BAGAMOYO
Na Mathayo Kijazi
Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), wametakiwa kufahamu kwamba kushiriki Hija, ni kukutana na Mungu, waongee naye, wamshirikishe shida zao.
Hayo yalisemwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Hija ya WAWATA, iliyoadhimishwa katika Kituo cha Hija - Bagamoyo, Jimbo Katoliki la Morogoro.
“Ndugu zangu wapendwa, tumekuja kufanya Hija hapa Bagamoyo kama WAWATA. Tumekuja kwenye Hija hii, lengo ni kukutana na Mungu katika mazingira haya ambayo ndipo Injili iliingilia kwetu Tanganyika,” alisema Askofu Musomba, na kuongeza…,
“Tunakutana na Mungu huyu ili tuongee naye, tumshirikishe shida zetu, tumshirikishe mambo ya familia zetu, tumshirikishe juu ya udhaifu wetu tulio nao, na tutafakari pamoja naye imani yetu, hasa katika tathmini kwamba tupo katika njia sahihi, au tumepotea, au tuna mahangaiko, au tumekengeuka, yeye mwenyewe atunyanyue na atuinue ili atuweke sehemu nzuri. Tumjue vizuri, tumtambue vizuri katika maisha yetu.”
Sambamba na hayo, Askofu Musomba aliwataka WAWATA kufahamu kwamba Hija hiyo waliyoshiriki siyo utalii, bali ni jambo la kiroho zaidi, kwani wanakutana na Mungu wanayemtafakari katika maisha yao.
“Na kwa sababu hiyo, Hija hii siyo utalii, ni jambo la kiroho zaidi. Mungu huyu tunayekutana naye, ni yule ambaye kwanza tunamtafakari katika maisha yetu, tunamtafakari katika roho zetu, na hivyo tunaingia kwake katika utulivu.
“Tunatambua kwamba ndiye aliyetuumba, tunatambua kwamba ndiye aliyeumba kila kitu. Kwa hiyo katika Hija, tunawiwa kumtambua zaidi na kumjua zaidi. Tumpende na kumtumikia ipasavyo tukiwa na lengo la kwenda kwake, ndiyo maana ya Hija hii kumwelekea yeye,” alisema Askofu huyo.
Pia, aliwataka WAWATA hao kutoukaribia uovu, ikiwa ni pamoja na kushawishika kwenda kwa waganga wa kienyeji, kwani katika Hija hiyo wapo katika mazingira ambayo Injili iliingilia.
Sambamba na hayo, aliwasisitiza kuendelea kumjua Mungu kwa kusoma Maandiko Matakatifu, kusoma Mafundisho ya Mama Kanisa, pamoja na kuyafuatilia inavyotakiwa.
Pia, aliwaasa kushiriki vizuri katika Liturujia za Mama Kanisa, kwani katika hiyo, wanaadhimisha maisha yao wenyewe pamoja na imani yao.
Katika homilia yake, Askofu Msaidizi Musomba aliwataka WAWATA kuendelea kusikiliza yale wanayoshauriwa na wenzao, pamoja na kuyachanganua, kwani kuna faida kubwa ya kupata mawazo mapya katika maisha.
“Tuendelee kusikiliza kila mara wenzetu wanatushauri nini katika maisha yetu, na vile vile kuchanganua kwamba rafiki wa kweli anatuongoza. Rafiki anayesema acha kusali, huyo siyo rafiki, na wala siyo wa kweli. Lakini yule anayesema tusali Rozari, tutafakari maisha ya Yesu na Mama Bikira Maria, huyo ndiye rafiki wa kweli,” alisema Askofu Musomba.
Kwa upande wake Mlezi wa WAWATA Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Joseph Mosha, ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Thomas wa Akwino – Chuo Kikuu, alimshukuru Askofu Msaidizi Musomba kwa kuadhimisha Misa hiyo, na kusema kwamba kwa muda mrefu walikuwa wanatamani wawe na Askofu katika Maadhimisho ya Misa hizo.
“Nichukue nafasi hii kumshukuru Baba Askofu kwa kutuongozea Ibada ya Misa Takatifu, imepita miaka kadhaa tulikuwa tunakosa Maaskofu wa kutusindikiza, lakini mwaka huu tunashukuru sana Baba umetusindikiza, wakinamama wamepata nguvu kweli kweli, asante sana Baba,” alisema Padri Mosha.
Naye, Mwenyekiti wa WAWATA jimboni humo, Stella Rwegasira aliwataka wanawake wenzake kutambua maana ya Hija pamoja na umuhimu wake, akiwasihi kuepuka kuifananisha Hija na safari nyingine za starehe.
“Tumepata mada inayohusu Hija, tumeweza kujua Hija maana yake nini, maandalizi yake yaweje, na kwamba tumefundishwa Hija siyo ‘piknik’, na Hija siyo kuja kuogelea, kwa mfano tunaokuja Bagamoyo…
“Kuna wenzetu wengine pia wamepata bahati ya kwenda Hija za nje ya Nchi, na kuna wengine ambao walijua wanakwenda ‘shopping’, ingawa kuna wakati fulani nilipata kesi, lakini haikufanikiwa, kuna mtu anakwenda Hija halafu anataka kuzamia, sasa wakiwa kule wanapiga simu, ‘Mama… kuna WAWATA wako huku,’ sasa kama wewe ni mama, ukienda kuzamia huko, huwi tena hujaji, unakuwa mama ni wale WAWATA wako,” alisema Stella Rwegasira, Mwenyekiti huyo wa WAWATA.
Stella Rwegasira alimshukuru Askofu Musomba kwa kuadhimisha Misa hiyo Takatifu, akiwashukuru pia Mapadri, WAWATA, pamoja na wote walioshiriki katika Adhimisho hilo.