DAR ES SALAAM
Na Esther Ngubes-TURDACO
Kamishna Msaidizi wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Michael Stephen Deleli, amesema kuwa ajali nyingi za bodaboda, zinatokana na usimamizi mbovu wa wamiliki wa vyombo hivyo, kutokana na baadhi yao kuwapa madereva wasio na weledi.
Akizungumza na gazeti Tumaini Letu katika mahojiano maalumu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Kamishna Deleli alisema kuwa wamiliki wengi wa bodaboda hawawasimamii vema watu wanaowapa pikipiki hizo ikiwemo kutozingatia kama wana leseni ama laa.
Aidha, alisema kuwa jambo lingine ni woga wa abiria kushindwa kuwaonya madereva pindi wanapotumia usafiri huo, hasa wanapokwenda mwendo kasi, na uwezekano wa kusababisha ajali.
“Katika tathmini yetu, tumegundua kuwa ajali nyingi hususan za bodaboda, zinasababishwa na ukosefu wa usimamizi wa vyombo hivyo vya usafiri kutoka kwa wamiliki wakuu…
“Pia, woga wa abiria pindi wanapotumia usafiri huo kwa kushindwa kuwaonya madereva wanapoendesha kwa mwendo kasi, hii ni kutokujua wajibu na haki zao za kimsingi wanapokuwa barabarani,” alisema Kamishna Deleli.
Alibainisha pia kuwa takwimu zinaonyesha kwamba ajali nyingi zinatokana na miundombinu mibovu ya barabara, ubovu wa vyombo vyenyewe vya usafiri, pamoja na makosa ya kibinadamu yanayosababishwa na ukosefu wa elimu kuhusu matumizi sahihi ya barabara kwa kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani.
Aidha, Deleli alisema kuwa kulingana na makosa hayo, baadhi ya madereva huvunja sheria kwa makusudi kutokana na sababu za kumchelewesha abiria, na sababu nyingine binafsi.
Alisema kuwa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kimeweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua kwa kiasi kikubwa, hususani ajali za pikipiki, ikiwemo kutoa elimu kwa madereva wa pikipiki kwa kuweka sheria kali zitakazosaidia kupungua kwa ajali hizo.
Kamishina Deleli alisema kuwa miongoni mwa adhabu hizo ni kifungo au faini kwa yeyote atakayejihusisha na uvunjifu wa sheria hizo.
“Natoa rai kwa wananchi wote, madereva, na wamiliki wakuu wa vyombo hivyo vya usafiri, hususani pikipiki, wahakikishe kuwa vyombo hivyo vya usafiri vipo katika mikono salama ya madereva hao.
“Nasisitiza sana kwa madereva wa pikipiki kujiepusha na uendeshaji wa mwendokasi, kuvaa kofia ngumu (helmet), kujiepusha na upakiaji hatarishi wa abiria zaidi ya mmoja, na uendeshaji wa pikipiki ukiwa umetumia kilevi au afya ya mwili ikiwa haipo vizuri,” alisema Kamishna Deleli.
Akizungumza na Tumaini Letu, mmoja wa madereva wa pikipiki aliyejitambulisha kwa jina la Temu, alisema kuwa Sheria za Usalama barabarani wanazifuata, lakini kutokana na makosa ya kibinadam na baadhi ya changamoto zinakuwa nje ya uwezo wao, hujikuta wakisababisha ajali hizo.