Dar es Salaam
Na Mathayo Kijazi
Waandishi wa Habari na Wadau wa Tasnia ya Mawasiliano nchini, wametakiwa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa upole, wakitambua kwamba kazi yao ni Daraja la kuwaunganisha watu.
Hayo yalisemwa na Ndugu Calist Tesha -OFM Cap, Padri Mmsionari wa Shirika la Wafransisko Wakapuchini wakati wa Mafungo ya Wafanyakazi wa Tumaini Media katika Kituo cha Mtakatifu Damiano - Msimbazi Center, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
“Papa Fransisko anataka wanahabari watoe habari wakiongozwa na upendo wa Kiinjili kwa kuzingatia kulinda utu wa kila mtu. Muwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari zilizopo ndani yenu kwa upole, kwa unyofu, na kwa hofu.
“Papa aliwataka Wanahabari na Wadau wa Tasnia ya Mawasiliano, kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa upole, na kwa hofu, wakitambua kwamba wanapaswa kuwa ni madaraja ya kuwaunganisha watu, na kamwe wasiwe kikwazo au kuta za kuwagawa,” alisema Padri Tesha.
Aliongeza kuwa huu ni wakati wa kutangaza na kushuhudia ukweli unaosimikwa katika tunu msingi za Kiinjili, na mtu hapaswi kuogopa kuutangaza ukweli na wala sio unaodhalilisha utu wa mtu.
Padri Tesha alisema kuwa katika kuutafsiri ujumbe wa Papa, ameona mambo ya msingi ambayo Papa anataka kuwaeleza watu, ikiwa ni pamoja na kuyaeleza kwa ufasaha na bila woga, mambo yote ya msingi.
Aliongeza kuwa ni jambo baya kuwaeleza watu mambo ya uongo, huku wakiwaaminisha kwamba ni ya kweli, akiwasisitiza wanahabari kuepuka kuyasema mambo hayo, ili waendelee tu kusema yale yanayostahili kusemwa.
Vile vile, aliwataka kuyazinga maadili ya Kiinjili katika utoaji wa habari, ikiwa ni pamoja na kuhimiza wito katika familia zao, na hata jamii kwa ujumla.
“Huo ni kama wito wetu, kama vile katika familia, baba ni lazima azingatie wito wake wa kuwa baba, kwa hiyo ni lazima afuate maadili ya kibaba, na kama ni mama, pia ni lazima azingatie maadili ya kimama.
“Padri nae kama wito wake ni kusimama kama Padri, maana yake kuna maadili yake pia. Kwa hiyo hata Wanahabari ni lazima kuzingatia maadili ya Kiinjili katika kazi yetu, katika wito wetu kama Wakristo. Kwa hiyo, ukweli uwe ‘constructive truth with good intention with accuracy, avoid unnecessary harm,’ na kujiuliza maswali muhimu ‘What I’m I report? Why should I report? When to report? Where to report?...’ hayo ni mambo muhimu,” alisema Padri huyo.
Alisisitiza kwamba kuna umuhimu mkubwa wa kupima ‘credibility’ ya taarifa kabla ya kuitoa, kwani hapo ndipo Papa alipowasihi Wanahabari kuzungumza ukweli katika upendo.
Aidha, Padri Tesha aliwataka Waandishi wa Habari kuepuka kuwa na upendeleo katika kazi zao, akisema kwamba upendeleo si tabia ya Kikristo wala ya Kiinjili, hivyo kama wataizingatia Injili, ni lazima pia waepuke kuonesha upendeleo katika kazi zao.
Katika mafungo hayo Padri Tesha aliwahimiza Waandishi wa Habari kufanya kazi zao kwa moyo, huku wakiepuka kukata tamaa, akiwataka kuiga mfano wa Yesu Kristo anayeadhimishwa katika kipindi cha Kwaresma, kwamba licha ya mateso aliyoyapata, bali hakukata tamaa, kwani yalikuwa mateso ya wokovu.