Dar es Salaam
Na Violet Tillya
Uongozi wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) Taifa, umepiga marufuku matumizi yasiyoidhinishwa ya nembo yake hasa kwenye kutengeneza vitenge.
Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa WAWATA Taifa, Bi. Evelyne Ntenga imetangaza vita dhidi ya wafanyabiashara, wachapishaji na wauza vitenge vyenye nembo ya WAWATA bila idhini.
Bi. Evelyne alisema nembo hiyo imesajiliwa kisheria na matumizi yake bila idhini ni makosa.
“Nembo ya WAWATA imesajiliwa kisheria na BRELA tangu tarehe 21 Desemba mwaka 2007 kwa namba TZ/T/2007/32519, Daraja la 25 na kwa mara ya mwisho tumeihuisha tarehe 21/12/2024 kwa miaka 10 ijayo,” inasema taarifa hiyo.
Uongozi huo umetaja sheria inayolinda matumizi ya nembo hiyo kuwa ni Sheria ya Alama za Biashara na Huduma, sura ya 326 toleo la 2023 kifungu cha 31 na 32, kinachowapa haki ya kipekee kama wamiliki halali na kuwabana wanaokiuka.
Uongozi wa WAWATA Taifa umesema hakuna mtu, kampuni au kikundi kinachoruhusiwa kutumia nembo ya WAWATA bila idhini, pia utengenezaji, uchapishaji na uuzaji wa vitenge, vikoi, mitandio na fulana zenye nembo hiyo lazima upate idhini halali na kwamba kuanzia Oktoba 16, 2026, yeyote atakayebainika kukiuka atachukuliwa hatua kali za kisheria mahakamani!.
Uongozi wa WAWATA Taifa umetoa wito kwa umma na kuwaomba wanawake Wakatoliki nchi nzima kutoa taarifa za siri kwa uongozi huo kama wakiona vitenge feki vinauzwa sokoni.
Taarifa hiyo pia imepelekwa kwa Mwenyekiti wa Utume wa Walei wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Mhashamu Askofu Edward Mapunda, Katibu Mkuu wa TEC, Padri Charles Kitima na viongozi wengine.











