha la usajili hapa nchini.
Katika dirisha dogo la sasa la usajili, Singida iliwatoa kwa mkopo wachezaji Mohammed Damaro na Marouf Tchakei kwenda Yanga, huku Yanga ikimtoa Mamadou Doumbia kwa mkopo kwenda Singida, jambo ambalo wadau wa soka wakalazimika kuweka hadharani shaka yao, kuhusiana na timu hizo mbili.