Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Hatua 6 zilizotumika kuandaa nyimbo miaka ya zamani

Na Arone Mpanduka

Katika miaka ya 1990 na kurudi nyuma, bendi nyingi nchini zilikuwa na ushindani mkubwa wa kimuziki, kulingana na mazingira halisi waliyokuwa nayo katika miaka hiyo, tofauti na sasa.
Sasa hivi muziki wa dansi Tanzania, pamoja na wanamuziki wake, umekuwa ukichechemea kufuatia mabadiliko makubwa ya teknolojia ambayo yameegemeza zaidi katika miziki ya kizazi kipya.
Upekuzi na udadisi wangu umebaini mambo kadhaa kuhusiana na muziki wa zamani, namna ulivyokuwa unaandaliwa, na wanamuziki wenyewe walivyokuwa wanajinoa kabla wimbo haujafika kwa wasikilizaji.
Yapo mambo kama 6 hivi ambayo yalikuwa yakifanyika, na hatimaye wimbo pendwa unakwenda sokoni ukiwa umekamilika na watu wakaufurahia.
UTUNZI WA WIMBO
Katika miaka ya zamani, bendi nyingi za muziki zilikuwa zikihusisha wanamuziki wengi ambao walikuwa wanaimba pamoja kwenye kumbi za starehe, na hata studio walikuwa wanakwenda pamoja kurekodi.Hii iliwarahisishia watunzi kutunga nyimbo zao kwa kushirikiana na kundi zima.
Mtunzi alikuwa anaweza kutunga wimbo wake, kisha akaufanyia uhakiki yeye mwenyewe ili kujiridhisha kama unafaa kuwapelekea wenzake, ama la.
Tungo ya muziki inaweza ikawa inazungumzia siasa, mapenzi, ama masuala yoyote yanayohusu maendeleo ya nchi, na mara nyingi walikuwa wakitunga kulingana na matukio halisi wanayoyashuhudia, na kisha kujazia na vionjo vingine vya kubuni ili kuleta ladha.
KUSHIRIKISHA WANAMUZIKI WENGINE
Baada ya kujiridhisha na tungo yake, mtunzi alikuwa anachukua andiko lake na kwenda nalo mazoezini na kuwashirikisha wenzake. Na hapo kila mmoja alikuwa makini kuangalia nini cha kuongeza, ili wimbo uwe mzuri kusikilizwa na kuchezwa na watu ukumbini.Na kama ikitokea wimbo haufai kabisa, labda kwa kukosa maadili, mtunzi hulazimika kurudia upya kuandika tungo zake, na kisha kuurudisha tena kwa wenzake.
Hapo mtunzi hulazimika kutafuta ‘tone’ ya kuimba mbele ya wenzake, huku wapiga gita, kinanda na ngoma wakiwa makini kusikiliza ili kuona vyombo vyao wanavipiga kwenye maeneo gani ya mistari hiyo.
KUUJARIBU WIMBO HADHARANI
Baada ya hapo, wanamuziki wote wa bendi hukubaliana kuujaribu wimbo huo mbele ya mashabiki zao, hasa pale wanapokwenda kutumbuiza nyimbo zao ambazo zimeshaingia sokoni. Kwa mfano, wanaweza kwenda kutumbuiza ukumbi wa DDC Kariakoo, na hatimaye huchomekea wimbo mpya na kisha kusikilizia hisia za mashabiki juu ya wimbo huo.
Wakati hayo yanafanyika, kunakuwa na kiongozi wa jukwaa ambaye kazi yake ni kuangalia muunganiko kati ya mashabiki na kile kinachotolewa na wanamuziki kupitia sauti zao, na mchanganyiko wa vyombo vyao.
MASAHIHISHO
Kama ikitokea mashabiki wamepoa wakati wimbo mpya unapigwa, basi kiongozi huyo wa jukwaa huamuru wimbo urudiwe mara kwa mara, na hali ikibaki hivyo, wakirudi kambini wanashirikiana kutafuta wapi walipokosea ili warekebishe.Hapo wanaweza kubadilisha hata staili ya kinanda, ama baadhi ya waimbaji. Na baada ya hapo, huujaribu tena kwenye onyesho lingine. Ikitokea mashabiki wameupokea wimbo kwa furaha, basi hukubaliana kwamba urekodiwe studio.
KUHAKIKIWA STUDIO
Kama wimbo umependwa na mashabiki, hupelekwa studio haraka kwa ajili ya kujadiliwa na kuhakikiwa ili itoke ruhusa ya kurekodiwa. Studio zenyewe kwa wakati huo zilikuwa ni za Redio Tanzania Dar es salaam (RTD), sasa hivi zikifahamika kama Tanzania Broadcasting Corporation (TBC).
Hapo wimbo unachujwa tena na kuboreshwa na wataalamu waliosomea muziki na lugha ya Kiswahili.Hiyo ilikuwa ni Kamati Maalum ambayo kazi yake ilikuwa ni kupitia nyimbo zilizoandikwa kwenye karatasi, na kisha huruhusu bendi kwenda kurekodi.
KUREKODI
Baada ya wataalam kuhakiki, walikuwa wakitoa ruhusa ya kurekodi wimbo ambapo kwa mujibu wa teknolojia kwa wakati huo, walitumia ‘Two track recording,’ mfumo ambao ulilazimisha mwanamuziki yeyote arekodi bila kukosea, akiwemo mwimbaji, mpiga ngoma, gita n.k. Na kama ikitokea mmoja amekosea, kazi huanza upya. Muda wao ulikuwa kuanzia saa 8 mchana hadi saa 12 kasoro, jioni.
Mfumo huo ulikuwa shirikishi, kwani ulilazimisha wanamuziki wa bendi nzima kuingia studio na kufunga vifaa vyao vya muziki, na kisha kurekodi.
Hizo ndizo njia 6 ambazo wanamuziki wa zamani walizitumia katika kuandaa wimbo hadi kuwafikia wasikilizaji.
Katika miaka ya sasa hali imebadilika kwani msanii anaweza kurekodi kwa kurudiarudia, kisha producer anakata vipande vilivyokosewa na kuacha vilivyo sahihi, na pia miaka ya sasa, msanii anaweza kutuma sauti yake kwa njia ya Whatsapp na kisha huchanganywa na za wengine, ili kukamilisha wimbo.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.