Dar es Salaam
Na Violet Tillya
Waamini wa Kanisa Katoliki katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, wameadhimisha Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu kwa sala, maombi, vifijo, nderemo na matumaini, licha ya changamoto za kiuchumi zinazowakabili wananchi.
Kwa mujibu wa mafundisho na mapokeo ya Kanisa, Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba huadhimishwa Septemba 14 kila mwaka. Sikukuu hii pia inahusishwa na kumbukumbu ya kupatikana kwa Msalaba wa Yesu Kristo na Mtakatifu Helena, mama wa Kaisari Konstantino, katika karne ya nne na baadaye kuwekwa katika eneo la Yerusalemu.
Hata hivyo, kutukuza Msalaba si kuabudu mbao, bali ni kumtukuza Kristo aliyekufa na kufufuka juu ya Msalaba huo. Kama ilivyoandikwa katika Injili ya Yohane 12:32: “Nami nikiwa juu nitawavuta watu wote kwangu.”
Waamini wakusanyika Pugu
Jumamosi ya Septemba 12, 2026, mamia ya waamini kutoka Parokia mbalimbali ndani ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam, walikusanyika katika Kituo cha Hija Pugu kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu.
Maadhimisho hayo yaliambatana na Adhimisho la Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu.
Akizungumza katika mahubiri yake, Askofu Msaidizi Mchamungu aliwakumbusha waamini maana halisi ya Msalaba katika maisha ya Mkristo.
Sikukuu hii inahusishwa na kupatikana kwa Msalaba wa Yesu Kristo, tukio linalohusishwa na Mtakatifu Helena, ambaye alikuwa mama wa Kaisari Konstantino. Kipindi cha utawala wa Konstantino kilifungua njia kwa Wakristo wa wakati huo kuabudu kwa uhuru zaidi baada ya kipindi kirefu cha mateso chini ya baadhi ya watawala wa Kirumi.
Askofu Mchamungu aliwataka waamini kutambua kwamba Msalaba si hirizi ya kuvaa kwa ajili ya kujilinda dhidi ya magonjwa, mabalaa au matatizo mbalimbali. Badala yake, Msalaba ni ishara ya imani inayowaalika waamini kutafakari maisha ya Kristo na kuishi mafundisho yake katika maisha yao ya kila siku.
“Msalaba ulio mzito kwetu sisi waamini ni wa kusamehe hata pale ambapo ni pagumu. Ukiweza kufanya hivyo, kwa kweli hapo ndipo utakapokuwa umebeba msalaba wako katika imani. Kumsamehe yule aliyekujeruhi ni jambo gumu, lakini hatuna budi kufanya hivyo.
“Ujumbe wa Kikristo si kwamba mateso ni mazuri yenyewe na hivyo tuyatafute. Yanapotujia, tuyabebe pamoja na Kristo. Kristo aliyabeba katika ubinadamu wake. Alijua yatakayotokea; atateswa na atakufa. Lakini sioni mahali katika Maandiko Matakatifu aliposema, ‘Jamani, nisulubisheni’. Alijua hayo yangetokea.
“Anasema: ‘Njooni kwangu ninyi nyote mnaosumbuka na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha’. Kwa hiyo, mateso unayokutana nayo yabebe pamoja na Kristo, nawe utapata faraja kwake.”
Aidha, Askofu Mchamungu alieleza kuwa kufanya Ishara ya Msalaba ni namna ya kutangaza imani ya Mkristo.
“Tunapofanya Ishara ya Msalaba tunatangaza imani yetu na kusema: Mimi ni wa Kristo. Ninaamini katika kifo na ufufuko wake. Msalaba unatukumbusha kuwa upendo wa Kikristo si wa maneno tu.”