Dar es Salaam
Na Bruno Bomola
Wakati Mwadhama Polycarp Joseph Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam anaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Ukardinali, sanjari na Miaka 52 ya Upadri wake, amekemea vitendo vya ushoga, akidai vikiendelea, dunia itamalizika.
Adhimisho la Jubilei hiyo pia limeambatana na kumbukizi ya Miaka 39 ya Uaskofu, tangu alipowekwa wakfu Januari 6, mwaka 1984 na Mtakatifu Yohane Paulo II (Papa-1978-2005), Mjini Roma, Italia.
Itakumbukwa kwamba Kardinali Pengo aliyezaliwa Agosti 5 mwaka 1944 katika Kijiji cha Mwazye, mkoani Rukwa, aliwahi kuwa Katibu wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga, kwa miaka miwili kuanzia Juni 1971 hadi 1973.
Akizungumza na Tumaini Media katika kusheherekea Jubilee hiyo, Kardinali Pengo alisema kuwa kwa nini Roma kuna Makardinali wengi kuliko katika Nchi nyingine, ni kwa sababu Roma ndiyo Makao Makuu ya Baba Mtakatifu, na hivyo inafanya kuwe na wasaidizi wengi wa karibu.
“Kazi kubwa ya Kardinali ni kumshauri Baba Mtakatifu, na ndiyo maana Roma wako wengi, ili wawe karibu naye, licha ya wengine kutawanyika katika nchi mbalimbali.
Agano lake na Mungu limetimia
Aidha, Kardinali Pengo alisema kwamba kuhudumu kwake kwa miaka 25 kama Kardinali, siyo kitu cha kawaida, kwa sababu mara nyingi Makardinali wanachaguliwa wakiwa na umri mkubwa, hali inayosababisha wasiishi miaka 25 baada ya hapo.
“Namshukuru Mungu kwa zawadi hii, kwani wanaofahamu historia yangu kwa miaka ya hivi karibuni, wakati wowote nilikuwa tayari kwenda kwa Mwenyezi Mungu, lakini mwenyewe alitaka niwepo hadi sasa,” alisema Kardinali Pengo.
Alibainisha pia kuwa katika jambo la kufurahisha ndoto aliyoota imetimia, kwani alitamani kabla Mungu hajamchukua, ashuhudie Jimbo Kuu la Dar es Salaam liwe limefikisha Parokia 100, na sasa Jimbo hilo lina Parokia 150 na Parokia Teule zinazoendelea vizuri.
“Nilipostaafu zilikuwa Parokia 137 na bado zimeongezeka, na kwa sasa tutafika 200. Ni baraka kwamba Mungu amesikiliza ombi langu, na nitoe moyo wa shukrani kwa waamini wa Dar es Salaam kwa sababu sasa hatutegemei tena wafadhili kutoka nje, kwani wanajikaza kufanya kazi hiyo waamini wenyewe,” aliongeza kusema Kardinali Pengo katika mahojiano maalumu na gazeti Tumaini Letu.
Alisema pia kuwa wakati anashika Madaraka ya kuliongoza Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, kulikuwa na Parokia 20 tu, hivyo hakutegemea misaada kutoka kwa wafadhili, na ndiyo maana amefikia hapo.
Ajivunia Umisionari ulivyoleta Padri Mzawa Mafia
Akizungumzia kuhusu Shemasi mzawa kutoka Parokia ya Mafia, mkoani Pwani, anayetarajia kupata Daraja Takatifu la Upadri Julai 7 mwaka huu, Kardinali Pengo alisema kuwa hiyo ni ishara ya baraka kutoka kwa Mungu, kwa sababu ni kitu ambacho watu walidhani hakiwezekani Mafia kutoa Mapadri kutokana na asili yake.
Kardinali Pengo alisema kuwa, “Hii ni mbegu na matunda ya mwanzo kabisa ya safari ya Umisionari kule Mafia. Natamani siku anakwenda kusherehekea Misa yake ya kwanza, Mungu akinipa uhai, na mimi niwepo kama nitapangiwa na Askofu Mkuu.”
Kuhusu Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu, Kardinali Pengo, alisema kuwa binafsi ana mapenzi na watoto, kwani ni kitu kilicho moyoni mwake, kwa sababu ni rahisi kuwafundisha watoto na kuelewa kwa haraka kuliko watu wazima.
Akemea Ushoga, atoa angalizo dunia kumalizika
Aidha, kuhusu vitendo vya kikatili vinavyoendelea nchini, Kardinali Pengo alisema kwamba wanadamu wameingia kwenye matatizo hayo kwa sababu wamemsahau Mungu, hivyo akiwataka Watanzania kuheshimu misingi iliyowekwa na Mungu, ili kuepukana na majanga hayo.
Kwa mujibu wa Kardinali Pengo, ni vizuri kutafakari namna dhambi ya kwanza ilivyoingia duniani kwa mwanadamu, kwa sababu ya kukaidi agizo la Mungu kwa kula tunda walilozuiliwa na Mwenyezi, kwani kukaidi maagizo ya Mungu, ni kusambaratika kwa watu.
“Kama wanadamu wote tungesema tuishi tu wanaume, tuishi peke yetu na wanawake waishi peke yao, tumechoka na makelele na shida za ndoa, mbona tungejimaliza, na watu bado wanapiga kelele ni uhuru wangu niweze kukaa na mwanaume mwenzangu halafu iwe nini tunapaswa kutambua Mwenyezi Mungu yupo,” alisisitiza Kardinali Pengo.
Alisema kuwa kama wanadamu wanataka kuishi, yawapasa kuziheshimu amri za Mungu, kwa amani na utulivu, kwani kutenda kinyume chake ni kujimaliza wenyewe na kupelekea kupunguza umri wa kuishi.
Ashangaa Mungu alivyomwokoa hatarini
Akieleza namna ambavyo kumtumikia Mungu kumemshangaza, ni baada ya yeye binafsi kukata tamaa na madakatari wakidhani sasa muda wake wa kuishi duniani umekwisha, lakini mpaka sasa Mungu bado amemtunza, na wengi wamekuwa wakishangazwa na hali hiyo akiwa na afya tele.
“Tumwachie Mwenyezi atuelekeze kule anapotaka kwa kila mmoja wetu, na tutekeleze yale yapendezayo machoni pake, hii ndiyo zawadi kubwa na shukrani kwa Mungu,”aliongeza kusema Kardinali Pengo.
Katika kutekeleza kazi ya uinjilishaji, Kardinali Pengo aliwataka waamini na Watanzania kwa ujumla kuendelea kiwezesha Kituo cha Tumaini Media ili kiweze kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa kwa Kanisa kwa ujumla.