Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Bendi ya Urafiki ilivyotamba na kufa kimyakimya

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Bendi ya Urafiki ilianzishwa mwaka 1970 na kiwanda cha nguo cha Urafiki ambacho kilikuwa ni kiwanda cha Umma kwa wakati huo. Kiwanda kilijengwa kwa msaada wa watu wa Jamhuri ya China.
Azma ya kuanzishwa bendi katika kiwanda hicho ilitokana na umuhimu wa kutangaza bidhaa zake ambazo zilikuwa ni Khanga na Vitenge, na hasa ikizingatiwa ushindani uliokuwepo wakati huo Tanzania, kulikuwa na viwanda vingi vilivyotengeneza bidhaa hizo.
Meneja Mkuu wa kiwanda cha Nguo cha Urafiki kwa wakati huo, Joseph Rwegasira aliubariki mpango huo wa kuanzishwa bendi ya dansi ya kiwanda na hivyo aliidhinisha malipo ya hundi ya shilingi 50,000/=   kununulia seti ya vyombo vya muziki katika duka la Dar es Salaam Music House, mtaa wa Samora Avenue.
Ili kupata kundi lililo bora, Menejimenti ya kiwanda cha nguo cha Urafiki ilimuajiri Juma Mrisho Feruzi, maarufu kama Ngulimba Wa Ngulimba, na kumuagiza atafute wapigaji kutoka popote ili kuunda kundi imara. Katika kuhakikisha bendi hiyo mpya inasimama barabara, Ngulimba alichukua wapigaji watano kutoka Orchestre Qwillado, bendi ambayo aliipigia kabla ya kuanza Urafiki. Na hii ndio maana nyimbo za mwanzoni za bendi ya Urafiki zilionekana kama zina mahadhi ya Orch. Qwillado.
Wanamuziki aliowachukua Ngulimba kutoka Orch. Qwillado walikuwa ni Maiko Vincent Semgumi, mpiga gitaa la Solo, Ayoub Iddi Dhahabu ,Besi, Abassi Saidi Nyanga (Tenor Saxophone) na Fida Saidi(Alto Saxophone). Ngulimba yeye akiwa mwimbaji na pia kiongozi wa bendi ya Urafiki.
Wanamuziki wengine wa mwanzoni ambao waliungana na hao watano waliotoka Orch. Qwillado  ambao tayari walikwisha ajiriwa kiwandani Urafiki, walikuwa Juma Ramadhani Lidenge(Second Solo), Mohamed Bakari Chachil(gitaa la kati), Ezekiel Mazanda(rhythm), Abassi Lulela(Besi), Hamisi Nguru(Mwimbaji), Mussa Kitumbo(Mwimbaji), Cleaver Ulanda(Mwimbaji), Maarifa Ramadhani(Tumba), Juma Saidi (Manyanga) na Hamisi Mashala(Drummer Boy).
Mtindo walioanza nao Urafiki ulijulikana ‘Mchaka Mchaka’ na baadae ukabadilika na kuwa ‘Chaka Chua’ na hatimae mwisho bendi inaelekea ukingoni walipiga mtindo wa ‘Pasua’ na ‘Patashika’
Mwaka 1971 Gidion Banda, mwanamuziki kutoka bendi ya Morogoro Jazz alijiunga nabendi ya Urafiki, yeye alikuwa mpulizaji ala ya upepo, Saxophone.
Bendi ya Urafiki ikiwa katika hali yake ya uchanga mwaka 1970 ilipata ajali ya gari, iligonga mti maeneo kona ya Kigogo na Msimbazi Mission wakati dereva akiwa katika spidi  kali. Walikuwa wakitokea kwenye onyesho la usiku lililofanyika Ukumbi wa Chang’ombe, Temeke.
Baadhi ya wanamuziki waliumia sana na gari lao, ‘VW Comby’ ilikuwa halifai kabisa.
Wapigaji walioumia walikuwa ni Hamisi Mashala Drummer Boy alivunjika mguu, Mohamed Bakari Chachil aliumia kichwani na kupata ‘stich’ na pia Ayoub Iddi Dhahabu na Maarifa Ramadhani walipata maumivu makali kwa ndani mwilini.
Bendi ilisimamisha maonyesho yake kwa muda hadi wasanii wake walipopata nafuu na kuanza maonyesho tena. Hali ya ajali ile ilileta fikra mbaya kwa wasanii wa Urafiki na wapenzi wao na ilionekana kana kwamba kulikuwa na mkono wa mtu katika ajali ile ambapo hakuwatakia mema wanamuziki wa Urafiki. Juma Mrisho ‘Ngulimba’ alitunga wimbo ‘Nimekosa Nini Jama’, wimbo ulioelezea kadhia hiyo.
Aidha, Bendi ya Urafiki ilipitiwa na wanamuziki wengi, baadhi wakiwa ni Thobias Cosmas Chidumule na Frank Mahulu. Waimbaji waliotokea Western Jazz (Saboso) mwaka 1973 na kuongeza nguvu katika safu ya uimbaji.  Waimbaji hao walishiriki nyimbo nyingi baadhi zikiwa Tausi Karuka, Jembe na Panga (Geza Ulole), Kosa la Nani, Mauaji ya Soweto, Rukia Hukusikia, Maonyesho ya Mtu Mweusi n.k.
Pia katika safu ya upulizaji  na magitaa waliongezeka Mkali na Hidaya kutoka Morogoro wakipuliza matarumbeta. Hao walikuja mwaka 1973 na Ali Saidi aliyetokea Cuban Marimba akipiga gitaa la kati (rhythm) na baadae mwaka 1975, Mganga Hemedi kutoka Tanga, akitokea Atomic Jazz, nae alijiunga na kuwa upande wa solo na rhythm.
Bendi ya Urafiki imetunga nyimbo nyingi, zaidi ya mia tatu zinazoelekeza kwenye siasa, mapenzi, nasaha na mafundisho na pia kukosoa. Baadhi ya nyimbo zake za siasa zilizopata umaarufu ni kama zile Mwenyekiti Nyerere, Mauaji ya Soweto, Jembe na Panga n.k.
Tungo au nyimbo zao zimesaidia kuhamasisha  ukombozi  wa Bara la Afrika na kutoa muelekeo wa sera za nchi kama vile Kilimo cha kufa na kupona na uhamasishaji wa kuhamia vijijini. Nyimbo hizo zimetoa mchango mkubwa sana katika siasa za Tanzania.
Mwaka 1975 Bendi ya Urafiki ilishiriki katika mashindano ya bendi za muziki wa dansi yaliyofanyika Mnazi Mmoja Dar es Salaam na bendi ya Urafiki ilishika nafasi ya tatu na Mzee Ngulimba, kama kiongozi wa Bendi ya Urafiki aliiwakilisha Tanzania pamoja na bendi ya Afro 70 iliyopata nafasi ya kwanza na baadhi ya vikundi vya utamaduni kutoka Tanzania Bara na Zanzibar nchini Nigeria katika maonyesho ya mtu mweusi yaliyofanyika huko.
Kufikia katikati ya miaka ya 1980, bendi ya Urafiki ikawa inasuasua kutokana na uchakavu wa vyombo na Menejimenti iliyokuwepo wakati huo haikuwa tayari kutoa pesa kununulia vyombo vipya.Na huo ndiyo ukawa mwisho wake kwa kufa taratibu.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.