DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Bonaventura - Kinyerezi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Francis Hiza, amewataka Waamini kutoshabikia unafiki, kwani hauna faida yoyote maishani.
Padri Hiza (pichani) alisema hayo wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika, iliyoadhimishwa parokiani hapo.
“Tujitahidi sana katika maisha yetu, tusiupe nafasi unafiki, kwa sababu hauna faida yoyote katika maisha ya Mkristo, na pia hauna faida ndani ya Kanisa;
“Wewe kama Mkristo, usikate tamaa katika maisha yako, kwa sababu licha ya changamoto unazozipitia, Mungu yuko pamoja nawe,” alisema Padri Hiza.
Padri Hiza aliwatada Waamini kutojiingiza katika dhambi ya ushoga, akisema kuwa dhambi hiyo ni kubwa sana, na anayejiingiza humo, hawezi kusamehewa na Mungu.
Padri huyo aliwasisitiza Waamini kulijenga Kanisa la ndani, yaani mioyo yao, kabla ya kulijenga Kanisa la nje, yaani Kanisa jengo.
Aidha, aliwakumbusha kujenga tabia ya kuwapenda zaidi wengine, badala ya wao kusubiri tu kupendwa, kwani upendo huo una nguvu kulingana na Maandiko Matakatifu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tumaini Media aliwashukuru Waamini wa Kinyerezi kwa majitoleo yao ya kuitegemeza Tumaini Media, huku akiwaomba kuendelea kukitegemeza chombo hicho.
Padri Massenge ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu, Makongo Juu, alitumia nafasi hiyo kuwaomba waamini hao, kuendelea kuvitumia vyombo vya habari vya Tumaini Media.
Alisema pia kuwa hata pale watoto wao wanapotaka kutazama Televisheni, wajitahidi kuwawekea chaneli ya Tumaini Tv.