Dar es Salaam
Na Nicholaus Kilowoko
Kuna michezo mingi sana ulimwenguni ambayo imekuwa ni kipenzi cha watu, lakini tenisi ni mchezo unaofurahiwa na watu wa rika zote na viwango vyote.
Mchezo wa tenisi umekuwa ukivutia watazamaji wake na wachezaji tangu mwanzoni mwa karne ya 12 ilipoanzishwa kwake na hapa kuna baadhi ya ukweli na matukio ya kuvutia yaliyotokea tangu historia ya awali ya tenisi ambayo natamani uyafahamu.
Kabla wachezaji wa tenisi hawajaanza kutumia raketi, watu walitumia viganja vya mikono yao kupiga mpira huku na huko juu ya wavu.
Katika karne ya 12, watu walipata shida ya mikono kuvimba na kuwa mekundu kutokana na mchezo ulioitwa “jeu de paume”, ambao unamaanisha “mchezo wa kiganja” ambapo ilienda hadi karne ya 16 ndipo raketi zilianza kutumika.
Mabadiliko ya rangi ya mpira wa tenisi
Kabla ya mipira ya tenisi kuwa ya rangi ya njano, ilikuwa ya rangi nyeupe.
Ilifika wakati wa mashindano ya Wimbledon mwaka 1986 ndipo mipira ya tenisi ya rangi ya njano ilipoanza kutumika.
Waandaaji waliamini kuwa mpira wa rangi ya njano ungekuwa rahisi zaidi kwa watazamaji kuufuata kwenye televisheni.
Utamkaji wa maneno “Racket” dhidi ya “racquet.”
Katika maajabu mengine ya mchezo huo ni namna ya kutamka maneno ya vifaa vyake ambapo imeufanya kuwa mchezo wa tofauti sana na michezo mingine.
Tahajia ya “racket” ndiyo njia ya kawaida ya kuandika jina la kifaa kinachotumika kuchezea katika michezo ya wavu kama vile tenisi.
Tahajia nyingine ni “racquet”. Neno “racquet” hutumika zaidi katika michezo kama vile ‘squash’ na ‘racketball’.
Ingawa tovuti nyingi zitakuambia kuwa “racket” ndiyo tahajia sahihi, shirika la USTA hutumia neno “racquet” mara kwa mara.
Ndugu walioshinda mara nyingi mataji ya tenisi
Venus na Serena Williams ndio dada wa kwanza kabisa kushinda medali za dhahabu za Olimpiki katika mchezo wa tenisi.
Dada hawa walishinda medali yao ya kwanza ya dhahabu ya Olimpiki katika Michezo ya Olimpiki ya Sydney mwaka 2000 na kwa sasa, wana medali nyingine mbili za dhahabu walizoshinda Beijing mwaka 2008 na London mwaka 2012.











