Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha
Makala

Makala (58)

Mzungu hajakubali kuwa bin-Adam wote ni sawa, wala kwamba wote ni wa baba mmoja,  Adam.
Pamoja na kwamba alituletea Msahafu wa dini – Biblia wenye kusisitiza “upendo,” hiyo ni ghiliba tupu kwa sababu inawabagua wana-Adam kati ya walio wana wa Taifa teule la Mungu (Israeli), na wana wa Mataifa yasiyo teule. Huko ni kukweza ngozi nyeupe.
Kwa kutumia Mungu wa kujiundia (Yahweh) na Msahafu wa kibeberu, wanaidhinishwa kutugeuza watumwa wao, eti kwamba:
“Na wageni watakuwa watumwa wa kulisha mifugo yenu; na wana wa Mataifa watawalimia na kutunza mashamba ya mizabibu yenu”. Huo ndio ubaguzi wa ubeberu wa kimataifa ambao umedumu hadi leo.
Ubaguzi huo kwa misingi ya rangi ulioasisiwa, kusimikwa na kukomazwa Kimataifa na Mjerumani Johann Friedrich Blumenbach (1752 – 1840) unawagawa bin-Adam kwa viwango vya ubora katika makundi sita ya Watu weupe (Coucassians) kama daraja la kwanza; Wamongolia (Mongoloid) daraja la pili; Watu weusi (Ethiopoid); Wamarekani wenye asili ya Kihindi (Red Indians) na Wahimalaya (Malayans) kama daraja la mwisho kwa ubora.
Wamefika mbali kwa kudai kuwa Mwafrika si Mwana-Adam, yaani hakuzaliwa na Adam. Dhana hiyo mpya inayoitwa “Pre-Adamisma inadai kuwa Mwafrika alikuwepo kabla ya kuumbwa Adam na alikuwa kiumbe asiye na roho.
Mwasisi na Mwenezi wa dhana hiyo inayoshika kasi kipindi hiki cha utandawazi ni Mfaransa Isaac La Peyrere (1596 – 1676). Dhana hiyo inapinga usahihi wa Biblia juu ya uumbaji, ikidai kuwa kulikuwa na watu kabla ya kuumbwa kwa Adam na Hawa.
Anasema kwamba kulikuwa na uumbaji mbili za watu: uumbaji wa kwanza ulikuwa wa dunia nzima na Mwafrika kama mtu wa kwanza; na uumbaji wa pili ulihusu Wayahudi kama Taifa ambalo Adam alikuwa mkuu wake.
Anadai kuwa, Mataifa yote hayatokani na Nuhu, kwamba watu wa Mataifa (wasio wa Taifa teule) hawakutenda wala hawahusiki na dhambi ya asili kwa sababu walikuwepo kabla ya Adam, na hivyo hawakupokea “Sheria” au Maagizo ya Mungu, bali ni Adam na uzao wake pekee. Chini ya dhana hiyo Wazungu ni Wana-Adam, na Mwafrika siye.
Dhana hii ina watetezi wengi miongoni mwa Mataifa ya Ulaya: Mathew Fleming Stephenson, katika kitabu chake “Adamic Race” anasema, “Mungu alitumia mamilioni ya miaka kuumba mtu duni (Mwafrika) kabla ya kuumba mtu bora aina ya Mzungu (Caucasian) juu yake”. Wengine, kwa kutaja wanataaluma wachache tu, ni pamoja na John Harris (The Pre-Adamite Race), Isabelle Duncan (Adamites and Pre-Adamites), na wengine.
Iwe ni kwa mtizamo wa dhana ya “Pre-Adamite”, “Uumbaji” au “Mageuko” (evolution), hakuna ubishi mpaka sasa, kwamba binadamu (mtu) wa kwanza aliishi Loliondo/Ngorongoro zaidi kabla ya mwaka 10,000, Kabla ya Vizazi (KV) ambao ndio mwaka unaosemekana Adam aliumbwa.
Ustaarabu wa mtu huyu ulianza na shughuli za Kilimo, ufugaji, ibada na makazi eneo ambalo sasa linajulikana kama Nubia, au Sudan Kaskazini. Utawala wa kwanza ulianzia Ta-Seti eneo hilo; watu hawa walijulikana kama “Anu”.
Nchi waliyokalia ilijulikana kwa majina mengi, kama vile, Nubia, Kermet, Kush, Ethiopia au Egypt (Misri) na Mji Mkuu ulikuwa Kerma. Nubia imetajwa kwenye Biblia, Kitabu cha Mwanzo 2:11 kama nchi ya Havillah.
Ni Ufalme ulioundwa na watu weusi kutoka eneo la Maziwa Makuu (ANU) miaka ya 5900 Kabla ya Vizazi (KV) na maelfu ya miaka kabla ya Kristo (KK). Hapa ndipo Gharika (la Nuhu) lilipowakuta watu hawa, wakaangamia isipokuwa mtu mmoja – Nuhu na wanae watatu – Yafeti, Shem na Hamu. Hiyo ilikuwa Mwaka 5000 KK. SOMA ZAIDI KWA KUNUNUA TUMAINI LETU.

VATICAN

Na Angela Rwezaura

Kitabu hiki kinapatikana katika lugha ya Kijerumani, ambacho kinasimulia historia ya Ukristo katika dunia.
Kitabu hicho kimeeleza kwa kina kuhusu safari za Papa Fransisko alizotimiza nchini Iraq mwaka 2021, na kuhusu diplomasia ya Vatican katika nchini Iraq.
Matthias Kopp ni mwandishi na Mtaalimumgu ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Baraza la Maaskofu nchini Ujerumani.
Desemba mwaka 2024, Baba Mtakatifu Fransisko alimteua kuwa mshauri wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano.
Dibaji ya Papa Fransisko:
Kwa shukrani ya kumbukumbu ya ziara yangu ya kitume nchini Iraq, ambaye licha ya janga la Uviko 19, na mashaka ya usalama, nilitimiza ziara hiyo kunako Machi 2021 ili kueleza kwa Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema katika Nchi hiyo, upendo wangu na mshikamano wangu.
Nchi hiyo inachukua nafasi daima na kila wakati katika moyo wangu katika sala.
Licha ya matatizo mengi ambayo Iraq inakabiliana nayo, ninatazama  Nchi hiyo kwa matumaini, kwa sababu inayo nguvu maalum.
Nguvu hiyo awali ya yote, ni watu hao hao  nchini Iraq, wale wote wanaoshiriki ujenzi wa jamii ya raia, ambao wanahamasisha demokrasia katika Nchi na ambao wanajibidiisha kwa ajili ya mazungumzo ya wazi na ya kweli kati ya dini.
Kwa njia hiyo, ziara yangu kwa Mkuu Ayatollah wa Najaf, Sayyid Ali Al-Sistani, ilikuwa muhimu na ya maana. Mkutano ule ulikuwa unataka kuwa alama kwa ulimwengu wote kwamba : kufanya vurugu katika jina la dini, ni matumizi mabaya ya dini.
Kama watu wa dini, tunawajibika kuelekeza amani, na lazima kuiishi, kufundisha na kuieneza amani hii.
Katika muktadha huo ninafikiri hata ziara yangu huko Ur, Kusini mwa Iraq, kwa maana kama wawakilishi wa dini mbali mbali, tulizungumza na kusali pamoja, chini ya maelfu na maelefu ya nyota zilizotazamwa na  baba yetu Ibrahimu alipoinua macho yake angani.
Urithi wa utajiri katika historia ya Bimillenaria del Cristianesimo kisayansi, karibu haijavumbuliwa.
Ninafikiri shule za kiteknolojia za Wakristo wa kwanza wa Mesopotamia, uwepo wa amani kwa mamia ya miaka kati ya Wakristo, na Waislamu kati ya Eufrate na Tigri, na tamaduni mbali mbali za ibada ya Kikatoliki katika kanda.
Aidha, mapambano kati ya Madhehebu ya Kikristo, katika nyakati za mateso mwanzoni mwa karne ya 20,  na visasi vingine vya kisiasa  na kwa mwendelezo wa uwepo wa Kikristo, hadi sasa.
Haya yote yanapendeza kwamba katika kazi ya Matthias Kopp, urithi huu na historia hiyo inakuja kuonesha katika muktadha wao mafunzo ya kidini, katika wingi na kwa kuzingatia fasihi nzito.
Mwandishi kwa namna ya pekee anaweka umakini katika jitihada za Kikanisa nchini Iraq na katika shughuli za Vatican,  kwa wawakilishi wake wa kidiplomasia, ambao wanamulika uhasishaji mwingi wa Mapapa kwa ajili ya Iraq na Wakristo wanaoishi ndani mwake.
Kwa njia hiyo, imezaliwa zawadi kama anavyoandika mwandishi mwenyewe, kwa Wakristo nchini Iraq, ambao ninawatia moyo kujihusisha kwa kina zaidi utajiri wao mkubwa wa kihistoria na kudumisha uhai wa urithi wao:
Kwa wakati ujao ambao hata leo hii unahatarishwa kwa sababu ya uhamiaji na ukosefu wa uhakika kisiasa.
Ninataka kueleza kwa kina na kuamini kwamba  haiwezekani kufikiria Iraq bila Wakristo, kwa sababu pamoja na Waamini wengine wote wanawakilisha kwa nguvu utambuzi maalum wa Nchi, ambao tangu karne za kwanza pamekuwa ni mahali pa kuishi, kuvumiliana na kukubaliana wao kwa wao.
Kwa hiyo, Iraq inaweza na kwa watu wake, kuonekana, katika Mashariki ya Kati na katika Ulimwengu kwamba inawezakana kuishi pamoja kwa amani, licha ya tofauti zao.

MOROGORO

Na Angela Kibwana

Katika nyumba moja huko Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro, Lucy Patrick (siyo jina lake halisi), mfanyakazi wa majumbani, anajikuta akifanya kazi kwa saa 18 kila siku, bila kupumzika.
Hajawahi kulipwa mshahara wake wa miezi mitatu, sasa, ambapo malengo yake ya awali ilikuwa ni kujiongezea kipato kusaidia familia yake na mara nyingi anakula mabaki ya chakula cha familia.
Kwa muda mrefu, sauti yake haikusikika, lakini sasa, juhudi za Chama cha Wafanyakazi Wakatoliki (CWW) zimeanza kuleta matumaini kwake baada ya kutoa mafunzo ya kuboresha mahusiano kati ya waajiri na wafanyakazi.”
Wafanyakazi wa majumbani wanakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo kutolipwa mishahara inayoendana na kazi zao, kunyimwa chakula, kupigwa, na kudhulumiwa haki zao za msingi.
Aidha, wengi wao hawana mikataba ya ajira, jambo linalowafanya kukosa ulinzi wa kisheria, hivyo wanajikuta wakifanya kazi kwa mazingira magumu bila msaada wowote wa kisheria au kijamii.
Victor Mackyao, mwanasheria na mwezeshaji wa mafunzo yaliyoandaliwa na (Chama cha Wafanyakazi Majumbani: CWM), anasema kuwa wafanyakazi wa majumbani, mara nyingi hawajui sheria za ajira, wala haki zao za msingi.
Wafanyakazi wa majumbani wengi wao ukiwauliza wanasema wanakumbana na vipigo, wananyanyapaliwa, wanatengwa,wanateswa maeneo wanayoishi siyo rafiki, wanakosa fursa ya matibabu wanapougua, wengine kukosa chombo maalum cha kuwasemea” alisema Mackyao.
Alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwaelimisha wafanyakazi hao wa majumbani ili kujua nini maana ya haki, lakini pia waajiri watambue wajibu wao ni upi kwa wafanyakazi hao ili kujenga usawa katika makundi yote mawili.
Alifafanua kuwa moja ya changamoto zinazochangia wafanyakazi hao wa majumbani kukosa hali zao msingi ni kutokana na vyombo au mamlaka mbalimbali ambazo zina dhamana ya kuwasimamia haki zao, kutowafikia kwa wakati kwa sababu wafanyakazi hao wanatoka kwa waajiri tofauti na maeneo tofauti.
Alisema kuwa tangu Cwm ilipoanza kutoa mafunzo hayo wamebaini kwamba baadhi ya wafanyakazi wa majumbani wanapohojiwa, ambao wanakaa kwao nje ya mwajiri wake, baada ya kuulizwa, wamedai kwamba wanalipwa kiasi cha shilingi elfu 30 au 50, wakati sheria inamtaka alipwe kuanzia 120,000/=.
“Wafanyakazi ambao wanakaa kwa waajiri wao sheria inawataka walipwe shilingi elfu 60, lakini hawalipwi kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo changamoto hizo ndizo zilizotufanya tuweze kupita na kutoa elimu kwa jamii lakini tutoe rai na tuviombe vyombo vyenye mamlaka ya kushughulikia masuala ya wafanyakazi wa majumbani, waweze kutumia mbinu kama tunazotumia sisi, ili waweze kuwafikia kujua changamoto zao na kazitatua wasikae tu mijini.”
Alisema kwamba kazi za majumbani si rahisi, na sheria inakataza ajira ya watoto katika kazi hizi kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, Sura ya 13, Hata hivyo, bado kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu,
Kwa kutambua changamoto hizi, CWM jimbo la Morogoro limeanza kutoa mafunzo kwa waajiri na wafanyakazi wa majumbani katika Dekania ya Kilosa.
Kwa mujibu wa CWM, kati ya wafanyakazi 161 waliopata mafunzo, asilimia 70 hawakuwa wanajua haki zao za msingi, na wala hawajui lolote kuhusu haki yao ya kuwa na mikataba ya kazi, ili kulinda haki zao.
Lengo ni kujenga mahusiano bora kati ya waajiri na wafanyakazi wa majumbani, kwa kuhakikisha haki na wajibu vinazingatiwa pande zote mbili.
Mratibu wa CWM, Edson Yeyeye, alisema kuwa mafunzo haya yalianza mwishoni mwa mwaka 2024 katika Dekania za Kihonda, Morogoro mjini, na sasa yamefikia Kilosa. Tayari wafanyakazi 161 na waajiri 62 wamepatiwa mafunzo hayo, huku Viongozi wa Dini na serikali 27 wakiungwa mkono katika juhudi hizi.
“Lengo letu ni kuhakikisha kila mfanyakazi wa majumbani anapata elimu ya haki zake na waajiri wanajua wajibu wao,” alisema Yeyeye.
Bahati Ramadhani, mmoja wa waajiri walioshiriki mafunzo hayo, alisema, “Ni muhimu elimu hii kufika vijijini kwa sababu huko ndiko wafanyakazi wengi wa majumbani wanatoka, Wengi wanapokuja mjini, wanakosa haki zao kwa sababu hawana mikataba wala hawajui sheria”.
Maria Chalalika, mshiriki mwingine, aliongeza kuwa kunahitajika kuundwa vyombo maalum vya kushughulikia haki za wafanyakazi wa majumbani, hasa kwa wale wanaopelekwa nje ya nchi, bila kujua wanachokwenda kukifanya
Kwa upande wake, Hosea Nikodemas Mgunda, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlimani Boma, aliwapongeza CWM kwa juhudi zao za kutoa elimu hiyo kwa jamii, ili haki za wafanyakazi wa nyumbani ziweze kulindwa na kuthaminiwa.
“Wafanyakazi wa majumbani wanapitia madhila mengi, hivyo tunahitaji kuwa na chama chao maalum ili kuwatetea na kuhakikisha wanapata haki zao.ili kupunguza vitendo vya ukatili miongoni mwao
Hata hivyo, Mgunda aliahidi kutumia mikutano yake ya kijamii kutoa elimu kuhusu haki za wafanyakazi wa majumbani ambavyo anatarajia kufanya kuanzia tarehe mosi Februari mwaka huu 2025.
Mafunzo haya yameongeza uelewa miongoni mwa wafanyakazi na waajiri, ambapo wengi wao sasa wanatambua umuhimu wa mikataba ya ajira, haki ya likizo, na mishahara inayotambulika kisheria.
Hata hivyo, changamoto bado zipo, hasa katika kuwafikia wafanyakazi walioko maeneo ya vijijini, na wale wanaofanyiwa ukatili wa kimya kimya.
Washiriki wa mafunzo hayo walipendekeza kuundwa kwa vyombo maalum vya kushughulikia haki za wafanyakazi wa majumbani, Kuongeza uhamasishaji kuhusu sheria za kazi vijijini na mijini, Kuwapatia wafanyakazi wa majumbani elimu ya malezi na maadili, kwani mara nyingi wao ndio walezi wa karibu wa watoto katika familia nyingi
Mratibu wa CWM, Edson Yeyeye, alisisitiza kuwa jitihada hizi zitaendelea hadi sauti za wafanyakazi wa majumbani zisikike na kuheshimiwa kikamilifu.
 “Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha haki na heshima kwa kila mfanyakazi wa majumbani, kwani mchango wao katika familia na jamii hauwezi kupuuzwa,” alisema Yeyeye.
Sasa ni wakati wa jamii kushirikiana ili kuhakikisha kwamba kila mfanyakazi wa majumbani anapata heshima anayostahili, na mahusiano ya kazi yanajengwa kwa misingi ya haki na usawa.
Nashauri wafanyakazi wa majumbani wapewe elimu ya malezi na maadili mara kwa mara, kwa sababu katika nyumba nyingi za mijini na hata vijijini, sauti ya mfanyakazi wa majumbani ndiyo inayopokelewa kwanza asubuhi, ikiongoza familia katika maandalizi ya siku.
Wakati mwingine, wao ndio waangalizi wa karibu wa watoto; wanahakikisha wanakula, wanavaa, na mara nyingi hata wanasaidia katika kujenga maadili ya msingi kwa watoto hao, ikiwa ni pamoja na kuwafundisha kusoma au kuandika. Hata hivyo, mchango huu wa kipekee mara nyingi unapuuzwa, ukifichwa na mwanga wa jukumu lao la kazi za nyumbani.

Dar es Salaam

Na Pd. Richard Mjigwa- C.PP.S

Mwenyeheri Giovanni Merlini ni Mtume mwenye ari na mwamko wa Fumbo la Pasaka ya Kristo linaloleta wokovu, shuhuda, amini wa Injili na mshauri mwenye busara.
Hayo yamo katika Waraka wake wa Kitume wa Baba Mtakatifu Fransisko wa kumtangaza Mwenyeheri huyo, ambaye Sikukuu yake itaadhimishwa kila mwaka Januari 12.
Mwenyeheri Giovanni (pichani) yeye alikuwa ni mhubiri mahiri; Mshauri mwenye busara na mjumbe wa matumaini na amani katika Kristo Yesu.
Katika maadhimisho ya Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Kristo Yesu, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu anajifunua, kwa watu wake waliokuwa wamepokea Ubatizo wa toba na maondoleo ya dhambi.
Hii ni siku ya Ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. “Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu ninayependezwa naye” (Mt, 3:13-17, Mk, 1:9-11, Lk, 3:21-22). Ni tukio linalotakatifuza maji yote ya Ubatizo, na umuhimu wa maisha ya sala. Rej Lk, 3:21 na katika kusali, Kristo Yesu anawafundisha Wafuasi wake kusali. Rej KKK 2607.
Huu ni mwaliko kwa Waamini kutafakri ufunuo wa Sura na Sauti ya Mungu. Ubatizo wa Bwana unahitimisha maadhimisho ya Kipindi cha Noeli, Mwanzo wa: maisha na Utume wa Kristo na ni siku maalum ya Ubatizo kwa watoto wachanga, changamoto na mwaliko kwa wazazi na walezi kuwarithisha watoto wao zawadi ya imani.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Fransisko, Dominika Januari 12, 2025 amemtangaza Mtumishi wa Mungu Giovanni Merlini, kuwa ni Mwenyeheri na ambaye alizaliwa tarehe 28 Agosti, 1795 huko Spoleto, Perugia nchini Italia.
Akapewa daraja Takatifu la Upadri Desemba 19, 1818. Agosti 15, 1820 akajiunga na Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, lililokuwa limeanzishwa na Mtakatifu Gaspari del Bufalo Agosti 15, 1815. Alijiunga na Shirika baada ya kuvutiwa sana na mahubiri yaliyotolewa na Mtakatifu Gaspari, kuhusu Fumbo la Ukombozi chemchemi ya upendo wa kimisionari.
Kumbe, Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu ni msaada kwa kila Mkristo kwa kuwa Damu ya Kristo ndiyo msingi wa ukombozi wa mwanadamu, na ni kielelezo cha juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa watu wote.
Tasaufi hii ina msingi wake katika, na Neno la Mungu na katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, ambalo ndilo chanzo na kilele cha maisha ya kila siku ya Kanisa, na maisha ya Mkristo kwa jumla.
Tena Ekaristi Takatifu ni ujumuisho mzima wa Imani ya Kikristo, na ni msingi wa mitazamo sahihi ya Kikristo. Rej KKK 1324 na 1327. Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu, Agano Jipya na la Milele, ikawa ni msingi wa maisha na sadaka, kwa bidii ya kutafakari na shauku ya kitume “cum ardore contemplativo et passione apostolica.”
Mwenyeheri Giovanni Merlini aliishi nyakati za Mapinduzi ya Napoleone, wakati wa mchakato wa mafundisho tanzu ya Kanisa. Papa Pio IX Desemba 8, 1854 akatangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili.
Mwenyeheri Giovanni Merlini akatangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili katika maisha ya kila siku kwa kutambua mbegu za Ufalme wa Mungu, na hivyo akajipambanua kuwa ni chombo cha huruma ya Mungu na amani; na shuhuda wa matumaini yasiyotahalisha. “Spes non confundit.”
Kati ya Mwaka 1847 hadi 1873 aliteuliwa kuwa ni Mkuu wa tatu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu. Kama kiongozi, akaonesha utakatifu wa maisha, udugu, ari na mwamko wa kimisionari; ukaribu na majadiliano katika ukweli na uwazi; kupima mang’amuzi ya maisha na utume wa Kimisionari mbele ya Msalaba. Ni katika wakati wa uongozi wake, Shirika likapanuka na kuenea nje ya mipaka ya Italia hadi Kaskazini mwa Ulaya na nchini Marekani.
Katika maisha na utume wake alibahatika kuwa ni kiongozi wa maisha ya kiroho kwa Mtakatifu Maria De Mattias, utume alioutekeleza kwa kipindi cha miaka arobaini na miwili.
Akasaidia kujenga na kuwaimarisha Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu, ASC. Katika mashauri yake alikazia: majadiliano katika utu, heshima na ukuaji wa maisha ya kiroho, daima wakitafuta mapenzi ya Mungu.
Mwenyeheri Giovanni Merlini, alisaidiana na Mtakatifu Gaspari del Bufalo kupyaisha maisha ya Waamini na Makleri kwa namna ya pekee kama yaliyoasisiwa na Papa Pio VII (1800-1823: wa 251) na Pio 1X kwa njia ya mahubiri, mafungo, na hata wakati mwingine akahatarisha maisha yake kwa kutangaza Injili miongoni mwa majangili, kielelezo cha mtume wa msamaha unaobubujika kutoka katika Damu Azizi ya Kristo.
Fumbo la Pasaka ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa na kwamba Waraka wa Kitume wa “Amantissimus human” wa Mwaka 1862 ulionesha umuhimu wa Tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo, na kunako mwaka 1849 katika Waraka wa Kitume wa “Redempti sumus,” Sikukuu ya Damu Azizi ya Yesu, ikatangazwa kuwa ni Sikukuu kwa Kanisa zima. Mwenyeheri Giovanni Merlini akaitupa mkono dunia tarehe 12 Januari 1873 kwa ajali.
Tarehe 10 Mei 1973, Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, likamtangaza kuwa ni Mtumishi wa Mungu. Tarehe 23 Mei 2024 Baba Mtakatifu Fransisko akaruhusu atangazwe kuwa ni Mwenyeheri. Katika Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Dominika tarehe 12 Januari 2025 akatangazwa kuwa ni Mwenyeheri.
Jumamosi tarehe 11 Januari 2025, kukafanyika Ibada ya mkesha wa nguvu ukiongozwa na AskofuVincenzo Viva wa Jimbo Katoliki Albano, nchini Italia. Misa ya shukrani imeadhimishwa Jumatatu, tarehe 13 Januari 2025 kwa kuongozwa na Askofu Mkuu Renato Boccardo wa Jimbo Kuu la Spoleto, Italia.
Baba Mtakatifu katika Waraka wake wa Kitume wa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Giovanni Merlini kuwa ni Mwenyeheri, anasema, kwa hakika alikuwa ni Mtume mwenye ari na mwamko wa Fumbo la Pasaka ya Kristo linaloleta wokovu, shuhuda amini wa Injili na mshauri mwenye busara.
Sikukuu yake itakuwa inaadhimishwa kila mwaka tarehe 12 Januari. Baba Mtakatifu Fransisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana alisema, Giovanni Merlini, Padri Mmisionari wa Shirika la Damu Azizi, alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume kwa watu wa Mungu, akawa mshauri mwenye busara kwa roho nyingi, na mjumbe wa amani.

Mwanza

Na Paul Mabuga

Kuna makundi kadhaa ya vizazi kutokana na mazingira na matukio katika nyakati mbali mbali.
Mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia, na hasa mapinduzi ya kidijitali, yamechangia zaidi kuongezeka kwa tofauti kati ya makundi ya vizazi, hali ambayo imeathiri mahusiano, mitindo ya maisha, na makuzi.
Uhusiano wa kizazi kimoja kwenda kingine, limekuwa ni jambo lenye changamoto kulimudu. Katika muktadha huo, mwandishi wetu Paul Mabuga  anaangalia uhusiano kati ya wanandoa kutoka zama za ‘baby boomer’ na ‘milenia’.
Harufu ya sangara anayekaangwa, imetanda katika nyumba moja iliyopo katika mtaa wa Nyamanoro jijini Mwanza. Kwa hakika inavutia, kwani hata kwa mwenye hisia ndogo ya kunusa, anaweza kuitambua, na kwa mwenye njaa aliye jirani, ni lazima aombe msaada.
Baba mwenye nyumba tunayemwita Adam Fungamwango, yupo sebuleni akisoma gazeti. Unamtazama, unapokewa na sura yenye mikunjo inayokutangazia kuwa Bwana huyu umri wake kwa makadirio ni miaka 64. Na wewe ni mgeni pekee sebuleni.
“Karibu, lakini kabla ya yote fanya ufanyavyo kwenye mahojiano, lakini jina langu sitaki lijulikane! Vinginevyo hakuna mahojiano hapa,” anasema bwana huyu akikukaribisha na kuendelea na mazunguzo baada ya kuhakikishiwa kuwa litatumika jina bandia ili kuficha utambulisho wake, “Mie nilikuwa dereva, na nimeendesha maafisa wengi wakubwa, na sasa ni miaka minne tangu nimestaafu.”
Anasema, mkewe ambaye naye, tunamtambulisha, kwa jina la bandia la Diana Fungamwango, bado ni mfanyakazi kama katibu muhtasis katika moja ya mashirika ya umma jijini Mwanza, na ana umri wa miaka 44 kwa sasa. Walioana miaka 23 iliyopita, na kwamba  Diana anatumia muda mwingi kazini isopokuwa siku za mwisho wa juma.
Diana ambaye ndiye anayekaanga samaki, hana makuu, katopea katika simu yake ya mkononi akitaradika na yaliyomo. Pengine anaanza leo wasanii gani wamechambana kwenye mitandao,  anashuka na wale wasemaji wa timu za mpira na washabiki wao, na baadaye anatambaa na darasa la sifa za mume bora, na kumalizia na hadithi. Yeye ameshika mbili na wala hazimponyoki, huku ana simu, na kule  anakaanga.
Hii ni ndoa kati ya mume  ambaye katika zama za vizazi, yupo kwenye kundi la ‘Baby Boomer,’ ambao wamezaliwa kati ya miaka ya 1946 na1964  na mke ambaye yupo kwenye lile linalojulikana kama ‘milenia’, ambao walizaliwa kati ya  1981 na1996. Makundi haya ya vizazi na mengine,  kila moja  lina sifa zake,
Kwa maana hiyo  watu katika kundi la ‘baby boomer’ wana umri kati ya miaka 61 na 79 kwa mwaka huu wa 2025. Kwa idadi kulingana na taasisi mbali mbali [Shirika la Takwimu la Taifa linalosimamia Sensa ya Watu na Makazi, (National Bereau of Statistics: NBS), na Benki ya Dunia, idadi yao hapa nchini ni kama milioni tatu, ama asilimia tano, ya Watanzania .  
Wale walioko kwenye kundi la milenia, wana umri kati ya miaka 29 na 44, na idadi yao kulingana na taasisi hizo,  inakadiriwa kuwa kama nilioni 12 ama asilimia 20 ya Watanzania kwa kadirio. Ni sawa na kusema ni  kundi lenye watu wengi, na ambalo kwa idadi, ni mara nne ya lile la ‘baby’ boomer. Licha ya changamoto kadhaa, lakini kuna ndoa baina ya makundi haya kama ilivyo katika makala haya.
“Ni kweli kuna tofauti za kimtazamo katika baadhi ya mambo kati yangu na mke wangu, mathalan, mimi najali sana mambo ya maendeleo kitaifa, nikiona mtu anaonewa siwezi kupita bila kuhakikisha haki inapatikana;
Ninajali majaliwa ya taifa letu siku za usoni, na nipo tayari kujitolea kwa ajili ya jamii yangu,” anasema Fungamwango wakati alipotakiwa kufafanua baadhi ya mambo   anayopendelea katika fikra zake,
Sifa hizi anazozieleza  Mfungamwango, zinaelezwa na watafiti kuwa zinatokana na ukweli kwamba, ‘baby boomers’ walizaliwa katika kipindi cha harakati za kuleta mabadiliko katika jamii, na kupambania haki za binadamu, na hii ndiyo sababu ya wao kuwa hivi,
Kwa upande mwingine, tafiti zinaonesha kizazi cha  milenia, kimetekwa na  teknolojia, hasa kwa sababu wamekulia katika mazingira ya kuibuka na kushamiri kwa matumizi ya  ‘internet’. Wana mapokeo yenye uwanda mkubwa ikilinganishwa na baby boomer na hivyo kuwafanya wao kuwa huru. Wanapenda kuwa wajasirimali na wanafanya kazi kwa uwiano na uhuru. Wanajali sana mitindo ya mavazi na vifaa vingine

DODOMA

Na Angela Kibwana

Watu wenye ulemavu sawa na makundi mengine katika jamii, wana haki ya kunufaika na upatikanaji  wa haki ya Afya  ya Uzazi, kama haki ya msingi ya binadamu bila vikwazo, unyanyapaa  na ubaguzi wa aina yoyote.
Haki ya Afya ya Uzazi kwa watu wenye ulemavu imetamkwa na kuelekezwa kwenye Sera, Miongozo na Sheria mbalimbali za Kimataifa, Kikanda na Kitaifa kama vile: Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (2006), kifungu cha 25 (Article 25), umesisitiza watu wenye ulemavu, wana haki ya kupata huduma za afya bila ubaguzi
Sheria ya Tanzania kwa Watu Wenye Ulemavu (2010) kifungu cha 26, Kifungu kidogo cha Kwanza hadi cha tatu limesisitiza kuhusu haki ya kupata huduma ya afya na utengamao kwa watu wenye ulemavu, bila ubaguzi,Sera ya Watu Wenye Ulemavu ya Mwaka 2004, imetambua suala la ulemavu kama haki za msingi za  binadamu.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, imeeleza watu wenye ulemavu ni wale wote wenye changamoto za muda mrefu za kimaumbile, kiakili na katika mfumo wa fahamu (intellectual or sensory), hivyo kukosa na kushindwa kushiriki sawa na makundi mengine ya kijamii katika kuzifikia fursa mbalimbali.
Takribani asilimia 11 ya watu kuanzia umri wa miaka saba (7) na kuendelea, wanaishi na ulemavu wa aina fulani, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 9.3 (Sensa Mwaka 2012).
Hata hivyo, takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watu wenye ulemavu inatofautiana kati ya kijijini kwa asilimia 11.5 na mjini asilimia 10.6.
Mkoa wa Dodoma una idadi ya watu 299,689, sawa na asilimia 12.3 zaidi ya kiwango cha kitaifa cha asilimia 11, ukiwa ni mkoa wa sita kwa idadi kubwa ya watu wenye ulemavu (Sensa Mwaka 2022) nchini.
Pamoja na jitahada zote zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika na serikali, asasi zisizo za kiserikali na wadau wa maendeleo, kundi la watu wenye ulemavu, wameendelea kukabiliwa na changamoto nyingi za afya ya uzazi, zikijumuisha changamoto za kimazingira na kisera zinazo athiri upatikanaji na ufikikaji wa huduma za Afya, kwa mfano miundo mbinu isiyo rafiki, umbali na gharama za huduma na kukosekana kwa teknolojia saidizi.
Pia, unyanyapaa na mtazamo hasi kutoka kwa wana familia, jamii na watoa huduma za afya dhidi ya  haki ya huduma za Afya ya Uzazi kwa watu wenye ulemavu; Ujumuishaji hafifu wa watu wenye ulemavu kwenye programu na mipango mbalimbali ya afya; watoa huduma za afya kutokuwa na uelewa kuhusu masuala yanayohusu mahitaji ya watu wenye ulemavu, kama vile lugha ya alama, pamoja na namna ya kutoa huduma rafiki kwao; matumizi hafifu, pamoja na kutokuwa na takwimu sahihi za watu wenye ulemavu ili kujumuishwa kwenye mipango, bajeti na huduma za afya katika ngazi ya halmashauri, vituo vya kutolea huduma za afya, na jamii kwa ujumla.
Changamoto hizo zimeongeza uhatarishi zaidi kwa makundi ya wanawake na vijanawenye ulemavu, hali ikiwa mbaya  zaidi kwa wale wanaoishi vijijini wakikabiliwa na umaskini uliokithiri, pamoja na  ukatili wa kingono, kama vile Ubakaji na ndoa za kulazimishwa.
Kwa kutambua changamoto na umuhimu wa haki ya hudumu za Afya ya uzazi kwa watu wenye ulemavu kama ilivyoainishwa katika Sera, Miongozo na Sheria za Kimataifa, Kikanda na Kitaifa; Shirika la Marie Stopes Tanzania, kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Watanzania chini, ya ufadhili wa Marie Stopes International (MSI) kupitia mradi wa Investiment Fund (IF), wameligeukia kundi hili ambalo halijafikiwa ipasavyo  kwa kuwekeza fedha, utaalam na miundombinu, ili kutengeneza mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu kuzifikia huduma bora za Afya ya Uzazi.
Hayo ni kama vile, Uzazi wa Mpango, Huduma wakati wa Ujauazito, Kujifungua, baada ya kujifungua, Ukatili wa Kijinsia na Ukatili dhidi ya watoto, elimu na taarifa sahihi kuhusu  Afya ya Uzazi na Ujinsia, pamoja na ushiriki wa watu wenye ulemavu katika masuala yanayo athiri maisha yao, ikiwepo Afya Uzazi na Ujinsia kama ilivyoelezwa na Ndugu Goryo Moris Kitege, mtoa huduma za afya ya uzazi wa mpango kutoka Marie Stopes Tanzania
Pia, Ndugu Goryo alisema kuwa Shirika la Marie Stopes Tanzania kwa kushirikiana na Serikali, wanaendelea kuona namna watakavyowajengea uwezo watoa huduma za afya namna kuwahudumia watu wenye ulemavu, pamoja na kufanya ulaghabishi (advocacy), kuhusu uboreshaji wa mazingira wezeshi ili kufikia kundi kubwa la watu wenye ulemavu wa aina mbali mbali nchini.
Kwa mujibu wa  Ndugu  Amina Issa anayeishi na ulemavu wa kusikia kutoka Chama cha Viziwi Dodoma, anasema,  “Mara nyingi hatupati huduma stahiki kutoka kwa watoa huduma za afya kwa kuwa watoa huduma  hawajui Lugha ya Alama”
Pia, Amina anatoa mfano wa unyanyapaa wanaokutana nao watu wenye ulemavu, akisema, “Kuna wakati unakutana na kauli za kudhalilisha, kama vile ‘Hata wewe mtu mwenye ulemavu umeweza kupata ujauzito?’ Kauli hizi zina tuumiza sana,” kwani na sisi tunahisia na tuna haki ya kuwa na familia, pamoja na kufurahia maisha ya mahusiano na ujinsia kama watu wengine” hali hii inakatisha tamaa kwenda kupata huduma.
Vile vile katika kuendeleza jitahada za kuwafikia watu wenye ulemavu katika masuala ya Afya Uzazi; Marie Stopes Tanzania kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), wameendelea kutoa elimu na huduma bora za Afya ya Uzazi ambapo watu zaidi ya 300 wenye ulemavuwamepatiwa huduma na elimu kuhusu afya ya uzazi.
Justus Ngwantalima, Katibu wa SHIVYAWATA, anasisitiza kwamba ni muhimu kwa jamii kuwa na mtazamo chanya dhidi ya watu wenye ulemavu, ili kufanikisha lengo la usawa katika jamii kwa mujibu wa sera na sheria za nchi.
Kwa mujibu wa Omary Lubuva,  Mwenyekiti wa SHIVYAWATA  Dodoma,kuna haja ya kuboresha mfumo wa mawasiliano ili kuimarisha upatikanaji wa huduma bora  kwa watu wenye ulemavu.
Pia, wataalamu wa afya wanapaswa kupewa mafunzo maalum ya kushughulikia mahitaji ya kundi hili.
Aidha, watu wenye ulemavu wanapaswa kushirikishwa katika kupanga, kutekeleza na kutathmini mipango na bajeti za afya kama ilivyoelekezwa kwenye sera na miongozo mbalimbali ya kimataifa, na ya nchi kwa ujumla.
Hata hivyo, aliwashukuru Marie Stopes Tanzania pamoja na serikali kwa jitahada zao katika kuwashirikisha kushughulikia mahitaji yao; kwani si jambo jepesi kulifikia kundi kubwa kama hili la watu wenye mahitaji maalumu kwa wakati mmoja, hivyo nguvu ielekezwe  pia  kwa watu wenye ulemavu  walio vijijini kwa njia shirikishi na  endelevu.
Katika mahojiano ya mwandishi wetu na Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto wa Wilaya ya Bahi, Ndugu Agnes Mwabungulu, anasema kuwa vituo vingi vya afya havina miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu.
Pia, anabainisha ukosefu wa wataalamu wenye ujuzi wa Lugha ya Alama kama changamoto kubwa.
Hata hivyo, amesema kuwa serikali kwa kutumia rasilimali chache zilizopo, pamoja na kupitia ushirikiano na wadau, wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali zinazo athiri utoaji, upatikanaji na utumiaji wa huduma za afya uzazi kwa watu wenye ulemavu, kulingana na sera na miongozo ya nchi.
Aliongeza kwa kusema  kuwa jitahada za kuwafikia watu wenye ulemavu, hazilengi tu kuwafikia katika hali yao ya uhitaji, bali kuzuia ulemavu kwa watoto wanaowazaa, unaoweza kuchangiwa na kukosekana kwa huduma bora kabla, wakati wa ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua. Hivyo kuongeza changamoto zaidi kwao, serikali, jamii na watoto watakaozaliwa na ulemavu wa aina mbalimbali.
Mwisho, amewashukuru Marie  Stopes Tanzania na wadau wa maendeleo kwa ushirikiano wa, na kazi nzuri wanayoifanya katika Halmashauri ya Bahi, ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za Afya ya Uzazi kwa mtoto na vijana.
Pia, wanawakaribisha kwa ushirikiano zaidi pamoja na wadau wengine, ili kuwakufikia watu wenye ulemavu, pamoja na makundi mengine yenye changamoto katika jamii.

DAR ES SALAAM

Na Pd. Gaston George Mkude

Amani na Salama!
Mwinjili Marko wakati anaandika sehemu ya Injili ya leo, himaya ya Kirumi ilikuwa imetoka katika vita na mabalaa mengi, mfano magonjwa ya milipuko na uvamizi wa wadudu katika mashamba yao.
  Si tu himaya ya Kirumi, bali hata Jumuiya ya Wakristo katika himaya ile walikuwa wametoka kupitia kipindi kigumu cha mateso na madhulumu ya Mfalme Nero, aliyewatesa na kuwaua Wakristo wale wa kwanza. Hivyo katika mazingira ya namna hii magumu na yenye mateso mengi waamini walikuwa wanajiuliza nini maana ya haya yote na kwa nini wanapitia hayo yote. Hata nasi leo dunia nzima tunajiuliza maswali mengi mintarafu majanga mbali mbali, kwa nini Mungu anaruhusu tujaribiwe, tupatwe na kupitia kipindi kigumu namna hii? Nini hasa maana na lengo lake?
Mwinjili Marko ni katika mazingira ya namna hii anaandika sehemu ya Injili hii ya leo yenye aina ya uandishi ya kiapokaliptiko. Apokaliptiko ni neno lenye asili ya Kigiriki litokanalo na maneno mawili ambayo ni apo likimaanisha kuweka mbali au tenganisha, pamoja na kaliptiko likimaanisha weka bayana.
Hivyo aina ya uandishi ya kiapoliptiko ni ile inayotumia lugha isiyo kuwa wazi sana, ni lugha ya mficho hivyo kupata ujumbe wake ni lazima kufunua au kufumbua mafumbo na lugha ile ya mficho. Tunaweza kutumia lugha ya vijana ya kileo ni kufungua code (decodification)!
Na ndio mwaliko wa Bwana wetu Yesu Kristo katika Injili ya leo anapotuonya tusidanganyike tunapoona mambo hayo yakitokea katika ulimwengu na nyakati zetu. Hata katika nyakati zetu kuna mengi yanayotokea, na hata mara kadhaa kushawishika kusema mwisho wa dunia umekaribia. Hiyo pia ilikuwa ni hofu ya Wakristo wale wa mwanzo, hivyo mwinjili anaona hitaji la kuwaandikia ujumbe huu wa kiapokaliptiko.
Marko mwinjili anatumia lugha ya picha ya kiapokaliptiko kama vile jua na mwezi na ishara nyingine za angani. Kwa watu wa mashariki ya kati walikuwa wanaabudu ishara za angani kama jua na mwezi kama miungu yao, na hivyo hata kutolea sadaka pale wanapoona kuwa mambo yao yanakwenda kinyume na matarajio yao.
Musa anawaalika Wanawaisraeli kumwabudu Mungu wa kweli na sio nyota au jua au mwezi wa angani. (Kumbukumbu la Torati 4:19) Hata Nabii Isaya pia anaawalika kumwabudu Mungu wa kweli na si nyota wala jua wala mwezi. “Nyota na vilimia vyake angani hazitaangaza; jua linapochomoza litakuwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake” (Isaya 13:10)
Ujumbe huu haukuwa kwa ajili ya kuwatisha na kuwaogofya, kuwa jua na mwezi na nyota zitaacha kutoa mwanga wake wa asili, bali kuwatia matumaini kuwa nuru na mwanga wa kweli unatoka kwa Mungu mwenyewe na si katika vitu vya angani. Hivyo ni ujumbe wa furaha na matumaini. Mwanga na nuru ya kweli ni Yesu Kristo mwenyewe katika maisha ya kila mfuasi wake.
Na ndio mwinjili Marko anaandika sehemu hii ya Injili, ambapo Yesu Kristo anatumia pia lugha hii ya kiapokaliptiko kwa lengo la kuwafariji waamini wanaopitia kipindi kigumu cha mateso na madhulumu. Na kwetu leo ni neno la faraja na matumaini hata kama tunapitia katika kipindi chenye magumu na changamoto nyingi katika maisha.
Ni kawaida kujiuliza maswali nini maana ya magumu na mateso katika maisha yetu, na hata tunapojibidisha kusali na kuwa waaminifu katika imani yetu, bado tunakutwa na mahangaiko katika maisha ya siku kwa siku. Nini maana ya mateso, kwa nini mateso na magumu katika maisha ya ufuasi?
Tunaalikwa kunyanyua vichwa juu kwani wokovu wetu unakaribia, ulimwengu mpya wa ufalme wake Mungu. Mwanzo mpya ambapo mtawala mpya ni Mungu mwenyewe anayetaka kukaa na kuwaongoza watu wake. Ni mwanzo wa ufalme wa Upendo, Amani na Haki.
Dhiki, jua kutiwa giza, mwezi kukoma kutoa mwanga wake, nyota zikianguka na nguvu za mbinguni kutikisika, zote hizi ni ishara ya yule muovu na uovu ulimwenguni. Ni kwa ujio wa Yesu Kristo ulimwenguni basi yule muovu na uovu hauna nguvu tena, hauna nafasi tena kwani tunaalikwa kuunda ulimwengu mpya, ndio ufalme wa Mungu kati yetu, katika maisha yetu.
Ni ujumbe wa faraja kuwa Mungu mwenyewe atamtuma malaika wake, hapa malaika pia ni lugha ya kiapokaliptiko likimaanisha mjumbe wa Mungu ambaye ujio wake sio kuja kuhukumu ulimwengu, bali kuwaunganisha wana wake kutoka pande zote za dunia baada ya kutawanywa na yule mwovu.
Mwana wa mtu hataruhusu wapotee bali atawakusanya wote. Ni mjumbe wa Habari Njema ya wokovu kwa watu wote bila ubaguzi wa aina yeyote, mjumbe huyu ndio kila mmoja wetu anaposhiriki katika kueeneza Ufalme wa Mungu hapa duniani, kuwa wajumbe wa kweli za Injili kwa maneno na matendo yetu. SOMA ZAIDI...

VATICAN

Na Sr. Angela Rwezaura

Katika Ripoti mpya kutoka UNESCO, inashutumu kuwa mwaka 2022-2023 wafanyakazi 162 wa vyombo vya habari waliuawa,karibu nusu katika maeneo ya vita na kutokujali kungali juu sana.
Idadi ya waandishi wa habari wanawake ambao walikuwa waathiriwa pia iliongezeka,14.
Hii ndiyo sababu hatua ya haraka inaombwa kutoka kwa Mataifa. Kampeni ya”Kuna historia nyuma ya historia”iliandaliwa na mwongozo wa usaidizi wa kisaikolojia ukachapishwa.
“Mnamo 2022 na 2023, kila baada ya siku nne mwandishi wa habari aliuawa kwa kufanya kazi yao: kutafuta ukweli. Katika idadi kubwa ya kesi hakuna mtu anayewajibisha.” Hii iliripotiwa na Audrey Azoulay, mkurugenzi mkuu wa UNESCO, ambaye alichapisha ripoti yake mpya Novemba 2, 2024 wakati wa Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Kutokujali kwa Uhalifu dhidi ya Waandishi wa Habari.
Asilimia 85 ya mauaji ya waandishi wa habari ulimwenguni kote hayaadhibiwi, takwimu ambayo inasisitiza uzito wa hali hiyo, licha ya maendeleo madogo tangu 2018, wakati kiwango cha kutokujali kwa mauaji yaliyorekodiwa tangu 2006 kilikuwa asilimia 89.
Asilimia 95 mwaka 2012
Pamoja na ripoti yake, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)linatoa wito kwa nchi zote wanachama wake kufanya zaidi ili kuhakikisha kwamba uhalifu huu haukomi bila kuadhibiwa,  Azoulay alieleza zaidi - kushitaki na kuwatia hatiani wenye hatia ni nyenzo ya msingi ya kuzuia mashambulizi ya baadaye dhidi ya waandishi wa habari.”
 Ingawa UNESCO inaona kuboreka kwa mwelekeo huo, ikizingatiwa kwamba kiwango cha kutokujali kilikuwa 95% miaka kumi na miwili iliyopita, inatoa wito kwa Mataifa “kuongeza kwa kiasi kikubwa juhudi zao za kuzuia uhalifu mpya dhidi ya waandishi wa habari.” Katika miaka miwili iliyopita waathirika 162, ambapo 14 wanawake.
Katika kipindi cha miaka miwili 2022-2023, kipindi kilichoakisiwa na ripoti mpya, waandishi wa habari 162 waliuawa, karibu nusu yao katika nchi ambazo migogoro ya silaha ilikuwa ikiendelea, wakati katika kipindi cha miaka miwili iliyopita asilimia ilikuwa asilimia 38.
Katika nchi nyingine, waandishi wa habari wengi wameuawa kwa kujaribu kusema ukweli kuhusu uhalifu wa kupangwa, rushwa au kuripoti maandamano ya umma. UNESCO pia inaripoti ukweli mwingine wa kutisha: idadi ya waandishi wa habari wanawake waliouawa katika kipindi cha miaka miwili, 14 kwa jumla, ni ya juu zaidi tangu 2017.
Kampeni “Kuna historia nyuma ya historia”
Ili kukabiliana na hali ya kutokujali, shirika la Umoja wa Mataifa leo linazindua kampeni mpya ya kila mwaka ya kimataifa ya kuhamasisha umma kuhusu ukatili dhidi ya waandishi wa habari.
Ukiwa na mada “Kuna historia nyuma ya historia, mpango huo unalenga kuleta umakini kwa uhalifu dhidi ya vyombo vya habari, kupitia makala na ushuhuda zilizochapishwa ulimwenguni kote.
Zaidi ya hayo, tarehe 6 Novemba, UNESCO itaandaa mkutano wa kimataifa kuhusu Usalama wa Waandishi wa Habari katika Migogoro na Dharura mjini Addis Ababa, kwa ushirikiano na Umoja wa Afrika.
Wakati wa hafla hiyo, Daftari la Kimataifa la Mbinu za Kitaifa za Usalama kwa Waandishi wa Habari litawasilishwa, ambalo linakusanya sera za ulinzi wa wanahabari zinazotekelezwa katika nchi 56 na angalau mipango 12 ya kitaifa.
Mwongozo wa msaada wa kisaikolojia
UNESCO pia itachapisha mwongozo kwa wanasaikolojia wanaofanya kazi na waandishi wa habari katika hali za dharura, kwa ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Vyombo vya Habari vya Wanawake (IWMF).
Mwongozo huo, unaolenga hasa wanawake, utawapa wanasaikolojia zana za kuleta utulivu wa michakato ya kihemko na kiakili ya waathiriwa wa matukio ya kiwewe, kuwasaidia kufanya maamuzi ya busara, ya msingi kwa maisha yao, na kupunguza tabia za msukumo ambazo zinaweza kuwaweka hatarini zaidi.
UNESCO, Umoja waonya
Likiwa na nchi wanachama 194, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) linachangia amani na usalama kupitia ushirikiano wa kimataifa katika elimu, sayansi, utamaduni, mawasiliano na habari.
Ikiwa na makao yake makuu mjini Paris, UNESCO ina ofisi katika nchi 54 na inaajiri zaidi ya watu 2,300.
 Inasimamia zaidi ya Maeneo elfu mbili ya Urithi wa Dunia, Hifadhi za Biosphere na Geoparks za Ulimwenguni, mitandao ya Miji Ubunifu, Jumuishi, ya Kujifunza na Endelevu, na zaidi ya shule elfu kumi na tatu zinazohusiana, viti vya vyuo vikuu, vituo vya mafunzo na utafiti.

KIGOMA

Na Mathayo Kijazi

Katika kuhakikisha familia, jamii, na hata Kanisa kwa ujumla linaendelea kuwa na watu wenye maadili ya kumpendeza Mungu, ni lazima familia zijengwe vyema, ili ziweze kudumu katika misingi iliyo bora.
Zipo njia mbalimbali zinazoweza kutumika kujenga jamii iliyo bora kupitia katika familia zao, zikiwemo semina za Kanisa, mikutano, makongamano, pamoja na mafundisho mbalimbali.
Katika jitihada hizo za kujenga familia, Utume wa Uimarishaji wa Familia Tanzania (UFATA), hivi karibuni ulifanya Mkutano wake Mkuu wa Kitaifa katika Jimbo Katoliki la Kigoma.
Vile vile, ndani ya Mkutano huo ilifanyika Semina iliyohusisha mada mbalimbali zilizolenga familia, mwenendo wake, pamoja na tafakari mbalimbali.
Akiwasilisha mada isemayo ‘Familia imara ni msingi wa utu wa mtu’, Mkuu wa Chuo cha Songea Catholic Institute of Technical Education, kilichopo Songea, mkoani Ruvuma, Padri Longino Rutangwelera Kamuhabwa wa Jimbo Katoliki la Bukoba, anasema kwamba kwa kuumbwa kwake na kwa hulka yake, utu wa mtu ni wa kuheshimiwa na umetakaswa.
Padri Kamuhabwa anasema kwamba Familia ni Taasisi ya Kimungu kati ya wanadamu, kwa ajli ya kuendeleza na kulinda heshima ya utu wa mtu, na kwamba kuheshimu familia na utu wa mtu, ni kumheshimu Mungu aliye chimbuko lake.
Anaongeza kwamba mwanadamu anatakiwa kuheshimiwa na kuthaminiwa kama njia mojawapo ya kumheshimu na kumthamini Mungu, kwani ameumbwa kwa malengo ya kumjua, kumpenda, kumtumikia Mungu na kutafuta Ufalme wake.
Padri huyo anabainisha pia kuwa mwanadamu ni wajibu wake kutambua kwamba ameumbwa pamoja na wanadamu wengine, kwani huo ni mpango wa Mungu kuwa mwanadamu atimize malengo ya kuumbwa kwake akiwa kundini.
Anasema pia kwamba mwanadamu ni muhitaji, mhanga na dhaifu, hivyo, anahitaji kuhubiriwa, kulindwa, kutetewa, kukemewa pamoja na kuelekezwa.
Anabainisha pia kwamba katika kuwa kiumbe muhitaji, mwanadamu kwa hulka yake, Mungu alimuumba mtu akiwa na njaa na kiu ya kufikia ukamilifu, na kuongeza kuwa ni katika hali hiyo, mtu hutafuta, husali, hufanya kazi ili afikie kile cha kumfanya awe mkamilifu. Katika kutafuta huko, Padri huyo anasema kwamba mwanadamu pengine hupatia, na pengine hukosea.
Pia, Padri huyo anasema kwamba nyenzo za kumsaidia wanadamu kufikia kile anachokihitaji, ni pamoja na Sala, Neno la Mungu, Maisha ya sakramenti, pamoja na Maisha ya familia.
Vile vile, anasema kuwa kwa hulka yake, mwanadamu ameumbiwa kwanye jamii (familia), na kwa asili yake, ana mwelekeo wa kuishi au kushirikiana na wanadamu wengine.
“Mwanadamu anafaidika kwa kushirikiana na wanadamu wengine. Kukamilisha na kukamilishwa na wengine (complementarity principle). Kutegemeza na kutegemezwa na wengine (synergy principle). Mtu ni ufunuo na uwepo wa Mungu kati ya watu (transcendental being)…
“Kadiri ya Edith Stein (Mtakatifu Theresa wa Msalaba) mtu ni Epiphania - anafunua wema na upendo wa Kimungu kwa wengine. Kadri ya Mtakatifu Thomas Aquinas, kupitia ubinadamu wetu, Mungu yu pamoja nasi = Emmanuel. Kristu aliutwaa ubinadamu wetu ili sisi tukwezwe na kuushiriki Umungu wake. Kwa hiyo, mtu ni ufunuo wa uwepo wa Mungu kati yetu. Mtu ni zaidi ya yale unayoyaona,” anasema Padri huyo.
Sambamba na hayo, Padri Kamuhabwa anaongeza kwamba mwanadamu ni kiumbe hisia, kwani kwa hulka yake anaweza kufurahi au kukasirika; kupenda au kuchukia; kuwa na vionjo mbalimbali; kukubaliana pamoja na kutofautiana na wengine.
Anasema kwamba hiyo inaleta uhalali wa mtu kupenda na kupendwa, kujali na kujaliwa, kuheshimu mawazo na maoni ya mtu, kumpa mtu nafasi ya kuchagua anachokitaka, na kuacha asichokipenda.
Kwa nini utu wa mtu uheshimiwe na kulindwa?
Padri Kamuhabwa anabainisha kwamba ni vizuri kutumia sababu moja kati ya hizi, ili kujenga hoja ya kulinda heshima na utu wa mtu; Mtu ni sura na mfano wa Mungu (Mwa, 1:26); Mtu kajaliwa akili na utashi wa kumtafuta Mungu (Isaiah, 1:17-19); Mungu kapitia kwa mtu kajifunua kwa viumbe wote (In, 14:8-9); pamoja na; Mungu kamchagua mtu na kuweka agano naye (Mwa, 9:13; Kut. 19:5).
Sambamba na hayo, anasema kwamba familia ni taasisi ya kuenzi na kuheshimu utu wa mtu, kwani hiyo ni taasisi ya wanadamu aliyoianzisha Mungu ili kupitia kwenye taasisi hiyo, watu washirikishane upendo wa Kimungu, na watu washiriki kazi ya Mungu ya uumbaji.
Pia, anabainisha kwamba taasisi hiyo ni ya wanadamu kwa sababu inaundwa na wanadamu (nuclear and extended). Na pia ni ya Kimungu kwa sababu mwasisi, mtegemezaji na malengo yake ni Mungu.
Vile vile, anasema pia kwamba taasisi hiyo ni ya upendo, kwa sababu kiungo chake ni upendo, ni ya uumbaji kwa sababu inaendeleza umbaji.
Njia za kuenzi na kuimarisha familia:
Akitaja njia zinazoweza kutumika ili kuimarisha familia, Padri huyo anabainisha kwamba ni lazima kuwepo na sala, kuiombea na kusali pamoja; ijikite katika kusoma na kuishi Neno la Mungu; Maisha ya Sakramenti; ipate neema za Sakrameti; malezi endelevu; ianze na Mungu na ibaki na Mungu; Maadhimisho endelevu; kushika amri ya mapendo, kufanya kumbukizi za matukio muhimu ya kifamilia, pamoja na kuhuisha mahusiano.
Matishio dhidi ya familia:
Akitaja mambo yasiyofaa na yanayoonekana kuwa tishio katika familia, Padri Kamuhabwa anasema kwamba mambo hayo ni pamoja na familia kuanzishwa kiholela.
Anaongeza kuwa kadri ya mpango wa Mungu, familia huanza kupitia ndoa halali, tofauti na hilo, ni mwanzo potofu, matokeo yake ni matokeo na mwisho potovu.
Vile vile, anasema kwamba upotoshwaji wa sifa za wanafamilia ni moja ya tishio, kwani familia huundwa na baba, mama na watoto. Upotovu katika jinsia za wazazi ni tishio la familia.

SOMA ZAIDI....

DAR ES SALAAM

Na Pd. Mujuni Audiphace

(Heri kwenda nyumbani mwa matanga kuliko kwenda nyumbani mwa karamu, maana huko ndiko mwisho wa binadamu wote, na walio hai wataweka moyoni,” Mhubiri 7:2)
Ndugu zangu Tumsifu Yesu Kristo.
Mwezi wa nane mwaka huu (2024) familia yetu tulijengea na kuweka msalaba mpya kwenye kaburi la Baba yetu aliyefariki miaka 37 iliyopita huko Kamachumu Kagera.
Siku moja kabla ya Misa ya kilele cha tukio hili nilifika nyumbani kuona kinachoendelea, nikakuta fundi yupo anakamilisha ujenzi akiwa na mdogo wetu wa mwisho wakiwa wawili tu pale kwenye eneo la makaburi.
Huyu bwana mdogo akawa anajisifia kuwa yeye tu ndiye haogopi makaburi, akaniambia kuwa wengine wote wamekimbia hii kazi ya msaidia fundi sababu inafanyika makaburini na ni ya kujenga kaburi.
Nilimuuliza kuwa: UNAFIKIRI HASA WANAOGOPA NINI KUHUSU MAKABURI?
Akanijibu kuwa: HAWAOGOPI MAKABURI, BALI WANAOGOPA KINACHOSABABISHA MAKABURI KUWEPO, YAANI KIFO. Hivyo wanafikiri kuyasogelea makaburi ni sawa na kukisogelea KIFO kwa makusudi.
NA HUU NDIO MTAZAMO WA BAADHI YETU TULIO WENGI
Wapendwa, makaburi yamekuwapo tangu mwanzo wa uwepo wa mwanadamu. Makuburi yameandaliwa na kutunzwa vyema na binadamu baada ya kuwa wamezikwa humo miili ya wapendwa wao.
Tunasoma Katika kitabu cha Mwanzo 23: 19-20, kuwa Abraham alinunua pango katika shamba la Makpela, na humo yakawa maziko ya watu ( Sarah, Abraham, Isaka, Yakobo, Lea, Raheli, nk). Eneo hili la makaburi liliendelea kutunzwa vizuri sana na watu wa wakati.
Kumekuwepo na Mila za kuyatumia makaburi kwa kufanya mambo ya hovyo na pia kuyahusishanisha na ushirikina kwa baadhi ya makabila ya kiAfrika. Hivyo Kila anayejishughulisha na makaburi anaonekana kuwa ni mtu wa Hovyo na mshirikina.
Kitabu Cha Muhubiri 7:2 kinasema kuwa “ Heri kwenda nyumbani mwa matanga kuliko kwenda nyumbani mwa karamu, maana huko ndiko mwisho wa binadamu wote na walio hai wataweka moyoni.”
Tunahimizwa kutembelea makaburi sababu ni swala la kusali.
Biblia inaendelea kutugundisha kuwa waliokufa sio adui zetu na wala sio mikosi kwetu tukiendelea kuwa karibu nao hata kwa kubeba masalia yao pale inapobidi, Yoshua 24:32 “mifupa ya Yosefu anazikwa Shekhem baadae ya waIsrael kusafiri nayo kutoka Misri. Eneo la Maziko linakuwa urithi wa Wana wa Yosef.”
Makaburi sio UCHURO ndugu zangu. Tunzeni maeneo yenu ya makaburi.
Kadiri ya maelekezo ya Mwenyezi Mungu kupitia kwa Nabii Elia, kutokuzikwa kaburini ni ishara ya kufa kifo kibaya (ukiwa mdhambi), Wafalme 9:33-44, “mdhambi mmoja anayeotwa Yezebel anakufa na mwili wake unaliwa na mbwa mitaani sababu ya wingi wa dhambi zake.”
Hivyo, kutokuzikwa baada ya kufa ni ishara ya laana, lakini waliozikwa vizuri ni ishara ya baraka.
Kuogopa makaburi ni sawa na kuogopa “kisichokuwepo.”
Kwa Kihaya uwa kuna methali inasema “kyakutinisa kita’kurwe”, jibu lake uwa ni “Mwilima.”
Tafsiri: “Kuna kitu kinakutisha lakini hakina nguvu ya kukula(kukuua),” na jibu lake ni “Giza.”
Kuogopa makaburi ni sawa na kuwa na “wasiwasi wa Bure” katika maisha, ni tatizo la AFYA YA AKILI. Tibu tatizo hili kwa kutunza vyema kumbukumbu za wapendwa wetu.
Wapendwa, shetani hakai makaburini, tukisoma Injili ya Mt. Marko 5:2-3, “Yesu baada ya kumtoa mapepo mtu aliyeishi makaburini akiwazuia watu wasiende makaburini, wale pepo walikimbilia baharini (sio makaburini).”
Tujifunze kwa Bwana wetu Yesu Kristo aliyekwenda makaburini kumfufua Lazaro (pamoja na kwamba dada yake Lazaro alimkataza Yesu kwenda makaburini, lakini Yesu alienda tu na Ufufuo ukafanyika).
Wapendwa tusisikilize kelele za wanaotuzuia/ kutucheka tunapokwenda makaburini kuyasafisha na kuwaombea waliolala huko, maana wote waliolala katika Kristo, watafufuliwa naye.
HITIMISHO
“Hata siku ya kwanza ya Juma, alfajiri na mapema, walikwenda kaburini wakiyachukua manukato waliyokuwa wameyatoa tayari,...” Luka 24: 1.
Wanawake watakatifu walienda”wakashuhudia UFUFUKO.
Makaburini.”  walimuona yesu mfufuka kwenye bustani za makaburi, hawakumuona shetani.
Tuwaombee waliolala makaburini waone uso wa Mungu.
Bwana awe nanyi nyote.
Pd. Mujuni Audiphace, Padri wa Jimbo Katoliki la
Bunda.

Page 2 of 5