Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Wiki iliyopita tuliwaletea historia ya mchango wa Kanisa wakati wa kupambana na athari ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia (1939-1945). Leo tunawaletea mrithi wa Papa Pio X11 (1939-1958: wa 260) ambaye ni Papa Yohana XX111, aliyepigiwa kura mara 12 kumpata. Sasa endelea.

Papa Yohana XXIII (1958 - 1963: wa 261), zilipigwa kura mara 12 kabla ya kumpata. Uchaguzi wa Papa wa kumrithi Papa Pio XII, haukuwa rahisi kama uchaguzi wake. Inasemekana kwamba kura zilipigwa mara 12 ili kumpata. Kulikuwepo na wengi ambao walidhaniwa wangemrithi, lakini sasa dunia ilihitaji zaidi Mchungaji kuliko Mtawala.
Papa Pio XII alikuwa labda Papa wa mwisho wa mapokeo ya kifalme. Katika hali ngumu ya kumpata mtu wa kukidhi mategemeo ya wote, walimchagua mtu wa mpito wakiwa wanajipanga vizuri.
Walimchagua mtu ambaye hisia zake zilikuwa za mkulima, mtu rahisi kuongea naye na kufikiwa. Umri wake, miaka 76, ulikuwa umekwenda, hivyo hakutegemewa kukaa muda mrefu.
Alichaguliwa Kardinali Angelo Ronccali ambaye alichukua jina la Papa Yohana XXIII. Kardinali Ronccali alikuwa na uzoefu wa kukutana na watu wa aina mbalimbali wa kutoka nchi mbalimbali.
Ni vema na haki kujua vizuri maisha ya Papa huyu aliyebadili mwelekeo wa Kanisa katika Ulimwengu wa sasa. Kinyume na mategemeo ya wote, alifanya kazi ambayo ilikuwa haijafanyika tangu Mtaguso Mkuu wa Trento katika karne ya 16.
Angelo Giuseppe Roncalli, mtoto wa tatu kati ya watoto kumi na watatu, alizaliwa tarehe 25 Novemba 1881 huko Sotto il Monte (Bergamo), kwenye familia ya wakulima. Alipadrishwa mwaka 1904, na akaendelea na masomo na kupata Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa.
Akiwa Katibu wa Askofu mpya wa Bergamo, Giacomo Radini –Tedeschi, Angelo alipigania haki za jamii, na baadaye alifundisha Seminarini Historia ya Kanisa, na masomo mengine. Wakati wa Vita Kuu vya Kwanza (1914-1918), mwaka 1915 alijitolea kama mhudumu wa kiroho (Chaplain) wa wanajeshi. Baada ya vita, alikuwa mlezi wa kiroho wa Seminari.
Mwaka 1921 aliitwa Roma na Papa Benedikto XV (1914-1922: wa 258) kusaidia kupanga upya Idara ya Uinjilishaji (Propaganda Fide). Mwaka 1925 alitumwa Bulgaria kama Mwakilishi wa Papa, na huko alijishughulisha na Makanisa ya Mashariki (Waortodosi). Mwaka 1934 alitumwa Uturuki na Ugriki, makao yake yakiwa Istanbul (Konstantinople ya zamani).
Huko, licha ya Wakristu Waortodosi, alikutana kwa karibu na Waislamu. Mwaka 1944 alitumwa kumwakilisha Papa huko Paris, Ufaransa, ili kusaidia Kanisa hilo kubwa kujiunda upya baada ya vita.
Hii haikuwa kazi rahisi kwa sababu Balozi aliyetangulia alishirikiana na Wajerumani. Hivyo serikali ya Rais De Gaule na Wafaransa, walimchukia pamoja na Maaskofu waliofuta, nyayo zake. Sasa Askofu Mkuu Roncalli, ilibidi afanye kazi ya ziada kutuliza hali.
Wakati huo alikuwa vile vile Mwakilishi wa Papa katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Watoto (United Nations International Children’s Emergency Fund: UNICEF). Baada ya kazi nzuri akiwa na umri wa miaka 71, mwaka 1953 aliteuliwa kuwa Kardinali na Patriarka wa Venezia.
Papa Pio XII alipofariki (Oktoba 1958), Makardinali walikuwa na wakati mgumu kukubaliana juu ya nani amrithi. Ilikuwa vigumu kupata theluthi mbili za kura kwa mtu mmoja. Hivyo, baada ya kupiga kura mara 11, waliona wampate Papa wa mpito atakayekubalika kwa wote wakati hali inaendela kuwa shwari.
Tarehe 9 Oktoba 1958 katika kura ya 12, walimchagua Kardinali Angelo Roncalli, mwenye umri wa miaka 76, mtu asiyekuwa na misimamo mikali, lakini mtu wa watu na Mwanadiplomasia mzuri katika kuleta mahusiano na watu.
Alichagua jina la Yohana XXIII. Mfano wa maisha yake na mtu ambaye alitaka kufuata nyayo zake alikuwa Mtakatifu Papa Pio X (1903-1914: wa 257) ambaye alizaliwa akiwa maskini, na kufa akiwa maskini. Naye kabla ya kuchaguliwa kuwa Papa, alikuwa Patriarka wa Venezia.
Katika hotuba zake za mwanzo, mara moja Papa Yohana XXIII aligusia mambo makuu mawili ambayo alitamani kuyatekeleza. Kwanza kuhuisha Kanisa ili lioane na nyakati, yaani kusoma alama za nyakati kama alivyoiita (Aggionamento).
Alitaka kulihuisha Kanisa kiroho. Pili aligusia kuita Mtaguso Mkuu wa Kanisa kufanya kazi hiyo muhimu. Papa Yohana XXIII alihisi kwamba amevuviwa na Roho Mtakatifu kutengeneza Kanisa na kulihuisha.
Wakati akiamini juu ya Neno la Mungu na Mapokeo rasmi ya Kanisa ambayo ni msingi wa Imani na hayawezi kugeuka, aliona mazoea mengine yaliyoingia kufuatana na utamaduni na mwenendo wa watu wa mahali, au wakati fulani yanaweza na mara nyingine yanapashwa kugeuka kukidhi mahitaji ya wakati na mahali.
Kwanza alianza na desturi za maisha ya Papa. Tofauti na watangulizi wake waliokaa ndani Vatikano, yeye alitoka nje mjini Rona na kwenda kuwatembelea watoto wagonjwa hospitalini, na hata wafungwa.
Alisisitiza kuwaona hata wafungwa sugu na hatari. Aliwaambia wafungwa: “Kwa sababu ninyi hamuwezi kuja kunitembelea, imebidi mimi nije kwenu.” Vile vile alikutana na watu ambao kabla haikufikirika kukutana na Papa kama mpwa wa Rais wa Urusi Nikta Khrushchev, Askofu Mkuu wa Kantebury, yaani Mkuu wa Kanisa la Anglikana, kasisi mkuu wa dini ya Shinto kutoka Japan, na wengine.
Kwa mara ya kwanza katika karne moja, alisafiri nje ya Roma na kwenda Asizi. Alipokutana na watu, hakujiona au kujionyesha kama Kiongozi Mkuu wa Vatikano, bali kama mchungaji au kama alivyosema “Mtumishi wa watumishi” (Servus Servorum), akiwa na sura ya Mchungaji kuliko ya Mtawala.
Papa Yohana XXIII aliliona Kanisa kama chombo cha kiroho kilicho juu ya madaraka yote ya siasa, na chenye jukumu la kuwapatanisha, mathalani wakati wa mzozo wa silaha za nuklia wa Cuba mwaka 1962, ambapo ilikuwepo hatari ya vita vikuu vya mabomu ya nuklia kati ya Urusi na Marekani kutokea.
Papa Yohana XXIII aliingilia kati baina ya John Kennedy wa Marekani na Khrushchev wa Urusi kwa kuzungumza nao, na hivyo akapunguza munkari. Mambo yalipotulia, wote wawili walimshukuru.
Papa Yohana XXIII aliongeza Jopo la Makardinali kiasi kwamba kufikia mwaka 1962, lilikuwa na Makardiali 89, ikiwa 19 zaidi ya wale 70 wa Kanuni iliyowekwa na Papa Sisto IV (1471-1484: wa 212) katika karne ya 15.
Kati ya Makardinali hao, aliwateua wengine kutoka Afrika, Filipino na Japan, licha ya Marekani na nchi nyingine. Kati ya Makardinali alimteua Mwafrika wa kwanza na mtu mweusi wa kwanza kuwa katika jopo hili, Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa, Mtanzania kutoka Jimbo la Rutabo, Bukoba, Kagera, Tanganyika wakati huo, mwaka 1959.
Kuna watu ambao hawakuamini kwamba mtu mweusi angelikuwa Kardinali. Ikumbukwe kwamba wakati huo karibu nchi zote za Afrika zilikuwa bado koloni na Marekani mtu mweusi hakuweza kupiga kura na hata kukaa sehemu moja na wazungu, kwani alitengwa kama mkoma. Katika uongozi wake, aliwateua Makardinali 54.
Kama Baba Watakatifu waliomtangulia, naye alitoa barua mbalimbali za kichungaji. Tofauti na wengine, barua zake hazikuwa za kulaumu, au za kutoa fasili ngumu za teolojia, bali mambo ya kawaida yenye ladha ya kichungaji yaliyowahusu na kuwagusa watu, bila ubaguzi.
Papa Yohana XXIII aliandika barua nane za kichungaji, na kati ya barua hizo  alizoziandika, mbili zilikuwa na msukumo mkubwa. Mater et Magistra (Kanisa kama Mama na Mwalimu), hii ilikuwa barua ya tano iliyotolewa tarehe 15 Mei 1961 ikiwa ni miaka 70 tangu barua ya Papa Leo XIII (1878-1903: wa 256) Rerum Novarum, na miaka 30 tangu barua ya Papa Pio XI (1922-1939: wa 259) “Quadragesimo Anno.”
Katika barua hiyo iliyosifiwa na kukubalika Ulimwengu mzima, ilijadili masuala ya jamii kama walivyofanya watangulizi wake kwa mtazamo chanya, huria na wa kujenga. Barua maarufu kuliko zote ni ile ya “Pacem in Terris“ (Amani Ulimwenguni) aliyoiandika tarehe 11 Aprili 1963, miezi miwili kabla ya kifo chake Papa Yohana XXIII.
Tofauti na barua nyingine za Baba Watakatifu wengine, Papa Yohanne XX111, aliwaadikia watu wote wenye mapenzi mema. Kweli ilikuwa inawafundisha na kuwaasa watu wa Ulimwengu mzima. Ulikuwa kama wosia wake wa mwisho kwa Ulimwengu.
Barua hii imechambua hali halisi ya kijamii Duniani. Papa Yohana XXIII anatutaka kuheshimu utu wa watu, na anadai kwamba kuheshimu haki za binadamu wote, ndio msingi wa haki na amani ya kweli.
Anaandika “Mwanadamu ana haki ya kuishi. Ana haki ya uadilifu wa mwili na njia zinazohitajika kwa maendeleo sahihi ya maisha, haswa chakula, mavazi, malazi, matibabu, mapumziko na, mwishowe, huduma muhimu za kijamii. Ana haki ya kutunzwa katika hali mbaya ya afya; ulemavu unaotokana na kazi yake; mjane, uzee; kulazimishwa kukosa kazi; au wakati wowote bila kosa lake mwenyewe, ananyimwa njia ya kujikimu.”
Licha ya kusisitiza juu ya utu na usawa wa binadamu, anaasa juu ya haki za wanawake, anawasihi kutoenezwa kwa silaha za nyuklia. Anafundisha juu ya umuhimu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuwaleta watu wote pamoja, kujadili na kuleta muafaka juu ya kutatua mafarakano na kuleta maendeleo ya kweli kwa watu wote.
Bahati nzuri, tafsiri ya barua hii iko katika Kiswhili, na inapatikana kwenye mtandao wa Vatikano.

LONDON, Uingereza
Mo Farah, mmoja wa wanariadha wakubwa wa Uingereza wa wakati wote, alimaliza wa nne katika mbio za mwisho za taaluma yake katika Great North Run.
Bingwa huyo wa Olimpiki mara nne mwenye umri wa miaka 40, aliteleza mapema katika mbio maarufu za maili 13.1 kutoka Newcastle hadi South Shields.
Alimaliza dakika tatu na sekunde 30 nyuma ya Muethiopia Tamirat Tola, ambaye alishinda kwa dakika 59, sekunde 58.
Alisema kuwa kukimbia ndiyo kila kitu kwake na ndiko kulikomuokoa na amewashukuru washabiki wake wote waliomuunga mkono katika nyakati zote za maisha yake kwenye kazi yake hiyo.
“Inatia moyo sana, kulikuwa na mengi yaliyokuwa yakipita akilini mwangu, ila ninachojua ni kukimbia, na hilo ndilo lililonifurahisha kwa miaka mingi,” alisema Farah.
Farah anastaafu akiwa na wasifu unaometa, kwani alikuwa Mwingereza wa kwanza kukamilisha Olimpiki ya mita 5,000 na 10,000 mara mbili kwa ushindi mbele ya umati wa watu wenye furaha huko London mwaka 2012, na kutetea mataji yake huko Rio mwaka 2016.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Raha za michuano ya soka ya Mataifa ya Afrika (Africa Cup of Nations: AFCON) zitarejea tena kuanzia Januari 13 hadi Februari 11 mwakani, huku Tanzania Ikiwa miongoni mwa washiriki tunaotarajiwa, ukiwa ni ushiriki wetu wa tatu tangu fainali hizo zilipoanzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1957.
Tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo, kumekuwa na matukio kadhaa ya kukumbukwa kuwahi kutokea.
Yapo matukio ya huzuni, furaha na ya kustaajabisha ambayo yamewahi kutokea katika fainali hizo tangu kuanzishwa kwake.
AJALI YA CHIPOLOPOLO MWAKA 1993
Aprili 27 mwaka 1993 timu ya taifa ya Zambia, maarufu kama Chipolopolo, ilikuwa safarini kwenda nchini Senegal kucheza mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia. Ndege iliyowabeba ilianguka na kutumbukia katika bahari ya Atlantic mita 500 tu iliporuka kutoka mji wa Libreville, Gabon. Wachezaji wote waliokuwa kwenye ndege hiyo, walifariki dunia.
Mwaka mmoja baadaye, Zambia ilijijenga vyema kwa kuunda wachezaji wengine na kufanya vizuri katika michuano ya Kombe la Mataifa Huru ya Afrika ya mwaka 1994. Walifika fainali ingawa walifungwa na Nigeria kwa mabao 2-1. Yalikuwa ni mafanikio makubwa licha ya changamoto iliyowakumba mwaka mmoja uliotangulia.
JEZI ZA CAMEROON
Mwaka 2002 katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika iliyofanyika nchini Mali, timu ya taifa ya Cameroon ilichukua Kombe la AFCON kwa kuifunga Senegal katika fainali kwa mikwaju ya penati 3-2, baada ya timu hizo kutoka suluhu ya kutokufungana.
Lakini habari kubwa ya Cameroon ilikuwa ni kuhusu jezi zao.Timu hiyo ilienda katika mashindano na jezi zilizokuwa katika mtindo wa ‘singlets (vests)’, jezi ambazo baada ya mashindano, Shirikisho la Soka la Kimataifa (Federation of International Football Association: FIFA) walizipiga marufuku.
Mwaka 2004 tena, Cameroon ilitinga katika michuano hiyo iliyofanyika nchini Tunisia ikiwa na jezi za ajabu zaidi zikiwa kwenye mtindo wa ‘Jump Suti’, yaani fulana na bukta zimeshikana. Fifa hawakukubali, wakawakataza mara moja kuacha kutumia jezi hizo, na kuwapiga faini ya dola 154,000 za Kimarekani, ambazo zililipwa na watengenezaji wa jezi hizo - kampuni ya Puma.
BASI LA TOGO KUSHAMBULIWA MWAKA 2010
Basi la timu ya taifa ya Togo lilishambuliwa na watu wenye silaha wakati timu hiyo ilipokuwa ikielekea mashindanoni nchini Angola.
Tukio hilo lilitokea Januari 8 mwaka 2010 wakati basi la timu ya Togo likisafiri kutoka Togo kwenda Angola ambako fainali hizo zilifanyika, watu watatu waliuawa, akiwemo mchezaji mmoja.
Nyota wa Arsenal kwa wakati huo, Emmanuel Adebayor, alikuwa ni miongoni mwa waliokuwa kwenye basi hilo, na kwa hasira akatangaza kutoichezea tena timu hiyo akishutumu uzembe wa Chama chake cha Soka kuwasafirisha kwa basi, badala ya ndege.
DROGBA ASULUHISHA AMANI
Mshambuliaji wa Ivory Coast, Didier Drogba alikuwa mahiri sana uwanjani kwa timu yake ya taifa ya Ivory Coast, na klabu wakati huo akiicheza timu ya Chelsea ya Uingereza, na pia alitumia hadhi yake kufanikisha amani nchini mwake.
Wakati wa vita kati ya 2002 na 2007, alipiga magoti moja kwa moja kwenye luninga akiwa na wachezaji wenzake kuwahimiza waliokuwa wanapigana kuweka silaha chini.
Amani ilitawala, na mwaka 2008 alisisitiza mechi ya kufuzu Kombe la Afrika ichezewe kwenye ngome ya zamani ya waasi, Bouake, kama wito kwa raia kuungana.
Mwaka 2006 na 2012, Drogba alisaidia taifa lake kufika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, lakini wakashindwa kwa mikwaju ya penati.
EBOLA MWAKA 2015
Mwaka 2015 kupitia msemaji wao, Mohamed Ouzzine, Morocco walisema kuwa kutokana na ripoti ya Shirika la Afya Duniani (World Health Organization: WHO), hawataweza kuandaa mashindano hayo kutokana na kuenea kwa kasi virusi vya ebola, ugonjwa uliokuwa unasambaa kwa kasi huko Afrika Magharibi.
Baada ya Morocco kujitoa kuandaa, mashindano hayo yalihamishiwa nchi ya Equatorial Guinea.
AFCON 2021 BADALA YA 2022
Fainali hizo za Cameroon ambazo zilifanyika mwaka jana na Senegal kuwa bingwa, zilikuwa zikiitwa AFCON 2021 licha ya kufanyika mwaka 2022 kwa sababu maandalizi yake yalilenga mashindano kufanyika mwaka 2021.
Ilishindikana kufanyika katikati ya mwaka 2021 kwa sababu katika kipindi hicho, Cameroon ilikuwa na majira ya mvua kubwa na mafuriko, hivyo Shirikisho la Soka Afrika (Confederation of African Football: CAF), likasogeza mbele.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Uwanja wa soka wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam, unatazamiwa kuiingizia Klabu ya Azam FC zaidi ya shilingi milioni 42.7 kupitia mechi za Kimataifa katika kipindi cha wiki mbili zilizobaki za mwezi huu.
Kwa kipindi kirefu, uwanja wa Azam Complex umekuwa msaada kwa timu mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa ambazo hazina viwanja vya nyumbani kuutumia kucheza mechi zake ndani na Kimataifa.
Kwa sasa timu za Simba, Yanga na Singida Fountain Gate zinautumia uwanja huo katika mechi zake za nyumbani za michuano ya Kimataifa, ambapo Singida inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika, huku Simba na Yanga zikiwa zinashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa mujibu wa Idara ya Habari ya Azam FC, timu ya Tanzania inayotaka kuutumia uwanja huo kwa ajili ya mechi moja, inatakiwa kulipia kiasi cha shilingi 5,900,000, huku timu ya kigeni ikitakiwa kulipa dola 5,000 ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi 12,527,945.
Katika kipindi cha kuanzia Septemba 15 hadi 30 mwaka huu, timu za Simba, Yanga, Singida Fountain Gate, Bumamuru (Burundi) na Artar Solar (Djibout) zitautumia uwanja huo kwa mechi zake za nyumbani kwenye michuano ya Kimataifa ngazi ya klabu.
Septemba 17 mwaka huu Singida Fountain Gate itaikaribisha Future FC ya nchini Misri katika mchezo wa Shirikisho Afrika, na mwisho wa mwezi huu Simba itaikaribisha Power Dynamo ya Zambia, na Yanga itaikaribisha Al Merreikh ya Sudan katika mechi za marudio za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa mechi hizo tatu, Azam FC itanufaika kwa kuvuna shilingi milioni 17.7 huku pia ikikusanya kiasi kingine cha dola 10,000 ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 25 kutoka kwenye mechi mbili za Kimataifa kutoka kwa timu za nje ya nchi za Artar Solar na Bumamuru, ambazo zinatumia uwanja huo kama wa nyumbani.
Bumamuru ya Burundi imeialika Mamelodi ya Afrika Kusini, na Artar Solar ya Djibout imeialika Zamalek ya Misri, zote zikitumia uwanja huo.
Jumla ya gharama ya mechi zote hizo ni zaidi ya shilingi milioni 42.7, kiasi ambacho ni tofauti na kile ambacho kitatokana na mazoezi ambayo timu za Singida Fountain Gate, Artar Solar na Bumamuru zinaendelea kufanya zikitumia uwanja huo.
Gharama ya mazoezi kwa timu ya ndani ni shilingi 600,000 kwa muda wa mchana, na usiku ni shilingi 1,500,000, huku timu za nje zikitakiwa kulipa dola 1,000.

NEW YORK, Marekani
Andy Murray amekiri kuwa Novak Djokovic anatazamiwa kutawala tenisi ya wanaume kwa miaka mingi ijayo, huku kizazi kipya cha wachezaji kikiwa bado chini ya kiwango chake.
Mserbia huyo mwenye umri wa miaka 36, alishinda taji la 24 la Grand Slam ambalo ni rekodi sawa na rekodi kwa kumshinda Daniil Medvedev katika fainali ya US Open mjini New York, Jumapili.
“Ni juu ya vijana kumsukuma Novak na kutafuta kumpita haionekani kama hilo linakaribia kutokea, kwani amekuwa mchezaji wa ajabu kwa muda mrefu sana, Uhai mrefu wa Novak umekuwa mkubwa zaidi. Amecheza kwa kiwango hiki kwa muda mrefu sasa,” alisema Murray.
Djokovic alishindwa katika fainali ya Wimbledon mwaka huu na Mhispania mwenye umri wa miaka 20, Carlos Alcaraz.
Mshindi mara tatu wa Grand Slam, Murray ambaye alikuwa akizungumza katika mkesha wa kampeni ya Davis Cup ya Uingereza, alisema kuwa hitimisho lisilo sahihi lilitolewa kutokana na kushindwa kwa Djokovic katika SW19.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amawasihi Wakatoliki kuacha woga kumtangaza Yesu Kristo, kwa sababu imani ndiyo inayowasaidia maishani.
Kardinali Pengo alitoa wito huo wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakrameti ya Kipaimara kwa vijana 25, wa Parokia ya Mtakatifu Andrea Mtume, Bahari Beach.
“Ndugu zangu Waamini nawaomba sana, huyu Kristo tuko naye, kwa hiyo kama yupo anayejifichaficha, aache tabia hiyo, tumtangaze Kristo, ili na yeye atusaidie katika maisha yetu:
“Utakuta watu wengine ni Wakristo wazuri sana, lakini wanapenda kuwa na tabia ya kujificha,” alisema Kardinali Pengo.
Alisema kuwa hata wakati wa kula chakula, hawapigi ishara ya msalaba, hawasali kabisa kwa sababu ya woga.
Kardinali Pengo alibainisha kuwa tabia ya Mkristo kuwaogopa watu wakati wa kuombea chakula, haifai, kwani Mkristo kamili hatakiwi kumwogopa mtu, bali anatakiwa kumtangaza Bwana Yesu Kristo mahali popote pale.
Aidha, Kardinali Pengo aliwataka vijana waliompokea Roho Mtakatifu kupitia Sakramenti hiyo kutokuwa na woga, wakamtangaze Yesu katika maisha yao.
Aliwakumbusha vijana hao kufahamu kwamba kupitia Sakramenti hiyo, wamekuwa Askari imara wa Kristo, hivyo wanatumwa kwenda kumtangaza yeye.
Kardinali Pengo alisema kuwa imani ndiyo msingi wa maisha ya kila mmoja, akiwasihi Waimarishwa hao kusali kila wakati, kwani kwa kufanya hivyo, Ufalme wa Mungu utakuwa wokovu kwao.
Kardinali aliwashukuru Waamini wa Parokia ya Bahari Beach kwa zawadi walizompatia, huku akiwapongeza kwa hatua kubwa waliyopiga parokiani hapo, ikiwemo ujenzi wa kanisa, akisema kuwa anatamani kuona ujenzi huo ukimalizika mapema, ili na yeye afike tena kwa ajili ya kusali pamoja na Waamini hao parokiani hapo.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Marko Loth alimshukuru Kardinali Pengo kwa kuwapatia Sakramenti vijana hao.
Naye Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Balozi Dk. James Msekela alisema kuwa hiyo ni siku kubwa kwao kwa kutembelewa na Kardinali Pengo, akiwaomba
Waamini wa Parokia hiyo kuongeza ushirikiano ili wamalize ujenzi wa kanisa lao kwa wakati uliokusudiwa.

Dar es Salaam

Na Mathayo Kijazi

Wazazi nchini wametakiwa kutambua kwamba namna wanavyoishi, na watoto wao pia wataishi kama wao.
Ili waweze kufuata maisha mema, wazazi hao wametakiwa kuishi maisha ya unyenyekevu na yenye kumpendeza Mungu, kwani watoto huiga mambo wanayofanya wazazi wao.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 158, wa Parokia ya Mtakatifu Monica, Matosa, jijini Dar es Salaam.
“Kwa hiyo, jinsi mnavyoishi ninyi wazazi, ndivyo watoto wenu watakavyoishi, kwa sababu hatua ya kwanza ya watoto, ni kuiga yale yanayofanywa na wazazi wao,” alisema Askofu Musomba.
Katika homilia yake Askofu huyo, aliwataka wazazi kuwaonyesha njia watoto wao, ili wafahamu namna ya kuwasiliana na Mungu katika maisha yao.
Aidha, Askofu Musomba aliwasisitiza wazazi hao kuwategemeza na kuwalinda watoto wao dhidi ya mashambulizi mbalimbali yaliyopo, ili wasiharibike katika ulimwengu huu.
Aliwasihi Waimarishwa wa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kutokuwa na hofu wala woga, kwani Roho Mtakatifu waliyempokea kupitia Sakramenti hiyo, atawapa nguvu ya kuyashinda majaribu wanayokutana nayo kila wakati.
Askofu Musomba aliwataka vijana hao kutosikiliza kelele zilizopo katikati yao, bali waisikilize sauti ya Kristo pekee.
Wakati huo huo, Askofu Musomba aliwaasa vijana hao kuwa wanyenyekevu katika maisha yao, kwani ndio utakaowasaidia kuisikia sauti ya Kristo katika maisha yao.

DAR ES SALAAM

Na Happiness Mthathia-TUDARCO

Serikali imesema kwamba imejipanga kupunguza kero ya usafiri kwa wanafunzi jijini Dar es Salaam, kwa kutekeleza mikakati iliyojiwekea, ikiwemo kutumia usafiri wa mabasi yaendayo haraka (Dar es Salaam Rapid Transit: DART) na Treni.
Hayo yalisemwa na Alhaji Maulidi, Afisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati akizungumza na gazeti Tumaini Letu katika mahojiano maalum yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam, kuhusu kero ya usafiri kwa wanafunzi. 
“Serikali inaendeleza ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka, ikiwemo barabara iendayo Gongo la Mboto kutoka mwanzo wa Barabara ya Nyerere, Msimbazi, Kariakoo. Pia, ina mkakati wa kujenga barabara kutoka Morocco (Kinondoni) kwenda Tegeta, na itafika mpaka Bunju ili kuwasaidia wanafunzi,” alisema Maulidi.
Alisema pia kuwa mpango wao ni kushirikisha sekta binafsi katika kutatua changamoto ya usafiri kwa wanafunzi jijini Dar es Salaam, kwani kwa sasa hali ni nzuri ikilinganishwa na ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.
Maulidi alisema kuwa jukumu la Serikali kwa wanafunzi ni kuwapatia elimu bora, na kuongeza kuwa wazazi wana jukumu la kuhakikisha watoto wanafika shuleni na kurudi nyumbani kwa kuwapatia nauli kwa ajili ya usafiri.
Afisa huyo aliwataka makondakta kuwahudumia wanafunzi waweze kusafiri kwa wakati ili kupunguza changamoto wanayokumbana nayo, na kuwakanya wanafunzi nao ili wajiheshimu.
Baadhi ya wanafunzi wameliambia gazeti hili kwamba wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya usafiri nyakati za asubuhi na jioni kwa kukataliwa na makondakta wa daladala, na hivyo kuchelewa kwenda shule na kurejea nyumbani.
Mmmoja wa wanafunzi hao, John Elias wa Shule ya Sekondari Kawe Ukwamani jijini Dar es Salaam, alisema kuwa wanakumbana na changamoto hiyo mara kwa mara.
“Tumekua tukikataliwa na makonda kuingia kwenye daladala kitu ambacho kinasababisha tuchelewe kufika shule pia kurudi nyumbani nyakati za jioni,’’ alisema John.
Kwa upande wao baadhi ya wazazi akiwemo Mama Jordan, Mkazi wa Mtaa wa Goba jijini Dar es Salaam, alithibitisha kuwepo kwa changamoto hiyo kwa wanafunzi, akisema kuwa sababu ya makondakta kuwakwepa wanafunzi ni kiasi cha nauli wanacholipa cha Shilingi 200/=, hivyo wanaona bora wanafunzi waachwe.

DAR ES SALAAM

Na Deus Kamanga

Waamini wametakiwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Kanisa katika kufanikisha maendeleo kwa vyombo vya Habari vya Kanisa ili viweze kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa watu wote Ulimwenguni, kwani kwa kufanya hivyo watajipatia neema na baraka kwa Mungu.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Padri Vitalis Kassembo, Mkurugenzi wa Walei Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam wakati akitoa homilia katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Shukrani ya Umoja wa Marafiki wa Tumaini Media (UMTUME), kuadhimisha Siku ya Mawasiliano Duniani iliyofanyika Parokia ya Bikira Maria Mama wa Fatima – Msimbazi, jijini Dar es Salaam.
Padri Kassembo ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Familia Takatifu - Mburahati, jimboni humo, alisema kuwa Kituo cha Tumaini Media jimboni Dar es Salaam, ni miongoni mwa vyombo vya Habari ndani ya Kanisa kinachofikisha ujumbe wa Mungu kwa watu, kikielimisha na kuhabarisha masuala mbalimbali ya kijamii yanayostawisha maelewano mazuri yenye kuleta mshikamano unaompendeza Mungu.
Padri Kassembo alisema kuwa jitihada zinazofanywa na Utume kwa ajili ya maendeleo ya Tumaini Media ni mfano dhahiri kwa waamini na watu wenye mapenzi mema na Kituo hicho cha Kanisa, hivyo akawataka waamini na watu wengine kuiga mfano huo kwa kuendelea kumshukuru Mungu, sanjari na kukichangia ili kisonge mbele.
Aliongeza pia kuwa ni jambo la msingi kwa kila mbatizwa kushirikiana na Kanisa na Taasisi zingine zenye nia njema ya kuviwezesha vyombo hivyo, wakiwemo UMTUME, kwa hali na mali kwa kuwa kufanya hivyo ni kujiwekea hazina mbinguni.
Awali Mkufunzi wa semina ya Umtume, Maalim Jeran Mushi aliwaasa Wanaumtume kudumisha upendo na umoja katika kutekeleza utume wao, kwa kutawaliwa na upole, unyenyekevu, hekima na amani.
Maalim Mushi alibainisha kuwa Wanaumtume wanapaswa kuwafikia watu wote katika hali ya unyenyekevu kwa kuwashirikisha lengo la kuisadia Tumaini Media kiuchumi, na kuacha tabia ya kukata tamaa kwa sababu Mungu Mwenyezi anaziona nia zao, na hawezi kuwaacha katika magumu yoyote.
Alifafanua kuwa kiasi hicho cha fedha kitaelekezwa kufanyia maboresho eneo la mapokezi katika ofisi za Tumaini Media, na wataendelea na maboresho kulingana na uhitaji wa maeneo mengine.

DAR ES SALAAM

Na Esther Ngubes-TURDACO

Kamishna Msaidizi wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Michael Stephen Deleli, amesema kuwa ajali nyingi za bodaboda, zinatokana na usimamizi mbovu wa wamiliki wa vyombo hivyo, kutokana na baadhi yao kuwapa madereva wasio na weledi.
Akizungumza na gazeti Tumaini Letu katika mahojiano maalumu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Kamishna Deleli alisema kuwa wamiliki wengi wa bodaboda hawawasimamii vema watu wanaowapa pikipiki hizo ikiwemo kutozingatia kama wana leseni ama laa.
Aidha, alisema kuwa jambo lingine ni woga wa abiria kushindwa kuwaonya madereva pindi wanapotumia usafiri huo, hasa wanapokwenda mwendo kasi, na uwezekano wa kusababisha ajali.
“Katika tathmini yetu, tumegundua kuwa ajali nyingi hususan za bodaboda, zinasababishwa na ukosefu wa usimamizi wa vyombo hivyo vya usafiri kutoka kwa wamiliki wakuu…
“Pia, woga wa abiria pindi wanapotumia usafiri huo kwa kushindwa kuwaonya madereva wanapoendesha kwa mwendo kasi, hii ni kutokujua wajibu na haki zao za kimsingi wanapokuwa barabarani,” alisema Kamishna Deleli.
Alibainisha pia kuwa takwimu zinaonyesha kwamba ajali nyingi zinatokana na miundombinu mibovu ya barabara, ubovu wa vyombo vyenyewe vya usafiri, pamoja na makosa ya kibinadamu yanayosababishwa na ukosefu wa elimu kuhusu matumizi sahihi ya barabara kwa kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani.
Aidha, Deleli alisema kuwa kulingana na makosa hayo, baadhi ya madereva huvunja sheria kwa makusudi kutokana na sababu za kumchelewesha abiria, na sababu nyingine binafsi.
Alisema kuwa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kimeweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua kwa kiasi kikubwa, hususani ajali za pikipiki, ikiwemo kutoa elimu kwa madereva wa pikipiki kwa kuweka sheria kali zitakazosaidia kupungua kwa ajali hizo.
Kamishina Deleli alisema kuwa miongoni mwa adhabu hizo ni kifungo au faini kwa yeyote atakayejihusisha na uvunjifu wa sheria hizo.
“Natoa rai kwa wananchi wote, madereva, na wamiliki wakuu wa vyombo hivyo vya usafiri, hususani pikipiki, wahakikishe kuwa vyombo hivyo vya usafiri vipo katika mikono salama ya madereva hao.
“Nasisitiza sana kwa madereva wa pikipiki kujiepusha na uendeshaji wa mwendokasi, kuvaa kofia ngumu (helmet), kujiepusha na upakiaji hatarishi wa abiria zaidi ya mmoja, na uendeshaji wa pikipiki ukiwa umetumia kilevi au afya ya mwili ikiwa haipo vizuri,” alisema Kamishna Deleli.
Akizungumza na Tumaini Letu, mmoja wa madereva wa pikipiki aliyejitambulisha kwa jina la Temu, alisema kuwa Sheria za Usalama barabarani wanazifuata, lakini kutokana na makosa ya kibinadam na baadhi ya changamoto zinakuwa nje ya uwezo wao, hujikuta wakisababisha ajali hizo.