Na Mathayo Kijazi
Katika kuzindua Jubilei ya Miaka 75 ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam ngazi ya Dekania ya Mtakatifu Thomas More, waamini wamekumbushwa kuitumia nafasi hiyo kuondoa changamoto za ubaridi wa kiimani na kutopokea Masakramenti, huku wakiwa wafariji kwa wenye shida na wanaopitia mazingira magumu katika maisha yao.
Hayo yalisemwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo, Mhashamu Vincent Mpwaji, wakati wa homilia yake katika adhimisho la Misa Takatifu ya Uzinduzi huo, iliyoadhimishwa katika Parokia ya Mtakatifu Gaspar - Mbezi Beach, jimboni humo.
“Kwa hiyo ndugu zangu, kupitia nafasi hiyo ya Jubilei ya Miaka 75 ya Jimbo Kuu la Dar es Saalam, tumwombe Mungu ili atuondolee changamoto mbalimbali tulizonazo, hasa za ubaridi wa kiimani na kutopokea Masakramenti,” alisema Askofu Msaidizi Mpwaji.
Askofu huyo aliwakumbusha waamini kuitumia Jubilei hiyo kama fursa ya kuimarika kiimani, kimaadili, kiutume na hata katika Umisionari wao.
Alitumia nafasi hiyo kuwasisitiza kila mmoja ndani ya Dekania hiyo, kuimarika katika umoja na uthabiti kama familia ya Mungu katika Kanisa mahalia jimboni humo, huku wakiwa chachu ya kuleta upyaisho ndani ya Jimbo lao.