Kufuatia ziara ya kitume ya kiongozi wa Kanisa Katoliki ulimwenguni, Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Ufaransa, Kanisa limekusudia kuchochea nguvu mpya ya utendaji kwa kuanzisha jukwaa pana na la wazi la mawazo na matendo, ambapo waamini na wasioamini wanaweza kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Aidha, kati ya mambo muhimu ambayo Baba Mtakatifu Leo XIV anagusia wakati wa hija yake ya kitume nchini humo, ni pamoja na Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; ujenzi wa haki na amani; changamoto ya teknolojia ya akili unde sanjari na utambulisho wa Bara la Ulaya.
Papa alisema kuwa Ufaransa ni nchi ambayo inatakiwa kutumia tunu zake za kitamaduni, kibinadamu na kidiplomasia ili kugundua upya na kuimarisha mwelekeo wake unaozingatia utu, heshima, haki msingi za binadamu pamoja na kukuza uhusiano na Mwenyezi Mungu, kwa kuzamisha mizizi ya Kikristo barani Ulaya na hatimaye kujikita katika mchakato wa utakatifu wa maisha, ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na kusaidiana; majadiliano katika ukweli na uwazi; bila kusahau ushirikiano wa Kimataifa ambao kwa sasa unaonekana kudhohofu sana.
Katika muktadha huo, Papa aliadhimisha ibada ya Misa Takatifu katika ‘Uwanja wa maridhiano; yaani “Place de la Concorde”, akisema kuwa hilo ni jambo jema na la kupendeza ndugu wanapoishi pamoja kwa umoja, ili kutangaza ukuu wa Mungu; kwa kuwaimarisha waamini katika imani, kuwahimiza kung’aa zaidi, kushirikishana maisha ya uzima wa milele, amani na upendo
unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, ili kumgeukia Kristo Yesu, chemchemi ya maji ya uzima, maji yanayozima kiu na kustawisha maisha na upendo wa Mungu.
Alisema kuwa hayo ni maji yaliyomiminwa mioyoni mwao kwa njia ya Roho Mtakatifu waliyopewa, huku kiu ya kumtafuta Mungu ikiwa ndani kabisa ya mioyo ya waamini, kilio cha moyo mnyenyekevu na wenye shauku kubwa ambao kiu yake ya ndani kabisa na ya msingi wa kuwepo kwake inaendelea kukua na kupanuka.
















