Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha
Burudani

Burudani (6)

Dar es Salaam

Na Arone Mpanduka

Kuimba ni kutamka maneno katika hali ya kimuziki, au pia twaweza kusema ni kutamka maneno moja baada ya jingine kwa sauti yenye lahani (sauti ya ala ya muziki,tyuni) au ghani (melodi).
Mwimbaji ni mtu yeyote mwenye uwezo wa kuimba kwa sauti yake  bila kutumia vyombo vya muziki.
Ikumbukwe pia kuwa katika vikundi vya uimbaji, wapo wale wanaoongoza wengine katika uimbaji (lead singers), na wengine kazi yao ni kuitikia (backing singers).
Kuna mitindo mbalimbali ya uimbaji. Wengine wanaimba huku wamesimama wima, wengine wanaimba huku wamekaa, na wengine wanaimba huku wakionesha ishara mbalimbali kwa mikono, miguu yao,au vyote viwili.
Mitindo ya uimbaji ni mizuri iwapo tu inasaidia kufikisha ujumbe kwa wahusika. Huduma ya uimbaji siyo “show.”

JINSI YA KUPATA WIMBO/MADA MPYA
Watu wengi wanapenda vitu vipya,mathalan kiatu kipya, gauni jipya, nyumba mpya,vyombo vipya, n.k. Vivyo hivyo, watu wanapenda kusikia nyimbo mpya. Lakini je, ni rahisi kwaya au watunzi wa nyimbo kutunga nyimbo mpya kila mara?
Mambo yafuatayo yanaweza kukusaidia kupata nyimbo au mada mpya.Ukisikia sauti ya wimbo (melody) moyoni mwako, fanya haraka kuirekodi kwenye kanda (kama una radio cassette na microphone au simu).ili usisahau.
Njia nyingine ni kusoma sana vitabu mbalimbali vya kisiasa, kiuchumi na historia za ndani na nje ya nchi, ili vikupe uelewa mpana wa kuimba maudhui unayoyataka.
Pia, unaweza kuwa mdadisi wa mambo kwa kuuliza wajuzi mbalimbali, na kufuatilia vyombo vya habari kuhusiana na yale yanayoendelea kujitokeza kila siku.
Wimbo unaweza kuwa na mada (topic) moja au zaidi. Lakini wimbo wenye mada moja ni mzuri zaidi. Kwa nini?
Wimbo wenye mada moja mara nyingi unaanza kwa utangulizi,baadaye unaelezea mada yenyewe, na kisha unatoa hitimisho.Kwa hiyo ni rahisi kukumbuka ujumbe wa wimbo huo.
Pia, hakikisha unakuwa na ufafanuzi wa kutosha. Beti 3 au 4 zinaweza kuzungumzia mada moja tu kwa kuifafanua. Mada ya wimbo inaweza kumlenga mtu mmoja au watu kadhaa.
Nyimbo nyingi zinaangukia katika makundi mbalimbali, kama vile nyimbo za mafundisho/maonyo, Nyimbo za Faraja, Nyimbo za Mahubiri,
Nyimbo za siasa, nyimbo za uchumi na nyimbo za kuburudisha ambazo ndani yake zinaweza kukosa ujumbe sahihi, lakini zikaishia kuwa na midundo mizuri kwa lengo la kusherehesha.

VYAKULA NA VINYWAJI KWA MWIMBAJI
Vilaji na vinywaji visivyofaa kabla ya kuimba, ni muhimu ili kuepuka kuimba  tumbo likiwa tupu kabisa. Kuimba ni kama riadha, inahitajika nguvu kwa ajili ya utendaji wako. Hata hivyo, ni muhimu pia kuepuka kuimba tumbo likiwa limeshiba sana.
Kumbuka kuimba ni kazi ngumu, unahitaji mafuta (you need fuel), hivyo inashauriwa kuwa na mlo wa kawaida wa saa moja au mbili kabla ya uimbaji.
Kulingana na mazoea yetu, vipo vyakula na vinywaji ambavyo ni vigumu kuachana navyo ghafla, mengine huchukua muda.

VYA KUZINGATIA UWAPO STUDIO YA MUZIKI
Mosi; Usikimbilie kwenye chumba cha kurekodia kabla hujawa tayari. Kusimama studio ili kurekodi inaweza kuwa ya kukatisha tamaa kwa waimbaji wapya. Hivyo, fanya mazoezi sana kabla ya kurekodi.
Pili; Jaribu kujirekodi mwenyewe kabla ya kuingia studio, na sikiliza kujua kile ulichokipenda, na kusahihisha usichokipenda. Chagua funguo sahihi ili kuweza kufikia nota za juu kwa wepesi, mbinu zako za kiuimbaji zinatakiwa kuwa nzuri kiasi cha kuzuia kupoteza muda katika studio kwa kurekodi mara nyingi, na kutumia tyuni nyingi.
Tatu; tumia vizuri microphone katika kuimba. Katika studio hakikisha kunakuwa na umbali fulani kutoka mdomoni mwako hadi kwenye microphone. Waimbaji wenye uzoefu mdogo kwenye microphones hujikuta wakiyumbisha vichwa vyao, kitu ambacho kinaweza kuharibu ubora wa sauti.Sogea karibu na microphone sauti inapokuwa ndogo, na mbali inapokuwa kubwa. Hii itakusaidia kuondoa tofauti ya kupanda na kushuka kwa sauti.
Nne; Epuka kusisitiza maneno yenye P na B ambayo mara nyingi huzalisha sauti yenye popp. Pia weka msisitizo kwenye maneno yenye F na S.
Tano; Dhibiti sauti za pumzi (kuhema kwa sauti). Kudhibiti sauti za pumzi wakati wa kurekodi itasaidia kuondoa usumbufu wakati wa kuhariri sauti.
Sita; Kabla hujaanza kurekodi, jaribisha aina tofauti za microphone kuona ni ipi inayofaa. Unaweza kurekodi ubeti mara kadhaa, na kusikiliza ipi inayofaa.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Bendi ya Urafiki ilianzishwa mwaka 1970 na kiwanda cha nguo cha Urafiki ambacho kilikuwa ni kiwanda cha Umma kwa wakati huo. Kiwanda kilijengwa kwa msaada wa watu wa Jamhuri ya China.
Azma ya kuanzishwa bendi katika kiwanda hicho ilitokana na umuhimu wa kutangaza bidhaa zake ambazo zilikuwa ni Khanga na Vitenge, na hasa ikizingatiwa ushindani uliokuwepo wakati huo Tanzania, kulikuwa na viwanda vingi vilivyotengeneza bidhaa hizo.
Meneja Mkuu wa kiwanda cha Nguo cha Urafiki kwa wakati huo, Joseph Rwegasira aliubariki mpango huo wa kuanzishwa bendi ya dansi ya kiwanda na hivyo aliidhinisha malipo ya hundi ya shilingi 50,000/=   kununulia seti ya vyombo vya muziki katika duka la Dar es Salaam Music House, mtaa wa Samora Avenue.
Ili kupata kundi lililo bora, Menejimenti ya kiwanda cha nguo cha Urafiki ilimuajiri Juma Mrisho Feruzi, maarufu kama Ngulimba Wa Ngulimba, na kumuagiza atafute wapigaji kutoka popote ili kuunda kundi imara. Katika kuhakikisha bendi hiyo mpya inasimama barabara, Ngulimba alichukua wapigaji watano kutoka Orchestre Qwillado, bendi ambayo aliipigia kabla ya kuanza Urafiki. Na hii ndio maana nyimbo za mwanzoni za bendi ya Urafiki zilionekana kama zina mahadhi ya Orch. Qwillado.
Wanamuziki aliowachukua Ngulimba kutoka Orch. Qwillado walikuwa ni Maiko Vincent Semgumi, mpiga gitaa la Solo, Ayoub Iddi Dhahabu ,Besi, Abassi Saidi Nyanga (Tenor Saxophone) na Fida Saidi(Alto Saxophone). Ngulimba yeye akiwa mwimbaji na pia kiongozi wa bendi ya Urafiki.
Wanamuziki wengine wa mwanzoni ambao waliungana na hao watano waliotoka Orch. Qwillado  ambao tayari walikwisha ajiriwa kiwandani Urafiki, walikuwa Juma Ramadhani Lidenge(Second Solo), Mohamed Bakari Chachil(gitaa la kati), Ezekiel Mazanda(rhythm), Abassi Lulela(Besi), Hamisi Nguru(Mwimbaji), Mussa Kitumbo(Mwimbaji), Cleaver Ulanda(Mwimbaji), Maarifa Ramadhani(Tumba), Juma Saidi (Manyanga) na Hamisi Mashala(Drummer Boy).
Mtindo walioanza nao Urafiki ulijulikana ‘Mchaka Mchaka’ na baadae ukabadilika na kuwa ‘Chaka Chua’ na hatimae mwisho bendi inaelekea ukingoni walipiga mtindo wa ‘Pasua’ na ‘Patashika’
Mwaka 1971 Gidion Banda, mwanamuziki kutoka bendi ya Morogoro Jazz alijiunga nabendi ya Urafiki, yeye alikuwa mpulizaji ala ya upepo, Saxophone.
Bendi ya Urafiki ikiwa katika hali yake ya uchanga mwaka 1970 ilipata ajali ya gari, iligonga mti maeneo kona ya Kigogo na Msimbazi Mission wakati dereva akiwa katika spidi  kali. Walikuwa wakitokea kwenye onyesho la usiku lililofanyika Ukumbi wa Chang’ombe, Temeke.
Baadhi ya wanamuziki waliumia sana na gari lao, ‘VW Comby’ ilikuwa halifai kabisa.
Wapigaji walioumia walikuwa ni Hamisi Mashala Drummer Boy alivunjika mguu, Mohamed Bakari Chachil aliumia kichwani na kupata ‘stich’ na pia Ayoub Iddi Dhahabu na Maarifa Ramadhani walipata maumivu makali kwa ndani mwilini.
Bendi ilisimamisha maonyesho yake kwa muda hadi wasanii wake walipopata nafuu na kuanza maonyesho tena. Hali ya ajali ile ilileta fikra mbaya kwa wasanii wa Urafiki na wapenzi wao na ilionekana kana kwamba kulikuwa na mkono wa mtu katika ajali ile ambapo hakuwatakia mema wanamuziki wa Urafiki. Juma Mrisho ‘Ngulimba’ alitunga wimbo ‘Nimekosa Nini Jama’, wimbo ulioelezea kadhia hiyo.
Aidha, Bendi ya Urafiki ilipitiwa na wanamuziki wengi, baadhi wakiwa ni Thobias Cosmas Chidumule na Frank Mahulu. Waimbaji waliotokea Western Jazz (Saboso) mwaka 1973 na kuongeza nguvu katika safu ya uimbaji.  Waimbaji hao walishiriki nyimbo nyingi baadhi zikiwa Tausi Karuka, Jembe na Panga (Geza Ulole), Kosa la Nani, Mauaji ya Soweto, Rukia Hukusikia, Maonyesho ya Mtu Mweusi n.k.
Pia katika safu ya upulizaji  na magitaa waliongezeka Mkali na Hidaya kutoka Morogoro wakipuliza matarumbeta. Hao walikuja mwaka 1973 na Ali Saidi aliyetokea Cuban Marimba akipiga gitaa la kati (rhythm) na baadae mwaka 1975, Mganga Hemedi kutoka Tanga, akitokea Atomic Jazz, nae alijiunga na kuwa upande wa solo na rhythm.
Bendi ya Urafiki imetunga nyimbo nyingi, zaidi ya mia tatu zinazoelekeza kwenye siasa, mapenzi, nasaha na mafundisho na pia kukosoa. Baadhi ya nyimbo zake za siasa zilizopata umaarufu ni kama zile Mwenyekiti Nyerere, Mauaji ya Soweto, Jembe na Panga n.k.
Tungo au nyimbo zao zimesaidia kuhamasisha  ukombozi  wa Bara la Afrika na kutoa muelekeo wa sera za nchi kama vile Kilimo cha kufa na kupona na uhamasishaji wa kuhamia vijijini. Nyimbo hizo zimetoa mchango mkubwa sana katika siasa za Tanzania.
Mwaka 1975 Bendi ya Urafiki ilishiriki katika mashindano ya bendi za muziki wa dansi yaliyofanyika Mnazi Mmoja Dar es Salaam na bendi ya Urafiki ilishika nafasi ya tatu na Mzee Ngulimba, kama kiongozi wa Bendi ya Urafiki aliiwakilisha Tanzania pamoja na bendi ya Afro 70 iliyopata nafasi ya kwanza na baadhi ya vikundi vya utamaduni kutoka Tanzania Bara na Zanzibar nchini Nigeria katika maonyesho ya mtu mweusi yaliyofanyika huko.
Kufikia katikati ya miaka ya 1980, bendi ya Urafiki ikawa inasuasua kutokana na uchakavu wa vyombo na Menejimenti iliyokuwepo wakati huo haikuwa tayari kutoa pesa kununulia vyombo vipya.Na huo ndiyo ukawa mwisho wake kwa kufa taratibu.

NEW YORK, Marekani
Andy Murray amekiri kuwa Novak Djokovic anatazamiwa kutawala tenisi ya wanaume kwa miaka mingi ijayo, huku kizazi kipya cha wachezaji kikiwa bado chini ya kiwango chake.
Mserbia huyo mwenye umri wa miaka 36, alishinda taji la 24 la Grand Slam ambalo ni rekodi sawa na rekodi kwa kumshinda Daniil Medvedev katika fainali ya US Open mjini New York, Jumapili.
“Ni juu ya vijana kumsukuma Novak na kutafuta kumpita haionekani kama hilo linakaribia kutokea, kwani amekuwa mchezaji wa ajabu kwa muda mrefu sana, Uhai mrefu wa Novak umekuwa mkubwa zaidi. Amecheza kwa kiwango hiki kwa muda mrefu sasa,” alisema Murray.
Djokovic alishindwa katika fainali ya Wimbledon mwaka huu na Mhispania mwenye umri wa miaka 20, Carlos Alcaraz.
Mshindi mara tatu wa Grand Slam, Murray ambaye alikuwa akizungumza katika mkesha wa kampeni ya Davis Cup ya Uingereza, alisema kuwa hitimisho lisilo sahihi lilitolewa kutokana na kushindwa kwa Djokovic katika SW19.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Women Jazz Band ilikuwa bendi ya muziki wa dansi jijini Dar es Salaam, Tanzania. Bendi ilianzishwa mnamo 1965 ikiwa na wanawake tupu, lakini baadaye ilileta wanaume kwenye upande wa kupiga vyombo.
Mwaka 1965 kundi jipya la muziki la aina yake lilianzishwa Tanzania. Lilikuwa ni bendi ya akina mama watupu. Akina mama hawa, wengine wakiwa wafanyakazi wa Government Press, walijichagua na kuanza kuhudhuria mafunzo ya muziki chini ya yule mwanamuziki mahiri Mzee Mayagilo, aliyekuwa kiongozi wa shughuli za muziki katika Jeshi la Polisi.
Akina mama hawa wakawa chini ya kitengo cha Polisi Jazz Band, wakaanza kufanya mazoezi ya nguvu. Bendi hiyo ya akina mama ilikuwa chini ya ufadhili wa TANU Youth League.
Wakati wakianza shughuli hiyo, walikuwa hawana ujuzi wowote wa muziki. Kutokana na jitihada waliyofanya, taratibu wakaanza kufanya maonyesho yao, hasa kwenye hafla za Serikali na Chama tawala wakati huo.
Tarehe 31 Mei 1966, Women Jazz band iliingia katika studio za Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na kurekodi nyimbo sita ambazo ni ‘Tumsifu Mheshimiwa’; ‘Leo Tunafuraha’, ‘Mwalimu Kasema’; ‘Women Jazz’; na ‘Sifa nyingi tuwasifu Viongozi na TANU yajenga nchi.’
Bendi hiyo iliundwa na Washiriki kama Mary Kilima (Mwimbaji); Juanita Mwegoha (Mwimbaji); Siwema Salum (Mwimbaji); Rukia Hassan (Mwimbaji); Kijakazi Mbegu (Solo Guitar); na Mwanjaa Ramadhan (Bass Guitar).
Wengine ni Chano Mohammed (Rhythm Guitar); Tatu Ally (Alto Sax); Mina Tumaini (Tenor Sax); Anna Stewart (Alto Sax); Rukia Mbaraka (Tenor Sax); Lea Samweli (Bongos, au Conga); Josephine James (Drums); Zainab Mbwana (Maracass); na Tale Mgongo (Timing).
Inaelezwa kuwa wazo la kuwa na bendi ya wanawake tupu lilianzia kwenye bendi ya wanawake ya Les Amazones De Guinee ya nchini Guinea kwa wakati huo.
Kipindi hicho, Rais wa Guinea ya Conakry, Sekou Toure alikuwa na tabia ya kuambatana na bendi yake hiyo katika ziara zake mbalimbali Barani Afrika, na nje ya Afrika.
Ndipo mwaka 1965, Rais huyo alipata fursa ya kufanya ziara nchini Tanzania na kuja na ndege iliyosheheni wasanii wengi wa kike kuliko wanasiasa, ambapo miongoni mwa bendi alizoambatana nazo kwenye msafara wake, ni ya Les Amazones.
Wakati walipowasili,baadhi ya mabinti wa TANU Youth League hapa nyumbani ndio walikuwa wenyeji wa wanamuziki hawa wa kike. Rais Sekou Toure na wasanii wake walipoondoka walikuwa wamepanda wazo la vikundi vya sanaa vya Taifa, na pia wazo la bendi ya wanawake.
Wanawake waliokuwa wakizunguka na wanamuziki wa kigeni, wengi wakiwa wanafanya kazi Government Press, waliazimia nao kuanzisha bendi ya wanawake, japo walikuwa hawana ujuzi wa chombo chochote cha muziki, lakini nia yao ilikuwa kuwa na bendi kama Les Amazones.
Women Jazz ilipata umaarufu kiasi cha kuanza kufanya safari nje ya Tanzania, na kuweza kufanya maonyesho Nairobi na Mombasa nchini Kenya, baada ya kutembelea miji kadhaa nchini Tanzania.
Wakati wa matayarisho ya kwenda China, kundi lilisambaratika. Kikubwa kilichosababisha hili ilikuwa ni wanamuziki kuona hawapati chochote kutokana na mapato yaliyotokana na muziki wanaoupiga.
Baada ya bendi kufa, TANU youth League ikachukua vyombo vyake na kuvihifadhi, hatimaye vyombo hivi vikawa ndivyo vyombo vilivyotumika kuanzisha Vijana Jazz Band chini ya Mzee John Ondolo, miaka kadhaa baadaye.
Vijana Jazz Orchestra ambayo ilikuwa inajulikana kama Vijana Jazz Band au Vijana Jazz) ilikuwa ni bendi ya muziki wa dansi ya Kitanzania iliyofikia kilele cha umaarufu katika miaka ya 1980.
Kama ilivyokuwa kwa bendi nyingi za dansi za enzi hizo, ilifadhiliwa na taasisi ya Serikali, yaani Umoja wa Vijana kupitia Tawi la Vijana la Chama Tawala cha Tanzania (TANU) kwa wakati huo.
Bendi hiyo ilianzishwa mwaka 1971 na John Ondolo Chacha. Mnamo mwaka wa 1978, serikali ya Tanzania ilipitisha sheria iliyoruhusu bendi kununua ala za kigeni (jambo ambalo hapo awali lilikuwa limekatazwa na Baraza la Muziki la Taifa (BAMUTA), baraza la serikali linalohusika na udhibiti wa biashara ya muziki).
Vijana Jazz ilikuwa mojawapo ya bendi za kwanza kuchukua fursa hii, na katika miaka ya 1980, ilipata umaarufu mkubwa kwa sababu ya sauti yake ya ubunifu iliyotumia sanisi na mashine za ngoma.
Mitindo maarufu (styles) iliyobuniwa na Vijana Jazz include sindimba, heka heka, koka koka, watoto wa nyumbani, na pamba moto. Baadhi ya wanamuziki mashuhuri waliowahi kutamba katika Vijana Jazz ni Hamza Kalala, Hemedi Maneti, Issa Chikupele na Manitu Musa.

Dar es Salaam

Na Arone Mpanduka

Bendi ya Extra Musica ambayo ilitamba sana zamani, ilianzishwa mwaka 1993 jijini Brazzaville, Jamhuri ya Congo, ikiasisiwa na wanamuziki akina Ibabi Okambi Rogatien ‘Roga Roga’, ambaye ni mahiri kwa kulicharaza gitaa la solo. Aidha, Roga Roga ndiye kiongozi wa kundi hilo hadi sasa.
Muasisi mwingine ni Espe Bass, ambaye ni muungurumishaji wa gitaa la besi. Mwaka 1995, wanamuziki wa bendi hiyo waliachia albamu yao ya kwanza ya Nouveaux Missiles, iliyowatambulisha vyema kwenye ulimwengu wa muziki.
Albamu hiyo ilipambwa na nyimbo nyingi kali, hususan ule Fred Nelson. Wanamuziki walioshiriki kwenye albamu hiyo, mbali na Roga Roga na Espe Bass, ni pamoja na Guy Guy Fall, Quentin Moyascko, Oxygen Mbon Slyvain, Dou Dou Copa ‘Elenga Laka Bienvenu’, Dominique, Christian na Herman Nagasaki, ambao wote ni waimbaji, pamoja na kunengua.
Wanamuziki wengine walikuwa akina Killa Mbongo aliyekuwa ‘rapa’, Durell Loemba, ambaye ni mcharazaji wa gitaa la rhythm. Kwa upande wa uchanganyaji ‘drums’, yupo Ngolali G’Ramatoulaye na Christian Kingstall aliyekuwa anabofya kinanda.
Wanamziki wa bendi hii ya Extra Musica walijizolea sifa lukuki, wakapendwa na wapenzi wengi kwa jinsi walivyo wajuzi katika kulishambulia jukwaa wakinengua katika maonesho yao yote, ikiwahusisha wanamuziki wenyewe kunengua, tofauti na bendi nyingine ambazo hutumia wanenguaji wa kike.
Ndiyo sababu wao walipenda kujiita ni La Difference, yaani, ni wa tofauti.
Kwenye albamu hiyo ya kwanza, kulikuwa na wanamuziki wengine ambao hawakupata nafasi ya kurekodi, wakiwemo akina Pinochet Thierry, Regis Touba, Cyrille Molanga na Arnaud Luguna.
Albamu hiyo ya Nouvoeaux Missiles, ilisababisha wanamuziki wengine nje ya bendi yao kuvutiwa nayo, mmojawapo alikuwa Samba Brice Abillissi, aliyeamua kujiunga nao.
Albamu ya pili ya Confirmation ya mwaka 1996, ilipelekea kundi hilo kuzidi kutikisa vilivyo, hadi wakapata mialiko mingi barani Afrika na Ulaya.
Inaelezwa kuwa albamu hiyo ya Confirmation iliuza nakala nyingi mno kuzidi ile ya mwanzo.
Lakini mafanikio hayo yalisababisha kuzuka kwa mgogoro mkubwa wa kimasilahi, hali iliyofanya baadhi ya wanamuziki wake wakiwamo akina Christian na Guy Guy Fall, kujiondoa kundini, japokuwa kuondoka kwa wanamuziki hao, Extra Musica iliendelea kuwa imara.
Ilipotoka albamu ya tatu ya Ouragan mwaka 1997, wanamuziki Herman Nagassaki na Samba Brice Abilliss, waliziba vilivyo mapengo ya Guy Guy Fall na Christian.
Mgogoro wa chini kwa chini ulikuwa ukifukuta miongoni mwa wanamuziki wa bendi hiyo, na uongozi. Baadhi ya wanamuziki walishindwa kuvumilia, wakaihama bendi hiyo. Wanamuziki hao walikuwa ni Arnaud Laguna, Quentin Mayascko, Durell Loemba, Cyrille Malonga, Regis Touba na Pinochet Thierry.
Wakaenda kuunda kundi lao jingine walilolipa jina la Z.I. International, chini ya uongozi wa Cyrille Malonga, Regis Touba, Pinochet Thierry na Durrell Loemba.
Baada ya bendi ya Extra Musica kukimbiwa na wanamuziki hao, walikaa chini na kuamua kuwatafuta wanamuziki wengine vijana wenye vipaji vikubwa.
Walifanikiwa kuwapata vijana hao akina Gildas Pozzi, na Emery Mboma. Wakati huo huo, Sonor alichukua nafasi ya ucharazaji wa gitaa la rhythm lilokuwa likishikwa na Durell Loemba.
Mara baada ya kuwaingiza vijana hao kundini, mwaka 1998 waliachia albam yao ya nne ya Extra Major. Albamu hiyo ilivunja rekodi ya mauzo ya albamu zote za awali na kuwaletea tuzo nyingi Barani Afrika, ikiwemo ya Kora kwa kuteuliwa kuwa bendi bora ya muziki katika Bara la Afrika.
Mwaka uliofuatia, waliachia albamu nyingine tano zilizokuwa kali mno.
Kati ya albamu hizo ile ya Shalai ilisababisha kuwapata wanamuziki wengine wakali, akina Papy Batin Maboulango na Boudouin Massipi.
Rapa wao wa kutumainiwa Killa Mbango, alijitoa kundini akaachana na muziki. Lakini baadaye alirejea kundini. Extra Musica, japo ilichukua kipindi kirefu kutoa albamu ya sita ya Trop C’Est Trop katika mwaka 2001.
Rapa mwingine alijulikana kwa jina la Arafat, nae alijiunga na bendi hiyo, akichukua nafasi iliyoachwa wazi kwa mara nyingine tena, na Killa Mbongo.
Baada ya kutoka na albamu hiyo, waliamua kubadilisha kidogo majina ya bendi yao ikaitwa Extra Musica Zagul.
Mara baada ya kutoa albamu ya saba ya Obligatoire mwaka 2004, mwimbaji wao Dou Dou Copa naye akajiondoa kundini, akafuatiwa na Oxygene mwaka 2005.Kuodoka kwa wanamuziki hao hakukuathiri Extra Musica Zagul, kwani waliachia albamu ya nane ya La Main Noire mwaka 2006, na nyingine ya tisa ya Sorcellirie ‘Kindoki’ katika mwaka 2011.
Licha ya hekaheka nyingi, bendi ya Extra Musica ilisimama tena na kwa sasa muasisi Roga Roga bado anakomaa na kundi la Extra Musica Original, huku wimbo wa Bokoko uliotoka mwaka 2021, ukiendelea kuwa maarufu.

Na Arone Mpanduka

Chimbuko la bendi ya Maquis du Zaire kwa nchi ya Tanzania lilianzia mwaka 1973, wakati Franco Luambo Luanzo Makiadi akiwa na bendi yake ya T.P. OK. Jazz alikuja hapa nchini na akafanya onyesho kamambe katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam(sasa uwanja wa Uhuru).
Mwaka mmoja baadae wa 1972, bendi ya Maquis du Zaire, nayo ikaingia kwa mbwembwe na kuweka makazi yake ya kudumu katika jiji la Dar es Salaam.
Bendi hiyo Maquis du Zaire iliyotokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikafia humu nchini miaka ya 1990.
Ilikuwa kivutio kikubwa kwa Watanzania na kuwapa hekaheka wanamuziki wa Tanzania katika miaka hiyo.
Kwa nchini Congo, bendi hiyo ilianza mwaka 1960, vijana wa wakati huo katika mji wa Kamina huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), waliungana na kuunda bendi yao, wakaiita Super Theo.
Bendi hiyo ilikuwa ikitoa burudani tosha kwa wapenzi wa muziki wa mji huo wa Kamina na vitongoji vinavyouzunguka mji huo. Baadae wakaibadilisha majina na bendi ikawa Super Gabby. Lakini uongozi wa Super Gabby ulitaka kuleta mageuzi katika muziki mwaka 1972, walipobadilisha majina rasmi na kuwa Maquis du Zaire.
Mwaka huo huo bendi hiyo iliingia hapa Tanzania wakipitia nchini Uganda.
Walipofika katika jiji la Dar es Salaam, walipata mkataba wa kupiga muziki katika ukumbi wa Mikumi Tours, uliokuwa maeneo la Tazara Buguruni, jijini Dar es Salaam.
Baada ya kumaliza mkataba wao, waliondoka wakaenda kupiga muziki katika Klabu ya Hunters kwa kipindi kifupi.
Kisha viongozi wa bendi hiyo wakafanya mazungumzo na mfanyabiashara Hugo Kisima, aliyekuwa akimiliki ukumbi wa Safari Resort, maeneo ya Kimara, jijini Dar es Salaam. Wakaanza kupiga muziki kwa mkataba na mfanyabiashara huyo.
Februari 1977 viongozi wa bendi hiyo ya Maquis du Zaire, waliamua kukiongezea nguvu kikosi chao. Hivyo walimtuma Tchibangu Katayi ‘Mzee Paul’ aliyekuwa mwanamuziki wa bendi ya Maquis du Zaire.
Pia alikuwa mmoja kati ya viongozi wa bendi hiyo.Mzee Paul aliwachukua baadhi ya wanamuziki ili kuja nao Tanzania kuongeza nguvu katika bendi ya Maquis du Zaire.
‘Mzee Paul’ alibahatika kuwachukua wanamuziki akina Kikumbi Mwanza Mpango, au ‘King Kiki’, mtunzi na mwimbaji, Kanku Kelly kwa upande wa tarumbeta., Ilunga Banza ‘Mchafu’, aliyekuwa akiungurumisha gitaa la besi, Mutombo Sozy aliyekuwa akizicharanga ‘drums’, na mnenguaji Ngalula Tshiandanda.
Wakati huo Maquis du Zaire walikuwa wakicheza muziki wakitumia mtindo wa ‘Chakula Kapombe’, ambao kwa Watanzania ulikuwa mpya, na ukapendwa mno na mashabiki.
Kufika kwa wanamuziki hao, kulileta changamoto kubwa katika muziki. Tungo nzuri za Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, zilikuwa chachu masikioni mwa wapenzi wa muziki wa dansi. Kiki pia yaelezwa kuwa ndiye aliyeleta Mapinduzi makubwa ya muziki hapa nchini Tanzania.
Maquis du Zaire wakaazisha mtindo mwingine wa ‘Kamanyola’, uliowapagaisha wapenzi na wadau toka pembe zote za jiji la Dar es Salaam.
Mwishoni mwa 1977, Marquis du Zaire walimaliza mkataba kwa Hugo Kisima, wakaondoka.Bahati nyingine ikawadondokea tena baada ya kuingia mkataba mwingine wa kupiga muziki kwa mzee Makao, aliyekuwa akimiliki ukumbi wa Savannah, maeneo ya Ubungo.Wakiwa Savannah, walianzisha mitindo ya ‘Sanifu’, na ‘Ogelea piga mbizi’.
Lakini ukumbi huo ukabadilishwa jina ukaitwa White House. Ikumbukwe kwamba Maquis pia ilikuwa ikipiga kwenye ukumbi wa Mpakani, maeneo ya Mwenge.Mwishoni mwa mwaka 1978, Maquis du Zaire  waliamua kuimarisha tena kikosi chao kwa kuwaleta wanamuziki wengine wapya kutoka DRC.Iliwaleta akina Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, Ngoyi Mubenga na Khatibu Iteyi Iteyi.
Bendi hiyo ilikuwa ikiongozwa na wanahisa akina Chinyama Chiyaza ‘Chichi’, Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’, Chimbwiza Mbangu Nguza au ‘Nguza Vicking’, Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Mbuya Makonga ‘Adios’.
Chini ya uongozi huo, katika miaka ya 1980 mafanikio makubwa yalionekana, mojawapo ni lile la kuanzisha Kampuni iliyofahamika kama Orchestra Maquis Company (OMACO).
Kampuni hiyo iliweza kumiliki shamba la matunda, wakalima kwa kutumia trekta zao maeneo ya Mbezi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Mazao yao walikuwa wakiyapeleka na kuuza katika Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam.OMACO pia ilimiliki mradi mwingine wa viwanja tisa na nyumba kadhaa, maeneo ya Sinza, jijini Dar es Salaam.
Kwa wakati huo, watu wengi hawakuwa na haja ya kuchukua teksi kurudi nyumbani, kwani muziki wa Maquis du Zaire ulikuwa unarindima hadi alfajiri. Muda ambao mabasi ya UDA ya Ikarus yalikuwa yameanza kazi. Wakati huo hazikuwepo ‘Dala dala’, Bajaji wala Pikipiki kwa maana ya Bodaboda.
Hata hivyo, baadae bendi hiyo ilianza kufa taratibu kufuatia baadhi ya wanamuziki kuondoka kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine, na wengine kusahindwa kufanya kazi hiyo kutokana na umri kuwa mkubwa, na magonjwa ya hapa na pale.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, bendi ilipotea kabisa na kuacha historia ya kipekee.
Baadhi ya nyimbo za Marquis du Zaire zilizovuma kwa uzuri na utamu wake ni ‘Ni Wewe Pekee; Makumbele; Kalubandika; na Promotion’.
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.