Print this page

Historia ya Umisionari Amerika ya Kusini

Mtakatifu Peter Claver. Mtakatifu Peter Claver.

Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki
iliyopita, tuliendelea kuwaletea historia ya Umisionari Amerika ya Kati. Leo tunaendelea na historia ya Umisionari katika Bara la Amerika ya Kusini. Sasa endelea…

Peru ilitekwa na Jenerali Pizarro mwaka 1532-35. Baadaye walifuata kwa wingi wamisionari Wafransiskani na Wadominikani. 
Kati ya wamisionari hao, wanajulikana sana Watakatifu Fransis wa Salano (1549 -1619), Mfransiskano na Luiz Betrand (1526 – 1581), Mdominikano. 
Mara nyingi tunasoma sana historia ya Mtakatifu wa kwanza mzaliwa wa Peru, Mtakatifu Rosa wa Lima (1586-1617), Mtakatifu Mtawa Mlei Mdominikano Mtersiali, aliyeishi maisha ya ufukara katika familia tajiri, akihudumia wagonjwa na maskini.  
Kazi hii ilikamilishwa na Mtakatifu Peter Claver (1580-1654), Mjesuiti aliyefanya utume kati ya watumwa weusi. Peter Claver aliwabatiza mwenyewe watumwa zaidi ya 300,000. 
Peter Claver anajulikana kama mtetezi wa haki za binadamu kwa kuwatetea na kuwasaidia watumwa. Na kulikuwa vilevile na Mtakatifu Chotara, Martin de Porres (1570-1639). 
Kama chotara alidharauliwa, lakini maisha yake ya utakatifu, huduma kwa wagonjwa na unyenyekevu wake, ulimpa heshima kubwa. 
Watakatifu wote hawa, wana historia nzuri ya kutia moyo na kuliwaza. Mtu akipata muda asome historia ya maisha yao.  
Peru imekuja kujulikana sana alipochaguliwa Papa Leo IV ambaye ingawa alizaliwa Marekani (USA), sehemu kubwa ya maisha yake ya kimisionari yalikuwa Peru na ana uraia pacha, Marekani na Peru.
Kutoka Peru, Wamisionari waliingia pamoja na wakoloni katika nchi za Venezuela mwaka 1520-40; Yucatan mwaka 1527-47; Colombia mwaka 1530 na Chile mwaka 1540. 
Baadaye Wajesuiti, waliinjilisha Paraguay na Brazil iliyokuwa chini ya Ureno. Mwaka 2010 katika nchi hizi za Amerika ya Kusini asilimia 91 ni Wakatoliki na wanafanya asilimia 35 ya Wakatoliki wote duniani. 
Brazil peke yake ina Wakatoliki milioni 134.5 ambao ni asilimia 87 ya wakazi wote wa Brazil, Colombia ina Wakatoliki milioni 32.3 au asilimia 91 na Argentina alikotoka Papa Francis, ina Wakatoliki milioni 31.5 au asilimia 91. 
Nchi hizi pamoja na Mexico ziko kati ya nchi 10 zenye Wakatoliki wengi duniani.
Uinjilishaji wa Amerika ya Kusini, ulifaulu kwa kuwapata watu wengi ila bahati mbaya mafundisho hayakuwa ya kina. Mara nyingine walibatiza hata watu 14,000 kwa siku na isingelikuwa rahisi kuwafundisha dini vizuri. 
Pili, palikuwepo na shida ya lugha. Hawa wamisionari ni wachache, walioelewa lugha ya wenyeji vizuri. Hali ya ukoloni ilichangia kuwachanganya watu kwa kutojua tofauti kati ya wazungu wakoloni na wamisionari. 
Ni kweli kwamba wamisionari mara nyingi waliwatetea wananchi wazawa Wahindi Wekundu hali ambayo mara nyingi ilileta kutoelewana kati ya wamisionari na wakoloni wakatili. 

•    Huko Mexico ndiko Bikira Maria alimtokea Juan Diego hapo Guardarupe na kuomba kanisa lijengwe. Miujiza mingi ilitendeka.
•    Tukio hili nchini Mexico, liliharakisha sana uongofu wa wenyeji, kwani Bikira Maria alionekana kama mwanamke wa kiasili (mwenye ngozi ya kahawia), jambo lililowafanya wenyeji wajisikie kukubalika katika Ukristo. 
•    Ibada ni kubwa huko hata wakati wa Serikali ya kikomunisti bado kila mwaka mamilioni ya wahujaji walienda huko.

Rate this item
(0 votes)
Japhet

Latest from Japhet