Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Askofu Ruwa’ichi akemea waamini wazembe, waoga

Dar es Salaam

Na Mathayo Kijazi

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, OFMCap, amekemea tabia ya baadhi ya waamini wenye uzembe, uoga na ulegevu katika imani kwa sababu wengi humkana Kristo na kuikataa imani yao hasa wanapokutana na watu wa imani nyingine.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi -OFMCap, alitoa kauli hiyo katika homilia yake kwenye adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara katika Parokia ya Mtakatifu Ambrosi – Tagaste, jimboni humo.
“Yesu ametupa onyo, ametuonya kwamba tuwe makini tusimkane, je, tunamkana Yesu kivipi? Tunamkana kwa kutopea katika dhambi, tunamkana kwa kuwa walegevu, tunamkana kwa kuwa wazembe, tunamkana kwa kuwa waoga. Wako Wakristo wengi wazembe na waoga. Wako Wakristo ambao wakiwa mbele ya watu wengine wa madhehebu mbalimbali, wanaikana imani yao,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Aliongeza kuwa mwamini yeyote atakayemsaliti Yesu Krsito, Kristo naye atamsaliti mtu huyo mbele ya Malaika, akiwasisitiza kuzingatia hilo na kuepuka Kristo asiwakane wala asiwakatae katika maisha yao.
Aidha, Wakristo Wabatizwa wametakiwa kuitambua vema heshima, wito na hulka yao, huku wakiepuka kuwa kama wapagani katika kuiishi, kuilinda na kuitetea imani yao.
“Kwa hiyo kama Wabatizwa, tunayo hulka yetu, tunayo hadhi yetu, tunao wito wetu. Ewe Mbatizwa zingatia vema wito wako, hulka yako na heshima yako. Usikubali kuishi haidhuru haidhuru kama vile ungekuwa mpagani. Ishi imani yako, mshuhudie Kristo, mtangaze mbele ya walimwengu,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Aliwasihi kila mmoja kuwa shahidi wa kweli katika kumshuhudia Kristo, hasa kuzingatia kile alichowaahidia kabla ya kuteswa, kufa na kufufuka kwake.
Askofu Mkuu huyo aliwakumbusha vijana waliopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwamba kwa Sakramenti hiyo, wanakamilishwa katika Neema ya Ubatizo, akiwasisitiza kuitambua vema hadhi hiyo.
Aliwaalika kutambua kwamba kwa Sakramenti hiyo, hawaitwi tena watoto, bali watu wazima, kwani Roho huyo waliyempokea haikuwa kwa mara ya kwanza, bali ni kwa mara nyingine.
Aliwataka kuwa na ufahamu, uthubutu na utayari wa kuiishi Injili pamoja na kumtangaza Kristo, huku wakisimama imara kwa kushirikiana na Roho Mtakatifu waliyempokea ili atende kazi ndani yao.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Onesmo Ngonyani alimshukuru Askofu Mkuu Ruwa’ichi kwa kufika parokiani hapo na kuadhimisha Misa hiyo Takatifu, akiwapongeza vijana hao 150 kwa kupokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara.
Aidha, Paroko aliwashukuru Makatekista kwa kuwafundisha vijana hao hadi kufika hatua hiyo ya kupokea Sakramenti hiyo Takatifu, akiwasihi vijana kuendelea kudumu katika imani yao, huku wakishiriki katika mambo mbalimbali yanayohusu Kanisa.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.