DAR ES SALAAM
Na Dk. Deoscorous B. Ndoloi
Mpendwa msomaji, karibu tena katika makala hii ya kuzungumza katika hadhara. Kwa wasomaji ambao watakuwa wageni katika safu hii, mada juu ya kuzungumza katika hadhara tuliianza katika makala ya 13 ya mwezi Novemba 2023. Baadaye, katika makala ya 17, ya mwanzo wa mwezi Desemba 2023, tuliona jinsi ya ‘kukabili na kumiliki jukwaa’. Kwa hiyo tumedumu katika mada hii ya namna ya kuzungumza katika hadhara, kwa takriban miezi mitatu. Ni matumaini yangu kwamba umefaidika na maarifa tunayoshirikishana, ili kujijengea stadi na weledi katika mawasiliano ya kibinadamu.
Leo, katika makala hii ya 28, tujadiliane namna ya ‘kuaga jukwaa’. Natumaini msomaji wangu ungetegemea niseme ‘kuaga hadhira au wasikilizaji’ lakini nimependa kuiita stadi hii ni ‘kuaga jukwaa’ kwa sababu zitakazokuwa wazi kwako baada ya kusoma na kuielewa mada hii. Yapo mambo muhimu ya kuzingatia unapofikia tamati ya mazungumzo. Nitayajadili kwa nambari ili yawe rahisi kukumbuka, na hasa kwa wale walioniambia kwamba huwa wanajadili mada hizi kama sehemu ya mafunzo yao chuoni, juu ya mawasiliano kwa umma (mass communication).
Kwanza, nikukumbushe – tulishauriana kwamba mwisho mzuri unaandaliwa toka mwanzo kabla ya wasilisho. Hivyo utakuwa umejipanga vizuri, kiratiba, iwapo utaacha dakika walao tano za kuhitimisha wasilisho lako. Ukijipanga vibaya utamaliza wasilisho ukiwa wamebakiza muda mrefu, hivyo kuanza kutafuta namna ya kujazilizia muda uliobaki. Kwa namna hii, unaweza kushawishika kuingiza masuala ambayo hayaendani na kusudio la mada husika. Unaharibu kazi nzuri uliyokwishafanya toka awali, unawavuruga au kuwachosha wasikilizaji. Afadhali ukimaliza yale uliyopanga, aga na uondoke. Kuna hata msemo kwamba, “mgeni mzuri ni yule anayefahamu muda wa kuaga”. Wakati mwingine ukijipanga vibaya unatindikiwa na muda, huku ukiwa umebakisha masuala muhimu ya kuwasilisha. Kwa namna hii, unaanza kuongeza kasi ya ajabu kuzungumza, kiasi kwamba hueleweki tena. Unaharibu ulichokwishasema. Jifunze kutumia muda.
Pili, wakati unatoa wasilisho, inawezekana wapo waliochelewa wasiweze kusikia usuli wa mada yako. Inawezekana wapo waliolazimika kutoka nje ya ukumbi kwa dharura wakati unatoa wasilisho. Pengine wengine walikosa utulivu, au wewe mwenyewe uliharibu mtiririko wa mawazo, hivyo ukawapoteza wasikilizaji, kwa muda. Wakati wa kuaga jukwaa, ndiyo muda wa fidia. Wakumbushe tena wasikilizaji, kwa kifupi sana, lengo la wasilisho lako; kwa maneno yaleyale uliyotumia mwanzoni. Kisha, tafuta walao mambo matatu au manne ambayo, ikiwa wamesahau mengi waliyosikia, basi haya waondoke nayo. Yape msisitizo wa kutosha.
Tatu, usiombe msamaha, labda kwa vile unahisi kuhufanya vizuri au hukuitendea haki mada husika. Kuomba msamaha, hasa ukiwa umefanya vizuri, ni kujifanya kuonesha unyenyekevu ambao unaweza kutafsiriwa kama unafiki. Wewe washukuru na waambie wasikilizaji kwamba una matumaini makubwa wote wamefaidika na wasilisho lako, na kwamba waliyoyasikia watayafanyia kazi na kuwashirikisha wengine.
Nne, usipoteze muda kuwashukuru waliokualika na waandaaji wa semina au kongamano. Hawa watashukuriwa mwishoni, na wenyeji wao kwa niaba ya kila mmoja aliyealikwa na aliyehudhurisha mada. Itoshe kusema, “Nawashukuru wote kwa usikivu wenu”. Hawa ‘wote’ ni pamoja na waandaaji wa kongamano. Hapo awali, katika makala ya 23, tuliona ‘aina za hadhira’; moja tuliita hadhira chuki (hostile audience) na nyingine hadhira mateka (captive audience). Tuliona kwamba hizi aina mbili za hadhira zinaweza kuwa na watu ambao wana mwamko wa chini sana, hivyo wasikupe ushirikiano wa kutosha wakati unatoa mada. Hata kama unahisi walikuwepo watu wa namna hii, usigusie jambo hili. Washukuru wote kwa ujumla kwa ‘usikivu mkubwa’ waliokuwa nao. Kumbuka – aga jukwaa na uso uleule ulioingia nao, wa kujiamini na kuwathamini wasikilizaji.
Tano, chukua na panga vifaa vyako kwa uangalifu (karatasi, kalamu, magazeti, matini, simu, kompyuta, nk), na teremka jukwaani huku umejiamini. ‘Usikumbe’ kila ulichokuwa nacho katika rundo, na kuondoka kama umebeba taka. Tena, wakati wa kuondoka, usioneshe dalili zozote za ‘kutoroka’ ama ‘kukimbia’. Haya tumewahi kuyaona kwa wawasilishaji fulani, ambao kuondoka kwao jukwaani kuliashiria kwamba walikuwa wanasubiri kundoka katika mateso waliyokuwa wanapitia. Kule kujiamini ulikokuwa nako wakati unakabili jukwaa (self-credibility), kuwe kulekule wakati wa kushuka toka kwenye jukwaa.
Sita, kumbuka semina au kongamano linaendelea, hata baada ya wasilisho lako. Wakati unaelekea kwenye sehemu ya kuketi, kwepa kumpa kila mtu mkono kwa nia ya kupongezana. Hayo yafanyike nje ya ukumbi baada ya shughuli rasmi kumalizika. Ikiwa hadhira iliamua kukupigia makofi ulipomaliza wasilisho lako, inatosha; teremka toka jukwaani, tembea kwa kujiamini, nenda kakae. Ikiwa unahitaji kwenda maliwato, usitoke kwenye jukwaa na kupitiliza. Nenda kwanza kwenye sehemu yako, kaa kwa muda, halafu simama tena.
Wiki ijayo tutaona kanuni za kuandaa na kutumia zana (presentation aids). Tumsifu Yesu Kristu!
Itaendelea wiki ijayo.