Na Celina Matuja
Waimarishwa wanatakiwa kuwa askari hodari wa Yesu Kristo kwa kujazwa nguvu na mapaji ya Roho Mtakatifu na kutumwa kuwa mashahidi wa Kristo, kama walivyoahidi walipopokea Sakramenti ya Kipaimara.
Hayo yamesemwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Vincent Mpwaji, katika homilia yake wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya utolewaji wa Sakramenti ya Kipaimara kwa waimarishwa 42 iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Tomas Mtume Vigozi, iliyopo Mbagala, Dar es Salaam.
Alisema ili wafanikiwe kuwa mashahidi wa Kristo Yesu, kila mara wanapaswa kujitahidi kuungama dhambi zao ili wanapokwenda kushiriki Ekaristi Takatifu wawe katika hali ya neema, wampokee Yesu Kristo na kumruhusu akae ndani yao siku zote za maisha yao.
Alisema lengo la kusanyiko hilo ni kumshukuru Mungu kwa waimarishwa hao 42 waliompokea Roho Mtakatifu, kama Mitume walivyompokea Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste.
Aidha, aliongeza kuwa kila mtu aliyebatizwa na kupokea Sakramenti ya Kipaimara ametumwa kuwa shahidi wa Kristo. Hivyo, jeshi la mashahidi wa imani linaendelea kuongezeka katika Taifa la Mungu.
Askofu Mpwaji alisema Yesu Kristo baada ya kufufuka, alikutana na Mitume wake na kuwapa maelekezo ya kubaki Yerusalemu mpaka watakapopokea nguvu ya Roho Mtakatifu kutoka juu.
















