Moshi
Na Paul Charles Mabuga
Wiki moja tu inatosha kunasa moyo wako, katika mtego mtamu wa pilikapilika za Moshi. Huu si mji wa kawaida, bali ni lulu iliyolala katika kivuli kitukufu cha Mlima Kilimanjaro.
Huku ukiahidi utulivu wa kitalii, uhalisia wake umejaa mizunguko ya kusisimua, milio isiyotarajiwa, na siri za kitabibu zinazofichwa kwenye glasi ya maziwa ya ngamia, na kikombe cha kahawa bora kabisa duniani.
Nilipowasili, hali ya hewa ilinikumbatia kwa ubaridi laini wa majira haya, ule unaochochea hamu ya kahawa ya moto hata mchana. Lakini ghafla, palikuwa na mabadiliko ya joto! Joto jipya lilianza kuhisiwa ghafla, kana kwamba Mlima Kilimanjaro ulikuwa umeamua kuachia pumzi yake ya joto badala ya baridi. Mabadiliko haya ya ghafla yananukia mabadiliko ya tabianchi, yanayobadilisha mood ya mji.