Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha
Makala

Makala (38)

DAR ES SALAAM

Na Pd. Gaston George Mkude

Amani na Salama!
Mwinjili Marko wakati anaandika sehemu ya Injili ya leo, himaya ya Kirumi ilikuwa imetoka katika vita na mabalaa mengi, mfano magonjwa ya milipuko na uvamizi wa wadudu katika mashamba yao.
  Si tu himaya ya Kirumi, bali hata Jumuiya ya Wakristo katika himaya ile walikuwa wametoka kupitia kipindi kigumu cha mateso na madhulumu ya Mfalme Nero, aliyewatesa na kuwaua Wakristo wale wa kwanza. Hivyo katika mazingira ya namna hii magumu na yenye mateso mengi waamini walikuwa wanajiuliza nini maana ya haya yote na kwa nini wanapitia hayo yote. Hata nasi leo dunia nzima tunajiuliza maswali mengi mintarafu majanga mbali mbali, kwa nini Mungu anaruhusu tujaribiwe, tupatwe na kupitia kipindi kigumu namna hii? Nini hasa maana na lengo lake?
Mwinjili Marko ni katika mazingira ya namna hii anaandika sehemu ya Injili hii ya leo yenye aina ya uandishi ya kiapokaliptiko. Apokaliptiko ni neno lenye asili ya Kigiriki litokanalo na maneno mawili ambayo ni apo likimaanisha kuweka mbali au tenganisha, pamoja na kaliptiko likimaanisha weka bayana.
Hivyo aina ya uandishi ya kiapoliptiko ni ile inayotumia lugha isiyo kuwa wazi sana, ni lugha ya mficho hivyo kupata ujumbe wake ni lazima kufunua au kufumbua mafumbo na lugha ile ya mficho. Tunaweza kutumia lugha ya vijana ya kileo ni kufungua code (decodification)!
Na ndio mwaliko wa Bwana wetu Yesu Kristo katika Injili ya leo anapotuonya tusidanganyike tunapoona mambo hayo yakitokea katika ulimwengu na nyakati zetu. Hata katika nyakati zetu kuna mengi yanayotokea, na hata mara kadhaa kushawishika kusema mwisho wa dunia umekaribia. Hiyo pia ilikuwa ni hofu ya Wakristo wale wa mwanzo, hivyo mwinjili anaona hitaji la kuwaandikia ujumbe huu wa kiapokaliptiko.
Marko mwinjili anatumia lugha ya picha ya kiapokaliptiko kama vile jua na mwezi na ishara nyingine za angani. Kwa watu wa mashariki ya kati walikuwa wanaabudu ishara za angani kama jua na mwezi kama miungu yao, na hivyo hata kutolea sadaka pale wanapoona kuwa mambo yao yanakwenda kinyume na matarajio yao.
Musa anawaalika Wanawaisraeli kumwabudu Mungu wa kweli na sio nyota au jua au mwezi wa angani. (Kumbukumbu la Torati 4:19) Hata Nabii Isaya pia anaawalika kumwabudu Mungu wa kweli na si nyota wala jua wala mwezi. “Nyota na vilimia vyake angani hazitaangaza; jua linapochomoza litakuwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake” (Isaya 13:10)
Ujumbe huu haukuwa kwa ajili ya kuwatisha na kuwaogofya, kuwa jua na mwezi na nyota zitaacha kutoa mwanga wake wa asili, bali kuwatia matumaini kuwa nuru na mwanga wa kweli unatoka kwa Mungu mwenyewe na si katika vitu vya angani. Hivyo ni ujumbe wa furaha na matumaini. Mwanga na nuru ya kweli ni Yesu Kristo mwenyewe katika maisha ya kila mfuasi wake.
Na ndio mwinjili Marko anaandika sehemu hii ya Injili, ambapo Yesu Kristo anatumia pia lugha hii ya kiapokaliptiko kwa lengo la kuwafariji waamini wanaopitia kipindi kigumu cha mateso na madhulumu. Na kwetu leo ni neno la faraja na matumaini hata kama tunapitia katika kipindi chenye magumu na changamoto nyingi katika maisha.
Ni kawaida kujiuliza maswali nini maana ya magumu na mateso katika maisha yetu, na hata tunapojibidisha kusali na kuwa waaminifu katika imani yetu, bado tunakutwa na mahangaiko katika maisha ya siku kwa siku. Nini maana ya mateso, kwa nini mateso na magumu katika maisha ya ufuasi?
Tunaalikwa kunyanyua vichwa juu kwani wokovu wetu unakaribia, ulimwengu mpya wa ufalme wake Mungu. Mwanzo mpya ambapo mtawala mpya ni Mungu mwenyewe anayetaka kukaa na kuwaongoza watu wake. Ni mwanzo wa ufalme wa Upendo, Amani na Haki.
Dhiki, jua kutiwa giza, mwezi kukoma kutoa mwanga wake, nyota zikianguka na nguvu za mbinguni kutikisika, zote hizi ni ishara ya yule muovu na uovu ulimwenguni. Ni kwa ujio wa Yesu Kristo ulimwenguni basi yule muovu na uovu hauna nguvu tena, hauna nafasi tena kwani tunaalikwa kuunda ulimwengu mpya, ndio ufalme wa Mungu kati yetu, katika maisha yetu.
Ni ujumbe wa faraja kuwa Mungu mwenyewe atamtuma malaika wake, hapa malaika pia ni lugha ya kiapokaliptiko likimaanisha mjumbe wa Mungu ambaye ujio wake sio kuja kuhukumu ulimwengu, bali kuwaunganisha wana wake kutoka pande zote za dunia baada ya kutawanywa na yule mwovu.
Mwana wa mtu hataruhusu wapotee bali atawakusanya wote. Ni mjumbe wa Habari Njema ya wokovu kwa watu wote bila ubaguzi wa aina yeyote, mjumbe huyu ndio kila mmoja wetu anaposhiriki katika kueeneza Ufalme wa Mungu hapa duniani, kuwa wajumbe wa kweli za Injili kwa maneno na matendo yetu. SOMA ZAIDI...

VATICAN

Na Sr. Angela Rwezaura

Katika Ripoti mpya kutoka UNESCO, inashutumu kuwa mwaka 2022-2023 wafanyakazi 162 wa vyombo vya habari waliuawa,karibu nusu katika maeneo ya vita na kutokujali kungali juu sana.
Idadi ya waandishi wa habari wanawake ambao walikuwa waathiriwa pia iliongezeka,14.
Hii ndiyo sababu hatua ya haraka inaombwa kutoka kwa Mataifa. Kampeni ya”Kuna historia nyuma ya historia”iliandaliwa na mwongozo wa usaidizi wa kisaikolojia ukachapishwa.
“Mnamo 2022 na 2023, kila baada ya siku nne mwandishi wa habari aliuawa kwa kufanya kazi yao: kutafuta ukweli. Katika idadi kubwa ya kesi hakuna mtu anayewajibisha.” Hii iliripotiwa na Audrey Azoulay, mkurugenzi mkuu wa UNESCO, ambaye alichapisha ripoti yake mpya Novemba 2, 2024 wakati wa Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Kutokujali kwa Uhalifu dhidi ya Waandishi wa Habari.
Asilimia 85 ya mauaji ya waandishi wa habari ulimwenguni kote hayaadhibiwi, takwimu ambayo inasisitiza uzito wa hali hiyo, licha ya maendeleo madogo tangu 2018, wakati kiwango cha kutokujali kwa mauaji yaliyorekodiwa tangu 2006 kilikuwa asilimia 89.
Asilimia 95 mwaka 2012
Pamoja na ripoti yake, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)linatoa wito kwa nchi zote wanachama wake kufanya zaidi ili kuhakikisha kwamba uhalifu huu haukomi bila kuadhibiwa,  Azoulay alieleza zaidi - kushitaki na kuwatia hatiani wenye hatia ni nyenzo ya msingi ya kuzuia mashambulizi ya baadaye dhidi ya waandishi wa habari.”
 Ingawa UNESCO inaona kuboreka kwa mwelekeo huo, ikizingatiwa kwamba kiwango cha kutokujali kilikuwa 95% miaka kumi na miwili iliyopita, inatoa wito kwa Mataifa “kuongeza kwa kiasi kikubwa juhudi zao za kuzuia uhalifu mpya dhidi ya waandishi wa habari.” Katika miaka miwili iliyopita waathirika 162, ambapo 14 wanawake.
Katika kipindi cha miaka miwili 2022-2023, kipindi kilichoakisiwa na ripoti mpya, waandishi wa habari 162 waliuawa, karibu nusu yao katika nchi ambazo migogoro ya silaha ilikuwa ikiendelea, wakati katika kipindi cha miaka miwili iliyopita asilimia ilikuwa asilimia 38.
Katika nchi nyingine, waandishi wa habari wengi wameuawa kwa kujaribu kusema ukweli kuhusu uhalifu wa kupangwa, rushwa au kuripoti maandamano ya umma. UNESCO pia inaripoti ukweli mwingine wa kutisha: idadi ya waandishi wa habari wanawake waliouawa katika kipindi cha miaka miwili, 14 kwa jumla, ni ya juu zaidi tangu 2017.
Kampeni “Kuna historia nyuma ya historia”
Ili kukabiliana na hali ya kutokujali, shirika la Umoja wa Mataifa leo linazindua kampeni mpya ya kila mwaka ya kimataifa ya kuhamasisha umma kuhusu ukatili dhidi ya waandishi wa habari.
Ukiwa na mada “Kuna historia nyuma ya historia, mpango huo unalenga kuleta umakini kwa uhalifu dhidi ya vyombo vya habari, kupitia makala na ushuhuda zilizochapishwa ulimwenguni kote.
Zaidi ya hayo, tarehe 6 Novemba, UNESCO itaandaa mkutano wa kimataifa kuhusu Usalama wa Waandishi wa Habari katika Migogoro na Dharura mjini Addis Ababa, kwa ushirikiano na Umoja wa Afrika.
Wakati wa hafla hiyo, Daftari la Kimataifa la Mbinu za Kitaifa za Usalama kwa Waandishi wa Habari litawasilishwa, ambalo linakusanya sera za ulinzi wa wanahabari zinazotekelezwa katika nchi 56 na angalau mipango 12 ya kitaifa.
Mwongozo wa msaada wa kisaikolojia
UNESCO pia itachapisha mwongozo kwa wanasaikolojia wanaofanya kazi na waandishi wa habari katika hali za dharura, kwa ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Vyombo vya Habari vya Wanawake (IWMF).
Mwongozo huo, unaolenga hasa wanawake, utawapa wanasaikolojia zana za kuleta utulivu wa michakato ya kihemko na kiakili ya waathiriwa wa matukio ya kiwewe, kuwasaidia kufanya maamuzi ya busara, ya msingi kwa maisha yao, na kupunguza tabia za msukumo ambazo zinaweza kuwaweka hatarini zaidi.
UNESCO, Umoja waonya
Likiwa na nchi wanachama 194, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) linachangia amani na usalama kupitia ushirikiano wa kimataifa katika elimu, sayansi, utamaduni, mawasiliano na habari.
Ikiwa na makao yake makuu mjini Paris, UNESCO ina ofisi katika nchi 54 na inaajiri zaidi ya watu 2,300.
 Inasimamia zaidi ya Maeneo elfu mbili ya Urithi wa Dunia, Hifadhi za Biosphere na Geoparks za Ulimwenguni, mitandao ya Miji Ubunifu, Jumuishi, ya Kujifunza na Endelevu, na zaidi ya shule elfu kumi na tatu zinazohusiana, viti vya vyuo vikuu, vituo vya mafunzo na utafiti.

KIGOMA

Na Mathayo Kijazi

Katika kuhakikisha familia, jamii, na hata Kanisa kwa ujumla linaendelea kuwa na watu wenye maadili ya kumpendeza Mungu, ni lazima familia zijengwe vyema, ili ziweze kudumu katika misingi iliyo bora.
Zipo njia mbalimbali zinazoweza kutumika kujenga jamii iliyo bora kupitia katika familia zao, zikiwemo semina za Kanisa, mikutano, makongamano, pamoja na mafundisho mbalimbali.
Katika jitihada hizo za kujenga familia, Utume wa Uimarishaji wa Familia Tanzania (UFATA), hivi karibuni ulifanya Mkutano wake Mkuu wa Kitaifa katika Jimbo Katoliki la Kigoma.
Vile vile, ndani ya Mkutano huo ilifanyika Semina iliyohusisha mada mbalimbali zilizolenga familia, mwenendo wake, pamoja na tafakari mbalimbali.
Akiwasilisha mada isemayo ‘Familia imara ni msingi wa utu wa mtu’, Mkuu wa Chuo cha Songea Catholic Institute of Technical Education, kilichopo Songea, mkoani Ruvuma, Padri Longino Rutangwelera Kamuhabwa wa Jimbo Katoliki la Bukoba, anasema kwamba kwa kuumbwa kwake na kwa hulka yake, utu wa mtu ni wa kuheshimiwa na umetakaswa.
Padri Kamuhabwa anasema kwamba Familia ni Taasisi ya Kimungu kati ya wanadamu, kwa ajli ya kuendeleza na kulinda heshima ya utu wa mtu, na kwamba kuheshimu familia na utu wa mtu, ni kumheshimu Mungu aliye chimbuko lake.
Anaongeza kwamba mwanadamu anatakiwa kuheshimiwa na kuthaminiwa kama njia mojawapo ya kumheshimu na kumthamini Mungu, kwani ameumbwa kwa malengo ya kumjua, kumpenda, kumtumikia Mungu na kutafuta Ufalme wake.
Padri huyo anabainisha pia kuwa mwanadamu ni wajibu wake kutambua kwamba ameumbwa pamoja na wanadamu wengine, kwani huo ni mpango wa Mungu kuwa mwanadamu atimize malengo ya kuumbwa kwake akiwa kundini.
Anasema pia kwamba mwanadamu ni muhitaji, mhanga na dhaifu, hivyo, anahitaji kuhubiriwa, kulindwa, kutetewa, kukemewa pamoja na kuelekezwa.
Anabainisha pia kwamba katika kuwa kiumbe muhitaji, mwanadamu kwa hulka yake, Mungu alimuumba mtu akiwa na njaa na kiu ya kufikia ukamilifu, na kuongeza kuwa ni katika hali hiyo, mtu hutafuta, husali, hufanya kazi ili afikie kile cha kumfanya awe mkamilifu. Katika kutafuta huko, Padri huyo anasema kwamba mwanadamu pengine hupatia, na pengine hukosea.
Pia, Padri huyo anasema kwamba nyenzo za kumsaidia wanadamu kufikia kile anachokihitaji, ni pamoja na Sala, Neno la Mungu, Maisha ya sakramenti, pamoja na Maisha ya familia.
Vile vile, anasema kuwa kwa hulka yake, mwanadamu ameumbiwa kwanye jamii (familia), na kwa asili yake, ana mwelekeo wa kuishi au kushirikiana na wanadamu wengine.
“Mwanadamu anafaidika kwa kushirikiana na wanadamu wengine. Kukamilisha na kukamilishwa na wengine (complementarity principle). Kutegemeza na kutegemezwa na wengine (synergy principle). Mtu ni ufunuo na uwepo wa Mungu kati ya watu (transcendental being)…
“Kadiri ya Edith Stein (Mtakatifu Theresa wa Msalaba) mtu ni Epiphania - anafunua wema na upendo wa Kimungu kwa wengine. Kadri ya Mtakatifu Thomas Aquinas, kupitia ubinadamu wetu, Mungu yu pamoja nasi = Emmanuel. Kristu aliutwaa ubinadamu wetu ili sisi tukwezwe na kuushiriki Umungu wake. Kwa hiyo, mtu ni ufunuo wa uwepo wa Mungu kati yetu. Mtu ni zaidi ya yale unayoyaona,” anasema Padri huyo.
Sambamba na hayo, Padri Kamuhabwa anaongeza kwamba mwanadamu ni kiumbe hisia, kwani kwa hulka yake anaweza kufurahi au kukasirika; kupenda au kuchukia; kuwa na vionjo mbalimbali; kukubaliana pamoja na kutofautiana na wengine.
Anasema kwamba hiyo inaleta uhalali wa mtu kupenda na kupendwa, kujali na kujaliwa, kuheshimu mawazo na maoni ya mtu, kumpa mtu nafasi ya kuchagua anachokitaka, na kuacha asichokipenda.
Kwa nini utu wa mtu uheshimiwe na kulindwa?
Padri Kamuhabwa anabainisha kwamba ni vizuri kutumia sababu moja kati ya hizi, ili kujenga hoja ya kulinda heshima na utu wa mtu; Mtu ni sura na mfano wa Mungu (Mwa, 1:26); Mtu kajaliwa akili na utashi wa kumtafuta Mungu (Isaiah, 1:17-19); Mungu kapitia kwa mtu kajifunua kwa viumbe wote (In, 14:8-9); pamoja na; Mungu kamchagua mtu na kuweka agano naye (Mwa, 9:13; Kut. 19:5).
Sambamba na hayo, anasema kwamba familia ni taasisi ya kuenzi na kuheshimu utu wa mtu, kwani hiyo ni taasisi ya wanadamu aliyoianzisha Mungu ili kupitia kwenye taasisi hiyo, watu washirikishane upendo wa Kimungu, na watu washiriki kazi ya Mungu ya uumbaji.
Pia, anabainisha kwamba taasisi hiyo ni ya wanadamu kwa sababu inaundwa na wanadamu (nuclear and extended). Na pia ni ya Kimungu kwa sababu mwasisi, mtegemezaji na malengo yake ni Mungu.
Vile vile, anasema pia kwamba taasisi hiyo ni ya upendo, kwa sababu kiungo chake ni upendo, ni ya uumbaji kwa sababu inaendeleza umbaji.
Njia za kuenzi na kuimarisha familia:
Akitaja njia zinazoweza kutumika ili kuimarisha familia, Padri huyo anabainisha kwamba ni lazima kuwepo na sala, kuiombea na kusali pamoja; ijikite katika kusoma na kuishi Neno la Mungu; Maisha ya Sakramenti; ipate neema za Sakrameti; malezi endelevu; ianze na Mungu na ibaki na Mungu; Maadhimisho endelevu; kushika amri ya mapendo, kufanya kumbukizi za matukio muhimu ya kifamilia, pamoja na kuhuisha mahusiano.
Matishio dhidi ya familia:
Akitaja mambo yasiyofaa na yanayoonekana kuwa tishio katika familia, Padri Kamuhabwa anasema kwamba mambo hayo ni pamoja na familia kuanzishwa kiholela.
Anaongeza kuwa kadri ya mpango wa Mungu, familia huanza kupitia ndoa halali, tofauti na hilo, ni mwanzo potofu, matokeo yake ni matokeo na mwisho potovu.
Vile vile, anasema kwamba upotoshwaji wa sifa za wanafamilia ni moja ya tishio, kwani familia huundwa na baba, mama na watoto. Upotovu katika jinsia za wazazi ni tishio la familia.

SOMA ZAIDI....

DAR ES SALAAM

Na Pd. Mujuni Audiphace

(Heri kwenda nyumbani mwa matanga kuliko kwenda nyumbani mwa karamu, maana huko ndiko mwisho wa binadamu wote, na walio hai wataweka moyoni,” Mhubiri 7:2)
Ndugu zangu Tumsifu Yesu Kristo.
Mwezi wa nane mwaka huu (2024) familia yetu tulijengea na kuweka msalaba mpya kwenye kaburi la Baba yetu aliyefariki miaka 37 iliyopita huko Kamachumu Kagera.
Siku moja kabla ya Misa ya kilele cha tukio hili nilifika nyumbani kuona kinachoendelea, nikakuta fundi yupo anakamilisha ujenzi akiwa na mdogo wetu wa mwisho wakiwa wawili tu pale kwenye eneo la makaburi.
Huyu bwana mdogo akawa anajisifia kuwa yeye tu ndiye haogopi makaburi, akaniambia kuwa wengine wote wamekimbia hii kazi ya msaidia fundi sababu inafanyika makaburini na ni ya kujenga kaburi.
Nilimuuliza kuwa: UNAFIKIRI HASA WANAOGOPA NINI KUHUSU MAKABURI?
Akanijibu kuwa: HAWAOGOPI MAKABURI, BALI WANAOGOPA KINACHOSABABISHA MAKABURI KUWEPO, YAANI KIFO. Hivyo wanafikiri kuyasogelea makaburi ni sawa na kukisogelea KIFO kwa makusudi.
NA HUU NDIO MTAZAMO WA BAADHI YETU TULIO WENGI
Wapendwa, makaburi yamekuwapo tangu mwanzo wa uwepo wa mwanadamu. Makuburi yameandaliwa na kutunzwa vyema na binadamu baada ya kuwa wamezikwa humo miili ya wapendwa wao.
Tunasoma Katika kitabu cha Mwanzo 23: 19-20, kuwa Abraham alinunua pango katika shamba la Makpela, na humo yakawa maziko ya watu ( Sarah, Abraham, Isaka, Yakobo, Lea, Raheli, nk). Eneo hili la makaburi liliendelea kutunzwa vizuri sana na watu wa wakati.
Kumekuwepo na Mila za kuyatumia makaburi kwa kufanya mambo ya hovyo na pia kuyahusishanisha na ushirikina kwa baadhi ya makabila ya kiAfrika. Hivyo Kila anayejishughulisha na makaburi anaonekana kuwa ni mtu wa Hovyo na mshirikina.
Kitabu Cha Muhubiri 7:2 kinasema kuwa “ Heri kwenda nyumbani mwa matanga kuliko kwenda nyumbani mwa karamu, maana huko ndiko mwisho wa binadamu wote na walio hai wataweka moyoni.”
Tunahimizwa kutembelea makaburi sababu ni swala la kusali.
Biblia inaendelea kutugundisha kuwa waliokufa sio adui zetu na wala sio mikosi kwetu tukiendelea kuwa karibu nao hata kwa kubeba masalia yao pale inapobidi, Yoshua 24:32 “mifupa ya Yosefu anazikwa Shekhem baadae ya waIsrael kusafiri nayo kutoka Misri. Eneo la Maziko linakuwa urithi wa Wana wa Yosef.”
Makaburi sio UCHURO ndugu zangu. Tunzeni maeneo yenu ya makaburi.
Kadiri ya maelekezo ya Mwenyezi Mungu kupitia kwa Nabii Elia, kutokuzikwa kaburini ni ishara ya kufa kifo kibaya (ukiwa mdhambi), Wafalme 9:33-44, “mdhambi mmoja anayeotwa Yezebel anakufa na mwili wake unaliwa na mbwa mitaani sababu ya wingi wa dhambi zake.”
Hivyo, kutokuzikwa baada ya kufa ni ishara ya laana, lakini waliozikwa vizuri ni ishara ya baraka.
Kuogopa makaburi ni sawa na kuogopa “kisichokuwepo.”
Kwa Kihaya uwa kuna methali inasema “kyakutinisa kita’kurwe”, jibu lake uwa ni “Mwilima.”
Tafsiri: “Kuna kitu kinakutisha lakini hakina nguvu ya kukula(kukuua),” na jibu lake ni “Giza.”
Kuogopa makaburi ni sawa na kuwa na “wasiwasi wa Bure” katika maisha, ni tatizo la AFYA YA AKILI. Tibu tatizo hili kwa kutunza vyema kumbukumbu za wapendwa wetu.
Wapendwa, shetani hakai makaburini, tukisoma Injili ya Mt. Marko 5:2-3, “Yesu baada ya kumtoa mapepo mtu aliyeishi makaburini akiwazuia watu wasiende makaburini, wale pepo walikimbilia baharini (sio makaburini).”
Tujifunze kwa Bwana wetu Yesu Kristo aliyekwenda makaburini kumfufua Lazaro (pamoja na kwamba dada yake Lazaro alimkataza Yesu kwenda makaburini, lakini Yesu alienda tu na Ufufuo ukafanyika).
Wapendwa tusisikilize kelele za wanaotuzuia/ kutucheka tunapokwenda makaburini kuyasafisha na kuwaombea waliolala huko, maana wote waliolala katika Kristo, watafufuliwa naye.
HITIMISHO
“Hata siku ya kwanza ya Juma, alfajiri na mapema, walikwenda kaburini wakiyachukua manukato waliyokuwa wameyatoa tayari,...” Luka 24: 1.
Wanawake watakatifu walienda”wakashuhudia UFUFUKO.
Makaburini.”  walimuona yesu mfufuka kwenye bustani za makaburi, hawakumuona shetani.
Tuwaombee waliolala makaburini waone uso wa Mungu.
Bwana awe nanyi nyote.
Pd. Mujuni Audiphace, Padri wa Jimbo Katoliki la
Bunda.

MWANZA

Na Paul Mabuga

Joep Lange [1954 – 2014], raia wa Uholanzi na Mtafiti aliyejikita katika tiba za virusi vya ukimwi, aliwahi kuhoji, iweje karibu kiila mahali katika bara la Afrika unaweza kupata bia ama soda ya baridi bila changamoto, lakini linapokuja suala la usambazaji na upatikanaji wa dawa, linakuwa tatizo la kuzungumzwa kila wakati.
Lange alifariki akiwa miongoni mwa abiria kwenye ndege shirika la ndege la Malaysia iliyoshambuluwa kwa bomu kutoka ardhini Julai 17, 2014, wakati akisafiri kutoka Amsterdam Uholanzi, kwenda Kuala Lumpur, Malaysia, kwenye kongamano la kila mwaka la UKIMWI.
Na huo ndio ukweli, kwamba  licha ya juhudi mbali mbali ambazo zimekuwa zikifanyika kwa miradi na mipango tofauti hapa nchini, lakini bado hilo limekuwa changamoto. Mathalani, wagonjwa wanaosumbuliwa na maradhi yasiyoambukiza, hususan kisukari na shinikizo la damu, wanaongezeka kutokana na mitindo yetu ya maisha, huduma zetu zinazidiwa na wingi wa watu, upatikanaji wa dawa kama inavyotakiwa unakuwa changamoto, umbali wa kufuata tiba nao unakuwa aghali, na uzingativu wa muda wa waganga kwa kila mgonjwa nao unakuwa mashakani. Lakini huko Zanzibar, kuna hatua imefikiwa
Mzee Omari Dadi Hamad, mkazi wa  Shehia ya Bopwe Wete, Pemba, katika umri wake wa miaka  65, pamoja na kuwa changamoto ya shinikizo la juu la damu, leo hii anaweza kupiga jembe na ardhi ikaitika. Ni katika shamba lake la miwa, ambayo ni mali ghafi katika kiwanda chake kidogo cha sharubati kinachotegemewa na familia yake ya watu tisa. Asingeweza kufanya haya kabla ya mwezi Aprili, mwaka jana.
Mzee Hamad amekuwa akisumbuliwa na shinikizo la juu la damu kwa miaka kumi sasa, hali ambayo hapo awali, kama ilivyo kwake na wenzake wanaosumbuliwa na magonjwa yasiyoambukiza, yaani shinikizo la damu la juu ama la chini la damu, na kisukari, imekuwa kikwazo kama changamoto ya kiafya na hata kiuchumi katika ustawi wao.
“Nilianza kujisikia kuchoka, nikitembea kidogo nachoka sana. Nikifika msikitini nahema, nashindwa kusali na ndipo nikashauriwa na mke wangu, Madhari upo katika hali hiyo  nenda hospitali kafanye vipimo. Nikaenda  nikapima sukari, nikapima presha na nikapima vingine, nikaambiwa ni presha [shinikizo la juu la damu], na kwa sababu hali haikuwa chronic sana, nikashailiwa kuanza dawa,” anasema Mzee Hamad katika mahojiano kwa ajili ya makala haya.
Anasema kuwa kuambiwa juu ya tatizo hilo, kulimkumbusha juu ya kisa cha marehemu kaka yake ambaye wakati anafanya kazi Kigamboni jijini Dar es salaam, zaidi ya miaka kumi iliyopita, alianguka ghafla na kupoteza na alipopelekwa hospitalini ilibainika kuwa alikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu, na  baadaye akapatwa na kiharusi.
“Kuanzia pale nilipopewa majibu kuwa nina presha , nikajua  afanaleikh, kumbe na mimi niliishaanza presha  na kuwa katika tishio la kuwa katika hali kama hiyo ya kaka yangu. Nikaanza dawa kidogo kidogo, lakini kwa sababu kulikuwa na usumbufu kidogo katika upatikanaji wa dawa. Uende hospitali ukaandkiwe dawa,ukienda dirishani hakuna.unaambiwa ukanunue.  Basi  ukimeza tembe mbili, unaweza kukaa hata wiki nzima humezi tena,” anasimulia Mzee Hamad.
Kulingana na simulizi ya Mzee Hamad, ukiacha changamoto hiyo ya upatikanaji wa dawa kama inavyotakiwa miongoni mwa wagonjwa wa shinikizo la damu na kisukari, lakini pia wingi wa wagonjwa katika vituo vya huduma uliosababisha yeye na wenzake kuchukua muda mrefu kwenye mistari kabla ya kupata huduma na hata kufuata huduma hizo mbali zaidi.
“Dokta akahangaika, akaniambia  wende Makunduchi [hospitali ya wilaya kwa ajili ya rufaa], mmh, wende wapi? Makunduchi sikai, Makunduchi, Upo! Sasa tulivyokwenda kule. Hapana hehee! Swalaa hiyo [Niliondoka alfajiri wakati wa adhana]. Natafuta gari kwa pesa [nauli] mpaka wap:?
Makunduchi! Makunduchi nateremka nenda hotel, hotel [Kula na baadaye napata matibabu] mpaka narudi kwetu saa nane au saa tisa, Upo! Yanakuijia [unaelewa]!” Anasimulia  Bibi Nali Kombo, mwenye umri wa miaka zaidi ya 70  na mkazi wa Mtende, Unguja, ikiwa ni uzoefu wake kuhusu matibabu kwa magonjwa yasiyoambukiza.
Hali hii ya huduma pia ilikuwa ni changamoto hata  kwa watoa huduma kama Dk. Fatmah Mohamed Amour, Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya cha Jadida, Pemba, anavyosema, “ licha ya kuwepo wagonjwa wengi lakini pia utunzaji kumbukumbu  ulikuwa tatizo kutuwezesha kufuatilia wagonjwa.
Pia, wagonjwa wengine wa kisukari walikuwa wanashindwa kuvumilia kusubiria vipimo, hivyo wanakwenda kula na kutufanya tusipate vipimo sahihi ambavyo vinahitaji sampuli kuchukuliwa kabla ya kula chochote.”
Kutokana na changamoto hizi ambazo zilitokana na ingezeko la wagonjwa wa kisukari na presha, Mraribu Msaidizi wa Kitengo cha Magonjwa Yasiyoambukiza Zuhura Saleh Amour, anasema Wizara ya Afya Zanzibar  kwa ushirikiano na PharmAccess na udhamini wa Sanofi, Aprili 2023, walianzishwa mradi wa huduma  kwa wagonjwa  wanaosumbuliwa na maradhi yasiyombukiza katika ngazi ya jamii.
Anasema kwamba chini ya mradi, zahanati zinawasaidia wagonjwa wanaotoka eneo moja kuunda  vikundi vya kijamii katika makazi yao na kupata huduma ya matibabu na dawa wanazopelekewa na muuguzi kila mwezi bila kuhitajika kwenda mbali.
Pia kuna wahudumu wa ngazi ya jamii katika kila kikundi ambao wamepata mafunzo ya kuchukua vipimo muhimu kuangalia mwenendo wa afya za wagonjwa kwa karibu na kuwashauri. Vipimo hivi huingizwa katika mfumo wa kidigitali, ambao unamwezesha daktari kufuatilia wagonjwa wote ambao wamepimwa katika siku husika. Pamoja na kuchukua vipimo, wahudumu wa ngazi ya jamii wamepewa mafunzo ya kutoa elimu ya namna bora ya kuishi na magonjwa yasiyoambukiza
“Kwa sasa, tunapata huduma kama inavyotakikana, dawa tunapata, siku ya kliniki, wauguzi  wanakuja kwenye jamii yetu. Wahudumu nao wanatupima na kutufuatililia. Sasa tunaweza kufanya hata kazi zetu,’’ anasema Mzee Hamad  baada ya kuanza kunufaika na kupitia mradi huo , wakati, Bibi Nali anashuhudia, “Dawa tunapata na maungoni zinaingia, na afya zinatengemaa. Hili begi hili [analioesha], ni la madawa.”
Nyendo Hassan Haji mkazi wa Mtende, Makunduchi na mnufaika wa mradi huu anasema umekuwa na manufaa anasema maana kabla yake walikuwa kama wananyanyasika  vile kwani “Ilikuwa usumbufu sana. Unafika kule unakuta watu wametia mabuku yao [daftari za kumbukumbu ya matibabu kwa wagonjwa], ukitaka kuweka lako wanakuambia, wenzako wamewahi, ilikuwa usumbufu mpaka wengine walikuwa wanaona heri wabaki nyumbani wajifie basi!”
Hawa ni miongoni mwa wananchi zaidi ya 800 wanaosumbuliwa na maradhi ya kisukari na sdhinikizo la damu, ambao wapo katika vikundi 25, ambavyo vimefikiwa na huduma chini ya mradi huo, na wanafikiwa kila mwezi katika vikundi vyao vilivyopo mahala wanakoishi na kupatikiwa huduma za dawa na matibabu.
Mganga Mfawidhi katika Kituo cha Jongowe Tumbatu, Dk Tumaini Zaidu    anasema kuwa kutokana na mradi huo, hata uhusiano wao na  wagonjwa umeimarika, kumbukumbu zimekuwa sawa, kazi imekuwa rahisi, na ufanisi umeongezeka na hata wamepungukiwa na wagonjwa kwa kuwa wengi wanapata huduma katika vikundi vya kijamii  katika mitaa yao, na kwamba wanaofika kwao ni wale ambao wanachangamoto za kirufaa. “kwa hawa ambao wanalazimika kuja hapa kliniki, tunapata muda wa kutosha wa kuwasikiliza matatizo yao, mienendo yao ya kimaisha na muda wa kutosha kuwapa elimu ya namna nzuri ya kuishi na magonjwa haya.
Meneja wa Programu wa Pharmaccess Zanzibar, Faiza Abbas, anasema katika kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar, kuwa taasisi yao iliona kuna haja ya kuwa na program bunifu, na kwa msaada wa teknolojia, ambao itaondoa matatizo katika utoaji huduma ili kupunguza tatizo la msongamano wa wagonjwa wa maradhi yasiyoambukiza katika vituo vya huduma, lakini pia kuboresha huduma kwa wagonjwa.
Katika moja ya  matumizi ya teknolojia, vipimo vya kila  mgonjwa kwenye vikundi huchukuliwa na kutumwa kwenye kituo cha mawasiliano ya afya, ambapo madaktari na wataalam wengine huwa na utaratibu wa kufuatilia mienendo ya wagonjwa hao, na kuwatambua wale wenye changamoto na kuwasiliana nao kwa hatua zaidi za kitabibu.
“Mimi mwenyewe binafsi mwanzo sikuwa sanasana na tamaa kama tunaweza kufika hatua hii. Lakini baada ya kwenda kuangalia, sasa nimeona kwa muda mfupi tumepata mafanikio makubwa sana. Baada ya kufanya evaluation tumegundua  kuwa mafanikio ni makubwa sana,” anasema Nassor Ahmed Mazrui, Waziri wa Afya, Zanzibar, na kuongeza, ‘’ PharmAccess wametusaidia sana kwa mambo mengi na  mafanikio haya ni lazima kuyafikisha katika wilaya zote, na manufaa ya mradi lazima yaendelezwa hata baada ya mfadhili kumaliza muda wake.”
Kwa Mzee Hamad, mafanikio katika mradi huu ni jambo muhimu katika maisha yao, kwani anasema, “Walahi mie nasema Mungu ajalie hawa wenye kuonesha mpango huu. Awape nguvu, awape kila hali uendelee na utanuke zaidi uwafikie wagonjwa wengi zaidi, kwa sababu bado wapo.”

DAR ES SALAAM

Na Joyce Sudi

Kitunguu saumu ni moja ya kiungo chenye ufanisi  mkubwa mwilini katika kuboresha afya ya mwili, Kiungo hiki huwa ni sehemu ya vyakula mbalimbali tunavyokula kila siku, vikiwemo vile vinavyoliwa vibichi kama vile kachumbari na saladi, pamoja na vyakula vilivyookwa au kuchemshwa.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Nchini Tanazania {TFN}, kitunguu saumu kina viondoa sumu {antioxidant} ambazo huondoa alkali huru {freeradicals} katika mwili, na hivyo kusaidia kuzuia uharibifu wa sumu hizo mwilini, na pia kina vitamini na madini mengi kwa afya ya mwili, ambayo ni madini ya manganese, calcium, phosphorus, selenium na vitamin B6 na C.
Kitunguu saumu ni moja wapo ya viungo ambavyo mara nyingi hutumika kuongeza ladha katika chakula, ambapo vipo vitunguu saumu vya rangi nyeupe ambavyo huwa na tumba kubwa chache, lakini vipo vyenye rangi ya zambarau au pinki, ambavyo huwa na tumba ndogo na nyingi, ingawa vitunguu hivyo vyote vina ubora sawa.
Licha ya kitunguu saumu kuwa maarufu kutumika kama kiungo, lakini pia hufaa kutumika kusaidia katika matatizo mbalimbali ya kiafya, kama vile kuzuia maambukizi yatokanayo na bakteria, baadhi ya virusi na fangasi, hasa katika utumbo, mapafu na sehemu za ukeni.
Vilevile husaidia katika uyeyushaji wa chakula, kuzuia kuhara na maambukizi yatokanayo na fangasi kwenye kinywa kutokana na viambata vinavyopatikana kwenye vitunguu saumu ambavyo ni; Allicin, Vitamini C, Vitamin B6 na Manganese.
Nini husababisha harufu kali mdomoni baada ya kula kitunguu saumu?
Watu wengi wamekuwa wakisumbuliwa na swali hili, kwamba pamoja na virutubisho na madini muhimu yaliyopo kwenye kitunguu saumu, lakini inakuwa ngumu kutafuna kwa kuhofia harufu kali.
Ukweli ni kwamba pale unapotafuna kitunguu saumu,kemikali za kibaiolojia zilizopo kwenye mfumo wa chakula kwa ajili ya kuvunjwa vunjwa kwa chakula kiweze  kufyonzwa vizuri, hubadilisha kiambata kilichopo kwenye kiungo hicho kiitwacho Allin kuwa Allicin na kisha kuvunjwa zaidi kuwa Ally Methyl sulfide, na hivyo kusababisha harufu kali  ambapo njia  rahisi ya kuepusha harufu hii, ni kunywa maziwa (fresh)yasiyoganda ya ng’ombe.
Taasisi ya Chakula na Lishe Nchini Tanzania {TFN}, imetuandalia  namna ya  kuandaa kitunguu saumu kwa ajili ya kusaidia kutuliza vidonda vya kooni kwa watu wenye maambukizi ya  Virusi vya Ukimwi {H.I.V}.
Mahitaji:
Kitunguu saumu tumba 4, maji kikombe kimoja, na sukari au asali.
Namna ya kuandaa:
i.Menya  maganda kwa kisu na katakata kitunguu saumu.
ii. Tia  kwenye maji yanayochemka, acha kichemke kwa dakika 10.
iii. Ipua, funika na acha ipoe, Kisha ongeza asali au sukari kwa ajili ya ladha.
Matumizi:
Kunywa kikombe kimoja kutwa mara tatu.
Pia kitunguu saumu kinaweza kutumika kama dawa ya kikohozi
Namna ya kuandaa:
i. Ponda kitunguu saumu kilichomenywa maganda .
ii. Weka kwenye kijiko cha chai, chukua kijiko cha chai cha asali au sukari.
Tumia mara mbili kwa siku kwa kikohozi.
Angalizo:
Matumizi ya vitunguu saumu yanaweza kuingiliana na ufanyaji kazi wa dawa mbalimbali za hospital, hivyo hakikisha unamuuliza daktari wako kama hujaanza kutumia kitunguu saumu kama dawa. Pia kwa wale wenye presha usitumie, kwanza pata ushauri wa daktari.
Dawa hizo ni kama Isoniazid ambazo zinatumika kutibu maradhi ya kifua kikuu, cyclosporine, dawa hizi hutumika kwa waliopandikizwa kiungo mfano figo, Dawa za H.I.V. ambapo  kitunguu saumu kinaingiliana na ufyonzaji wa dawa hizi, na hivyo kupelekea dawa kutokufanya kazi.
Pia, Nonsteroidal anti-inflamatory drugs {NSAIDs], dawa hizi ni kama ibrufen, na Naproxen ambazo zikitumiwa pamoja na kitunguu saumu, huongeza kuvuja kwa damu.

DAR ES SALAAAM

Na Dk. Felician B. Kilahama

Mungu Mwenyezi alituumba binadamu kwa ‘sura na mfano wake’ (Kitabu cha Mwanzo, 1:26); akatuweka duniani na kutupa madaraka ya kumiliki na kutawala vyote alivyoviumba.
Akisema: binadamu “wakatawale samaki baharini, ndege angani, wanyama, nchi yote vile vile, kila kiumbe kitambaacho juu ya nchi.” Vile vile, Mungu akahitimisha uumbaji akiwaagiza mwanamume na mwanamke: “zaeni mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuimiliki”.
Tangu kuumbwa Adamu na Eva/Hawa, ni miaka mingi imepita. Hata hivyo, takwimu zinaashiria kuongezeka idadi ya watu duniani, ikiwa takriban bilioni nane (8), hii leo.
Hiyo ni ishara kuwa dunia inazidi kujaa watu wakati mataifa kama ‘China’ na ‘India’ yakiongoza kwa takriban asilimia 40 ya idadi ya watu wote. Tanzania yenye ardhi kubwa (hekta 94.55 milioni), kwa takwimu za 2022, kuna watu 61,741,120.
Kwa uwiano wa ukubwa wa nchi, bado tunatakiwa kuzaa na kuijaza nchi. Tunatumiaje ‘vipawa’ tulivyopewa na Mungu Mwenyezi? Vijana vipaumbele vyenu ni nini kama siyo kwanza kuwa baba hodari wa familia bora na yenye kumcha Mungu. Je, vijana wetu wamekengeushwa na nini: utandawazi, mifumo-dijitali na kuiga yasiyofaa, au ni mifumo kijamii na kiutawala?
Hakuna shaka mataifa yaliyoendelea hayajali chochote wanafanya kulingana na matakwa yao, kwenda kinyume na agizo la Mungu wakichochea maovu, mfano, kuhamasisha ndoa kati ya mwanaume na mwanaume (ushoga); mwanamke na mwanamke (ulezibiani), ikiwemo kutunga Sheria ‘kuharibu na/au kutoa mimba, na kuchochea wanawake wasipate ujauzito’.
Masuala hayo ni machukizo kwa Mungu aliyetuumba, akatujalia neema tuzae na kuongezeka. Wakati nikiwa mdogo, nilikuwa nasikia watu vijijini wakisema, “kuzaa watoto wengi ni baraka” familia zilikuwa zinafurahia kuzaa watoto na kuishi kwa uelewano mkubwa kama jamii moja. Nyakati hizi hali imekuwa tofauti kiasi cha ‘vijana’ kuoa na kuzaa watoto ni dhiki kubwa au kama ni laana, wakati ni baraka/zawadi kwa familia.
Maisha ya babu/bibi zetu yalikuwa yameegamia kwenye misingi/mifumo ya kijadi, kiutamaduni wakiabudu miungu mingine (ingawa walifahamu yupo Mungu Muumbaji. Mtazamo huo hautofautiani na ilivyoandikwa katika Matendo ya Mitume kwamba Mtume Paulo wakati akipita huku na huko akiwa ‘Athene’ akaona ‘Madhabahu’ iliyoandikwa: “Kwa Mungu Asiyejulikana”.
Ikawa baada ya kuyaona hayo, akawahubiria habari njema kuhusu huyo Mungu wanayemwabudu bila kumjua (Mdo, 17:23). Hivyo na wahenga wengi wa kale yalifanya hivyo hadi Injili ilipowafikia, takribani miaka 100 iliyopita.
Tukumbuke kuwa maisha yetu yamejengwa kwenye misingi ya mifumo ya kiroho ,ambayo Mungu aliiweka kimpangilio. Hivyo vijana wetu wanapaswa kufahamu kuwa kukiuka kuyatekeleza maagizo ya Mungu; mafanikio yatakuwa haba kwa kukosa maarifa yatokayo kwa Mungu.
Kilichonisukuma kuyasema hayo ni hali ya vijana wetu hususan wa kiume; kujisahau kuwa wao ni wanaume wanaotegemewa kujenga familia zilizo bora na endelevu. Nimekuwa nikisia msemo “dunia inawayawaya” ukimaanisha binadamu kukosa utulivu/umakini kwa kuhangaika huku na huko mpaka kupayapaya bila kujua mustakabali wa maisha kwa ujumla.
Ukitafakari hali hiyo kwa umakini mkubwa, utagundua kuwa hali ya sasa tunayoishuhudia kwa vijana wetu wa kiume, hakika ni matokeo ya kuhangaika kidunia zaidi, kuliko kusimama imara kwa msingi na maagizo ya Mungu Mwenyezi.
Moja ya athari kubwa kwa vijana Tanzania; ni ‘unywaji pombe’ uliokithiri. Kawaida Watanzania wengi vijijini/mijini wapo wanaokunywa pombe aina mbalimbali. Wakati nikiwa kijana kabla na baada ya kuanza shule; nilikuwa naona wanaokunywa pombe walikuwa watu wazima (wenye familia), hakuna kijana aliyekuwa hajaoa angeweza kuruhusiwa kujumuika nao.
Hata kama angekuwa ameoa, lakini bado hajawa na uzoefu wa kutosha kimaisha, haikuwa rahisi ajumuike na watu wazima. Mifumo kijadi au kimila ilikuwa imezuia vijana kutojitosa kwenye unywaji pombe bila ya kujijengea msingi imara wa kuweza kuyamudu maisha yake na familia.
Nyakati hizi maisha ni kidijitali, kisiasa, kisaikolojia, kiteknolojia, kimaendeleo hadi kusema kila mtu yuko huru kufanya anavyotaka ili mradi amefikisha umri wa miaka 18 au zaidi. Hali hiyo inakinzana na Sheria, Kanuni pamoja na Mifumo ya Kiroho aliyoiweka Mungu. Kadhalika, Serikali kwa dhamira ya kupata mapato zaidi, ikapunguza bei ya pombe.
Kimsingi, mapato ya Serikali yanapoongezeka, kwa namna moja au nyingine, tunatarajia huduma za kijamii kuboreshwa na kuimarisha miundombinu kwa maendeleo endelevu. Kuna pombe ambazo vijana wanachangamkia, mfano, “sungura” na “konyagi.” kadhalika, usambazaji pombe kwa kutumia vifungashio vyenye ujazo mdogo mdogo, unahamasisha vijana wengi wanywe pombe zaidi kwa bei poa.
Kuwepo vyanzo vya mapato kwa Serikali hasa ambavyo haviumizi walipa kodi na wananchi kwa ujumla ni jambo jema; lakini tunapotafakari suala la unywaji pombe ee-vijana wengi wanaathirika sana kwa kiwango cha taifa kuelekea pabaya.  Mbali na pombe, changamoto nyingine ni “dawa za kulevya”; zikiwa kama ‘pacha’ wa pombe, kwa kutumiwa na vijana wengi.
Uzoefu unaonyesha kuwa kijana akishazoea dawa zinazolewesha, kuacha inakuwa kizaazaa. Kuna wakati Serikali ilijitahidi kudhibiti kwa kiasi kukubwa, matumizi ya dawa zinazolewesha kwa kuhakikisha haziingizwi nchi hovyo.
Hata hivyo, “operesheni iliyofanywa na Mamlaka ya Kuzuia na Kudhibiti Dawa za kulevya; iliyofanyika kati ya Agosti 24 na Septemba 2, 2024”; imedhihirisha kuwa sasa-upo udhaifu mkubwa katika mifumo husika ya kudhibiti uagizaji na uingizaji dawa zinazolewesha. Ripoti iliyotolewa na Mamlaka Septemba 10, ilionyesha kuwa kiasi kikubwa cha dawa hizo zilizoingizwa nchini, zikamatiwa Manispaa za Kinondoni na Ubungo kwa kuwanasa watuhumiwa kadhaa.
Swali linabaki. Je, dawa hizo zimepitia wapi bila kugundulika mpaka zikawa mitaani kiasi-hicho? Kadhalika, matumizi ya “bangi” (Cannabis sativa) pia yamekuwa yakiongezeka kila kukicha. Je, tunakwama wapi hadi taifa kushindwa kudhibiti matumizi ya dawa zinazolevya?
Tujitathimini kwa kina miaka michache ijayo nguvukazi nchini itakuwa ya namna gani Iwapo vijana wengi wa umri kati ya miaka 20 hadi 40 inakuwa katika hali hii isiyoridhisha, na huenda vijana wanaoinukia nao wakatumbukia kwenye janga hili. Nini hatima ya Tanzania? Kwanza, viongozi wajao watakuwa wa namna gani, wenye mwelekeo gani je, watakuwa na maarifa gani?
Je, Vijana wataishi maisha ya namna gani kama mwelekeo wao kwa sasa ni kunywa/kulewa kupindukia? Agosti, 2024 mtaa mmoja Jijini-Kati Dar-es-Salaam, karibu na Posta ya Zamani, niliona vijana wanne wamejibanza mahali akiwepo binti mmoja.
Kwa kuwa nilikwa nikitembea kwa miguu, nikapunguza mwenda taratibu kuona nini kinachoendelea. Nilichokishuhudia walikuwa wakinywa, lakini kwa kutunia chupa moja wakipokezana. Vile vile, walikuwa wanavuta kitu kama sigara pia kwa kupokezana: niliduwaa kwa hali niliyoiona bila kuwakaribia.
Mbele yangu alikuwa mama, mtu-mzima akielekea nilikokuwa natoka; baada ya kusalimiana. Nikamuuliza hiyo ni ishara gani kwa vijana wetu. Mama alisema hiyo ndiyo ‘hali halisi’ kwa vijana wa Tanzania. Tukaishia kusema: “Mwenyezi Mungu uwarehemu vijana hawa na wengine wa aina hiyo, maana wanaangamia kwa kukosa maarifa (akili zao zimepinda)”.
Tutamwomba Mungu, lakini kwa utashi aliotupa kuweza kufanya uchaguzi sahihi, mathalani, ufanye nini, ule nini, unywe nini, uvaeje au uishi maisha gani! Hivyo, inabidi tuwajibike kwa maisha tunayoishi. Dunia moja, ‘binadamu wote sawa’ lakini tunatofautiana katika uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kuishi, vizuri bila kukengeuka hadi kupoteza ‘afya ya akili’ zetu.
Vijana kutumbukia kwenye unvwaji pombe na matumizi dawa zinazolevya, Mungu hahusiki hata kidogo, maana Mungu anatupenda na anatuwazia mema, pia huzibariki kazi za mikono yetu. Kadhalika, ili tubarikiwe, lazima ‘vigezo na masharti’kuzingatiwa ipasvyo. Kinyume cha hapo, ni laana mpaka huruma ya Mungu ipatikane kupitia toba ya kweli; pia kwa kufunga vile vile kuomba bila kukata-tamaa.
Ombi langu kwa Serikali, unywaji ‘pombe kupindukia’ ikiwemo ‘dawa-zinazolevya,’ hatua madhubuti zichukuliwe kwa kupandisha bei za ‘vileo’ vyote, pia kuhakikisha dawa-zinazolevya, zinadhibitiwa kwa hali ya juu sana kwa dhamira njema ili kuokoa nguvukazi ya taifa.
Vile vile, atakaye thibitishwa Kisheria kufanya biashara haramu, adhabukali zichukue mkondo wake bila kuoneana haya wala huruma, ili tusiendelee kuliangamiza taifa kwa maslahi binafsi. Taifa bora linahitaji ‘vijana’ imara, wenye nguvu, afya na akili timamu pamoja na maarifa ya kimbingu.
Kumbuka ‘kumcha Mungu’ ndiyo chanzo cha maarifa, na taifa lenye hofu ya Mungu hutenda haki kwa wote na kuuchukia ‘uovu’ kwa sababu ‘uovu’ ni janga kwa taifa, husababisha watu walaaniwe. Hivyo, tuwe makini tujiepushe na hali hiyo.

MWANZA

Na Paul Mabuga

Maureen Mwanawasa, Mke wa Rais wa zamani wa Zambia, Levy Mwanawasa [2002 – 2008], amefariki  Agost 13, 2024, jijini Lusaka nchini humo baada ya kuugua kwa muda mfupi. Kama ulipata nafasi ya kumfahamu, bila shaka utajiuliza kwa nini akina mama huku kwetu wanashindwa kuwashawishi wanaume wanne wao kwenda kanisani hasa baada ya kuonekana mahudhurio yao ni hafifu na yenye kulalamikiwa.
Fikiria mama wa ‘kibongo’ anaweza kumshawishi mume wake, kulipia hadi shilingi elfu 30 ama hata hamsini, kwa ajili ya kusuka nywele ili apendeze, ama anunulie gauni la mtoko la hadi shilingi 60,000/- na kumsaidia marejesho ya mikopo ya kausha damu, lakini anashindwa kumbembeleza mwanaume ahudhurie kanisani, jambo ambalo hata hivyo haligharimu fedha yoyote.
Safari yangu ya kukutana na Maureen Mwanawasa ilianzia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Keneth Kaunda jijini Lusaka, ambapo wakati natoka nje  nikiwa miongoni mwa wageni waliowasili, nilipokelewa na mzee mmoja raia wa Tanzania. Nilishangaa baada ya kuwa licha ya mzee huyo kunizidi umri, lakini alipokea begi langu   ambalo lilikuwa mzigo wangu pekee, na kunielekeza kwenye gari ndogo tukielekea katikati ya jiji la Lusaka. Juhudi zangu za kukataa mzee huyu kunibebea mzigo ili kulinda mila za Kiafrika, zilizogonga mwamba.
Hapo safari ikawa moja kwa moja hadi katika hoteli ya Pamodzi [yaani pamoja] ambayo baadaye niliambiwa kuna Marais na Wakuu wa Nchi 14 wanalala hapo, na ndiyo maana ulinzi ulikuwa mkali. Nikajisemea kimya kimya, itakuwaje siye kwa mazoea ya kabila letu kwamba ukinywa hata kabia kamoja, unaanza kuimba. Lakini kwa bahati, mratibu wa mambo akaniambia, “Bwana mdogo twende huku.’’ Nikapelekwa hoteli nyungine jirani ambayo nayo ilikuwa kubwa. Hii ilikuwa ni Agosti 15, 2007.
Jioni hiyo kukawa na zoezi ambapo watu wote waliokuwa wanatarajia kuingia katika vikao vya Marais na wakuu wa Nchi katika Jumuiya ya Nchi zilizo Kusini mwa Afrika [SADC], walitakiwa kufika katika kituo maalum, ambapo baada ya kuhakikiwa, walipigwa picha na kupewa Kitambulisho maalum. Hakuna aliyekuwa akiachwa kwenye hatua hii, isipokuwa mabwana wakubwa.
Wakati nimefikia hatua ya kupigwa picha, akaingia mama mmoja aliyevaa kitamaduni, na baadaye nikabaini kuwa ni mmoja wa wafanyakazi katika Ikulu wa King Mswati lll wa Eswatini. Kwa heshima yake na kwamba anatoka katika familia ya kifalme, jambo ambalo inaelekea Wazambia wanalijali, nikaambiwa nimpishe ahudumiwe kwanza yeye. Nikafanya hivyo, na mimi baadaye nikapata kitambulisho changu.
Asubuhi wakati nakwenda kwenye mkutano, ile naingia geti la kwanza, nikakutana na askari ambaye baada ya kutambua kuwa ninatoka Tanzania, akanionesha kitambulisho cha mmoja wa Mawaziri wa  huku kwetu ambacho kumeokotwa. Akaniuliza, unamjua huyu na mimi nikamwambia, naam namjua ni mmoja wa mawaziri wetu, na akanionya, mtafute umpe hiki kitambulisho, vinginevyo hataingia humo ndani. Niliifanya kazi hiyo na baadaye kumkabidhi kitambulisho chake.
Wakati wa mapumziko, nilifanikuwa kuwa karibu na aliyekuwa Rais wa Namibia, Hifikipunye Pohamba, jamaa mrefu hivi, baada ya kumsalimia kwa Kiingereza na kuonesha nia ya kufanya naye mahojiano, aliinama na kusoma kutambulisho changu ambacho kilikuwa kikionesha pia ninatoka nchi gani. Baada ya kugundua ninakotoka akabadili lugha na kuniambia kwa Kiswahili, “habari za Dar es salaam, vipi Buguruni, mambo poa” Wakati naendelea kutafakari hatua ya kufuata, akaanza kuondoka na kuniaga. “Haya bwana, kazi njema!”
Jioni wakati wa mpango wa kazi, nikaitwa na mkuu wangu, nakwambiwa kuwa siku inayofuata, nitaambatana na wake wa Marais na Wakuu wa Nchi ambao watakuwa katika ziara wakiongozwa na mwenyeji wao, Mke wa Rais wa Zambia Maureen Mwanawasa. Siku hiyo ilipofika, tulianza ziara tukiwa katika mabasi mawili, moja likiwa la hao akina Mama Waheshimiwa na jingine la watu waliokuwa  kwenye kazi mbali mbali, tukiwemo wanahabari wachache.
Tulipomaliza ziara iliyochukua hadi muda wa mchana, tulirudi katika hoteli ya Pamodzi, ambapo kulikuwa na maonesho ya bidhaa mbali mbali  zinazozalishwa na wanawake nchini humo, ikiwa ni pamoija na vito. Mama Maureen hakusita kuwaambia kwa lugha yao akina mama wale, wafanye biashara, kwani hao waliowatembelea ni wake wa Marais. Nilitafsisriwa hicho alichokisema na mwandishi wa gazeti moja la nchini humo.
Baada ya ziara hiyo, akina mama hao wakawa na kikao chao, Mama Maureen Mwanawasa ambaye alikuwa Mwenyekiti wao, alisimama na kuwaambia juu ya ajenda muhimu, iliyohusu azimio lao la kutaka  wanawake kupewa nafasi ya madaraka katika kile kinachojulikana kama hamsini kwa hamsini, yaani kama mkakati wa kijinsia wanawake wapewe nafasi katika ngazi mbali mbali katika kiwango cha uwiano sawa na wanaume.
Cha kufurahisha ni kwamba aliwaambia kesho yake watawasilisha hoja, na kwamba kila mmoja aitangulize hoja hiyo kwa mwenzi wake. Na inawezekana kila mmoja aliwasilisha hoja hiyo, maana ilipowasilishwa  na Mama Maureen Mwanawasa siku iliyofuata mbele ya  Wakuu wa Nchi, hakukuwa na mjadala bali Viongozi hao  walipiga makofi kama ishara ya kuiunga mkono, na ikapita, na kuanzia hapo imekuwa ajenda ya kudumu katika Nchi hizo.
Ukiacha hilo, lakini Maureen Mwanawasa amekuwa na ushawishi mkubwa katika mambo mbali mbali enzi ya uhai wake, ikiwa ni pamoja na harakati ya kupambana na umaskini, na pia akiongoza Wake wa Marais na Wakuu wa Nchi katika Jumuiya ya SADC katika kupambana na madhira ya UKIMWI na Virus vya UKIMWI.
Ni Mwanamke ambaye alitumia nguvu ya ushawishi wake katika kupeleka ajenda. Anasifika pia katika kuendesha kampeni za kisiasa kupigania ushindi wa mume wake katika chaguzi.
Maureen alizaliwa April 28. Mwaka 1963 katika eneo la Kabwe nchini Zambia. Aliolewa na Mwanasheria Levy Mwanawasa Mei 07, 1987. Mumewe alifariki mwaka 2008 akiwa madarakani, na Mwenyezi Mungu aliwajalia  watoto wanne, ambapo watatu ni wa kike na mmoja ni wa kiume.
Kwa njia ya ushawishi wa akina mama kwenye hamsini kwa hamsini, dada zetu, shemeji zetu, shangazi na mama zetu wanashindwaje kuwashawishi wanaume kushiriki kwenda kanisani? Kwa nini nguvu hii ambayo haihitaji rasilimali fedha, haitumiki kupunguza changamoto hii, ambayo inaelekea kuwa sugu?
Kuna wakati ukihudhuria kanisani, unakuta uwiano ni wanawake kuwa theluthi mbili na wanaume theluthi moja. Unakaa kwenye jumuia unakuta ni wanawake na watoto, labda na mwanume mmoja. Kama akina mama wanaweza kuzengea fedha ya kucha, nywele na marejesho wanashindwaje kuwashawishi wanaume kwende kanisani?

TAFAKARI SOMO LA INJILI DOMINIKA YA 19

Amani na Salama!
“Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye, hataona kiu kamwe.” Haya ndiyo maneno ya hitimisho la somo la Injili ya Dominika iliyopita. Yesu anajitambulisha kwa wasikilizaji wake kwa namna ambayo iliwakwaza, ni maneno yaliyoweka imani yao njia panda, na hapa ndipo tunaona wasikilizaji wake ambao Mwinjili anawatambulisha kama “Wayahudi,” walimnung’unikia Yesu kutokana na maneno hayo.
Wayahudi waliamini kuwa na ukweli wote, na ndiyo Torati na Manabii. “Atamlisha mkate wa ufahamu, na kumnywesha maji ya hekima.” (Yoshua bin Sira, 15:3) Hivyo, ndiyo kusema kuwa mkate wa uzima ni Neno la Mungu ambalo Wayahudi waliamini kuwa nalo katika ukamilifu wake, ndiyo Torati na Manabii na Vitabu vingine vya Maandiko Matakatifu.
Kwao ilikuwa ni makwazo makubwa, kwani Yesu leo anajitambulisha kuwa ni Yeye aliye mkate wa uzima wa milele utokao mbinguni, ni kwa kulisikiliza na kulishika Neno lake, kila mwenye njaa na kiu atashibishwa, na hivyo hataona njaa wala kiu tena.
Wayahudi walishindwa kuupokea utambulisho wa Yesu kama chakula cha uzima, na wakabaki kumwona kama mwana wa Yusufu tu, na tena waliyemfahamu vyema hata kazi na ujira wake kuwa ni ule duni kabisa, na zaidi sana hata mama yake pia walimfahamu. Ni watu waliomfahamu vyema na vizuri, na kwa nini basi anajitambulisha na kujifananisha kuwa ni Mungu, ni kutoka mbinguni?
“Wakasema, huyu siye Yesu, mwana wa Yusufu, ambaye twamjua babaye na mamaye? Sasa asemaje huyu, ameshuka kutoka mbinguni?” Na tunasikia manung’uniko haya hawakumwelekezea Yesu, bali yalikuwepo baina yao, miongoni mwao, kati yao wenyewe.
Kunung’unika siyo kitendo kile cha kulalamika tu. Naomba kieleweke, na Mwinjili anakitumia kitenzi hicho kuonesha mkwamo wao wa kiimani, kukwazika na kujikwaa kwao kwa fundisho lenye utambulisho mpya kumhusu Yesu, utambulisho ambao unamfunua Yesu kuwa si tu mwanadamu kweli, bali pia ni Mungu kweli, ametoka kwa Mungu, amekuja kuifunua katika ukamilifu sura halisi ya Mungu. Kwao haikuwa jambo rahisi na lenye kueleweka kuwa kwa njia ya Yesu, hekima ya Mungu imejimwilisha na kukaa kati yao, na kuwa katikati yao. Soma zaidi Tumaini Letu.

Amani na Salama! Tumekuwa tukisoma na kutafakari Injili ya Marko, leo Liturjia inatualika kugeukia Injili ya Yohane na hasa sura ile maarufu ya sita, juu ya Yesu kama chakula cha uzima. Mwaka B wa Kiliturjia wa Kanisa kwa kawaida tunasoma Injili ya Marko, lakini Liturjia ya Mama Kanisa ameingiza pia Injili ya Yohane sura ile ya sita kwa Dominika tano mfululizo. Injili ya Marko inatupa masimulizi mawili juu ya muujiza wa Yesu kulisha makutano mikate. Na ndipo tunaona kwa jinsi anavyotoa mkazo na msisitizo huo, hapo Mama Kanisa ameona ili kupata mafundisho ya kina hatuna budi kugeukia sura ya sita ya Injili ya Yohane. Leo tunasikia juu ya muujiza ule wa kugawa mikate kwa watu wengi, na baadaye zaidi katika dominika zijazo tutasikia juu ya mafundisho ya Yesu mkate wa uzima, aliyoyatoa akiwa katika sinagogi la Kapernaumu.
Ni vema ili kupata ujumbe kusudiwa wa Mwinjili Yohane, badala ya kuwahi kuhitimisha juu ya fundisho la Yesu la Ekaristi Takatifu, ambalo kwa kweli linagusiwa sio mwanzoni mwa sura ile ya sita bali mwishoni kabisa, hivyo niwaalike kusoma na kubaki na kile ambacho kipo mbele yetu ili kukwepa kupotoka au kupata maana inayokuwa siyo ile inayokusudiwa na Mwinjili.
Kati ya miujiza iliyofanywa na Bwana wetu Yesu Kristo, ni muujiza huu wa kugawa mikate unaosimuliwa mara nyingi zaidi na Wainjili wote wanne. Wainjili wote haidhuru mara moja wanatupa masimulizi ya muujiza huu, na Wainjili Matayo na Marko wanasimulia mara mbili juu ya muujiza huu, hivyo kufanya masimulizi juu ya kugawa mikate kuwa sita.
Na ndio hapo tunaweza kujiuliza, kwa nini Kanisa lile la mwanzo linatoa msisitizo mkubwa kabisa juu ya muujiza huu? Yesu alitenda miujiza mingine mingi tena mikubwa zaidi, lakini kwa nini Wainjili wote wanne wanatoa mkazo na msisitizo mkubwa kwa muujiza huu? Na kama ndivyo, kwa nini basi miujiza mingine inasimuliwa mara moja peke yake tofauti na muujiza huu wa leo?
Muujiza wa mikate kama unavyosimuliwa na Mwinjili Yohane ni tofauti na jinsi inavyosimuliwa na Wainjili wengine. Na ndio mwaliko wangu leo kujaribu kuingia ndani ya Injili hii ili tuweze kwa pamoja kuchota ujumbe unaokusudiwa kwetu. Na ndio tunaona pia Mama Kanisa ameingiza sura ile ya sita ya Injili ya Yohane kwa Dominika tano mfululizo, ili tuweze kuchota mafundisho ya kina kabisa juu ya utambulisho wa Yesu kama mkate wa uzima.
Tafakari hizi zitusaidie na kutusindikiza tunapoelekea kwenye kilele cha Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa hapo Septemba katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Yesu wa Ekaristi Takatifu ni nani haswa katika maisha yako na yangu, katika maisha ya kila mwamini na kwa Kanisa kiujumla. Mababa wa Mtaguso wa II wa Vatikano wanatualika kuona Ekaristi Takatifu kama chemuchemu na kilele cha maisha ya Kanisa. Ni Ekaristi Takatifu inayolifanya Kanisa liwepo, na Kanisa linadumu hata ukamilifu wa dahari kwa kuadhimisha Ekaristi Takatifu.
Kwanza yafaa kutambua kuwa Mwinjili Yohane hauiti kama muujiza bali kama ishara, na pia hatusikii moja kwa moja kuwa Yesu aliifanya mikate na samaki kuwa mingi na wengi ili kuwatosha watu wote, na badala yake ni mikate ile ile na samaki wale wale kidogo waliwekwa kwa ajili ya wote mpaka kila mmoja akapata kadri ya haja na mahitaji yake na hata kusaza.
Na bado wakaweza kukusanya mabaki vikapu kumi na viwili vya mikate, ndio kusema waliweza kupata kila mmoja na bado hawakuweza kumaliza chote kilichowekwa mbele yao. Hivyo tunaona mara moja msisitizo wa somo la Injili ya leo haupo katika ongezeko la mikate wala samaki, na badala yake moyo na roho ile ya kushirikiana kidogo kinachokuwepo kwa wote kadri ya uhitaji wa kila mmoja wetu.
Falsafa ya ulimwengu wa leo ni kuwa na kila kitu kwa wingi katika maisha, iwe ni pesa, afya, elimu, miaka ya kuishi, marafiki, mafanikio, na kadhalika na kadhalika. Na huu ndio ugonjwa wa wengi wetu, wa kujikusanyia, wa kujilimbikizia, wa kujijali na wenye kutaka na kusaka zaidi na zaidi. Ugonjwa huu wa kujilimbikia unaakisi hasa utamaduni wa kifo, unaotokana na maisha yenye kujaa hofu ya kifo, na ndio dalili ya wazi ya kukosa imani, kwani tunakuwa watumwa wa vitu na mali na badala ya kuwekeza katika upendo kwa Mungu na kwa jirani.
Somo la Injili ya leo, Yesu anatufundisha juu ya ugonjwa huu wa kujilimbikizia na kujikusanyia kila kitu, ugonjwa wa kutaka zaidi na zaidi katika maisha, ni njaa ya vitu na mali.Yesu leo anatupa dawa ya ugonjwa wetu huu, dawa ambayo ni kinyume kabisa na mantiki na utamaduni na falsafa ya ulimwengu wetu, Yesu leo anatuonesha njia salama na sahihi ya ugonjwa wa ubinafsi na umimi ni ile ya kushirikiana sote kwa pamoja bila ubaguzi kidogo kinachokuwepo mbele yetu.
Pasaka, ndiyo sikukuu ya Wayahudi ilikuwa karibu. Mwinjili Yohane anatuonesha ni wakati gani Yesu alitenda ishara ile. Ndio kusema mazingira yalikuwa ni pale walipokumbuka kukombolewa kwao kutoka utumwani Misri.
Ndiyo kusema Mwinjili anajaribu kuoanisha na kuhusianisha tukio la ishara ya mikate, pamoja na tukio la kihistoria la kutoka utumwani Misri. Yesu leo anavuka kama vile Musa alivyowavusha Wanawaisraeli katika bahari ile ya Shamu, na ndipo tunaona leo hakuna chombo kinachotajwa kumvusha Yesu.
Kama vile Musa alivyowaongoza watu wengi, ndivyo na Yesu leo wanamkusanyikia watu wengi na hapo anatenda ishara kama vile Musa nyakati za kuwakomboa Wanawaisraeli. Mara mbili Yesu anapanda juu mlimani, ni kama Musa alivyokuwa akipanda juu mlimani na huko kupokea maagizo ya jinsi ya kuliongoza taifa lile teule.

Page 1 of 3