Dar es Salaam
Na Remigius Mmavele
Kila kinapofika kipindi cha Krismas mwezi Desemba wimbo Kakolela Viva Christmas unasikika sana kwenye Vituo vingi vya Redio nchini Tanzania na maeneo mengine. Mtunzi wa wimbo huo ni Baba Gaston akiwa na bendi yake Orchestre Baba National.
Baba Gaston alizaliwa Julai 5, 1936 katika eneo linaloitwa Likasi mji ambao wakati huo ulikuwa unajulikana kwa jina la Jadotville unaopatikana karibu na Lubumbashi katika mkoa wa Shaba uliopo Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Alibadilisha jina lake kuwa Ilunga Chenji Kamanda wa Kamanda Gaston Omer baada ya Rais wa Zaire wakati huo Mobutu Sese Seko kuamuru kwamba raia wa Zaire wabadilishe majina yao ya Kikristo yawe ya kiafrika.
Safari ya muziki ilianza alipopata mafunzo yake mapema kutoka kwa mpiga piano wa Kigiriki, Leonides Rapitis akiwa katika hatua za mwanzo za kujifunza muziki aliimba wimbo maarufu unaoitwa “Barua kwa Mpenzi Gaston” wimbo ambao alitunga na kuimba akiwa bado shuleni. Alipokuwa na umri wa miaka 20 alianzisha bendi yake aliyoipa jina la Orchestre Baba National.
Katika miaka ya 1970 hali ya kisiasa na kiuchumi nchini Zaire sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilikuwa na misukosuko mingi iliyowalazimu wanamuziki wengi kutafuta fursa nje ya nchi yao.
Kutokana na hali hiyo, bendi nyingi za rumba kutoka mashariki mwa Kongo zilianza kusafiri katika nchi mbalimbali za Afrika zikiwemo Zimbabwe, Zambia, Uganda na maeneo mengine.