Dar es Salaam
Na Remigius Mmavele
Mzee anajiuliza, huku Pepe Kalle wala hamjali, akamfuata Djouna pale alipokua amesimama, akaanza kumkaripia, wewe inakuaje nilikuambia uwe unafika nyumbani sasa umetimiza mwezi mzima hujatokea tangu tumesafiri hadi tunarudi hujafika hata mara moja. Djouna akaomba samahani, basi Pepe Kalle akatoa begi la nguo nakumpa Djouna kama zawadi, ishara ya upendo na uaminifu.
Baada ya Pepe Kalle kuondoka, Baba yake Djouna alimwita mwanae kwa mazungumzo na kumuuliza swali moja tu: “Kati ya masomo na muziki, unachagua nini?” Djouna akajibu bila kusita: “muziki”.
Baba yake akambariki.
Siku iliyofuata baada ya mazungumzo yao ya kwanza ya kina, Pepe Kalle alifika nyumbani anakoishi Djouna Mumbafu akiendesha gari lake aina ya Mazda. Akamtazama na kumwambia maneno ambayo yamebaki moyoni mwa Djouna Mumbafu hadi leo: “Sikiliza kijana, wewe uko hapa si kwa kupendeza watu hapana. Wataendelea kukuwekea vikwazo na vijembe. Unachotakiwa ni wewe kufanya kazi vilivyo, uthibitishe uwezo wako. Najua kabisa kama unaweza”.
Bahati nzuri, safari mpya ilikuwa imepangwa ziara ambayo ingewafikisha hadi Mali, wakianzia na onesho kubwa nchini Burkina Faso. Huo ulikuwa mwanzo wa safari zake za kimataifa akiwa na Empire Bakuba. Walipowasili Burkina Faso, walitarajiwa kutumbuiza katika uwanja uliofurika watu. Ndani ya kundi lao, alikuwepo pia Zwazwe, dansa mwenye kipaji cha kipekee. Kati ya Djouna Mumbafu na Zwazwe kulizuka ushindani wa kisanii; nani angeutawala uwanja?
Siku ya onesho, Zwazwe alikuwa wa kwanza kupanda stejini na bila kuchelewa akaanza show. Alimiliki jukwaa kwa ustadi wa ajabu, akicheza kwa umahiri na fimbo yake. Uwanja mzima ukalipuka kwa makofi.
Ndipo Pepe Kalle akamgeukia Djouna Mumbafu na kumpa ishara ya kwamba akaingie yeye kazi kwake sasa. Djouna akiwa mwanamichezo na mchezaji wa judo aliyepata mafunzo, alipiga sarakasi kujirusha kuanguka kwa kishindo kikubwa, akawatolea rapa zake zilizowasha moto wa umati. Alivua shati lake, akapanda hadi kwenye majukwaa ya watazamaji na umati ukashangilia kwa nguvu.
Kwa kumaliza mchuano huo wa furaha, Pepe Kalle akapaza sauti yake maarufu: “Zabale! Zabale Chacha!” Akiashiria mwisho wa sehemu hiyo, kisha akamtania: “Wewe mwizi, rudi hapa!” (Kicheko.) Kwa Djouna Mumbafu kukubalika zaidi ndani ya kundi, alijiweka karibu kwa wazee ambao walikua tayari ni wakongwe ndani ya kundi ambao ni Vieux Elvis Nkunku, Mpiga Bass Layo Layo na Mpiga solo ya Doris.
Baada ya ziara yao Burkina Faso na Mali, walirejea jijini Kinshasa,
ndipo wakatangaziwa kuwa yupo mtayarishaji wa muziki (Producer) ambaye amejitokeza kuwapeleka ziara Ulaya. Kila mtu aliingia kwenye maombi ili jina lake liongezwe kwenye orodha.