Dar es Salaam
Na Mwandishi wetu
Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Bonaventura, Kinyerezi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Francis Hiza, amewasihi wanaume kuhakikisha wanajitoa kwa dhati katika kuhudhuria Jumuiya na kanisani, kwani uwepo wao ni mihimu kwa kuwa wao ni nguzo ya Kanisa.
Padri Hiza alitoa wito huo hivi karibuni wakati akizungumza katika hafla fupi ya Wanaume Wakatoliki Parokia ya Kinyerezi (UWAKA DAY), iliyofanyika Jumatatu ya Pasaka parokiani hapo, ikiwa ni utaratibu wa Parokia kuadhimisha UWAKA Day.
“Katika kuwatia moyo kwa mara ya kwanza nimeaandaa sherehe kwa pesa ya Parokia kwa mwaka huu ili kila kitu wafanye wenyewe. Kwa hiyo hii inanipa mwanga kwamba tunasonga mbele kama wanaume,”alisema Padri Hiza.
Padri Hiza alisema pia kuwa malengo makuu ya kuwakutanisha Wanaume Wakatoliki kukaa pamoja na kujadiliana maisha ya kiimani, ni kuwajenga ili washiriki kikamilifu shughuli za Kanisa, kwani wao ni nguzo ya Kanisa.
Alisema kuwa kila Mwanaume Mkatoliki anatakiwa kuhakikisha anauishi uamaume wake, hasa kwa kutambua kwamba wao ni kichwa cha famiilia, hivyo uhalisia huo lazima udhihirishwe kwa vitendo.
“Mwanaume ni kichwa cha familia, hivyo ni wajibu kwetu lazima tujipange ili tusije kuzidiwa na wanawake na hata katika Kanisa,”alisema Padri Hiza.
Kwa mujibu wa Padri Hiza, wanaume wasikubali kuuza haki zao za kuzaliwa wa kwanza, na kuliacha Kanisa likaangamia, kwani kufanya hivyo wataiangamiza pia jamii.
Kwa upande wake Paroko Msaidizi wa Parokia hiyo, Padri Benson Mapunda, aliwataka Wanaume hao waamke katika maisha ya sala na maisha ya ibada kila mara.
Alisema kuwa UWAKA wanatakiwa kujitahidi walau kila mwezi kusali katika Jumuiya na Misa za Dominika walau mara moja na kufanya maungamo, kwani ni jambo muhimu katika maisha yao.
Padri Mapunda alisema kwamba kila Baba anatakiwa kuhakikisha anazungumza na mwenza wake katika maisha yao ya kila siku, hasa katika mambo ya kiroho, na kuhimizana kufanya maungamo ili kuzirudishia roho zao uhai.
Alibainisha pia kuwa maungamo ya pamoja yanasaidia kwa kiasi kikubwa katika kudumisha mahusiano yao ya ndoa.
Naye Didas Ndyemela-Mwenyekiti wa UWAKA Parokia ya Mtakatifu Bonaventura, Kinyerezi, alisema kuwa huo ni utaratibu wa kawaida unaofanyika kila mwaka katika Siku ya Jumatatu ya Pasaka, ili kutafakari nguvu ya upendo kwa Wanaume Wakatoliki.
“Tunabadilishana mawazo ili tuweze kuona namna gani ya kuendeleza Parokia yetu sisi kama UWAKA,”alisema Ndyemela.
Hata hivyo alisema kuwa UWAKA imefanya kazi kubwa katika kufanikisha ujenzi wa kanisa, nyumba za Mapadri na vituo vya njia ya Msalaba, kwani Kituo cha Tano kimejengwa na UWAKA.