Dar es Salaam
Na Mwandishi wetu
Waimarishwa wameelezwa kwamba kumpokea Roho Mtakatifu kupitia Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, ni kupewa jukumu la kuisimamia, kuilinda na kuitetea imani, pamoja na kuitangaza Habari Njema kwa maneno na matendo.
Fundisho hilo limetolewa hivi karibuni na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara katika Parokia ya Bikira Maria Malkia - Kilimahewa, jimboni humo.
“Kwa upande wetu pia ni siku muhimu ya kukumbuka Vipaimara vyetu. Tulipompokea Roho Mtakatifu katika Kipaimara, tukapewa kazi ya kusimamia imani, kulinda imani na kuitetea, tukapewa kazi hiyo ya kutangaza Habari Njema, kumshuhudia Kristu kwa maneno yetu na matendo yetu,” alisema Askofu Musomba.
Aliongeza kwamba kupitia kumbukumbu hiyo, ni vizuri pia kutathmini na kuona ni kwa kiasi gani Wakristu wamefanikiwa, na kwamba ikiwa hawajafanikiwa, waache nafasi ili Kristu aweze kupenya na kutawala katika maisha yao.
Vile vile, Askofu Musomba aliwasihi Waamini kuondoa hali yoyote ya ukaidi, woga, ubaguzi, ubinafsi pamoja na roho zozote ambazo haziendani na mambo muhimu katika kuitangaza Habari Njema katika maisha yao.
“…maana yake tunaambiwa alama ya kwanza katika ujio wa Roho Mtakatifu, ni uvumi kama upepo mkali kutoka mbinguni, ukajaza chumba kile. Tunaona kwamba upepo ukiwa mkali, mtu anaweza akachukuliwa akashangaa anapeperushwa…
“Lakini lengo la upepo mkali ni kuondoa yote ya zamani, kuondoa ukaidi, kuondoa woga, kuondoa roho zozote zile ambazo haziendani na yale ambayo ni muhimu katika kutangaza Habari Njema, kuondoa ubaguzi, kuondoa ubinafsi, walitikiswa, na haya yote yakaondoka,” alisema Askofu Musomba.
Aliongeza kwamba upendo wa Mungu ndio unaowafanya watu wasiwe na ubaguzi, huku akiwasisitiza kuepuka kuwa na roho za usengenyaji pamoja na kuwachafua wengine katika jamii walipo, kwani kufanya hivyo siyo upendo wa Mungu unavyoelekeza.
Aliwataka Wakristo kuweka pembeni mambo yote yasiyompendeza Mungu katika maisha, badala yake wawe kitu kimoja, huku wakizungumza lugha moja.