VATICAN CITY, Vatican
Baba Mtakatifu Fransisko amewataka Waamini kuwahubiria maskini Habari Njema, kuwatangazia wafungwa uhuru wao.
Aliyasema hayo katika Adhimisho la Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, katika Dominika ya Januari 26 mwaka huu wa 2025, ambapo ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Dominika ya VI ya Neno la Mungu iliyoanzishwa na Papa mwenyewe mwaka 2019.
Aidha, katika fursa hiyo, ilitolewa pia Huduma ya Usomaji wa Neno la Mungu kwa waamini 40 kutoka mataifa mbalimbali duniani, ambayo pia ilikuwa ni Adhimisho la Misa Takatifu ya Kufunga Jubilei ya Ulimwengu wa Mawasiliano, iliyoanza tangu Januari 24 kwa ufunguzi wa Misa.
Katika homilia yake Baba Mtatifu Fransisko alisema kuwa Injili waliyoisikia katika Adhimisho hilo inatangaza utimilifu wa unabii unaofurika katika Roho Mtakatifu, na yule anayeitimiza ni Yeye ajaye kwa nguvu za Roho.
“Neno la Mungu liko hai, linatembea nasi kwa karne nyingi, na kupitia nguvu za Roho Mtakatifu linafanya kazi katika historia. Bwana kiukweli siku zote ni mwaminifu kwa ahadi yake, ambayo huiweka kwa sababu ya upendo kwa wanadamu. Hivi ndivyo alisema Yesu katika sinagogi la Nazareti. Leo Maandiko haya yametimia masikioni mwenu,” alisema Baba Mtakatifu.
Baba Mtakatifu alisema kuwa ni bahati iliyoje yenye furaha katika Dominika ya Neno la Mungu, ambapo bado wakiwa mwanzoni mwa Jubilei, ukurasa huo wa Injili ya Luka unatangazwa, ambamo Yesu anajidhihirisha kuwa Masiha aliyewekwa wakfu kwa kupakwa mafuta na kutumwa kutangaza mwaka kwa neema ya Bwana.
Papa alisema kuwa katika Dominika hiyo iliyowekwa maalum kwa ajili ya Neno la Mungu, ni wajibu wa kila mmoja kumshukuru Mungu kwa kuwa amewaelekezea Neno lake lililomfanya mtu kwa wokovu wa ulimwengu.
Aliongeza pia kuwa hilo ndilo tukio ambalo Maandiko yote yanazungumza juu yake, ambayo yana watunzi wao wa kweli, yaani watu na Roho Mtakatifu, na kwamba Biblia nzima inamkumbuka Kristo na kazi yake, na Roho hufanya uwepo katika maisha yao na katika historia.
“Tunaposoma Maandiko, tunapoomba na kuyasoma, hatupokei habari kuhusu Mungu tu, bali tunamkaribisha Roho ambaye hutukumbusha yote ambayo Yesu alisema na kutenda (Taz Yh 14:26). Hivyo mioyo yetu, ikiwa imewashwa na imani, inangojea kwa matumaini ujio wa Mungu,” Papa alisema.
Aliongeza kuwa kila mwamini lazima awe na mazoea zaidi ya kusoma Maandiko, na kwamba katika hilo, alipendekeza tena kuwa kila mtu awe na Injili ndogo mfukoni ya Agano Jipya, na kubeba katika mfuko, na wakati wa mchana kuisoma.