DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Vijana wanapopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, wametakiwa kusimama imara, kujitambua na kuelewa wajibu wao wa kuishi maisha bora ya Imani Katoliki kama walivyofundishwa.
Kauli hiyo ilitolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba OSA, wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa vijana 166 katika Parokia ya Mtakatifu Agustino – Ukonga, jimboni humo.
Askofu huyo alisema kuwa dhambi ni kikwazo katika ubinadamu, ambacho kinawafanya watu wawe vipofu na kushindwa kumwona Mungu katika maisha yao.
“Kwa hiyo ndugu zangu tutambue kwamba dhambi ni kikwazo katika ubinadamu, ambacho kinawafanya watu wawe vipofu na washindwe kumwona Mungu. Tuishi maisha ya kumpendeza Mungu,” alisema Askofu Musomba.
Vile vile, aliwasihi vijana waliopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kuepuka kuyumbishwa, huku akiwasisitiza kubaki katika imani yao Katoliki kwani wao wamekuwa ni Askari hodari wa Kristu.
Aliwaagiza Wazazi, Walezi na Waamini wote kwa pamoja, kushirikiana katika kusimamia malezi ya vijana hao, kwani kwa kufanya hivyo, Kanisa litapata watendaji walio bora.
Katika homilia hiyo Askofu Musomba pia aliwasihi Waamini kutokuisaliti imani yao na kutokuionea haya, akisema kwamba kufanya hivyo, ni kupotea katika imani.
Pia, alisisitiza kuepuka kiburi na majivuno katika mazingira wanayoishi, akiwasisitiza kuguswa na Roho Mtakatifu pamoja na kusikiliza kila wanachoelezwa.
“Epukeni kiburi na majivuno, kwamba bila mimi, hiki hakiwezi kufanyika. Jitahidini kuishi maisha ya kuguswa na Roho Mtakatifu huku mkisikiliza kila mnachoelezwa,” alisema Askofu Musomba.
Aliwataka Waamini kutambua kwamba ni wajibu wao kuiishi pamoja na kuishuhudia imani siku zote za maisha yao, kwani wao ni sura na mfano wa Mungu.
Katika hatua nyingine Askofu Musomba aliwashukuru Waamini wa Parokia ya Ukonga kwa ukarimu waliouonyesha kwake, kwani hiyo imemfanya ajihisi kuwa yuko nyumbani.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri James Mweyunge alisema kuwa alipo Askofu, ndipo Kanisa lilipo, hivyo ni furaha kwao kusali pamoja na Askofu katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu.
Padri Mweyunge aliwashukuru walimu (Makatekista) waliowafundisha vyema vijana hao hadi wameweza kufahamu mambo mengi yanayohusu Imani Katoliki.
IFAKARA
Na Celina Matuja
Wakati Serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, Mbunge wa Jimbo la Rufiji, kutangaza rasmi kuanza kwa mbio za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu, Askofu wa Jimbo Katoliki la Ifakara, Mhashamu Salutaris Libena, ametoa ya moyoni.
Uchaguzi huo ni muhimu kwani utatoa fursa kwa wananchi kuwachagua Viongozi wa mitaa na vijiji, na ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wa mwakani.
Askofu Libena alisema hayo hivi karibuni katika Mahojiano Maalumu na gazeti Tumaini Letu ofisini kwake Jimboni Ifakara, kuhusu uchaguzi huo.
Alisema kwamba ni muhimu kwa Waamini wote kujitokeza kushiriki katika masuala ya kitaifa kwa kuwa ni haki ya kila raia Mtanzania, bila kujali dini, ili kupata viongozi wazuri na wanaowataka kwa maendeleo yao.
Askofu Libena aliwataka Waamini wa Jimbo hilo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, kugombea kupiga kura, kugombea na kushiriki katika Uchaguzi huo ili kupata viongozi bora wa Serikali za Mitaa kwa maendeleo ya Nchi, na Kanisa kwa ujumla.
Aliongeza kuwa ni vizuri pia kuwapatia elimu vijana kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuzingatia uzalendo, na wasitumiwe na mamluki kuuza haki yao ya kuchagua au kuchaguliwa katika ngazi zote za uongozi serikalini.
Alisema pia kuwa vijana ni hazina ya Taifa, hivyo wasipoelimishwa vizuri, watapotea na kupoteza haki yao ya kuchagua au kuchaguliwa.
Askofu Libena alisisitiza waamini kujiandikisha sasa wakati tangazo la serikali limeshatolewa, ili wasipate shida wakati wa kupiga kura, lakini pia kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kuonyesha ukomavu wa kisiasa badala ya kujiandikisha na kuwaachia wengine kupiga kura.
Kwa mujibu wa Askofu Libena, ni muhimu kwa Mkristo kujitokeza na kushiriki uchaguzi huo na ujao, kwani utampatia nafasi ya uwakilishi katika kuiongoza Jamii na Kanisa kwa ujumla.
Inavyoeleza Katiba kuhusu Uchaguzi:
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Ibara 145 na 146 inaelezea uwepo wa Serikali za Mitaa pamoja na madhumuni yake. Mojawapo ya madhumuni ya kuwepo kwa Serikali za Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi.
Aidha, Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura 287 na Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura 288, zinaelekeza kufanyika kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Lengo ni kuzifanya Serikali za Mitaa ziongozwe kidemokrasia.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 201A cha Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura 287 na Kifungu cha 87A cha Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura 288, Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa ana mamlaka ya kutunga Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambazo hutumika kuongoza uchaguzi huo.
Viongozi wanaochaguliwa katika ngazi hizi ni Wenyeviti wa Vijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji, Wenyeviti wa Mitaa, Wajumbe wa Kamati za Mitaa na Wenyeviti wa vitongoji.
Uchaguzi wa mwisho wa Serikali za Mitaa ulifanyika mwezi Novemba mwaka 2019, hivyo, uchaguzi mwingine unatakiwa kufanyika Novemba, 2024.
Uchaguzi huu unaongozwa na Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ngazi ya Vijiji, Vitongoji na Mitaa katika Mamlaka za Wilaya na Mamlaka za Miji, kwa mujibu wa Matangazo ya Serikali Na. 571, 572 573 na 574 ya Mwaka 2024.
Kwa mujibu wa Kanuni hizi, Waziri wa TAMISEMI anapaswa kutoa Tangazo la Uchaguzi likiainisha ratiba, shughuli za uchaguzi zinazohusika na masharti muhimu ya uchaguzi.
Masharti muhimu ya kuzingatia katika Uchaguzi huo ni kama ifuatavyo:- (a) Nafasi zitakazogombewa katika uchaguzi huu ni Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (kundi mchanganyiko la wanaume na wanawake), Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (kundi la wanawake) na Wenyeviti wa Vitongoji katika Mamlaka za Wilaya.
Kwa nafasi hizo, uchaguzi utaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Wilaya za Mwaka 2024 (Tangazo la Serikali Na. 571 la Mwaka 2024), (ii) Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji Midogo.
Kwa nafasi hiyo, uchaguzi utaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji Midogo za Mwaka 2024 (Tangazo la Serikali Na. 572 la Mwaka 2024) (iii) Mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (kundi mchanganyiko la wanaume na wanawake), wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (kundi la wanawake) na wenyeviti wa vitongoji katika Mamlaka za Miji.
Kwa nafasi hizo, uchaguzi utaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji za Mwaka 2024 (Tangazo la Serikali Na.573 la Mwaka 2024) (iv) Mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wa kamati ya mtaa (Kundi Mchanganyiko la Wanaume na Wanawake) na wajumbe wa kamati ya mtaa (Kundi la Wanawake) katika Mamlaka za Miji.
Kwa nafasi hizo, uchaguzi utaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa katika Mamlaka za Miji za Mwaka 2024 (Tangazo la Serikali Na. 574 la Mwaka 2024).
RUVUMA
Na Mwandishi wetu
Naibu Waziri Nishati, Judith Kapinga amesema kwa Serikali imetenga takribani Shilingi bilioni 4.6/- kupeleka umeme kwenye maeneo ya migodi mkoani Ruvuma.
Kapinga (pichani) aliyasema hayo wakati akizindua Kituo cha Mauzo ya Makaa ya Mawe ya kampuni ya Market Insight Limited (MILCOAL), inayojihusisha na uchimbaji, uuzaji na usambazaji wa makaa ya mawe, Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.
SIMANJIRO
Na Mwandishi wetu
Wachimbaji wa madini ya Green Garnet eneo la Lemshuku, Kata ya Komolo Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamelalamikia kwa Waziri wa Madini, Anthony Mavunde juu ya changamoto ya ukosefu wa maji, nishati ya umeme na kuwa na ubovu wa barabara.
Mmoja wa wachimbaji madini ya Green Garnet, Mkurugenzi wa Kampuni ya Chusa Mining Ltd, Joseph Mwakipesile alisema hayo wakati akizungumza na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde baada ya kutembelea machimbo ya Lemshuku.
Mwakipesile alisema kuwa huduma ya maji ni changamoto kubwa kwenye machimbo ya Lemshuku, na hakuna nishati ya umeme, hivyo kushindwa kufanya uchimbaji kwa uhakika.
“Maji yanafuatwa umbali wa kilomita 17 kutoka kijiji cha Komolo hadi hapa machimboni, na tulikuwa na kisima cha maji, ila hivi sasa tuna maji tunafuata mbali, na pia barabara ni mbovu,” alisema Mwakipesile.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini (MAREMA), Tawi la Lemshuku, Swalehe Abdalah aliiomba Serikali kufanikisha utatuzi wa changamoto hizo ili waweze kufanya shughuli za uchimbaji kwa uhakika.
“Tunakushukuru Waziri Mavunde kwa kufika Lemshuku na kuona mazingira ya hapa Lemshuku, tunaomba serikali imalize vikwazo tulivyonavyo ili tufanye kazi vyema,” alisema Swalehe.
Akijibu malalamiko hayo, Waziri Mavunde alisema atakutana na Mawaziri husika ili kuhakikisha changamoto hizo zinafanyiwa kazi kuwawezesha wachimbaji hao waweze kufanya kazi zao ipasavyo, na Serikali iongeze mapato.
Waziri Mavunde alisema miundombinu ikiboreshwa na changamoto zikipatiwa ufumbuzi, Watanzania hao watatajirika kwa kupata fedha nyingi, na serikali itaongeza mapato kupitia kodi.
Hata hivyo, ili kumaliza changamoto ya ukosefu wa huduma ya afya, ameendesha harambee ya ghafla ya ujenzi wa zahanati na kupatikana Sh23 milioni matofali 3,000 na mifuko 185 ya saruji
Aliuagiza uongozi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) Wilaya ya Simanjiro, kuhakikisha pampu iliyozama kisima cha maji Lembole inatolewa ili wachimbaji wapate huduma wakati wakisubiri mradi mkubwa wa maji.
Akizungumza kuhusu mawasiliano alisema kwamba atazungumza na waziri husika ili mnara wa simu ufungwe kwenye machimbo hayo na hivyo mawasiliano yapatikane.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Fakii Lulandala alisema kuwa hii ni mara ya kwanza Waziri wa madini kufika kwenye machimbo ya Lemshuku, hivyo Waziri Mavunde anapaswa kupongezwa.
Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini nchini, Femata John Bina alisema Waziri Mavunde ni kiongozi wa pori kwa pori asiyekaa ofisini ndiyo sababu amefika Lemshuku huku Mwenyekiti wa chama cha mabroka Tanzania (Chamata) Jeremiah Kituyo amewaasa wanunuzi wa madini kukata leseni ili waweze kuwa huru na biashara yao.
Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka naye alisema wachimbaji hao wa Lemshuku wakitatuliwa changamoto zao watanufaika ikiwemo wachekechaji.
LINDI
Na Mwandishi wetu
Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, (NEEC) limewataka viongozi wa Mkoa wa Lindi, kutengeneza mkakati kabambe utakaozuia mimba za utotoni kwa wasichana kuwakatiza masomo na kuzima ndoto zao.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Beng’i Issa wakati baraza hilo lilipozindua programu ya Imarisha Uchumi na Mama Samia (IMASA)mkoani humo.
“Mkoa huu una matatizo ya wasichana kuacha masomo, hata wakiwa wamefaulu kujiunga na shule za sekondari hawaendi na inakadiriwa asilimia 30 yao hukatisha masomo kutokana na mimba za utotoni…mimba za utotoni zinakatisha ndoto za kiuchumi za wasichana,”alisema Beng’i.
Alisema programu ya IMASA imekuja kuwezesha Makundi ya kinamama, vijana, na makundi maalum. Hivyo makundi ya vijana yakipata elimu, ni nyenzo kubwa ya kufikia malengo yao ya kiuchumi na ukizingatia mkoa huo una fursa nyingi za kiuchumi.
Beng’i alisema kwamba mkoa huo wananchi wanajishughulisha na kilimo cha korosho,alizeti,uvuvi, mazao ya mwani, hivyo programa hiyo itashirikiana na mkoa huo kuweka vipaumbele ili kuandaa programu kwa ajili ya uwezeshaji wake.
Alisema pia kuwa program ilipokelewa vizuri mkoani humo na wananchi walitamani sana programu ianze haraka, na washiriki wengi walikuwa ni wafanya biashara, wakulima, wakulima wa kuongeza thamani mazao, na madalali wa kilimo.
Aidha, aliutaka uongozi wa Mkoa huo kuendelea na programu zao za kawaida katika kilimo cha korosho, ubanguaji korosho kuongeza thamani mazao na uvuvi, na zile za uwezeshaji za asilimia kumi na kuendelea, kufuata maelekezo ya serikali.
Naye Katibu wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Manispaa ya Lindi, Zuhura Meza alisema anamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha programu hiyo ambayo imekuja kuwainua kiuchumi wanawake kupitia mafunzo ya ujasiriamali na uwezeshaji watakaopewa.
“Nikirirudi nyummbani naenda kuwaelimisha watu wenye ulemavu, wale ambao hawajajisajili na programu ili nao waende kujisajili ili kupata fursa ya mafunzo na uwezeshaji,” alisema.
Naye Mkulima wa Mwani kutoka Kata ya Lindi Mjini ya Kitumbi, Kwela, Manispaa ya Lindi, Rukia Selemen alisema yeye ni mkulima na mchakataji wa bidhaa za mwani. Anashukuru ujio wa program hiyo kufika katika manispa yao kutoa elimu ya ujasiriamali na itamwezesha kufanya vizuri zaidi.
Mjasiriamali toka Kilwa Masoko Fatuma Juma alisema anajishughulisha na usindikaji wa mazao mbalimbali, yakiwemo ya maziwa (yogati), juice ya mwani na anatengeneza bidhaa za urembo kama nguo, na alidai kwa kusema kuwa programu hiyo imewaingiza katika mfumo na hivyo kufanya kazi kwa ubora.
DAR ES SALAAM
Na Laura Chrispin
Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewaasa Waamini kutambua kwamba ufukara na umaskini isiwe ni sababu ya wao kuikana imani.
Kardinali Pengo (pichani), alitoa wito huo hivi karibuni wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, iliyoadhimishwa Parokia ya Bikira Maria wa Fatima-Msimbazi, jimboni Dar es Salaam.
“Kuna baadhi ya watu kutokana na umaskini na ufukara wao, wamediriki kuikana imani yao ili mradi wapate baadhi ya vitu walivyokuwa wakihitaji,”alisema Kardinali Pengo.
Aliendelea kusema, “Nanyi Waamini na watoto mnaopokea Sakramenti ya Kipaimara, inawapasa kufahamu, hata Yesu alikuwa ni mtu fukara zaidi, lakini bado aliishi katika imani…hivyo basi nanyi inawapasa kuishi katika imani hiyo hiyo aliyokuwa nayo Yesu Kristo mwenyewe, ikiwa kama kielelezo na mfano bora wa maisha ya Mkatoliki.”
Kardinali Pengo alisema wanatakiwa kutambua kuwa Mwenyezi Mungu hana shida na fedha za mtu yeyote, bali anahitaji watu waongoke na kuiamini Injili.
Inawapasa kufahamu “maskini anayeongelewa na Muinjili Mathayo, si maskini wa mavazi, malazi au makazi, bali ni maskini yule asiyelifahamu Neno la Mungu”
Kardinali Pengo alisema kwamba Yesu Kristo alikuja duniani kwa kazi moja ya kuwahubiria Injili watu maskini na kuwakomboa wanadamu.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba-OSA katika Kigango cha Mtakatifu Antoni wa Padua – Nyeburu, Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo II – Buyuni, Adhimisho la Misa Takatifu ya Somo wa Kigango hicho. (Picha na Michael Ally)
DAR ES SALAAM
Na Israel Mapunda
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na Sekta Binafsi kwa kuweka mazingira wezeshi, ili kuhakikisha Sekta ya anga inakua na kuchangia ukuaji wa Pato la Taifa.
Waziri Kihenzile (pichani), alisema hayo jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea anga ya kampuni ya Ndege ya Precision, kukutana na kuzungumza na Wakurugenzi watendaji wa Coastal Aviation na Flightlink.
Katika ziara yake hiyo, Naibu Waziri Kihenzile alisema kwamba uwekezaji unaofanywa na Serikali kwenye eneo la kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege, utakuwa na matokeo makubwa pale ambapo sekta binafsi pia itawekeza katika ununuzi wa ndege.
Kihenzile aliongeza kuwa Serikali ipo katika hatua mbalimbali ya kufanya maboresho kwenye sera ya Uchukuzi na Sheria ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, kwa lengo la kuimarisha sekta ya usafiri wa anga.
Naye Mkurugenzi wa Precision, Patrick Mwanri alisema kwamba katika mpango kazi wake, imepanga kuongeza ndege ambazo zitakwenda sambamba na ongezeko la vituo ambavyo kampuni itakuwa ikitoa Huduma nchini.
Mkurugenzi Mwanri aliiomba Serikali kupitia Naibu Waziri Kihenzile, kuzisaidia kampuni binafsi za ndege kuweza kupata mikopo kupitia benki za ndani, ili kuziimarisha kwenye uendeshaji.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Flightlink, Kapteni Munawer Dhirani aliishukuru Serikali kwa kutekeleza dhamira yake ya kuweka mazingira mazuri ya sekta ya anga, na kuhakikisha makampuni binafsi yanaendelea kuwekeza kwa kununua ndege nchini.
Kapteni Munawer aliongoza kuwa mazingira yaliyowekwa yameiwezesha Kampuni ya Flightlink kuweka mipango ya kuongeza mtandao wa safari, ambapo mapema mwisho wa mwaka, Kampuni hiyo itaongeza kituo cha Mwanza.
DAR ES SALAAM
Na Laura Chrispin
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwai’chi amewataka waimarishwa kuwa Manabii wa kweli na kusikiliza sauti ya kichungaji wanapoitwa na Mungu.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema hayo wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti Takatifu ya Kipaimara iliyoadhimishwa katika Parokia ya Mwenyeheri Antonio Rosmini - Mpigi Magoe, jimboni humo.
“Muimarishwa unaitwa kuhubiri Habari Njema za Kristu, pamoja na kufanya mambo yaliyo mema na yenye kumpendeza Mungu, na si kuwa nabii wa uwongo,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Aliongeza kuwa zama za sasa zimekuwa na manabii wengi wa uongo, ambao lengo lao ni kudanganya, na si kutangaza Neno la Mungu.
Aidha, Askofu Mkuu Ruwai’chi alisema kuwa Mkatoliki aliyebatizwa, hapaswi kuwaamini manabii wa uongo, bali anatakiwa kuishi katika imani yake.
Aliwakumbusha Waamini kwamba manabii wa uwongo wamekuja kwa kazi ya kutafuta fedha tu, na si kwa ajili ya kuhubiri Neno la Mungu, akiwasisitiza kusimama imara katika imani yao.
“Nabii wa kweli hutokana na kusema ukweli, na siku zote maisha yao si rahisi, kwa sababu ndani yao mara zote kumejaa manyanyaso ya kusakamwa, ya kusutwa, pamoja na kudhulumiwa,” alisema Askofu Mkuu, na kuongeza,
“Hata katika Somo la Kwanza anazungumziwa Nabii Yeremia ambaye ni kati ya manabii mahiri zaidi katika Agano la Kale, ambaye mara zote alikuwa anawaambia watu wamrudie Mungu kutokana na mambo yao waliyokuwa wakitenda.
“Lakini, kwa sababu alikuwa ni nabii aliyesimama katika ukweli zaidi, watu hao walimkamata na kumuhukumu kifo, lakini ni kwa sababu Yeremia aliwataka watu wabadilike kwa kutubu ili yasije kujitokeza tena yale ya Sodoma na Gomora. Hiyo inaonesha fika ni kwa jinsi gani Manabii wa ukweli wanavyoteseka.”
Aidha, Askofu Ruwa’ichi aliwakumbusha Waamini kutubu na kuamini Injili, ikiwa kama ujumbe wa Yesu aliowaachia wanafunzi wake, akiwataka kutokufanya maamuzi ya haraka, bali wafikiri zaidi na kutenda ili baadaye wasije kujuta.
Aliwakumbusha Waimarishwa kuwa siku ya Ubatizo walizaliwa mara ya pili kama hekalu la Roho Mtakatifu, akiwataka watambue na wajiheshimu kwa kuuishi vyema wito wao.
Aliwasisitiza kushuhudia matendo makuu ya Mungu, akiwaasa kuwa kipaumbele ni kuzungumza habari njema kwa watu, na kuwakumbusha kutokuwa manabii waliokufa, wala manabii wasiokuwa na uthubutu.
Hata hivyo, Askofu Mkuu aliwataka wazazi na wasimamizi kuwa mfano bora wa kuigwa na watoto, kwa kuwasaidia kuishi vyema wito wao siku zote za maisha yao.
DODOMA
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amewaasa wataalamu wa sekta za mifugo na uvuvi kupeleka na kufundisha teknolojia za sekta hizo vijijini, ili kuwapa elimu wafugaji kuhusu ufugaji wa kisasa, na hivyo kuleta tija.
Alisema hayo alipotembelea kwenye Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa (Nane Nane) yaliyofanyika Kitaifa mkoani humo.
MOROGORO
Na Winfrida Kobelo-SJMC
Wakazi wanaoishi karibu na Hifadhi ya Hululu iliyopo Kata ya Bunduki, mkoani Morogoro wametakiwa kuitunza hifadhi hiyo.
Kauli hiyo imekuja wakati huu Taifa linapoendelea na harakati za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ambayo yamezidi kuwa tishio duniani kote.
Wakizungumza na gazeti Tumaini Letu hivi karibuni, baadhi ya viongozi wa mazingira wa kata hiyo walisema kuwa kwa sasa wanatumia njia mbalimbali kudhibiti uharibifu wa hifadhi hiyo, ikiwemo kufanya doria za mara kwa mara.
Afisa Misitu wa Kata hiyo, Protches Elias alisema kwamba wamekuwa wakitoa elimu kwa wanakijiji, ili wahakikishe mazingira yanatunzwa, ikiwemo kutokuchoma moto katika misitu iliyomo ndani ya vijiji hivyo.
“Tumekuwa tukitoa elimu kwa vijiji na vitongoji kuhusiana na majanga ya moto pamoja na uanzishwaji wa vitalu vya miti, na upandaji miti. Pia tunafanya doria za mara kwa mara ili kukabiliana na vitendo vya uharibifu kama vile ukataji miti, kilimo na upitishwaji wa mifugo ndani ya hifadhi,” alisema Afisa Misitu huyo, na kuongeza,
“Suala lingine ni ulinzi na uimarishaji wa mipaka ya hifadhi kwa kufyeka na kusafisha mipaka ili miti iliyopo mpakani ikue vizuri na hivyo kuzuia majanga ya moto ambayo yanaweza kusababishwa na mashamba ya wenyeji yaliyo jirani.”
Akizungumzia changamoto wanazokumbana nazo katika kuitunza hifadhi hiyo, Afisa Misitu huyo alisema kuwa changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa watumishi, na baadhi ya wananchi kufanya shughuli za kilimo katika maeneo ya pembezoni mwa hifadhi hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Mazingira katika Kijiji cha Vinile kilichopo karibu na hifadhi hiyo ya Hululu, Paulo Joseph alisema kuwa wananchi ndio watunzaji namba moja wa hifadhi kutokana na kamati mbalimbali za mazingira ambazo zimeundwa kwa ajili ya kusimamia misitu na kupanda miti, kwani misitu ndiyo chanzo cha upatikanaji wa maji.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo aliwaasa wananchi kuendelea kutunza na kuyathamini mazingira kwa kuachana na tabia za kukata miti, kuchoma moto misitu, pamoja na kuharibu vyanzo vya maji, ili kuepuka madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake Veronica Mwenda, mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Mazingira katika Kata ya Bunduki, alieleza kuwa bado wanakumbana na changamoto za matukio ya uharibifu wa misitu, kama vile ukataji hovyo miti.
Naye mkazi wa Kijiji cha Maguruwe kilichopo Kata ya Bunduki, Josephina Christopher, alisema kuwa wameunda baadhi ya vikundi vya upandaji miti katika vitalu kwa ajili ya kutokomeza uhaba wa miti katika misitu hiyo.
“Kwa mfano, pale kijijini kwetu tumekuwa na baadhi ya vikundi mbalimbali mahsusi kwa kupanda miti, na hii ni kwa sababu tunaipenda hifadhi ya Hululu, maana ile ni hazina ya asili tunayojivunia,” alisema Josephina.
Aidha, hifadhi ya Hululu kwa jina lingine hujulikana kama Maporomoko ya Maji ya Hululu, na yana urefu wa sentimita 80 kutoka yanapotoka hadi yanapotiririka, yaliyopo ndani ya msitu wa hifadhi ya mazingira asilia ya Uluguru.
RUKWA
Na Lusungu Helela
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu, amesema kuwa Serikali imepanga kutangaza jumla ya ajira mpya 37, 616, huku ajira za kada ya Ualimu, Afya na kada nyinginezo, ikiwemo kada ya Uhasibu na Ugavi, zikiwa tayari zinaendelea kutangazwa, lengo likiwa ni kupunguza tatizo la upungufu wa watumishi nchini.
Sangu alisema hayo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika vijiji vya Kitete, Laela, Kamsamba na Kavifuti vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipouteliwa kushika wadhifa huo.
Akizungumzia nafasi za ajira ya Ualimu ambazo tayari zimeshatangazwa na Sekretarieti ya Ajira kwenye ngazi ya mikoa kulingana na mahitaji ya mkoa husika,. Sangu alisema kuwa utaratibu wa kuwapata waalimu kwa mwaka huu umeanza kuwa wa tofauti ukilinganisha na ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.
Alifafanua kuwa usaili huo umeanza kufanyika kwa kada ya Ualimu kwa sababu nafasi za ajira za Ualimu ni chache, ukilinganisha na idadi ya walimu wa shule ya msingi na sekondari waliohitimu vyuo mbalimbali hapa nchini, ambapo zaidi ya waalimu 100,000 wapo mitaani wakiwa hawana ajira.
Alisema kuwa Serikali imekuja na uamuzi huo ili kuchagiza dhana ya ushindani kwa lengo la kuhakikisha kila mwenye sifa stahiki, anapata ajira katika mazingira aliyopo pasipo kulazimika kusafiri kwenda Dodoma au Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya usaili.
Kufuatia hatua hiyo. Sangu alitoa wito kwa vijana waliohitimu vyuo mbalimbali hapa nchini kuchangamkia nafasi hizo za ajira, huku akiwataka wajiandae ipasavyo kwa ajili ya usaili huo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kada hiyo ya Ualimu kufanya usaili
Alitumia fursa hiyo kuwatoa wasiwasi wote walioomba nafasi hizo za Ualimu, huku akiwahakikishia kuwa Ofisi yake yenye dhamana ya kusimamia masuala ya ajira nchini, imejizatiti kuhakikisha mchakato huo wa kuwapata waalimu wenye sifa stahiki utakuwa huru na wa haki.
DAR ES SALAAM
Na Mathayo kijazi
Imeelezwa kuwa kila mmoja anatakiwa kujiwekea utaratibu wa kuwasaidia wahitaji, badala ya kujilimbikizia mali, ikiwemo fedha, kwani hakuna aliyefilisika kwa kutoa msaada kwa wenye shida.
Wito huo ulitolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 53 katika Parokia ya Mtakatifu Rita wa Kashia – Temboni, jimboni Dar es Salaam.
“Elisha alivyopewa ile mikate, angeamua kubaki nayo peke yake, lakini aliona kubaki nayo siyo sawa, akaamua kuwagawia wengine. Kwa hiyo ndugu zangu Waamini, nawaomba sana tujiwekee utaratibu huo wa kuwashirikisha wengine, kwa sababu hiyo itasaidia kutuwekea hazina mbinguni,” alisema Askofu Mchamungu.
Aliongeza kuwa fedha haziwezi kumkumbuka mtu aliyezimiliki kwa muda mrefu, bali atakapoamua kuwasaidia wengine, watamkumbuka na kumwombea hata akiwa hayupo duniani.
Alisema pia kuwa hata kama watu wanajitahidi kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia kipato, watambue kwamba hawatakiwi kuwa wabinafsi na mali wanazozipata, kwani uhai walio nao na nguvu za kufanya hivyo, wamepewa na Mungu.
Aliongeza kuwa wapo watu ambao Mungu amewajalia kuwa na fedha ili zitumike kwa ajili ya kuwasaidia wengine, hivyo ni vyema kutekeleza wajibu huo wa kusaidiana.
Aliwasisitiza vijana kutowaacha wazee wahangaike kwa kutokuwasaidia, akiongeza kuwa kupitia Adhimisho hilo la Misa Takatifu ambayo pia ni Siku ya Kuwakumbuka Wazee, wajitahidi kuwasaidia.
Wakati huo huo alitoa wito kwa Waamini kwa pamoja kutokuwasahau wazazi wao waliopo vijijini, kwani wakiwakumbuka, kuwajulia hali, na kuwasaidia, wazee wao watafarijika.
Vile vile, alisema kuwa yeyote anayewasaidia wazazi wake, hubarikiwa, bali anayewaacha wakihangaika na kuteseka, hawezi kufanikiwa katika kila analolifanya.
Alitoa wito kwa Waimarishwa wa Sakramenti Takatifu ya Kipamiara, kuishi maisha ya kumpendeza Mungu na wanadamu, akiwataka kufahamu kwamba, ‘Kipaimara, siyo kwa heri Kanisa’.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Festo Ngonyani alimshukuru Askofu Msaidizi Mchamungu kwa Adhimisho hilo la Misa Takatifu ya kuwaimarisha vijana 53 wa parokia hiyo.
Padri Ngonyani aliongeza kwamba siyo tu kwa ajili ya Kipaimara, bali hata kwenda kuwasalimia kwa mara nyingine, watafarijika kumuona.
Naye Katibu wa Halmashauri ya Walei wa Parokia hiyo, George Kashushura aliwakumbusha wasimamizi kuwafanya vijana hao kuwa ni sehemu ya familia zao.
DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Imeelezwa kuwa moja kati ya dhambi kubwa zinazowasakama wanadamu, ni kigeugeu, wakiaswa kuishi maisha yaliyo mema, huku wakijihami dhidi ya ugeugeu.
Hayo yalisemwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 78 katika Parokia ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu – Makongo Juu, jimboni humo.
“Moja kati ya dhambi kubwa zinazowasakama wanadamu, ni kigeugeu. Kwa hiyo ndugu zangu, nawaomba sana mjiepushe dhidi ya ugeugeu,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Aliwataka waamini hao kuacha tabia ya kwenda kwa waganga wa kienyeji kuaguliwa ili wafanikiwe, akiwasihi kuendelea kumtegemea Yesu Kristo kila wakati, kwani Kristo hapendi njia za mkato katika kufanikiwa.
Aidha, aliwasihi kujifunza kuundwa kwa njia za kuwajibika, akisema kuwa hiyo ndiyo njia pekee itakayowaepusha na njia za mkato.
Katika homilia yake Askofu Mkuu Ruwa’ichi, aliwataka Waamini kuacha uzembe, akiwasisitiza kuwa watu wa kupokea Neno la Mungu na mwili wa Kristu katika maisha yao.
“Tuache uzembe, tuwe watu wa kulishwa Neno la Mungu, na tuwe watu wa kupokea mwili wa Kristu, yaani Ekaristi Takatifu. Hayo mawili, tuyapokee katika hali ya kuwa na Roho safi. Tusipokee Neno la Mungu na mwili wa Kristu katika hali ya Roho zenye masizi, Roho zilizosakamwa na dhambi;
Alisema pia kuwa Mkristo hatakiwi kuona aibu kutokana na kujaa neema, bali aone aibu kutokana na kusakamwa na dhambi katika maisha yake.
Aidha, Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwasihi Waamini kutohangaikia chakula chenye kupita, bali wajitahidi kuhangaikia chakula chenye kudumu, ambacho ni Mapenzi ya Mungu, kwani yeyote anayekula chakula hicho, amekula chakula cha uzima.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Joseph Massenge, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tumaini Media alimshukuru Askofu Mkuu kwa kuadhimisha Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara.
Padri Massenge aliwakumbusha wasimamizi kuwasaidia watoto hao kupokea Sakramenti ya Kitubio, kwani asiyepokea Sakramenti hiyo, ni sawa na mtu asiyeoga.
“Wasimamizi nawaomba sana, wasaidieni watoto hawa kupokea Sakramenti ya Kitubio, kwa sababu asiyepokea Sakramenti ya Kitubio, ni sawa na mtu asiyeoga. Na kama mnavyojua, mtu asiyeoga ananuka, si ndiyo jamani,” alisema Padri Massenge.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei wa Parokia hiyo, Deogratius Mwarabu alimshukuru Askofu Mkuu, huku akimkabidhi kiasi cha fedha Shilingi milioni moja iliyoandaliwa na Parokia hiyo, ikiwa ni kumpongeza kwa Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu huyo.