DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Thomas More - Mbezi Beach, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Ladislaus Kapinda amewataka Waamini kuwa watu wa upendo na jirani zao katika jamii wanamoishi.
Padri Kapinda aliyasema hayo hivi karibuni katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Uzinduzi wa Kanda mpya ya Bethlehemu inayoundwa na Jumuiya nne za Mtakatif Rita wa Kashia; Mtakatifu Monika; Mwenyeheri Isdori Bakanja; na Mtakatifu Michael Malaika Mkuu.
“Kuweni na upendo na jirani zenu katika jamii zenu mnamoishi. Muwe watu wa sala, huku mkiwa na furaha huko mnakoishi, mkiwa kama Jumuiya moja, Kanda au hata Parokia... tambueni kwamba ninyi ni wamoja katika Kristo Yesu, akasema,
“Inawapasa kula chakula pamoja, maana mmekuwa ndugu na Wanajumuiya, hivi ndivyo Kristo anavyotaka, ndiyo maana ametuachia zawadi ya upendo,” alisema Padri Kapinda.
Padri Kapinda alisema kuwa msalaba huo ndio mafanikio makubwa katika imani moja ya Kanisa Katoliki, huku akiwasihi Waamini kutumia msalaba huo ili uwaletee neema katika maisha yao.
Aliongeza kuwa msalaba huo ni alama kwa kila Mkristo, huku akiwakumbusha kufahamu kwamba kila mmoja amekombolewa na msalaba.
“Mimi niwaombe sana muwe Waamini wazuri na wenye kulitunza Kanisa pamoja na kuilinda imani yenu kama Kristo mwenyewe. Kupokea msalaba ndiyo alama kuu kwa Mkristo,” alisema Padri Kapinda.
Wakati huo huo pia, Padri Kapinda aliwakumbusha waamini kuulinda Ukristo wao ili wasije wakaukataa kwa kudanganywa na watu wasio waminifu mbele ya Mungu.
“Waamini nawaomba sana, msiache kutoa michango ili Kanisa letu liweze kuisha kujengwa, maana bila michango yenu, hatutaweza. Kwa hiyo, Kanisa tutajenga bila hofu, maana msalaba umefika na kuzunguka maeneo yote ya Kanda na Jumuiya zetu,” alisema Padri huyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Walei Parokia hiyo, Juliana Palangyo alisema kuwa Parokia yao imebarikiwa kuwa na imani, huku akiwaasa Waamini wenzake kwamba kwa kupitia msalaba huo, wamwombe Mungu azidi kuwapa baraka katika maisha yao.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kanda hiyo, Deogratius Kweka aliwasihi Waamini kutambua kwamba kanisa bado halijaisha, hivyo waendelee kutoa michango yao ili kuweza kukamilisha ujenzi huo.
Adhimisho hilo la Misa Takatifu lilikwenda sanjari na kupokea Msalaba wa Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya Ndogo Ndoko za Kikristo (JNNK), unaoendelea kutembezwa katika Parokia hiyo.