Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Polisi yadhibiti kasi dawa za kulevya

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania, Aretas Lyimo. Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania, Aretas Lyimo.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini kati ya Oktoba na Novemba mwaka huu, na kufanikiwa kukamata kilogramu 1,066.105 za dawa za kulevya.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA), Aretas Lyimo, alisema  kuwa mpaka sasa watuhumiwa 58 wamekamatwa kwenye operesheni hiyo.
“Katika dawa za kulevya tulizozikamata, ni pamoja na mililita 447 za dawa tiba zenye asili ya kulevya, na tumeweza kuteketeza jumla ya ekari 157.4 za mashamba ya bangi, na lita 19,804 za kemikali bashirifu,”alisema Kamishna Lyimo
Aidha alisema kuwa kati ya dawa hizo, kilogramu 687.32 za skanka na kilogramu moja (01) ya hashishi, zilikamatwa katika eneo la Goba, Dar es Salaam, zikiwa zimefichwa ndani ya nyumba ya mtuhumiwa.
Alisema kuwa uchunguzi umebaini kuwa wateja wengi wa skanka ni wanawake, ambao hudai kutumia dawa hizo kupunguza msongo wa mawazo na kujistarehesha.
“Skanka ni aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu, inayosababisha madhara makubwa kiafya. Vile vile, hashishi ambayo hutengenezwa kwa mchanganyiko wa maua na mafuta ya mbegu za bangi, inapovutwa huzalisha kemikali hatari zinazoweza kusababisha magonjwa ya akili kwa haraka. Mara nyingi jamii huamini kuwa watu wanaopatwa, na magonjwa haya wamerogwa,”alisema Lyimo.
Adiha, alisema kwamba katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Mamlaka ilikamata mililita 120 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Codein, zikiwa zinasafirishwa kwenda nje ya nchi, pamoja na mililita 327 zilizokutwa nyumbani kwa mtuhumiwa eneo la Tabata Kinyerezi, jijini Dar es Salaam.
“Dawa hizi ziliingizwa nchini kinyume na taratibu, zikiwa zimewekwa chapa bandia ya dawa za kuogeshea mbwa na paka, ili kuepuka kubainika. Kukamatwa kwa dawa hizi ni ishara ya uwepo wa tatizo la matumizi holela ya dawa za tiba zenye asili ya kulevya, Hali hii inachangiwa na kuimarika kwa udhibiti wa dawa za kulevya, na kusababisha wafanyabiashara na watumiaji kutumia dawa tiba ya kulevya kama mbadala wa dawa za kulevya,”alisema Kamishna Lyimo.
Kamishna Lyimo alisema kuwa mkoani Dodoma, Mamlaka imewakamata watuhumiwa wawili Suleiman Mbaruku Suleiman (maarufu Nyanda), mwenye umri wa miaka 52, na Kimwaga Msobi Lazaro (miaka 37) wakazi wa mtaa wa Kinyali, Kata ya Viwandani.
“Watuhumiwa hao walikamatwa na jumla ya gramu 393 za heroin. Nyanda anafahamika kama kinara wa biashara ya dawa za kulevya mkoani humo, na amekuwa akifuatiliwa kwa muda mrefu,”alisema.
Kupitia operesheni za kanda, DCEA pia imekamata kilo 303.553 za bangi, gramu 103.8 za heroin, na kilo 63 za mirungi katika maeneo mbalimbali nchini.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inawaomba wananchi waendelee kuunga mkono jitihada hizi kwa kufichua wafanyabiashara wa dawa za kulevya, na kuhamasishana kutoshiriki katika biashara na matumizi ya dawa za kulevya.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.