DAR ES SALAAM
Na Nicholaus Kilowoko
Uongozi wa klabu ya soka ya Azam FC, umesema kuwa baada ya kocha kurejesha ripoti yake ya msimu mzima, wanatarajia kusajili wachezaji wa kazi watakaoisaidia timu.
Mkuu wa Kitengo cha Habari, Thabith Zakaria Zaka marufu Zakazi Zaka alisema kwamba, msimu huu umekuwa na mambo mengi na kuwafanya washindwe kutimiza malengo yao, lakini wanaamini mara baada ya kupokea ripoti hiyo, itatafsiri muelekeo wao ujao.
Alisema kuwa msimu huu unavyohitimishwa unategemea ripoti ya kocha, ambayo itawaongoza wao katika usajili wa wachezaji ambao wataisaidia timu hiyo msimu ujao.
Aliongeza kuwa kusajili kwao ni lazima, haijalishi wachezaji watawatoa katika timu zao za vijana au nje ya nchi, lakini lazima wakiimarishe kikosi chao msimu ujao kutokana na matokeo ambayo waliyapata msimu ulioisha.