Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Westlife ni kundi la muziki la nchini Ireland, lililoundwa Machi 3 mwaka 1998 na kuvuma duniani kote.
Asili ya kundi hili linajumuisha wanamuziki kama vile Nicky Byrne, Kian Egan, Mark Feehily, Shane Filan na Brian McFadden ambaye ameacha kuimba tangu mwaka 2004.
Kwa sasa Feehily na Filan ndio wanaotumika kama waimbaji wakuu katika bendi hii.
Bendi hii ya Westlife ndiyo bendi pekee katika historia ya muziki wa Uingereza kuwahi kuwa na nyimbo za kwanza saba moja kwa moja hadi namba moja, na pia wameweza kuuza hadi nakala zaidi ya milioni arobaini na tano dunia nzima ambayo inajumuisha nyimbo zilizorekodiwa studio,video, na albamu zenye kujumuisha nyimbo mbalimbali.
Mwaka 2008, walitangazwa kushika nafasi ya tisa wanamuziki matajiri zaidi walio chini ya umri wa miaka 30, na kushika nafasi ya 13, kwa ujumla. Kwa upande wa Uingereza wamekuwa na nyimbo za peke peke yaani singels hadi kumi na nne, na kushika nafasi ya tatu katika histoia ya Uingereza.
Kundi hili la muziki limewahi kuvunja rekodi mbalimbali kama vile, wanamuziki waliowahi kuwa na miziki mingi katika nafasi ya kwanza nchini Uingereza na pia kwa uuzaji mkubwa zaidi katika eneo la Wembley
Katika miaka mingi ya kazi zao,kundi la Muziki la Westlife wamekuwa wakitengeneza nyimbo za vijana maarufu  za aina ya pop na kutilia mkazo katika nyimbo aina ya ballads.
Wanamuziki wote wanaojumuisha kundi hili ni waandishi wa nyimbo. Lakini nyimbo zao nyingi zimeandikwa na waandishi kutoka nje ya kundi lao. Moja kati ya waandishi maarufu waliowahi kutengeneza nyimbo za kundi hili ni pamoja Steve Mac na Wayne Hector.
Juni mosi mwaka 2008, Westlife walifanya maadhimisho ya miaka 10, ambapo walifanya tamasha katika jiji la Dublin katika eneo la Croke Park na ambapo watu zaidi ya 83,000 walihudhuria hafla hiyo maalumu.
ALBAMU YA WEST LIFE
Westlife ni albamu kutoka kwa kundi la Westlife, moja ya albamu iliyofanya vizuri katika maeneo mbalimbali. Albamu hii ilitoka tar.1 Novemba 1999, nchini Uingereza.
Albamu hii pia ilijumuisha single tatu ambazo ni “Swear It Again”, “If I Let You Go” na “Flying Without Wings”, ambapo single zote tatu zilifanikiwa kufika katika nafasi ya kwanza katika chati ya nchini Uingereza.
Albamu hii ilingia katika chati na kushika nafasi ya pili, ikiwa na mauzo ya nakala zaidi ya 83,000, wakati kati ya hizo nakala 1,000 ziliuzwa wakati albamu hii ikiwa katika nafasi ya kwanza. Albamu hii ilikuja kutolewa katika nafasi ya kwanza na wimbo wa “Steptacular” ulioimbwa na Steps.
Albamu hii ilishika nafasi ya nane kwa upande wa mauzo kwa mwaka 1999 nchini Uingereza. Albamu ya Westlife imefanikiwa kuuza nakala zaidi ya milioni nne dunia nzima.
Albamu ya Westlife ilitoka nchini Marekani mwaka 2000, lakini ikiwa na orodha ya nyimbo tofauti na kuongeza wimbo kama “My Private Movie” uliotayarishwa na Cutfather akishirikiana na Joe.
Albamu hii inabaki albamu pekee ya Westlife kuwahi kuingia katika chati ya muziki ya nchini Marekani, ambapo ilishika nafasi ya 129 kati ya nyimbo 200 bora za Billboard.Ilishika nafasi ya 15 nchini Australia. Single ya More Than Words, ilitolewa nchini Brazi na kushika nafasi ya 2.
Mwezi Desemba mwaka huo huo, single za ‘I Have a Dream’ na ‘Seasons in the Sun’ zilishika nafasi ya kwanza kama nyimbo bora za Krismasi kwa mwaka huo, na bado ndizo single zilizowahi kupata mafanikio zaidi katika bendi ya Westlife.
Mwezi Machi mwaka 2000, single ya tano na ya mwisho kutoka katika albamu hii Fool Again ilitoka na kufikahadi nafasi ya kwanza.
Na kwa sababu hii, Westlife wakawa na single tano kutoka katika albamu moja kufika katika nafasi ya kwanza ndani ya mwaka mmoja, rekodi ambayo bado haijavunjwa hadi hii leo.
Albamu hii ilitolewa katika vijiboksi vikiwa na albamu ya Turnaround Januari 25, 2005 huku kukiwa hakuna kilichabadilishwa katika albamu ya kwanza.
WAPARAGANYIKA NA KURUDI UPYA
Kikundi hicho kilisambaratika mwaka wa 2012 baada ya uhai wa miaka 14 na baadaye kuungana tena mwaka wa 2018.
Mnamo Machi 17, 2021, walitangaza rasmi kwamba walitia saini mkataba mpya wa albamu kupitia Warner Music UK na East West Records.
Walitumbuiza kwenye hafla ya BBC Radio 2 kwenye Ukumbi wa Ulster, Belfast mnamo Agosti 25,2021 ambayo ilitangazwa mnamo 10 Septemba 2021.
‘Starlight’, wimbo wa kwanza kutoka kwa albamu yao ya kumi na mbili, ilitolewa tarehe Oktoba  14, 2021. Albamu hiyo, Wild Dreams, ilitolewa Novemba 26, 2021.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Mashindano maalum ya FIFA Series yamekuwa yakiwaacha njia panda Watanzania wengi ambao wamekuwa na maswali mengi hasa pale walipoiona Taifa Stars ikishiriki kule Azerbaijan.
Michuano ya FIFA Series ya 2024 ni msururu wa mechi zinazotambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa FIFA, zinazohusisha timu za taifa kutoka mashirikisho tofauti ya mabara mbalimbali duniani.
Tayari uzinduzi wa mashindano hayo umefanyika mwezi huu ambao umehusisha mechi za makundi matano tofauti, iliyofanyika katika nchi tano mwenyeji kuanzia Machi 21 hadi 26 mwaka huu.
Mashindano hayo ya kirafiki yalitangazwa kwa mara ya kwanza kama mpango wa FIFA mnamo Desemba 2022 yakiwa najina la ‘FIFA World Series’, na baadaye kuthibitishwa na Rais wa FIFA Gianni Infantino mnamo Machi 16,2023 kufuatia kuchaguliwa tena kwa wadhifa huo wakati wa Kongamano la 73 la FIFA. mjini Kigali, Rwanda.
Shindano hili litaleta pamoja timu za taifa za wanaume kutoka mashirikisho yake sita katika msururu wa mashindano ya kirafiki wakati wa dirisha la mechi za FIFA na kufanyika Machi kila mwaka.
Mashindano hayo yananuiwa kuvipa vyama wanachama wa FIFA nafasi muhimu za kucheza kwa kuwaruhusu kucheza mara kwa mara timu kutoka mashirikisho mengine ambayo vinginevyo hawatakabiliana nayo, na hivyo kuruhusu fursa zaidi za maendeleo ya kiufundi.
Kwa mfano kumekuwa na ugumu kwa timu za barani Afrika kukutana na timu za Ulaya hasa kwa kukosa nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia mara kwa mara, hivyo FIFA Series hutoa faida kwa timu hizo kukutana.
Inakusudiwa pia kutoa vyama vya wanachama na fursa za ziada za kibiashara na mengine mengi.
Fainali hizo za mwaka 2024 zinafanyikakama hatua ya awali ya majaribio ya shindano hilo.
FIFA Series imegawanywa katika vituo vikuu sita ambavyo ni Algeria, Azerbaijan, Misri, Saudi Arabia A, Saudi Arabia B na Sri Lanka.
Kituo cha Algeria kinahusisha timu kama Algeria, Andorra, Bolivia na South Africa huku cha Azerbaijan kikiwa na timu za  Azerbaijan, Bulgaria, Mongolia na Tanzania.
Kituo cha Misri kina mwenyeji Misri, Croatia, New Zealand naTunisia wakati kituo cha Saudi Arabia A kina timu za Cambodia, Cape Verde, Equatorial Guinea na Guyana.
Saudi Arabia B ina timu za Bermuda, Brunei, Guinea na Vanuatu wakati Sri Lanka ina Bhutan, Central African Republic, Papua New Guinea na wenyeji Sri Lanka.
Mabara sita yaliyounganishwa kupitia FIFA Series ni Afrika(timu tisa), Asia(timu tano), Amerika Kusini(timu moja), Amerika Kaskazini(timu mbili), Oceania(timu tatu) na Ulaya(timu nne).
Katika FIFA Series ya mwaka huu. Misri pekee ndiyo ilikuwa na muundo wa mtoano, huku washindi wakiamuliwa kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ndani ya muda wa kawaida.
FIFA Series ya Misri ni tofauti kidogo ambapo yenyewe inajulikana kama Kombe la Soka la Kimataifa la ACUD, ikiwa imefanyika Cairo na Mji Mkuu Mpya wa Utawala mnamo Machi 22, 23 na 26, na imehusisha wenyeji Misri (CAF), Croatia (UEFA), New Zealand (OFC) na Tunisia (CAF).

PARIS, Ufaransa
Bondia wa Ireland Amy Broadhurst anafikiri nafasi yake ya kushiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Paris imekwisha.
Bingwa huyo wa Dunia, Ulaya na Jumuiya ya Madola amesema Chama cha Ndondi cha Riadha cha Ireland [IABA] kimemjulisha kwamba hatafanyiwa tathmini ya mashindano ya pili ya kufuzu kwa Dunia, yanayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Mei huko Bangkok.
Kwa mujibu wa Broadhurst, Kitengo cha Utendaji wa Juu kinataka kumtathmini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 na bingwa mwingine wa dunia, Lisa O’Rourke, kwa ajili ya mashindano yajayo ya Ulaya badala ya kuwapeleka Thailand.
Anasema hilo halitafanyika.
“Nimemjulisha mwanasaikolojia wangu ili kuwafahamisha kuwa sitakuwa katika kituo cha utendakazi wa hali ya juu kwa siku zijazo, na nitakuwa nikifikiria sana kutorudi nyuma hata kidogo.”
Ilipowasiliana na BBC Sport (Northern Ireland Sport: NI), IABA haikuwa na maoni ya kutoa kujibu matamshi ya Broadhurst, kwani uteuzi katika vizito vyote, bado haujafanywa.
Inaonekana kuwa bingwa wa Ireland Grainne Walsh atachaguliwa kwenda Thailand, ingawa uteuzi wa kufuzu kwa Olimpiki bado haujafanywa.
Bondia huyo wa Offaly alikosa kushiriki Olimpiki ya Paris mapema mwezi huu alipopata kipigo cha kushtukiza cha uamuzi katika pambano la upendeleo.

MADRID, Hispania
Watu sita wamekamatwa baada ya ofisi za Shirikisho la Soka la Hispania pamoja na nyumba ya Rais wa zamani wa Shirikisho hilo, Luis Rubiales kuvamiwa na maafisa wa upelelezi kama sehemu ya uchunguzi.
Uchunguzi huo unahusu utakatishaji fedha na rushwa katika kashfa ya kuhamishwa kwa mashindano ya Super Cup ya Hispania kwenda Saudi Arabia.
Hadi sasa nyumba 11 zimepekuliwa juu ya kashfa hiyo inayokadiriwa kuwa na thamani ya pauni milioni 30.
Mamlaka nchini Hispania zimethibitisha kuwa Rubiales ni mmoja kati ya watu wengine watano ambao wameanza rasmi kuchunguzwa.
Maafisa hao hawakufanikiwa kumkuta Rubiales, kwani taarifa zinaeleza kuwa yupo nje ya nchi hiyo.
Ofisi ya waendesha mashtaka wa Serikali ya Hispania imesema kuwa polisi wakishirikiana na wapelelezi wa Europol walikuwa wakitafuta nyaraka fulani.
Ikumbukwe kuwa Rubiales ana kesi nyingine ya kumbusu mchezaji wa timu ya soka ya taifa ya wanawake ya Hispania baada ya fainali za Kombe la Dunia la wanawake zilizofanyika mwaka jana.

GEITA

Na Joel Maduka-Geita

Kufuatia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kuendelea kusaidia kuinua michezo kwa kununua magoli, mdau mmoja wa michezo mkoani Geita, Hussen Makubi amejitokeza na kuongeza dau kwa Simba na Yanga kwa kila goli watakalolifunga kwenye mechi zao za Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Yanga inapambana kuhakikisha inaitoa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika hatua ya Robo Fainali huku Simba ikitaka kuondokana na mazoea ya kuishia robo fainali kwa kutaka kuiondosha mashindanoni Al Ahly ya Misri.
Makubi maarufu kama Mwananyanzara ambaye tangu awali alikuwa na utaratibu wa kutoa shilingi laki tano kwa kila goli, sasa amepandisha dau kwa kuahidi kutoa shilingi milioni moja kwa kila goli.
Akizungumza na Tumaini Letu Makubi alisema amesikia Rais Samia amepandisha dau kutoka shilingi milioni tano hadi 10 kwa kila goli kwa timu hizo, hivyo na yeye kwa uwezo wake ameamua kutoka kwenye kiwango cha shilingi laki tano hadi milioni moja.
“Nimepandisha dau kwa kila goli litakalofungwa na Yanga na hata watani zetu Simba nao nitafanya hivyo hivyo.Lengo langu ni kuona timu hizo zinafanya vizuri kimataifa,”alisema Makubi ambaye ni shabiki mkubwa wa Yanga mkoani Geita.
Makubi aliahidi kuchinja ng’ombe na kuwanywesha supu wakazi wa Geita mjini kama ikitokea timu yake ya Yanga ikapata fursa ya kusonga mbele kwenda nusu fainali.
“Tutafunga mitaa Geita yote hii na kushangilia kama Yanga itafanikiwa kuwatoa Mamelodi na kwenda nusu fainali, na nitachinja ng’ombe na kuwanywesha supu mashabiki wote.Ninaamini hata mikoa mingine itaiga kwa hiki ninachokifanya,”alisema Makubi.
Baadhi ya wadau wa soka mkoani Geita akiwemo Emmanuel Ikolongo Otto na Emily Kimamba, wamempongeza Makubi kwa kujitoa kuzipa hamasa timu hizo.
“Mwananyanzala anafanya vizuri kwa sababu anaonyesha kwamba Geita ina wadau wa michezo wanaopenda maendeleo,” alisema Otto.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Waamini wametakiwa kuendelea kujitolea damu bila kuogopa, ili kuokoa maisha ya wengi wenye uhitaji.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na Walezi wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu, walipofanya matendo ya huruma katika Hospitali ya Kardinali Rugambwa, Ukonga, jijini Dar es Salaam.
“Wanaotoa damu kwa kweli tunawashukuru sana, kwani wanaokoa maisha ya watu wengi. Pengine kuna wengine wanaogopa kutoa damu. Kwa hiyo, naomba msiogope, unapotoa damu ujue kwamba unaokoa maisha ya mtu.
“Siyo kwamba ni wakinamama wanaojifungua ndio tu wanaohitaji kuongezewa damu, lakini kuna wengine pia ambao pengine wamekutwa na upungufu wa damu, wapo wengine waliopata ajali ambayo imesababisha damu nyingi kumwagika, kwa hiyo unapotoa damu, unaokoa maisha ya watu hao,” alisema Askofu Mchamungu.
Askofu Mchamungu aliwahimiza Walezi hao kuendelea kuwalea watoto katika malezi bora, ili liweze kupatikana Taifa lenye kujaliana.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Timothy Nyasulu Maganga, aliwashukuru Walezi hao kwa kufanya matendo ya upendo, huku akiwapongeza kwa majitoleo yenye thamani ya Shilingi 10,150,000/=, kwani mwaka jana ilikuwa Shilingi milioni tisa.
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kardinali Rugambwa, Dk. Jane Manyahi, aliwashukuru Walezi hao kwa kufanya matendo ya upendo hospitalini hapo, huku akiwaomba kuwa hayo waliyoyafanya yasiwe mwisho, bali yawe endelevu.
Aliwaomba wale wote wenye vigezo vya kuchangia damu kwenda kufanya hivyo, kwani wakichangia, watapewa kadi maalum za kuwatambulisha kwamba ni wachangiaji, ili na wao au ndugu zao watakapohitaji kuchagiwa damu, waweze kuchangiwa.
Akisoma historia fupi ya Hospitali ya Kardinali Rugambwa, Katibu wa Hospitali hiyo, Honest Antony alisema kuwa Hospitali hiyo ilianza Mei 22 mwaka 1986 kama Zahanati, wakati huo Kanisa lilikuwa na zahanati nzuri katika maeneo ya Pugu kwenye shule ya Mtakatifu Fransisko, iliyotaifishwa mwaka 1970.
Alisema kuwa Serikali ilitaka pia kuchukua Zahanati hiyo iliyoendeshwa na Masista wa Baldeg. Kardinali Laurean Rugambwa aliyependa kuwa na hospitali ya Jimbo akishauriana na viongozi jimboni, alisisitiza wabadilishane na Zahanati ya Serikali iliyokuwa hapo Ukonga.
“Ukonga palikuwepo tayari Parokia, na Paroko wake Padri Zakeo, Mfransiskani Mkapuchini, alifanya kazi kubwa katika mchakato mzima wa makabidhiano. Bahati nzuri Waamini wa Ukonga walimpenda sana Padri Zakeo, nao wote kupitia Halmashauri ya Walei ya Parokia ya Ukonga, walikuwa nyuma yake katika shughuli nzima, hasa kazi ya kukabidhi umiliki wa viwanja,” alisema Katibu, na kuongeza,
“Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa aliwaomba Masista wa Shirika la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu wa Bukoba waje kusimamia zahanati hii ya Ukonga, na Viongozi wao wakakubaliana Septemba 17 mwaka 1984 Shirika liliwatuma Masista wawili wauguzi na wakunga, Sista Ariadina Bijuka na Sista Mechtilda Lwakalema, ambao bado wako hai mpaka leo.”
Katibu alisema kuwa wakati mchakato wa makubaliano na Serikali ukiendelea, Kardinali Laurean Rugambwa alianza kujenga Konventi ya Masista katika kiwanja cha Kanisa Parokiani Ukonga. Baadaye Jimbo Kuu lilipata kiwanja cha zahanati na kujenga nyumba nyingine ya Masista mwaka1995, na konventi ya kwanza ilibadilishwa na kuwa nyumba ya Mapandri.
Alibainisha kuwa mazungumzo juu ya makabidhiano yalikuwa magumu kwa sababu ya uwepo wa wengine ambao walitaka kuchukua zahanti hiyo. Mwadhama Kardinali Laurean Rugambwa ilibidi atie nguvu na ushawishi sana, akisaidiwa na Padre Zakeo na waamini, hasa wa Parokia ya Ukonga.
Alisema kuwa Mei 22 mwaka 1986, Sista Ariadina Bijuka alikabidhiwa uongozi wa zahanati ya Ukonga, akiwa bado mwajiriwa wa Serikali, na wafanyakazi wote wakiwa wa Serikali na Zahanati ikiwa bado serikalini. Wakati huo Zahanati haikuwa na madawa zaidi ya makopo kidogo ya Panadol. Hivyo, Masitsa waliamua kuwalipisha kidogo wateja na kununua dawa pole pole, watu wakaipenda zahanati, na wakaja wingi kutibiwa.
Aliongeza kuwa Machi 14 mwaka 1989, Serikali ilikabidhi jengo la zahanati, vifaa vyote na wafanyakazi kwa Kanisa.  Mwadhama Kardinali Rugambwa alimtuma Monsinyori Deogratius Mbiku (hayati), kupokea makabidhiano kwa niaba ya Jimbo.
Kwa mujibu wa Katibu huyo, mwaka 1997 ilitambuliwa rasmi kama Zahanati ya Huduma ya Uzazi ya Ukonga. Kwa upendo na heshima kwa Mwadhama Kardinali Rugambwa, mashirika ya Ulaya kwa namna ya pekee Misereor, waliendelea kusaidia zahanati hata baada ya Kardinali kuustaafu, kwa mfano mwaka 1996 Padri Stanislaus Kutajwaha alimsindikiza Kardinali Rugambwa kwenda Roma na Aachen Ujerumani, kule alishuhudia jitihada zake katika uzee wake alivyoendelea kupigania Hospitali ya Rugambwa, pale Ukonga.
Anasema, “Shughuli zake huko Aachen zilionyesha wazi kwamba hata katika uzee, tamaa yake Mwadhama ilikuwa bado ni kujaribu kwa uwezo wake wote, kuinua hali ya watu wake kiroho na kimwili.
Wakati huo pia ndoto yake ilikuwa kuboresha makao ya masista wa Shirika Jipya la Masista wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, na kupanua Hospitali ya Ukonga kwa ajili ya hudma za afya kwa wananchi.
Alisema pia kuwa mwaka 2001 kituo cha Ukonga kiliweza kutoa huduma za upasuaji, hasa kwa akinamama wajawazito na watoto. Kutoka mwaka 1999 hadi 2008, Shirika la Kiitaliani ola CUAMM likiongozwa na Dkt. Flavio Bobbio lilileta misaada mingi katika Mradi wa Uzazi Salama wakitoa vifaa, dawa, mafunzo, hata na usafiri wa gari ya wagonjwa.
Katibu huyo alisema kuwa kwa sasa wanamshukuru Mungu kwa kuweza kupata cheti rasmi cha kupandishwa ngazi ya Hospitali hiyo hadi kuwa Hospitali ya Mkoa kuanzia Januari 27 mwaka 2022.
“Tunaendelea taratibu katika maboresho mbalimbali ya kukidhi huduma zinazopaswa kutolewa katika Hospitali ya Mkoa. Basi ninyi kama wadau wakubwa wa Kanisa letu Jimboni Dar es Salaam, tunaendelea kuwaomba mtushike mkono ili tuweze kuikamilisha hii kazi iliyopo mbele yetu ya upanuzi wa Hospitali, ili wananchi wote waweze kupata huduma bora kutoka katika hospitali yetu hii,” alisema Katibu.
Aliwashukuru Walezi hao kwa kufika katika hospitali hiyo, huku akiendelea kuwaomba zaidi ufadhili wao ili waendelee kusonga mbele.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya limepata Askofu mpya Msaidizi Mhashamu Askofu Mteule Godfrey Jackson Mwasekaga.
Baba Mtakatifu Fransisko alifanya uteuzi huo hivi karibuni ambapo kabla ya uteuzi huo, Askofu Msaidizi Mteule Godfrey Jackson Mwasekaga, alikuwa Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Fransisko wa Assisi, Mwanjelwa, Jimboni Mbeya, na pia alikuwa Makamu Askofu wa jimbo hilo.
Alisoma katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Augustino, Peramiho, Jimbo kuu Katoliki la Songea, na hatimaye akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 14 Julai, 2005 kwa ajili ya Jimbo kuu la Mbeya. Hadi kuteuliwa kwake alikuwa ni Makamu Askofu Jimbo Kuu la Mbeya, Mkurugenzi wa Idara ya Katekesi Jimbo, na Mkurugenzi wa Kituo cha Katekesi na Paroko wa Mwanjelwa.
Askofu Msaidizi Mteule Godfrey Jackson Mwasekaga (pichani) alizaliwa Machi 17 mwaka 1976 huko Kyela, Mbeya. Alisoma katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Augustino, Peramiho, Jimbo Kuu Katoliki la Songea, na hatimaye alipewa Daraja Takatifu ya Upadri Julai 14 mwaka 2005 kwa ajili ya Jimbo Kuu la Mbeya.
Tangu wakati huo kama Padri, aliteuliwa kuwa Paroko-usu Parokia ya Mtakatifu Claver, Mlowo, kati ya Mwaka 2005 hadi Mwaka 2008. Mkurugenzi wa Idara ya Katekesi Jimbo, na Mkurugenzi wa Kituo cha Katekesi kati ya Mwaka 2006 hadi mwaka 2008.
Alitumwa na Jimbo Kuu la Mbeya kujiendeleza kwa masomo katika Taalimungu katika Taasisi ya “Salesiano San Tommaso Messina” nchini Italia.
Baadaye akazama zaidi katika Taalimungu na kujipatia Shahada ya Uzamivu katika Taalimungu kutoka katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wasalesian, kilichoko Roma, kati ya Mwaka 2008 hadi mwaka 2017.
Baada ya masomo yake, alirejea Jimboni Mbeya na kuteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro Claver, Mlowo, kati ya Mwaka 2018-2019.
Kuanzia mwaka 2017 ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Katekesi Jimbo Kuu la Mbeya, Mkurugenzi wa Kituo cha Katekesi na Mratibu wa Liturujia ya Kanisa. Na pia kuanzia mwaka 2019, akateuliwa kuwa Makamu Askofu Jimbo Kuu la Mbeya, na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Fransisko wa Assisi, Mwanjelwa, Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya.

Na Mwandishi wetu

Mfuko wa Self (Self-Microfinance Fund) unaomilikiwa na Serikali chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, umefanikiwa kuikuza Sekta Ndogo ya Fedha na Wajasirimali kwa kutoa mikopo yenye thamaini ya Shilingi bilioni 324 katika kipidi cha kufikia Desemba 31 mwaka 2023.
Aidha, Self imejipanga kuhakikisha inasogeza zaidi huduma zake kwa kuongeza matawi nchi nzima kutoka 12 ya sasa hadi kufikia 20 ifikapo mwaka 2026, kwa kutengeneza mifumo mizuri ya ufuatiliaji na usimamizi wa fedha ili kuwafikia watu wengi, wakiwemo wakulima katika maeneo ya vijijini.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Self, Mudith Cheyo alisema hayo hivi karibuni katika Mkutano wake na Wahariri na Waandishi wa Vyombo yya Habari nchini, akielezea mafanikio, mipango mikakati na changamoto katika Taasisi hiyo ya fedha.
“Sisi kama Self, tangu tulipokabidhiwa mamlaka hii mwaka 2015 kuiinua sekta ndogo ya fedha, tumeweza kufanya kazi kubwa katika utoaji wa mikopo kwa wajasiriamali na Taasisi 200 nchi nzima …na katika hilo tumesaidia sana katika kuikuza na kuiendeeleza Sekta Ndogo ya Fedha nchini,” alisema Cheyo.
Cheyo alisema kuwa pamoja na mambo mengine, kwa sasa Self inaendelea na mikakati yake ya kujiimarisha zaidi, kwani tangu ilipopewa mtaji na serikali ili kuikuza na kiendeleza Sekta Ndogo ya Fedha kwa njia ya mikopo, wameiwezesha taasisi hiyo kujitegemea, na haijawahi kurudi serikalini kuomba tena mtaji.
Cheyo alifafanua kwamba Serikali iliwapatia mtaji wa Shilingi bilioni 56, na kwa usimamizi mzuri wa Taasisi hiyo, wameweza kutengeneza faida na sasa wamefikisha Shilingi bilioni 62, na imekuwa ikitoa gawio la Shilingi milioni 240 hadi milioni 250 kwa Serikali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa Mfuko wa Self, Petro Mataba, alibainisha kuwa katika kutekeleza majukumu yake, Self ilitoa elimu ya fedha kwa wajasiriamali 1517, kuhusu namna ya kusimamia fedha na uendeshaji biashara.
Akizungumzia changamoto zinazoikabili Self, Mataba alisema kuwa wakopaji wengi wamekuwa wakishindwa kurejesha mikopo yao, lakini uongozi wa Taasisi hiyo umejipanga na kufanikisha kudhibiti mikopo chechefu kwa asilimia 10.
Aidha, alisema kuwa changamoto nyingine ni wakopaji kushindwa kutekeleza mipango waliyojiwekea, na hivyo kuelekeza fedha za mikopo katika mambo ambayo hawajakusudia, matokeo yake wanakwama kulipa madeni yao.
Kwa upande wa mipango ya baadaye ya Taasisi hiyo, Mataba alisema kuwa mfuko huo umejipanga kupanua wigo wake kwa kuwafikia watu wengine hadi maeneo ya vijijini, ili kuwawezesha watu wengi katika sekta ndogo ya fedha kupata mikopo ili kujikwamua kiuchumi.
Mpango mwingine ni kuongeza ufanisi kwa kutumia njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ili kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi, na kutoa huduma endelevu kwa watu.

Na Mwandishi wetu

Mbunge wa Jimbo la Segerea Wilayani Ilala, Jijini Dar es Salaam, Bonnah Kamoli, amesema kuwa dhamira yake ni kuhakikisha barabara za Jimbo hilo zinapitika wakati wote, ikiwa ni pamoja na kujengwa kwa kiwango cha lami, zege au changarawe.
Kamoli alisema hayo katika hafla ya Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tanzania Rural and Urban Roads Agency: TARURA) Wilaya ya Ilala, kukabidhi mradi wa ujenzi wa barabara ya Zimbili-Kichangani ya kilomita 0.5 kwa Mkandarasi Kampuni ya SERC Constructions Co.Ltd, katika Kata ya Kinyerezi.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Waliokuwa wanafunzi katika Shule za Seminari nchini, wamekutana na kutafakari Neno la Mungu katika mafungo yaliyoandaliwa na Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, huku wakiaswa kutambua kwamba hata Mtu anapojiona ni Mtakatifu kiasi gani, lakini bado mbele za Mungu, ni mdhambi, kwani Mungu ndiye Mtakatifu pekee.
Kauli hiyo ilitolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi katika Mafungo ya ‘Former Seminarians’, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, yaliyofanyika katika Kituo cha Hija – Pugu, jimboni humo.
“Mbele ya Mungu hata kama uko Mtakatifu kiasi gani, mbele ya Mungu ambaye ndiye utakatifu wote, ndiye ukamilifu wote, ni lazima ujitambue kwamba uko mdhambi, kwa kuwa Mungu tu ndiye peke yake Mtakatifu, Mungu tu ndiye peke yake mwenye haki, na Mungu tu ndiye peke yake asiye na lawama yoyote. Sisi wote tumeshaguswa na dhambi,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Aidha, Askofu Mkuu aliwasihi Waseminari hao kutokuona haya kumwomba Mungu toba, au kujikabidha mbele za Mungu na kuomba huruma yake, kwani yeye ndiye anayewastahilisha, anayewatakasa na kuwawezesha.
Aliwataka kutokuogopa kufuata mfano wa mtoza ushuru, ambaye kwa kujitazama mapungufu yake, alisimama mbali na kujipiga kifua, huku akiomba toba.
Aliwaonya kuacha kujitokeza mbele za Mungu na kumkumbusha kwamba wao ni wenye haki kutokana na mambo wanayoyafanya katika maisha yao.
“Yaani mtego wa kufanya mazoezi fulani ya kiroho au ya kidini, na kujidhani sasa wamemuweka Mungu sawa, na kujidhani kwamba sasa sisi ni wenye haki, ndivyo alivyofanya yule Mfarisayo aliyeenda mbele ya Altare akaanza kumkumbusha Mungu jinsi yeye Farisayo alivyo na fadhila.
“Niwakumbushe tu kidogo, alimwambia Mungu, tazama mimi nilivyo mwenye haki, nafanya kadha wa kadha. Siko mzinzi, siko mwizi, siko mwongo, siko mvivu…… Yaani ni kama Mungu anatangaziwa hizo fadhila kusudi iweje. Kusudi mategemeo ni kwamba Mungu atampigapiga mabegani, na kumwambia ‘well done’. Lakini Mungu siyo wa hivyo, Mungu harubuniwi,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Alisema kuwa malezi waliyoyapata Waseminari hao pindi wakiwa Seminarini, yamewaunda na kuwapa fursa ya kupambanua na kuitikia wito wa Mungu.
Askofu Mkuu alisema kuwa kijana mdogo katika kukua kwake anapojitambua, asaidiwe ili akue katika mtindo ambao unamjenga kiutu, kiroho, na unamsababisha afanye maamuzi sahihi.
Aliwataka wale walioondolewa Seminarini ambao bado wana majeraha, kuondoa majeraha hayo, ili waamue kujikabidhi kwa Mungu na kuomba neema ya kukua katika njia zake, pamoja na kusamehe.
Pia, alisema kuwa mtu asiyesamehe, anaendelea kubeba mizigo, hivyo akawataka walioondolewa Seminarini, kuacha kujibebesha mizigo ya hasira, na ya kutaka kulipiza kisasi.
Kwa upande wake Mkuu wa Majeshi Mstaafu (CDF), Venance Mabeyo, akizungumza kwa niaba ya Waseminari wa zamani, alisema kuwa hiyo ni fursa kubwa kukutana katika Adhimisho hilo, kwani wengine hawafahamiani kutokana na wingi wao.
Mabeyo aliwasihi Waseminari wenzake wa zamani kuwa watu wa kusameheana pale wanapokoseana, huku wakiepuka kuwa na jazba, akisema kwamba yeyote mwenye jazba, neno ‘msamaha’ halikai katika msamiati wake.
Alisema pia kuwa kila mmoja anatakiwa kujitafakari na kujiuliza, je, anafanya mara ngapi matendo ya huruma? Huku akisisitiza kuishi vizuri na watu wa hulka tofauti tofauti katika jamii zao.