DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Moja ya Mambo muhimu na ya Msingi ambayo Baba Mtakatifu Fransisko ameyakazia na kuyasisitizia katika ziara ya Kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan na ujumbe wake aliyoifanya hivi karibuni mjini Vatican, ni malezi na makuzi ya Watoto.
Katika ziara hiyo ya Kitaifa, Mama Evaline Malisa Ntenga, ambaye ni miongoni mwa ujumbe huo wa Rais, anasema kuwa Baba Mtakatifu Fransisko amekazia umuhimu wa malezi na makuzi ya watoto, sanjari na kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.
Dalmas G. Gregory, M/Kiti Halmashauri Walei Jimbo la Zanzibar, anasimulia yale yaliyomgusa. Leonard Mapolu, Mwenyekiti wa VIWAWA, Taifa, anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka kupitia kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (Tanzania Episcopal Conference: TEC).
Imegota takribani miaka 12 tangu Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania alipotembelea mjini Vatican na kukutana na Baba Mtakatifu Benedikto XVI tarehe 19 Januari 2012.
Katika mazungumzo ya dakika kumi na tano, viongozi hawa wawili waligusia kuhusu: Majadiliano ya kidini, amani katika eneo la Maziwa Makuu, Afya, Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Ni katika muktadha wa kujenga na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican, tarehe 12 Februari 2024, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania alikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Fransisko mjini Vatican.
Aidha, Rais Samia alibahatika pia kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu Mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa.
Katika mazungumzo yao ya faragha yaliyodumu kwa takribani dakika 25 wameridhika na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Tanzania; mchango na dhamana ya Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania, hususan katika sekta ya: elimu, afya, ustawi wa jamii pamoja na changamoto ambazo Tanzania inapitia kwa sasa.
Mama Evaline Malisa Ntenga, Mjumbe wa Bodi Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa Wanawake Wakatoliki Afrika WUCWO Afrika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa, nchini Tanzania, katika mahojiano maalum na Radio Vatican, alionesha furaha kwa heshima waliyopewa waamini walei kuungana na Rais Samia Suluhu Hassan katika ziara yake ya kikazi mjini Vatican.
Mama Ntenga alimpongeza Rais Samia kwa juhudi zake za kukuza: Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kusonga mbele; mambo yanayofumbatwa katika falsafa ya “Four R.” Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Fransisko alipokutana na kuzungumza na Mama Ntenga amekazia umuhimu malezi na makuzi ya watoto sanjari na kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.
Amewasihi waamini walei waendelee kushikamana na kutembea pamoja kama sehemu muhimu sana ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi nchini Tanzania; ujenzi ambao kimsingi unafumbatwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume. Ameipongeza Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, (WAWATA), kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kwa malezi na makuzi ya Utoto Mtakatifu nchini Tanzania.
Pamoja na mambo mengine, Rais Samia Suluhu Hassan alikazia umuhimu wa kujenga, kuendeleza pamoja na kudumisha maridhiano ili kuendeleza misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya Tanzania.