Na Mathayo Kijazi
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi OFMCap, amesema kuwa wito wa kujiibua mwenyewe si wito wa kweli bali ni wito bandia.
Aliyasema hayo katika homilia yake wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya Daraja Takatifu ya Upadri kwa Shemasi Richard Mlay, CP, katika Parokia ya Mtakatifu Fransisko Ksaveri - Chang’ombe, jimboni humo.
“Ndugu zangu, wito wa kujiibua mwenyewe siyo wito wa kweli, huo ni wito ‘fake’. Huyu Shemasi anayepokea Daraja ya Upadri leo hakujiibua mwenyewe, bali ameitwa na Mungu,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Sambamba na hayo, Askofu Mkuu aliongeza kuwa wito una madai, sadaka na majitoleo yake na kwamba wito wa kweli ni ufuasi.
Alisema kuwa yeyote anayetaka kumfuata Kristo, anapaswa kutambua kwamba Kristo ni nani na anataka nini.
Aliongeza kuwa kila wito chimbuko lake ni Ubatizo na kwamba kila mmoja katika maisha yake ana wito wake.
Vilevile, alisema kuwa hakuna mtu mwenye mastahili ya kuwa Padri na kwamba kila Padri ameshirikishwa, kwani mwenye kustahili wito huo ni Kristo mwenyewe.