Na Edvesta Tarimo
Maumivu ya mara kwa mara, kulazwa hospitalini, kukatiza masomo, gharama za matibabu na hofu ya maisha ya baadaye ni miongoni mwa changamoto zinazoweza kuambatana na maisha ya watu wenye ugonjwa wa selimundu.
Hata hivyo, nyuma ya maumivu yanayoonekana mwilini, kuna mzigo mwingine ambao mara nyingi haupewi uzito unaostahili; afya ya akili.
Kwa baadhi ya wagonjwa, changamoto haziishii katika maumivu ya mwili pekee, bali huambatana na huzuni, upweke, hofu, msongo wa mawazo na kupoteza kujiamini.
Kwa wazazi na walezi, safari ya kumhudumia mtoto mwenye ugonjwa huo inaweza pia kuathiri maisha ya familia, kazi na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takribani watu bilioni 1.2 duniani waliishi na tatizo la afya ya akili mwaka 2023, sawa na karibu mtu mmoja kati ya saba. Takwimu hizo zinaonesha ukubwa wa changamoto za afya ya akili duniani, ingawa hazimaanishi kuwa kila mtu mwenye selimundu atapatwa na tatizo hilo.
Selimundu ni nini?
Selimundu ni ugonjwa wa kurithi unaoathiri himoglobini, protini inayopatikana ndani ya chembe nyekundu za damu na inayosaidia kusafirisha oksijeni mwilini.
Kwa mtu mwenye ugonjwa huu, chembe hizo zinaweza kuwa na umbo la mundu, kukakamaa na kuziba mishipa midogo ya damu, hali inayoweza kusababisha maumivu makali na matatizo mengine ya kiafya.
Ugonjwa huu hutokea pale mtoto anaporithi mabadiliko yanayosababisha selimundu kutoka kwa wazazi wake. Kwa mfano, ikiwa baba na mama wote wana vinasaba vya selimundu, kwa kila ujauzito kuna uwezekano wa asilimia 25 mtoto kurithi ugonjwa huo, asilimia 50 kuwa na vinasaba vya selimundu bila kuwa na ugonjwa wenyewe na asilimia 25 kutorithi vinasaba hivyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), inakadiria kuwa mwaka 2021 watu milioni 7.74 duniani walikuwa wakiishi na ugonjwa wa selimundu, huku watoto wapya takribani 515,000 wakizaliwa na ugonjwa huo.
Karibu asilimia 80 ya watoto hao walizaliwa katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, jambo linaloonesha uzito wa tatizo hili katika ukanda huo.
Tanzania: Maelfu ya watoto huzaliwa na selimundu kila mwaka
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, idadi ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa wa Selimundu nchini imeongezeka kutoka takribani watoto 8,000 hadi 14,000 kila mwaka, hali inayoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye mzigo mkubwa wa ugonjwa huo Afrika na duniani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya mwezi Juni 2025, Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazoshika takwimu za juu duniani ikishika nafasi ya nne kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa selimundu (selimundu) ikitanguliwa na Nigeria, India na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Huku Takwimu za Shirika la Afya Dunia (WHO), zikionesha kuwa zaidi ya watoto 300,000 huzaliwa na Selimundu (Selimundu) kila mwaka duniani, Tanzania peke yake ikiwa na takribani watoto 14,000 wanaozaliwa na ugonjwa huo kwa mwaka sawa na watoto 14 kati ya kila watoto 1,000.
Soma zaidi kwenye Rifaly au App ya Tumaini Media











