DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Utume wa Wanaume Katoliki (UWAKA) wametakiwa kujadiliana na kupambanua kuhusu mambo msingi, ili waendelee kuwa nguzo imara katika Kanisa.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Padri Vincent Sabiit –SDS, wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Siku ya UWAKA (UWAKA Day) Parokia ya Mtakatifu Polycarp Askofu na Shahidi – Kilamba, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
“Ipo haja ya UWAKA kujadiliana na kupambanua juu ya mambo mbalimbali yenye tija, ili muendelee kuwa nguzo imara katika Kanisa...
“Katika kujadiliana huko, ipo haja ya kujadiliana pia kuhusu mambo yanayomhusu Mungu, ikiwemo kuwatia moyo wale wote wanaochechemea kiimani,” alisema Padri Vincent.
Padri huyo aliwasihi UWAKA kutenga muda na kuamua kujadili mambo yenye tija, huku wakiepuka kuwa na mijadala inayosababisha mipasuko na huzuni katika maisha ya watu.
Pia, aliwasisitiza kusaidiana wao kwa wao, huku wakihakikisha pia wanawasaidia vijana, hasa wale wanaosumbuliwa zaidi na malimwengu katika maisha yao.
“Sisi kama UWAKA tunaposherehekea leo, tunapaswa kujiuliza kwamba, je, kweli sisi ni nguzo imara? Je, sisi ni nguzo iliyosimama sawasawa au imeelemea upande mmoja na inataka kuanguka?
“Tukumbuke kwamba tunalo jukumu kubwa la kuendelea kujadiliana juu ya mambo yaliyo mema, ili tuzidi kuwa nguzo imara katika Kanisa letu na katika familia zetu, na pia kuweza kuwa na vijana bora watakaolisaidia Kanisa letu siku zijazo,” alisema Padri huyo.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo ya Kilamba, Padri Timothy Nyasulu Maganga alimshukuru Padri Vincent kwa homilia yake aliyoitoa katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu.
Padri Nyasulu aliwashukuru UWAKA kwa kufika kwa wingi katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu, akiwasihi kuendeleza umoja na mshikamano wao, ili kuendelea kukuza chama hicho cha kitume parokiani hapo.
Naye Mwenyekiti wa UWAKA Taifa, Cassian Njowoka, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika siku hiyo ya UWAKA Parokiani hapo, aliwapongeza wana UWAKA wa Parokia hiyo kwa kuandaa Adhimisho hilo la Misa Takatifu ya Siku yao.
Njowoka aliwashauri wanaume kujiunga na chama hicho cha kitume cha UWAKA, kwani kuna faida kubwa watakazozipata ndani ya chama hicho, ikiwemo kusaidiana wakati wa magonjwa na matatizo mengine.
Vile vile, alitumia nafasi hiyo kuwaasa Wanaume Wakatoliki na Waamini wengine, kushiriki katika suala zima la Uchaguzi Mkuu mwaka ujao 2025, ikiwemo kujiandikisha na kupiga kura ili kuwachagua viongozi watakaowaongoza.
Aliwasisitiza pia kuwaunga mkono Waamini wenzao pale wanapohitaji kugombea nafasi wanazozihitaji, kwani kwa kupitia viongozi hao, watampeleka Kristo katika nafasi watakazozipata.
“Kwa hiyo, tunaaswa na Mababa tujitokeze, tujiandikishe kwa wingi, tupige kura, na kama una sifa ya kupigiwa kura, jitokeze ugombee. Na kama tunaona mwenzetu amejitokeza anataka kugombea nafasi fulani, ‘tum-support’ tusianze kupambana naye, ili ampeleke Kristu katika nafasi ambayo yeye atakuwa ameipata,” alisema Mwenyekiti huyo wa UWAKA Taifa.
Aliongeza kwamba Mungu Mwenyezi amewapa Wakristo Wakatoliki uwezo mkubwa wa kutambua mambo mbalimbali, hivyo yeyote atakayejitokeza, awe mwanaume au mwanamke, ana haki ya kuungwa mkono katika nafasi anayowania.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWAKA Parokia ya Kilamba, Venance Kavishe, ambaye pia ni Mwenyekiti UWAKA Dekania ya Mbagala, alimshukuru Padri Timothy Nyasulu Maganga kwa kuendelea kuwaunga mkono katika kila wanalolifanya wana UWAKA parokiani hapo.